Mjadala: Athari za 'Magonjwa Adimu' pamoja na Huduma zake

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
626
938
1708875459016.jpeg

Je unajua kwamba kuna watu Milioni 300 Duniani wanaishi na magonjwa Adimu?

Magonjwa Adimu ni matokeo ya maambukizi ya Bakteria au virusi na sababu za mazingira au kansa adimu. 5% ya idadi ya watu Duniani wanakabiliwa na Magonjwa Adimu kwa sasa. 72% ya Magonjwa yote ya adimu yanatokana na urithi wa vinasaba.

Kuna magonjwa zaidi ya 6000+ yanayotambuliwa kama magonjwa Adimu.

Kujifunza zaidi kuhusu Magonjwa haya, JamiiForums itaendesha Mjadala na Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Taasisi ya Magonjwa Adimu - Ali Kimara, Hospitali ya Aga Khan, Chama cha Wataalamu wa Vinasaba vya Binadamu (THGO) na Lupus Warriors siku ya Jumanne Februari 27, 2024 Saa 12:00 Jioni hadi Saa 2:00 Usiku kupitia XSpaces ya JamiiForums

Link ya Mjadala https://jamii.app/MagonjwaAdimu

Karibu!

---

Prof. Francis Furia (Daktari MNH)
Tunapozungumzia Magonjwa Adimu tunazungumzia Magonjwa yanayoathiria Watu wachache. Magonjwa yanayoathiri Mtu mmoja kati ya Watu 2,000 hayo tunayaweka kwenye kundi la Magonjwa Adimu Mpaka sasa kuna Magonjwa takriban 6,000 ambayo yameshatambulika kuwa kwenye Magonjwa Adimu, ambapo kuna Magonjwa ya #Saratani, Moyo, Ngozi na kadhalika

Kikawaida Kila Mwaka huwa inaazimishwa Siku ya Magonjwa Adimu ambapo ilichaguliwa iadhimishwe kwenye Siku ya Mwisho ya Mwezi Februari. Hivyo hata kwa Mwaka wenye Siku 29 kama huu Maadhimisho yatakuwa kwenye Siku hiyo ya mwisho.


Dkt. Mariam Noorani (Aga Khan):
Kitakwimu hatuwezi kusema kwamba #Tanzania tuna Idadi kamili ya kujua ni Watu kiasi gani wameathiriwa na Magonjwa Adimu Mwaka huu tumeamua kufuatilia zaidi kuhusu tatizo hili kwasababu ya Changamoto ya kupata Takwimu, hivyo tunataka kufahamu kwa kila Daktari Mfano wa Watoto ni Watoto wangapi ambao anakutana nao wenye Changamoto


Dkt. Mohamed Zahir (MUHAS):
Naweza kusema karibu Asilimia 80 ya Watu wanaoathirika na Magonjwa Adimu wanapata tatizo kutokana na Vitu vinavyojenga Vinasaba Mpangilio wa Vinasaba huwa ni wa Kipekee kwa kila Binadamu hivyo inapotokea Mabadiliko yoyote husababisha Matatizo

Ni muhimu sana hata kwenye kufanya Utafiti ni vizuri kufahamu Vinasaba vimejengekaje kati ya Binadamu mwenye tatizo pamoja na wale ambao hawana tatizo ili kujua ni Mtu amepata Ugonjwa wa aina gani

Kwa hapa #Tanzania kupata Vipimo vya Genetics ni ghali sana na hii ni hata kwa Dunia nzima, Vipimo hivi gharama zake zipo juu

Pia, kwa Tanzania bado tuna Changamoto ya kupata Madaktari Bingwa wa hizi Genetics (Vinasaba). Ndio maana tunataka kuanzisha Research Funds ili tuweze kujua Watu hawa wenye tatizo wanaishi Maeneo gani na tunaweza kuwasaidia. Hili litawezekana kwa kuwa na hizi Kanzidata


Dkt. Mohamed Zahir (MUHAS):
Asilimia 20 ya Wagonjwa wanaobaki ni wale ambao hupata Magonjwa kutokana na Sababu za Kimazingira, Mfano Mtu ambaye anavuta Sigara

Ni muhimu kwa Kila Nchi kuwa na Mfumo wa kufanya #DNAScreening kwa Watoto wanaozaliwa ili kufahamu Vinasaba vyao vimeundwaje ili kurahisisha Msaada wa kumpatia Mtoto pale anapokuwa Mtu mzima


Prof. Francis Furia (Daktari MNH):
Kuna Vipimo ambavyo vinaweza kufanyika mapema kabisa ili kutambua tatizo tangu Mtoto akiwa Mdogo

Kwa Nchi za wenzetu ambazo zimeendelea wanaweza kufanya Kipimo cha kutambua Ugonjwa kwa Mtoto tangu akiwa Tumboni na hii hufanywa zaidi na Wazazi ambao yawezekana walishapata Mtoto wa awali ambaye ana Changamoto

Wengine wakishafanya Vipimo na kugundua kuna tatizo huwa wanachagua kusitisha Ujauzito


