Membe ni tajiri wa fikra, taaluma yake haina chembe ya shaka

Jabirimakame

Member
Jan 15, 2014
71
37
Nimeisoma makala ya Bwana Yericko Nyerere katika mtandao wa Jamii Forums akimzungumzia Bernard K. Membe. Bwana Yericko amenifanya nianze kuamini kwamba sifa ya kutopenda kujifunza ambayo wakati wote watanzania tunatunukiwa inastahili kwetu.

Ukilisoma kwa makini hili andishi hupati shida kubaini kwamba aliyeandika ni mtu ambaye hajafanya utafiti juu ya kile anachotaka kukiandika, na badala yake ameokota maneno ya mtaani na kuyafanya ndiyo makala ya kumuelezea Mwanadiplomasia huyu Nguli barani Afrika na duniani.

Bwana Yericko anamzungumzia BM kuwa hakuwa na uwezo mkubwa wa kitaaluma darasani. Ukitaka kuujua uwezo wa Membe jaribu kujipa muda kufuatilia kazi zake anazozifanya, mahojiano anayoyafanya ndani na nje ya nchi, uchambuzi anaoufanya katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Katika matokeo yake ya kidato cha nne Membe alikuwa ni miongoni mwa vijana watatu waliofaulu vizuri sana, na hivyo kumfanya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mtwara wakati huo, Marehemu Maurus Libaba, kuamua kuwahamishia Itaga Seminari, ambayo ilikuwa ni seminari pekee ya Kikatoliki iliyokuwa na masomo ya kidato cha tano na sita. Matokeo yake ya Chuo Kikuu DSM, shahada ya sayansi ya siasa na utawala BM alifaulu kwa GPA 4.1, hatimaye kupewa barua ya kuajiriwa kuwa mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha DSM.

Lakini kutokana na uwezo wake mkubwa na umuhimu wake katika usalama wa taifa letu mwajiri wake hakuwa tayari kumruhusu BM kuondoka ikulu. Shahada ya Uzamili BM amesoma katika Chuo Cha Johns Hopkins nchini Marekani, Chuo ambacho ni miongoni mwa vyuo bora duniani. Unawezaje kujitokekeza hadharani na kutia shaka, uwezo wa BM kitaaluma?

Mbona hujazungumza uadilifu wake na uwezo wake mkubwa kusimamia misimamo juu ya masuala yenye tija Tanzania na barani Afrika.

Msimamo wake juu ya rushwa na ufisadi na mambo mengine. PILI Bwana Yerecko anazungumzia kulegalega kwa diplomasia ya Tanzania na amegusia migogoro ya kidiplomasia kati yetu na Ruanda, Malawi, Uingereza na katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ameshindwa kufanya uchambuzi wa vyanzo vya hii migogoro na kazi iliyofanywa na wizara ya mambo ya nje katika kuitatua.

Hakuna mgogoro wowote kati ya hiyo ambayo imesababishwa na Kulegalega kwa wizara. Mgogoro wa Ruanda chanzo chake ilikuwa kauli ya kiungwana iliyolenga kuleta amani ya kudumu Ruanda, iliyotolewa na Rais Kikwete alipokuwa Ethiopia, kauli ambayo iliungwa mkono na Rais wa Uganda kumshauri Paul Kagame akae meza moja ya mazungumzo na waasi.

Mgogoro ndani ya Afrika Mashariki, chanzo chake ni hatua ya Kenya, Uganda na Ruanda kuitenga Tanzania na Burundi katika masuala kadhaa ambayo yalihitaji Ushirikiano wa nchi zote. Mgogoro wa ziwa nyasa ulianza baada ya Malawi kutamka kwamba ziwa nyasa lote ni la Malawi. Membe hakua chanzo cha hii migogoro na Tanzania haikuwa chanzo cha hiyo migogoro.

Katika migogoro yote Mwandiplomasia namba moja Dr. JK na Mwanadiplomasia namba mbili Ndugu BM waIishughulikia migogoro yote kwa weledi usiyo kifani na sasa imefikia katika hatua mzuri.

KWA FAIDA YA BWANA YERICKO na wengine ambao wangependa kujifunza juu ya nafasi ya Tanzania katika diplomasia, naweka link ya makala ya Balozi mstaafu aliyefanya kazi kwa muda wa miaka 28 katika wizara ya mambo ya nje akitoa uchambuzi wa kina juu ya nafasi ya Tanzania katika diplomasia.


======================

KUMEKUWEPO na mijadala mingi kuhusu safari za Rais, nje ya nchi. Sehemu kubwa ya mijadala hii imehitimisha kwamba Rais Jakaya Kikwete anasafiri sana. Bahati mbaya, wenye kujadili na wenye kujivika sura ya wachambuzi katika mijadala hiyo, hawatendi haki kwa kuwa hawatoi uchambuzi wa kina na wenye ushahidi na vithibitisho kuhusu madai yao.

Wachambuzi wanashindwa kuonesha mabadiliko katika diplomasia ya dunia kwa vipindi mbalimbali ambayo yanalazimisha nchi fulani kuchukua mkondo ule na kuacha huu kwa manufaa ya taifa hilo. Diplomasia ya Tanzania, kwa mfano, baada ya uhuru ilikuwa ya ukombozi kutoka kwenye makucha ya ukoloni na siasa za mrengo wa kijamaa na zile za kibepari. Diplomasia hii ilibadilika baada ya nchi nyingi barani Afrika na duniani kujikomboa na hivyo, diplomasia yetu sasa inajikita zaidi kwenye uhusiano na faida za kiuchumi.

Nimepata msukumo wa kuandika makala haya baada ya kusoma makala za mchambuzi mashuhuri wa siasa nchini, Komredi Jenerali Ulimwengu, kuhusu diplomasia ya Tanzania na safari za Rais kwenye gazeti hili la Raia Mwema. Napenda kukiri mapema kuwa nimesoma makala hizo kwa kina na kwa jicho la kiuchambuzi. Makala hizo kwa namna fulani zinapungukiwa taarifa fulani sahihi na hata takwimu za kuthibitisha hoja inayojadiliwa.

