- Asema Viongozi Wameficha mabillion Ulaya, Marekani
- Ataka wanaonga'tuka, watangaze utajiri waliopata
- Asema wapo walio madarakani, wengine wastaafu
MWENYEKITI wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, amesema kuna kundi kubwa la viongozi wastaafu na walio madarakani, waliosafirisha mabilioni ya fedha na kuziweka katika benki za Ulaya na Marekani.
Ametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa, fedha zinarejeshwa nchini ili zitumike kujenga uchumi wa nchi.
Mengi alisema hayo jana katika mjadala wa wazi wa kujadili rushwa na maadili, ulioandaliwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB), na kufanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam.
"Uadilifu na heshima si vitu vya kupewa, bali unavipata katika maisha yako, naiomba serilali ihakikishe fedha zilizowekwa nje zinarudishwa nchini.
"Wanaojihusisha na biashara za rushwa na fedha haramu, na kuziweka katika mabenki ya huko Amerika na Ulaya, wazirudishe nchini fedha zote walizopata kwa rushwa, na walipe kodi, na baadaye wamrudie Mungu," alisema Mengi.
Pamoja na ‘kulipua bomu' hilo, Mengi hakuwa na ujasiri wa kuwataja viongozi wastaafu na walio madarakani ambao ana hakika wametoroshea fedha nje ya nchi.
Akijibu hoja ya Mengi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alisema: "Msiwe na wasiwasi na vyombo vya dola nchini, kama mtu yeyote anamfahamu kiongozi aliye madarakani au aliyestaafu, aliyeweka fedha nje, amtaje na serikali itamshughulikia, na hata kama hakutaja jina la kiongozi, basi ataje hiyo taasisi ya fedha ya nje."
Mengi hakuishia kwenye hoja hiyo pekee, bali aligusia pia ufisadi miongoni mwa viongozi wa umma.
Alisifu utaratibu wa kisheria wa viongozi kutaja mali wakati wakiingia madarakani, lakini akasema utaratibu huo hautakuwa na maana kama viongozi wanashindwa kutaja ukwasi wanaoondoka nao baada ya kustaafu.
"Tunataka viongozi wataje mali mwanzoni wanapoingia madarakani na mwishoni, tunataka kujua wana nini, hatuna wivu, na hii ndiyo itakuwa njia sahihi ya kudhibiti rushwa kwa viongozi," alisema Mengi.
Maoni ya Mengi yanashabihiana na maoni ya wengi, ambao wamehoji mno kitendo cha viongozi katika awamu iliyopita, kutotangaza hadharani mali walizoondoka nazo.
Rais msaafu Benjamin Mkapa; na Waziri Mkuu, mstaafu, Frederick Sumaye, walitangaza kwa mbwembwe mali zao wakati wakiingia madarakani mwaka 1995, lakini hawakutaja ukwasi walioondoka nao miaka 10 baadaye.
Katika mjadala huo, Ofisa Uhusiano wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Josephine Mwakyuse, alisema pamoja na PCB kujitahidi kupambana na rushwa, imekuwa vigumu kufuatilia ushahidi kwa wale wanaoomba rushwa ya ngono, jambo linalosababisha wanawake kuendelea kukandamizwa.
"Ndugu Mwenyekiti, iko wapi haki ya mwanamke anapodaiwa rushwa ya ngono? Kuna ofisa mmoja wa jeshi amemsimamisha kazi na hatimaye kumfukuza kazi mwanamke kwa madai ya kuwa na matatizo ya akili, lakini baadaye imegundilika kuwa yule mama ni mzima ila alikataa kutoa rushwa ya ngono kwa mkuu wake wa kazi. Je, PCB itamsaidiaje mama huyu?" alihoji Josephine.
Akijibu hoja hiyo, Marmo alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa wa rushwa ya ngono inategemea ushirikiano atakaotoa mwanamke anayeombwa rushwa, kwa kuwa si rahisi kumkamata kama ilivyo kwa rushwa ya fedha.
Akizungumzia zawadi zinazotolewa kwa watumishi wa serikali pindi waendapo vijijini au nje ya nchi, Marmo alisema kuwa utaratibu unamtaka mtumishi kuchukua sehemu ndogo ya zawadi na nyingine apeleke serikalini.
Washiriki waliomba serikali iipe madaraka PCB kwa kuwa hali ilivyo sasa haikiwezeshi chombo hicho kufanya kazi zake kwa uhuru.
"PCB wamebaki na sera, lakini hawana uwezo wa kumkamata ofisa wa polisi anapopokea rushwa, wamekuwa kama jogoo mkubwa aliyewekwa ndani ya tenga, hata akiwika hatanui mabawa, na wananchi sasa tuko katika gari ambamo sote ni viwete, lakini dereva na konda ndio wazima.
"Tunaisaidia PCB, lakini wao hawako tayari kutusaidia, hasa tukiwa na ushaidi wa polisi kupokea rushwa," alisema Mchungaji Nkuba ambaye alisema ni muathirika wa vitendo vya PCB kushindwa kuwakamata polisi.
Nkuba alisema aliwasilisha vielelezo vyote PCB vinavyohusu polisi waliomuomba rushwa, lakini badala yake hawakufanywa kitu, na sasa anatishiwa maisha, kiasi kwamba familia yake imesambaratika na yeye anaishi katika kijiji ambacho hataki kukitaja kwa kuhofia usalama wake.
Mkurugenzi wa PCB, Edward Hosea aliwataka wananchi kuwa na imani na taasisi yake kwa kuwa sasa inafungua ukurasa mpya.
Amewaagiza maofisa wa taasisi hiyo nchini kote, kuweka hadharani namba za simu ili waweze kuwasiliana na wananchi.
CHANZO: Tanzania Daima - ISSN 0856 - 9762 Toleo Na 733 - Jumatano, Desemba 6, 2006