Dkt. Mariam Noorani(Aga Khan):
Kuhusu Matibabu kwa Magonjwa Adimu mengi hakuna Matibabu ya moja kwa moja bali kuna Tiba za kumsaidia Mgonjwa kurahisisha Maisha yake ya Kila Siku

Mfano Kutokana na aina ya Ugonjwa kuna ambao huhitaji Vifaa vya Mazoezi ya Viungo (Physiotherapy) au wengine huhitaji Dawa au Mitungi ya Oksijeni pamoja na Mashine za Kupumulia

Kwa #Tanzania Matibabu haya Gharama ni kubwa na wengi wanashindwa kumudu vile wanavyohitaji

Pia, bado hatujawa na Matibabu ya Genetics (Vinasaba) kwa hapa Nchini kwetu, kwa Upande wa Dawa zinapatikana japo ni ghali sana. Tumepiga hatua ila bado kuna mengi ya kufanya


Maureen Manyama (Anaishi na Lupus):
Mimi ninaishi na Ugonjwa wa #Lupus na ni Miaka 5 sasa tangu kugundulika Upande wa Changamoto kwanza ni ngumu kuugundua Ugonjwa Mapema.

Mimi niliwaona Madaktari wengi sana mpaka ilipofikia kipindi cha Figo kutaka 'kufail' ndio ikagundulika kwamba ninasumbuliwa na Ugonjwa wa Lupus

Changamoto nyingine ni Gharama za Matibabu. Mfano kuna kipindi nikiwa Hospitali ilikuja Bill ya karibu Milioni 60. Sasa kwa Sisi wengi ambao tunatokea kwenye Familia Masikini inaleta Ugumu wa kupata tiba

Shida nyingine ni Gharama za kuishi na huu Ugonjwa, kuna vitu vingi ambavyo Mtu anakuwa anashindwa kuvifanya yeye mwenyewe. Mfano kwa Sisi wenye Lupus Jua linatuathiri hivyo inabidi uwe na namna ya kujikinga

Pia, kuna Changamoto ya Bima ya Afya ya Taifa kutogharamia baadhi ya Matibabu na Gharama ni kubwa

Mfano, mpaka sasa kuna Dawa ambazo Mimi mwenye #Lupus siwezi kuzipata kupitia Bima. Hivyo, Changamoto ni nyingi japo najitahidi kukabiliana nazo mpaka nikaweza kurudi Shule na kumaliza Masomo yangu.


Prof. Francis Furia(Daktari MNH):
Tafiti zitatusaidia kwanza kujua tuna Wagonjwa wa aina gani, wameathirika kiasi gani na kujua hata Matibabu ambayo tunatakiwa kuwapatia

Mfano Wagonjwa wenye #Lupus wengi huwa wanatibiwa kama vile wana Kifua Kikuu kwasababu bado wengi hawawezi kuyatambua haya Magonjwa

Hata kuna Dawa ambazo huwa hatuziagizi tukiamini kwamba hawa Wagonjwa hawapo hivyo Tafiti zitaweza kutusaidia ni Dawa za aina gani tunahitaji kuwa nazo


Dkt. Mariam Noorani(Aga Khan):
Cha kufanyika kwanza ni Jamii kutambua kuhusu Magonjwa Adimu pamoja na Dalili za kuangalia. Jamii itambue kwamba ni Maradhi na sio Mashetani kama wengine wanavyoamini

Mfano, Mtoto ambaye anaumwa kila mara Magonjwa au kupata Maumivu sehemu tofauti tofauti za Mwili huyu inabidi tumuangalie huenda ana Magonjwa Adimu

Pia, kuna Dalili ya Mtoto kushindwa kukua kwa kufuata Hatua za Ukuaji zinavyotakiwa au mwingine alifika kwenye hatua fulani ya Ukuaji ila ghafla anaanza kurudi nyuma, huyu huenda ana Magonjwa Adimu


Sharifa Mbarak(Mama mwenye Mtoto mwenye Magonjwa Adimu)
Kuuguza Mtoto mwenye Ugonjwa Adimu kunahitaji kujitoa na kujiandaa kwa Emergency yoyote inayoweza kutokea

Ali alianza kuumwa akiwa na Miaka 2 na hakuonesha Dalili yoyote, aliamka tu Siku moja akaanza kukohoa na Homa kupata na mpaka tunafika Hospitali alikuwa ameishiwa Oksijeni na kuwekwa ICU

Mpaka sasa hatujajua anasumbuliwa na tatizo gani hasa lakini tuliambiwa ana Changamoto ya Misuli. Hivyo tunaenda naye na vile anavyokuwa wakati huo, Mfano hatakiwi kabisa kupata Mafua hivyo huwa tunamtenga na Visababishi vya Mafua

Kwasababu ya kuwa na Mtoto mwenye Ugonjwa Adimu ambaye anakuhitaji muda wote, kuna gharama huambatana na hali hiyo, Mfano kama unafanya Kazi itabidi uache Kazi au kupunguza Muda wa Kazi pamoja na gharama nyingine

Vifaa pia vya Matibabu ni gharama sana, Ukitumia Oksijeni, au Betri ya Kifaa chake cha kupumulia ikiisha nguvu unakuwa huna Uhakika kama utapata Betri nyingine