Si kusudio langu kuanzisha malumbano wala mjadala mrefu ila kujaribu kuuonesha umma wa Tanzania kuwa yaliyoandikwa yamekuwa na upungufu. Komredi Jenerali ni mchambuzi ninayemheshimu, ana historia ndefu na sina shaka na dhamira yake njema kwa taifa hili. Tatizo langu ni kuwa, watu wa aina ya Jenerali Ulimwengu wasiposahihishwa, wanawalisha 'kasa' wananchi ambao wanawaamini (akina Jenerali) kama mamlaka zao za ufahamu.

Natambua Jenerali Ulimwengu aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana Afrika yenye makao makuu yake Algeria. Nafasi hiyo, ilimpatia fursa ya kuishi pembezoni mwa diplomasia ya Tanzania enzi hizo iliyojikita katika siasa za kiitikadi na ukombozi wa Bara la Afrika. Pengine, uzoefu wake huo sasa umepitwa na wakati, na wakati huo hautarudi tena. Jenerali anaweza kuwa mchambuzi mzuri wa siasa na jamii, eneo hilo analiweza, lakini hili la diplomasia linaelekea kumtatiza kidogo.

Kinachonifanya niendelee kumsifu na kumheshimu, ni uungwana aliouonyesha kwa kukiri mwanzoni mwa makala yake pale aliposema, nanukuu: "Pasi na shaka pia, haya ni maoni yangu binafsi ambayo Kiingereza yanaweza kuitwa ‘subjective' kwa sababu hayana vigezo vya uyakinifu vya kuweza kuyathibitisha". Hapa ndipo Jenerali anapojitofautisha na wachambuzi wengine wenye kujifanya wanajua kila kitu, tena kila wakati. Jenerali ni muungwana, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

Diplomasia ya Tanzania inaweza kuwa na matatizo yake. Hatuna sababu ya kutoyasema matatizo hayo au kuyafumbia macho. Kufanya hivyo, hakumaanishi kubeza kila kitu hata vitu vizuri ambavyo vimefanyika. Wajibu wangu ni kuelezea manufaa, ili msomaji akiyapima pamoja na upungufu ulioibuliwa na Komredi Jenerali, aweze kupata majibu na uelewa mkubwa zaidi.

Andiko langu lina lengo la kujazia mapengo aliyoyaacha Komredi Jenerali Ulimwengu, na pia kufafanua baadhi ya masuala aliyoyaibua. Nawajibika kufanya hivyo kwa kuwa taifa lilinipa fursa ya kutumikia Diplomasia ya Tanzania hadi nilipostaafu miaka mitatu iliyopita katika ngazi ya Balozi. Cheo cha Balozi ndio ngazi ya juu katika kada ya Utumishi wa Mambo ya Nje, ambayo uteuzi wake hufanywa na Mkuu wa Nchi. Hivyo, ninayo mamlaka ya ufahamu wa suala ninalolizungumzia, pia kama 'raia mwandamizi' nawiwa na wajibu wa kuelimisha pale penye kasoro.

Diplomasia na Sera ya Nje ni nini?

Maneno Diplomasia na Sera ya Mambo ya Nje yamekuwa yakitumika wakati mwingine kumaanisha kitu kimoja, pamoja na kuwa yana maana tofauti. Diplomasia ni uhusiano wa kimataifa kati ya nchi na nchi na kati ya nchi na mashirika ya kimataifa. Uhusiano huu hutengenezewa mbinu na mikakati ya utekelezaji wake kwa kila nchi kupitia sera zao za mambo ya nje.

Sera ya Mambo ya Nje ni tamko la nchi lenye kutoa mwongozo na mwelekeo kuhusu madhumuni, malengo na misingi ya nchi katika kuhusiana na nchi, mashirika ya kimataifa na wadau wengine nje ya nchi. Tamko hili pia ni mwendelezo wa sera ya ndani ya nchi. Sera ya Mambo ya Nje ya nchi ni chombo kinachobeba zana na mbinu za utekelezaji wa diplomasia.

Sera huainisha pia misimamo ambayo nchi inaipigania na ile inayoipinga. Tamko hili ni muhimu kwa kuwa ni utambulisho wa nchi kimataifa, na tamko hili huakisi sera na misingi ya ndani ya nchi. Mratibu mkuu wa utekelezaji wa sera hii ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na sera hii hutekelezwa na serikali nzima na wadau wengine ndani ya nchi, ambao shughuli zao zinahusiana na masuala ya kimataifa. Ifahamike pia, Mkuu wa Nchi ndiye Mwanadiplomasia namba moja, na Waziri wa Mambo ya Nje ni Mwanadiplomasia namba mbili katika nchi yoyote.

Sera ya nje, tulipotoka na tulipo

Komredi Jenerali Ulimwengu katika makala yake amesema; "... diplomasia yetu imeshindwa kutuletea matunda ambayo tungetaraji kuyavuna kama diplomasia yetu ingekuwa imefanya kazi ipasavyo". Kwa vyovyote vile, unaposema kuwa diplomasia ya nchi imefeli, maana yake Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wamefeli. Shutuma hii ni nzito, ni nzito zaidi pale inapotolewa na mwandishi aliyebobea bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha, na hasa bila kuainisha kwa vigezo au kipimio cha kufanikiwa au kutokufanikiwa.

Sera ya Mambo ya Nje ya 2001 ndiyo inayotoa mwongozo katika kufikia malengo ya nchi nje. Sera hiyo inatambua na kulinda misingi ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote, kutetea wanyonge, kudumisha ushirikiano wa kimataifa, kuunga mkono juhudi za kimataifa, ujirani mwema na kudumisha uhuru wetu. Sera, imetambua pia mafanikio yaliyopatikana katika diplomasia ya siasa na mchango wake kwenye ukombozi wa nchi za Afrika.

Sera hii imeelekeza misingi yote idumishwe, na juhudi zote sasa zilenge kupanua maslahi yetu ya kiuchumi kwa kupanua wigo wa marafiki, ushiriki wetu kimataifa na ushirikishaji mpana wa wadau, ikiwamo sekta binafsi. Diplomasia yetu sasa tofauti na awali, inatakiwa ilete manufaa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kufungua masoko kwa biashara za Watanzania, bidhaa, kuvutia wawekezaji na kuongeza watalii. Mkakati huu wa kutekeleza sera, umepewa jina la Diplomasia ya Uchumi.

Diplomasia, kama ilivyo mikakati mingine inayo vigezo na vipimo vyake. Diplomasia hufanyiwa tathmini mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya kidunia. Diplomasia ya nchi, hupimwa kwa kulinganisha na diplomasia ya nchi nyingine. Hivyo, kusema kuwa Diplomasia yetu imefanikiwa au kufeli, tunapaswa kuipima dhidi ya malengo yaliyoainishwa kwenye sera, kisha kuilinganisha Diplomasia ya nchi nyingine zinazoshabihiana.

Uimara wa diplomasia yetu

Uimara wa diplomasia ya nchi ni ushawishi wake kimataifa. Ushawishi wa nchi, kihistoria umekuwa ukiambatana na nguvu ya kiuchumi au kijeshi (Diplomasia ya Nguvu). Nguvu hizi mbili ni matokeo ya sera za ndani ya nchi. Hata hivyo, si lazima kuwa kila nchi yenye moja au vigezo hivyo viwili kufanikiwa katika diplomasia. Ziko nchi, ikiwamo Tanzania ambazo zimefanikiwa sana kuwa na ushawishi mkubwa, pamoja na kutokuwa na nguvu hizo duniani, kutokana na uimara wa sera yake ya mambo ya nje, na wanadiplomasia wake (Nguvu ya Diplomasia).

Ni dhahiri kuwa hatuwezi kulinganisha diplomasia ya Tanzania na diplomasia ya nchi zilizoendelea kama Marekani, China, Ufaransa, Uingereza na Urusi. Nchi hizi ni nchi kubwa katika anga la kimataifa, ni wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wenye kura ya turufu, ni nchi zenye nguvu za kijeshi na kiuchumi na nchi zenye maslahi mapana duniani. Kukua au kudorora kwa uchumi wa dunia kunategemea sana maendeleo ya chumi za nchi hizo.

Diplomasia ya Tanzania inaweza kupimwa kwa kulinganishwa na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, maana kimataifa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara huwekwa katika kapu moja. Nchi zinazoaminiwa kuwa na nguvu kubwa za kijeshi na kiuchumi kusini mwa Jangwa la Sahara ni Nigeria na Afrika Kusini. Jambo linaloshangaza wengi duniani ni kuwa, Tanzania imeonekana kung'ara na kuwa na ushawishi mkubwa kimataifa sawa au pengine kuzidi nchi hizo mbili, pamoja na kutokuwa na nguvu kubwa ya uchumi au jeshi. Hakuna nchi nyingine, ukiondoa hizo mbili, yenye ushawishi na sauti kimataifa zaidi ya Tanzania.

Nataka kuepuka kufanya kile ambacho Komredi Jenerali Ulimwengu amefanya cha kuzungumza bila ushahidi. Maana wako Watanzania wanaoamini kuwa sifa njema au jambo jema haliwezi kufanywa na serikali, tena Serikali ya Awamu ya Nne. Hawa watataka kubeza hoja yangu kuwa kiushawishi barani Afrika, Tanzania iko katika ligi moja, na pengine inazidi nchi za Afrika Kusini na Nigeria, nchi ambazo zina nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi.

Kujenga taswira nzuri ya nchi na ushawishi kimataifa ni moja ya kielelezo cha nguvu ya diplomasia ya nchi. Jukumu hili, ni moja ya jukumu gumu sana katika diplomasia. Hii ni kwa sababu, taswira ya nchi inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mipango au sera za nchi nyingine za kiuchumi dhidi yako. Mfano, ikiwa nchi yako ikionekana ni kitovu cha ugaidi, nchi inaweza kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na hivyo kugharimu uchumi wa nchi husika.

Taswira ya nchi hulindwa kwa kila hali na baadhi ya nchi hutumia gharama kubwa kwenye propaganda kulinda taswira ya nchi zao. Katika ripoti ya 2009-2010 ya kampuni za Marekani zenye kutoa huduma za uwakala kwa nchi nyingine inaonyesha kuwa nchi za Afrika zinatumia fedha nyingi kuosha taswira zao kwenye Bunge na Seneti ya Marekani. Katika nchi hizi, Kenya inashikilia nafasi ya nane kati ya kumi za juu ikiwa imetumia kiasi cha dola za Marekani milioni moja na laki saba ($1.7 milioni), huku Afrika Kusini ikitumia ($18 milioni), Angola ($7 milioni), Nigeria ($1.8 milioni).

Taarifa hiyo inaeleza, mwaka 2008 Kenya ilitumia kiasi cha dola za Marekani milioni mbili na laki nne ($2.4 milioni) kuilipa Kampuni ya Chlopak, Leonard Schechler and Associate kwa lengo la kurekebisha taswira yake nchini Marekani baada ya machafuko ya 2007. Itakumbukwa kuwa, wakati huo, Tanzania ilitembelewa na Rais George Bush wa Marekani katika ziara ambayo haijawahi kufanywa na Rais wa Marekani kuitembelea nchi kwa siku nne, kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanzania imeyapata hayo bila kutumia mawakala na wapiga debe ndani ya Marekani.