Kuuguza mtu mwenye Ugonjwa wa Adimu kunahitaji nguvu ya jamii na nguvu ya Serikali kutokana na mahitaji

Kama Nchi hatuna Takwimu au Sera kuhusiana na Watoto wanaoumwa Magonjwa Adimu, nashauri tafiti zifanyike ili kupata idadi ambayo inaweza kusaidia katika kujua jinsi ya kuwasaidia wenye changamoto hizo


Prof. Francis Furia (Daktari Bingwa Magojwa ya Figo na Rheumatism-MNH):
Nilijifunza kuhusu Ugonjwa wa #Lupus nikiwa nasomea Shahada ya Tatu lakini Wanafunzi wangu wanajifunza wakiwa Shahada ya Kwanza, hiyo inaonesha kuna mwamko wa kuanza kufahamu na kupata #Elimu ya Magonjwa Adimu


Dkt. Mohamed Zahir (Mtaalamu wa Molecular Biology na Mhadhiri wa MUHAS):

Zaidi ya Asilimia 80 ya Magonjwa Adimu yanasababishwa na hitilafu au changamoto katika Vinasaba, hii ni elimu ambayo inatakiwa kuelezwa zaidi katika Nchi zetu Afrika ili kutusaidia kupata uelewa

Tunahitaji programu ambazo zinaweza kutengeneza Madaktari Bingwa, tunahitaji Watafiti wenye uelewa mkubwa ikiwemo Watu wa Maabara, Washauri wa Vinasaba wanaoweza kushauri Familia na Watu wengine wenye uwezo wa kuchakata 'data'

Kuna 'Data' nyingi zinazoweza kupatikana kupitia mchakato wa kufuatilia hitilafu za DNA, hivyo aina ya Mtu au Watu wanaoweza kufanya yote hayo wanatakiwa kuwa na uwezo mkubwa

Tanzania na Nchi nyingi Afrika hatuna Wataalam wa aina hiyo

Ushauri wangu, tunatakiwa kuongeza nguvu katika #Elimu na mafunzo ili kupata majibu sahihi wakati tunapofanya mchakato wa kutatua changamoto za Magonjwa Adimu


Sharifa Mbarak (Mzazi wa Mtoto mwenye Magonjwa Adimu):
Taasisi ya Ali Kimara kwa kushirikiana na #MUHAS tunashirikiana kufanya tafiti ambazo tunaamini zinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya Sera za Afya Nchini

Mfano; Kuna haipatikani Nchini, Serikali na Sekta nyingine zinaweza kuweka mkono kusaidia kupatikana na Dawa kwa kuwa ni gharama kubwa kujihudumia matibabu ya Magonjwa Adimu


Dkt. Mariam Noorani (Daktari Bingwa wa Watoto): Mtoto akizaliwa Siku 2 au 3 baadaye anatolewa damu kwa ajili ya vipimo (newborn screening), kila nchi ina Magonjwa yake inayopima kutokana na aina ya changamoto zilizopo ili kama ana magonjwa au ugonjwa fulani ijulikane jinsi ya kupatiwa tiba

Lazima kuwe na jinsi ya kuwasiliana kwa maana njia ya Mawasiliano ya kimfumo baada ya kufanyika kwa vipimo (newborn screening), ili hata kama Mtoto kazaliwa Mji fulani Mzazi wake akihamia sehemu nyingine iwe rahisi rekodi zake kujulikana kwenye mfumo


Prof. Francis Furia (Daktari Bingwa Magojwa ya Figo na Rheumatism-MNH):
Homa ya Ini sio miongoni mwa Magonjwa Adimu, ni Ugonjwa unaosababishwa na Virusi, unaweza kuambukizwa kwa njia ya majimaji kutoka mwilini, Damu, Mate au kwa njia ya Ngono


Dkt. Mohamed Zahir (Mtaalamu wa Molecular Biology na Mhadhiri wa MUHAS):

Kwenye Jamii kuna watu wanaimani tofauti kuhusu Magnjwa Adimu, baadhi yamesababisha familia kuvunjika au watu kukimbia, pia tafiti nyingi zimeonesha kuwa Magonjwa Adimu yanayohusisha Vinasaba yanasababishwa na baba zaidi na sio mama

Jamii iache kulaumu hasa kwa Wamama, matokeo yake mtoto hapati huduma stahiki, anaachwa, anapata msongo wa Mawazo na kujiingiza kwenye matatizo mengine yanayoweza kusababishwa na kuharibika kwa Saikolojia yake


Sharifa Mbarak (Mzazi wa Mtoto mwenye Magonjwa Adimu):

Wazazi wanapokuwa na Mtoto mwenye Magonjwa Adimu nao pia wanaathirika Kisaikolojia, hiyo inaweza kutokea kwenye majibu yao na vitu kama hivyo, inabidi Jamii iwaelewe

Pia, nashauri Wazazi wanapokuwa na Mtoto Mgonjwa wampeleke Hospitali mapema, waache kukaa na Mgonjwa nyumbani, wawapeleke sehemu sahihi na kwa haraka
 
Back
Top Bottom