Njia nyingine ya kupima uwezo na ushawishi wa Diplomasia ya Tanzania ni kuangalia uwekezaji ambao Tanzania inaufanya katika Diplomasia na kulinganisha na nchi zingine za Afrika. Ni muhimu kabla ya kuhukumu kuangalia ukubwa wa bajeti, watumishi na mtandao wa Balozi katika kuhukumu ikiwa Diplomasia yetu imefeli ama kufaulu. Maana, hatuwezi kusema mtu amefeli kama hatukumpa nyenzo za kufanyia kazi, maana atakuwa amefeli kabla hajaanza. Katika hili, nitalinganisha nchi za Nigeria, Afrika Kusini, Kenya na Tanzania ili tuweze kupata picha kamili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ina maofisa wapatao 2,000, Balozi 87 nje ya nchi na Balozi zipatazo 70, na Balozi ndogo 37 zinazowakilisha nchi zao nchini Nigeria. Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilitengewa kiasi cha dola za Marekani milioni mia tatu ishirini na tatu ($ 323 milioni) kwa mwaka 2012 kwa ajili ya kazi zake. Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini kwa upande wake inao wafanyakazi wapatao 4,535, Balozi 104 nje ya nchi, Balozi 126 za nje ya nchi zilizoko Pretoria na mwaka 2012 ilitengewa Bajeti ya Randi Bilioni 5.1 sawa na Dola za Marekani milioni 483. Jirani zetu Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya inazo Balozi 53 nje, Balozi 75 za nje ya nchi zilizoko Nairobi na Wizara ilitengewa kiasi cha dola za Marekani milioni 172 kwa mwaka wa fedha 2012.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania inazo Balozi 33 tu nje ya nchi na ni mwenyeji wa Balozi 55 na Mashirika ya Kimataifa 22 nchini. Aidha, Wizara ina wafanyakazi wasiozidi 350 tu ikijumuisha kada zote, ndani na nje ya nchi, na mwaka 2012 Wizara ilitengewa Bajeti ya shilingi bilioni 97 tu ambayo ni sawa na dola za Marekani milioni 60.8. Ikumbukwe kuwa, fedha hiyo ni asilimia 44 tu ya mahitaji halisi ya bilioni 222 yakihusisha ufunguzi wa Balozi mpya, kuongeza rasilimali watu balozini, kukarabati majengo ya Ubalozi na kutekeleza mkakati wa Diplomasia ya Uchumi.

Kwa hesabu nyepesi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapata theluthi moja ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya. Kwa lugha nyingine, Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ni mara nne ya Bajeti yetu, na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ni mara nane ya Bajeti ya Wizara yetu. Haihitaji miujiza kukubali kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania inafanya kazi kubwa sana ikilinganishwa na kiasi cha fedha, rasilimali watu na mtandao wa Balozi ilizonazo.

Takwimu hapo juu zinatupa sababu ya kujivunia kuwa Tanzania ina 'Nguvu ya Diplomasia' kuliko 'Diplomasia ya Nguvu'. Kirasilimali na kimtandao, Tanzania haifui dafu kwa wenzetu wa Nigeria, Afrika Kusini na hata Kenya. Pamoja na hayo, nguvu ya ushawishi wa Tanzania duniani ni sawa au zaidi ya nchi hizo. Haihitaji akili nyingi za kiuchambuzi kukubali kuwa, Tanzania inavuna zaidi ya inachopanda katika Diplomasia. Inashangaza kuwa, watu wa nje wanaona hivyo na wanajifunza kutoka kwetu, lakini wenzetu wa ndani wanabeza. Ni vyema, kuzingatia takwimu hizo hapo juu ili kuoanisha na mafanikio ya Diplomasia nitakayoainisha hapa.

Mafanikio ya Diplomasia yetu

Mafanikio ya diplomasia yanaweza kupimika kwa kutumia viashiria. Viashiria hivi hutumika kama vielelezo vya nguvu ya diplomasia ya nchi yoyote. Kwa madhumuni ya makala hii, viashiria vitano vimetumika. Viashiria hivi si timilifu, viashiria vingine lukuki hutumika kutokana na mahitaji mahsusi. Viashiria vitano ninavyotumia hapa, vinatosheleza kwa madhumuni ya makala hii kama ifuatavyo;-

Nafasi za Kimataifa

Moja ya kipimo cha nchi cha nguvu yake ya diplomasia ni nafasi yake kimataifa. Nafasi ya nchi kimataifa inajumuisha nafasi za uteuzi na uchaguzi ambayo nchi hupata kimataifa. Kuteuliwa na kuchaguliwa huko, ni kielelezo cha kukubaliwa na kuaminiwa kwa nchi katika Jumuiya ya Kimataifa.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Tanzania imepata nafasi nyingi kimataifa ikiwemo Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (2004/2006), Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (2008/2009), Uenyekiti wa Asasi ya Ulinzi na Usalama ya SADC (2008/2009 na 2012/2013) na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika (2012/2013 na 2014/2015).

Tanzania iliweka historia katika Uenyekiti wa AU chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kukumbana na mapinduzi katika nchi nne za Mauritania, Guinea, Guinea Bissau na Madagascar. Ni katika wakati huo kwa mara ya kwanza, tena kwa kupendekezwa na Tanzania ilikubaliwa AU haitautambua uongozi wowote utakaopindua serikali na kisha kugombea uchaguzi mkuu kwa lengo la kutakatisha mapinduzi.

Azimio hilo liliweka mwanzo mpya katika Afrika, na hadi leo, hakuna kiongozi aliyepindua ambaye amegombea uchaguzi mkuu baada ya mapinduzi. Ushahidi wa hivi karibuni ni huu wa Rais Andy Rajoelina kutogombea uchaguzi Madagascar kwa kubanwa na kipengele hicho. Isisahaulike pia, ni katika kipindi hicho Tanzania iliongoza AU kwenda kung'oa uasi wa Kanali Bakar wa Kisiwa cha Anjuani huko Comoro. Ilipomaliza muda wake, nchi za Afrika zilishawishi Tanzania kuendelea na Uenyekiti wa AU jambo lisilo la kawaida, lakini Rais Kikwete akasimamia msingi wa Tanzania wa kuheshimu vipindi vya madaraka.

Tanzania imefanya mambo makubwa pia katika kipindi chake SADC ikiwemo kuongoza jitihada za amani nchini DRC kulikozaa Azimio la Umoja wa Mataifa la kupeleka kikosi maalumu cha kulinda amani dhidi ya waasi wa M23. Kazi iliyofanyika huko si ya kusimulia, maana kila mwenye masikio amesikia. Ushiriki wa Tanzania katika kutokomeza waasi wa M23 kuna faida tatu kubwa; kwanza: kuleta amani kwa wananchi wa DRC Mashariki, pili: kuepusha nchi yetu na tatizo la wakimbizi na utapakaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi, jambo linalotishia amani na usalama wetu, na tatu: kufungua fursa za kiuchumi na kibiashara baina ya watu wetu na wale wa DRC kutokana na kurejea kwa amani mashariki ya DRC. Hii ni Dipomasia ya Uchumi.

Mafanikio haya ni mengi, nilichogusia ni vitu vichache sana kuonyesha nafasi ya taifa letu duniani, Afrika na kusini mwa Afrika. Tunao pia Watanzania waliochaguliwa na wengine kuteuliwa kushika nyadhifa kubwa kimataifa ikiwemo nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyoshikiliwa na Dk. Asha-Rose Migiro; Balozi Wilfredy Ngirwa, kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti Huru wa Baraza la Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO); Rais Kikwete ameteuliwa kushika nyadhifa nyingi kimataifa ikiwemo uenyekiti wa Kamati ya Marais Kumi wa Afrika kuandaa msimamo wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Jopo la Wasuluhishi wa Mgogoro wa Ivory Coast, na hata majuzi, alipewa nafasi ya kipekee kuzungumza kwenye mazishi ya Rais Mstaafu, Nelson Mandela. Mtu yeyote anayeitazama Tanzania kwenye medani za kikanda na kimataifa hatachelea hata kidogo kupaza sauti na kusema kuwa diplomasia ya Tanzania iko katika daraja la juu sana kwa kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote kile.

Ushawishi na misimamo katika uamuzi

Tanzania imeendeleza desturi yake ya kuwa na misimamo isiyotetereka katika masuala mbalimbali duniani. Desturi hii ni mwendelezo wa Diplomasia ya Siasa na Ukombozi chini ya Mwalimu Julius Nyerere. Leo hii, Tanzania ni moja ya nchi chache zenye uthubutu wa kutofautiana na nchi kubwa duniani na hata kutamka misimamo inayopishana nayo, na bado ikaheshimika.

Yoyote mwenye kuhofu juu ya jeuri hii ya Tanzania anapaswa kuwa huru kufuatilia upigaji kura wa Tanzania katika maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayohusu kukemea vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba, Haki ya Wapalestina kujitawala na Haki ya Wapalestina kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Elimu (UNESCO). Aidha, Tanzania haijasita kukemea kilichofanywa na nchi za NATO dhidi ya Libya na imepiga kura ya kuzuia matumizi ya nguvu ya NATO nchini Syria kwa kuzuia kile cha Libya kujirudia.

Pamoja na Tanzania kuwa na misimamo mikali kwenye mambo ya msingi, imeendelea kuaminiwa na kuheshimiwa na mataifa makubwa na nchi zote duniani. Tunaheshimiwa kwa kuwa, sisi si wanafiki na tunamaamisha tunachosema. Rekodi yetu inazungumza yenyewe na hivyo ni taifa linaloaminika, na mfano barani Afrika. Ndio maana, katika masuala makubwa ya dunia, na Afrika, Tanzania hualikwa, kwa kuwa sauti yake ni muhimu kimataifa.

Ushawishi huu katika uamuzi wa kimataifa na kikanda unatokana pia na uzito wa Mwanadiplomasia namba moja na namba mbili wa Tanzania, yaani Rais Kikwete na Waziri Bernard Membe. Rais Kikwete ni mwanadiplomasia mkongwe, amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 kabla ya kuwa Rais. Waziri Membe amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 7 sasa, jambo linalomfanya kuwa Waziri mkongwe katika AU, ambapo mawaziri wakongwe wamebaki wanne yaani Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Lesotho, Uganda na Zimbabwe. Uzoefu huu unawafanya waaminike na wakabidhiwe majukumu mengi, na hivyo kualikwa mara kwa mara kwenye mikutano ya kimataifa.

Ziara za viongozi

Ziara za viongozi wa nje nchini na mialiko ya kiongozi wa nchi nje ni kiashiria cha nafasi ya nchi duniani, hususan katika ulimwengu wa diplomasia. Tanzania tumetembelewa na viongozi wa nchi kubwa duniani achilia mbali nchi za kati. Nyingi ya ziara hizi ni za kirafiki na kikazi. Tanzania imetembelewa na Rais George Bush wa Marekani na Rais Hu Jintao wa China mwaka 2008. Kama haitoshi, mwaka 2013, Tanzania ikatembelewa tena na Rais Xi Jinping ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Afrika baada ya kuingia madarakani, na akatumia fursa hiyo kutangaza Sera ya China barani Afrika. Mwaka huo huo, Rais Barack Obama naye akatembelea Tanzania na akachagua Tanzania kuwa sehemu ya kutangazia Sera ya Marekani katika ushirikiano wa Nishati na Bara la Afrika, Power Africa Initiative (PAI). Wakati Rais Obama anafanya ziara ya kikazi, rais wengine wawili wastaafu wa Marekani (George Bush na Clinton) nao walitembelea Tanzania. Kwa mara ya kwanza katika historia ya dunia, marais watatu wa Marekani wanatembelea nchi kwa wakati mmoja.

Tanzania ilitembelewa pia na Waziri Mkuu wa India na Rais wa Brazil, mataifa haya ni sehemu ya nchi zinazounda kundi la nchi zenye uchumi mkubwa duniani yaani Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICS). Hapa sijaweka orodha ya utitiri wa mawaziri wakuu na mawaziri wa ushirikiano waliofika nchini. Tukumbuke kuwa, viongozi hawa wakubwa hawatembelei nchi yoyote tu. Kutembelea kwao Tanzania ni kipimo cha imani yao kwa nchi na Rais Kikwete na sera yake ya nje. Nchi zingine Afrika zingependa sana kupata ugeni mzito wa aina hii lakini hawana ushawishi wa kutosha kidiplomasia kutafutwa na viongozi wa nchi kubwa duniani.

Fursa za kiuchumi

Diplomasia yetu leo, tofauti na Diplomasia ya Siasa na Ukombozi tuliyokuwa nayo huko nyuma, imejikita katika kulinda na kupanua maslahi ya kiuchumi. Diplomasia ya Siasa na Ukombozi ilitufanya tuchague maadui na marafiki, ziko nchi hatukushirikiana nazo ikiwemo Afrika Kusini, Korea na Israel. Sasa, tunashirikiana na kila nchi katika kupanua fursa za kiuchumi zikiwemo nchi hizo tatu. Sasa, tofauti na zamani, Diplomasia inautumikia uchumi na si uchumi kutumikia siasa kama ilivyokuwa huko nyuma.

Diplomasia ya Uchumi ya Tanzania inalenga kama ilivyoelekezwa na Sera ya Mambo ya Nje kujishughulisha na kujenga uchumi wa nchi. Viongozi na Balozi zetu zimekuwa zikifanya kazi hiyo, tena katika mazingira magumu ya uhaba wa bajeti kama nilivyochanganua hapo awali. Mabalozi wetu sasa si tu wanakutana na mabalozi wenzao, bali pia wafanyabiashara na wawekezaji.

Fursa za kiuchumi na kijamii ambazo zimefunuliwa na Diplomasia ya Uchumi ni lukuki. Ziara ya Rais George Bush akiwa nchini alisaini makubaliano ya kuipatia Tanzania dola za Marekani milioni 698 kwa ajili ya miundombinu, nishati na afya. Fedha zile ndizo zimejenga barabara ya Masasi-Songea-Mbaba Bay, Tanga-Horohoro na kujenga miundombinu ya kusambaza umeme. Mshindo wa miradi hii katika uchumi wetu hauwezi kupuuzwa, miundombinu hii imeifungua nchi, sasa maeneo kama Mbamba Bay yaliyokuwa pembezoni, sasa yanafikika.

Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa China, imetufungulia fursa ya kujengwa itakayokuwa bandari kubwa kuliko zote Afrika Mashariki huko Bagamoyo, itakayogharimu takribani dola za Marekani bilioni 10. Bandari hiyo itawezesha meli kubwa za kimataifa zenye uwezo wa kupakia makontena 6,000 kuweka nanga Bandari ya Bagamoyo. Bandari hiyo itageuza Bagamoyo kuwa Jiji la Bandari litakalounganishwa kwa barabara na reli na Jiji la Dar es Salaam na hadi Msata. Tayari taarifa za ujenzi wa bandari hii zimekwisha leta kiwewe juu ya uhai wa bandari za majirani zetu. Yote haya ni matunda ya Diplomasia ya Uchumi ya Tanzania.

Hali kadhalika Tanzania imepatiwa fursa ya kuuza bidhaa China ambalo ndilo soko kubwa kwa sasa. Sasa Tanzania inaweza kuuza tumbaku China, nchi ambayo inanunua tumbaku kwa wingi kuliko nchi yoyote duniani. Juhudi hizi zimetokana na hasara waliyopata wakulima wa tumbaku wa Tanzania katika msimu wa 2011/2012 ambako, tani 30,000 zilikosa soko baada ya nchi za Ulaya kupunguza matumizi ya tumbaku. Ikumbukwe kuwa, nchi haiwezi kuuza tumbaku nchini China bila ya kuwa na mkataba maalumu, ambao ni zao la juhudi za Waziri Membe baada ya mkutano wa China na Afrika uliofanyika Beijing, mwaka 2012.

Mikataba ya aina hii imesainiwa pia Oman, Kuwait na nchi nyingine mashariki ya kati. Baadhi ya sekta binafsi tayari zimekwisha changamkia fursa hizi ikiwamo Benki ya CRDB iliyofungua tawi huko Bujumbura na Benki ya Exim iliyofungua tawi huko Moroni, Visiwa vya Comoro. Ziko kampuni nyingine nyingi za Tanzania ambazo zinachangamkia fursa hizi, hali iliyopelekea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutunukiwa tuzo ya mwaka 2013 na Taasisi ya CEO Round Table, kutokana na mchango wake wa kuisaidia sekta binafsi kufanya kazi vizuri na serikali. Ni vizuri walio na wasiwasi kuhusu uwezo wa Wizara ya Mambo ya Nje wa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi wakauliza taasisi mbalimbali za sekta binafsi kama CEO Round Table.

Uwakilishi Nje ya Nchi

Tanzania imepanua uwakilishi wake nje na kuongeza Balozi sita mpya kati ya 2005 hadi 2013. Balozi mpya zimefunguliwa katika maeneo ambayo yanakuwa kwa kasi kiuchumi, na yenye maslahi ya kiuchumi kwa Tanzania. Leo Tanzania tunazo Balozi zetu Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Malaysia, Brazil, na hivi karibuni visiwa vya Comoro na Uholanzi. Katika kipindi hicho hicho, Balozi za Brazil, Oman, Korea Kusini na Qatar zimefunguliwa nchini, pamoja na mashirika ya kimataifa.

Idadi ya Balozi ambazo zimefunguliwa nje katika kipindi cha miaka minane ni ndogo. Tanzania bado haijaweza kufikia nchi nyingi katika mtandao wake wa Balozi. Jitihada zimefanywa kufungua Balozi za Heshima 18 kwa ajili ya kutoa huduma za kikonseli kwa watalii na wawekezaji. Uchache huo hautokani na upungufu wa dhamira bali fedha. Hata pale ambapo inazo Balozi, bado ina uhaba wa waambata biashara, waambata uchumi na waambata utalii kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kukuza utalii, biashara na uwekezaji.

Tunapaswa kupongeza juhudi za wanadiplomasia wetu kwani hata mafanikio tunayoyapata ni zaidi ya kiasi tulichowekeza. Idadi ya Balozi zetu nje ni theluthi tu ya Balozi za Nigeria na Afrika Kusini na nusu ya Balozi za Kenya. Upande wa rasilimali watu, idadi ya wanadiplomasia wetu wizarani na balozini ni chini ya asilimia 10 ya idadi ya wanadiplomasia wa Afrika Kusini, na robo ya idadi ya wanadiplomasia wa Nigeria. Tofauti za kibajeti ndio tusiguse maana ni kubwa kupindukia. Bado, Tanzania inapishana viwiko na Afrika Kusini na Nigeria katika nyanja ya Diplomasia. Tunapaswa kujipongeza si kubeza.

Je, Rais Kikwete anasafiri sana?

Eneo ambalo limeibua hisia za wachambuzi wengi kwenye Diplomasia ya Tanzania ni ziara za Rais nje ya nchi. Imesemwa kuwa Rais Kikwete anasafiri sana. Nasikitika pia kuwa, wenye mamlaka ya kulisemea hili wamekuwa na uzito wa kulisemea, kiasi kuwa wananchi sasa wanaamini hivyo. Picha inayojengwa hapa ni kuwa Rais Kikwete ni mzururaji na anafuja fedha, kiasi kuwa bajeti ya safari kwa mwaka 2013/2014 imeshavuka kikomo kabla ya wakati, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari. Inasemwa pia, kazi ya maofisa wa Tanzania ni kusafiri safiri tu, kukimbiza posho ambazo, Komredi Jenerali Ulimwengu amediriki kusema ni kubwa kuliko za Umoja wa Mataifa na Afrika nzima.

Hoja ya kusema safari za Rais ni nyingi ni hoja nyepesi ya kisiasa na rahisi kutumia kuamsha hisia za watu. Inatengenezwa taswira kama Rais anastarehe. Sisi tulio kwenye Diplomasia tunauzoefu tofauti, tukiwa ziarani tunafanya kazi zaidi, tena zaidi ya saa za kazi kuliko tukiwa nchini. Mikutano ya kikanda na kimataifa hufanyika hadi usiku wa manane, na unahusisha kusoma na kuandika sana. Wengi hasa Rais hukosa hata huo muda wa kufanya 'shopping'. Ni jambo la kawaida kabisa kukuta Mwanadiplomasia amesafiri miji mingi lakini haijui hata mitaa ya miji zaidi ya viwanja vya ndege, kumbi za mikutano na hoteli.

Isitoshe tunapaswa kutambua kuwa tunamchagua Rais ili pamoja na kazi nyingine asafiri nje. Maana Rais wetu kwa mujibu Katiba ni Mkuu wa Nchi, na hivyo Mwanadiplomasia nambari wani wa nchi, ndio maana tunamnunulia ndege. Pia, Rais huyu ni Rais wa Tanzania nchi yenye ushawishi mkubwa kimataifa. Aidha, Rais mwenyewe tuliyenaye ni Mwanadiplomasia aliyebobea, ambaye kabla ya kuwa Rais, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10. Sifa zote hizi, zinamfanya alazimike kusafiri.

Tukiachilia mbali wajibu wake wa kusafiri kwa sifa nilizoainisha hapo juu, napata taabu kuelewa wale wanaosema Rais Kikwete anasafiri sana wanamfananisha na nani? Maana kipimo cha Rais wetu kusafiri au kutosafiri, chafaa kipimwe dhidi ya Rais mwingine. Maana humu ndani ya nchi, sidhani kama yuko kiongozi anayesafiri ndani ya nchi na kwenda vijijini kukutana na wananchi kuliko Rais Kikwete. Hali kadhalika, sidhani kama yuko Rais wa Tanzania ukiondoa Mwalimu Nyerere ambaye ametembea ndani ya nchi hii kushinda Kikwete.

Rais Kikwete hasafiri sana ukilinganisha na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini wala Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria. Hawa pia ndio wenye misafara mikubwa na viwango vya posho vya serikali zao pia ni vikubwa kuliko vya Tanzania. Tusisahau kuwa, hizi ndio nchi mbili zenye nguvu ya kiuchumi na kijeshi barani Afrika. Pamoja na kutowazidi kwa safari, Rais Kikwete anawazidi 'wasta' kimataifa. Aidha, Rais Kikwete hamfikii Rais Paul Biya wa Cameroon ambaye huweza kumaliza mwezi mzima au zaidi nje ya nchi, kwa ziara zisizo za kikazi. Ziara za Rais Kikwete ni za kikazi, katika kutimiza wajibu wake. Marais hawa wa Afrika Kusini na Nigeria ndio wa kuwalinganisha na Rais Kikwete, marais wengine hawako ligi moja kidiplomasia na Rais Kikwete, hivyo hatuwezi kuwalinganisha na Rais wetu.

Ziara za viongozi kutoka nje hutokana pia na ziara za viongozi wetu nje. Ni muhimu ikaeleweka kuwa, katika diplomasia iko kanuni ya 'nikune-nikukune' kwa kimombo ikiitwa 'reciprocity'. Marais hukaribishana wanapotembeleana. Aidha, Rais hawezi kujiendea tu kwenye nchi nyingine bila kualikwa au ridhaa ya mwenyeji maana mapokezi ya Rais yanaambatana na itifaki nyingi na kubwa. Ziara za Rais nje hubeba agenda nyingi za wazi na siri, na mara nyingi hufuatia baada ya kazi iliyofanywa tayari na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Ieleweke kuwa, si kwamba marais wa nchi nyingine hawasafiri, bali hawaalikwi, hawaalikiki, na wakati mwingine wana matatizo ya kiusalama nyumbani yanayowafanya kushindwa kutimiza majukumu yao kama wanadiplomasia namba moja. Kisichofahamika na wengi ni kuwa, Rais Kikwete hukataa safari nyingi tu kuliko anazoenda. Mara nyingi, Rais hukasimisha majukumu yake ya nje kwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo ya Nje, hata Waziri Mkuu wamuwakilishe nje ili kumpa nafasi ya kushughulika na masuala ya ndani ya nchi.

Rais husafiri tu anapolazimika kufanya hivyo. Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maziwa Makuu (ICGLR). Rais hawezi kukwepa kuhudhuria Mikutano ya Wakuu wa Nchi ya Jumuiya hizo inayofanyika kila mwaka. Mbali na hiyo, ana majukumu ya Diplomasia ya Uchumi ambapo yeye kama Mwanadiplomasia namba moja, ana wajibu wa kufungua uhusiano mpya.

Rais yeyote ambaye angetawala awamu ya nne angesafiri kama Rais Kikwete. Hii ni kutokana na ukweli huwa, ametawala wakati ambao, nchi inapanua wigo wa uhusiano kunakoendana na uchumi kupanuka. Tukishapanua uhusiano wetu, Rais hatakuwa na haja ya kusafiri sana nje, itabaki kazi ya Waziri wa Mambo ya Nje kupalilia uhusiano. Hivyo, Rais wa Awamu ya Tano hatalazimika kusafiri sana. Kulalamika kusafiri kwa Rais sasa ni sawa na kulalamika barabara kujengwa kwa wingi wakati huu na si kabla.

Ni imani yangu, nimejitahidi kufafanua na kutoa mwanga kuhusu Diplomasia yetu. Naamini nimetekeleza wajibu wangu wa kuelimisha na kuhabarisha, kwa kutoa uchambuzi kwa jicho la mwanadiplomasia. Nimejitahidi kutoa mwanga huu ili wachambuzi wa siasa waendelee kutoka katika msingi huu, ili wanapohukumu ikiwa Diplomasia yetu imeporomoka au la, wafanye hivyo kwa haki. Naamini kwa dhati kuwa, katika Sera ya Nje, Rais Kikwete amefanikiwa sana. Mnyonge Mnyongeni, Haki yake Mpeni!


Chanzo:
Raia Mwema
 
Asante kwa uchambuzi wako wa upande wa pili wa shilingi....

waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni
 
Yeriko ni mpiga zumari tu. ametimiza wajibu wake ili mradi mkono uende kinywani
 
Akili ya Yeriko Nyerere sawa na ya bosi wake, Mr. Zero, anaandika maandiko akiwa amevaa gwanda la CHADEMA unTegemea aandike nini?
 
Yericko ni msaka lishe CDM hivyo anatoa maandiko pasipo kufanya uchambuzi wa kina. Hongera sana kwa kumuumbua
 
Ruanda ipo bara gani hapa duniani??

Posted by: SUPU YA MAWE (PhD Holder)

sidhani kama katika uandishi hakuna makosa...kuweka ruanda badala ya rwanda ni kosa la kawaida katika uandishi as long as kilichoandikwa kinaeleweka..jabiri makame ahsante kwa uchambuzi mzuri sana.yericko ni kijana mwenye akili ila inapotoka sababu ya kupotoshwa na wahuni wachache!membe ni mseminari mwenye maadili..ni kati ya watanzania wachache pekee duniani waliopata bahati ya kuwa wahadhiri wasaidizi nchini marekani chuo cha john hopkins...hili linatosha kumjibu yericko kuwa yeye ndio ana matatizo.
 
Last edited by a moderator:
Kwa Tanzania ya Leo nisipomsikia mtu akikemea ufisadi na ubadhirifu wa Mali za umma Kwakweli nakuwa sina imani naye,hii Nchi imechoka jamani,tazameni afya za Watanzania,tazameni maisha yao,tazameni elimu wanayopata......... Tunataka kiongozi hata kumuangalia tu kwa macho tujue kweli huyu anaguswa na shida zetu na katika hao Membe hayumo........... Nimekumbuka kauli ya jk kule songea kuwa watu makini wa Kuliongoza hili Taifa hata kujitokeza hawajajitokeza,hata wakiambiwa watuongoze wanasita,mtu wa hivyo anajua shida ya kuliongoza Taifa maskini,anaguswa na shida za Taifa........Kuhusu Membe mteteeni tu lakini Kiukweli.......Nope!hafai.
 
rosemarie ni uongo kusema membe kabadili dini....membe bado ni mkristo muumini mzuri wa dhehebu la roman katoliki
 
Last edited by a moderator:
sifongo inaelekea huwa hufuatilii siasa za nchi hii..membe ndiye kada wa ccm anayetajwa katika urais mwaka huu anayekemea ufisadi kila kukicha bila kificho
 
Sijashawishika na maelezo marefu ya Mh Balozi mstaafu.Kikubwa alichokifanya ni kumtetea bosi wake kwa malengo anayoyafahamu.Tunachokifahamu sisi ni kwamba JK na jamaa zake wamekuwa madalali wazuri wa rasilimali zetu kwa Mataifa yaliyoendelea kiviwanda.Hizo faida sijui za kuheshimiwa sijui kupata nafasi za viti ktk baraza la usalama la umoja wa mataifa hayatokani juhudi zetu binafsi zitokanazo na mafanikio yetu kiuchumi bali tunapewa heshima hizo kama fadhila kwa kuwakarimu fursa za kujichotea rasilimali zetu.Mfano ni huu uhusiano uliopo kati ya urafiki wa mashaka wa India na Tanzania na uingizwaji wa kimagendo wa madini yetu ya TANZANITE nchini humo.Kwakweli ni lazima wajifanye ni marafiki zetu kwasababu TANZANITE zetu zinachangia kuujenga uchumi wa.Hayo Mataifa ya Magharibi na taifa la China ndiyo sina hata la kusema kwa namna wanavyoimarisha mazingira ya wao kukwapua rasilimali zetu tukishuhudia,wanatuvika vilemba vya ukoka (ziara za viongozi wao nchini,Kikwete kutunukiwa tuzo za kimataifa mara kwa mara,Migiro kupewa unaibu katibu mkuu UN,Kupata viti vya uwakilishi UN,JK kupata mialiko mingi nje) basi tumefurahi wenyewe na kuridhika.Wakati huo huo tukifanya kazi nzuri sana ya kudhohofisha uchumi wetu kwa kuyaua au kuyadhohofisha mashirika na makampuni yetu ya umma kama vile TRC,ATC, Posta na Simu,NBC,nk ambayo ni nguzo muhimu ktk ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu.Sijui sasa ni aina gani ya diplomasia tunayojaribu kuijenga wakati uchumi wenyewe tunaudhohofisha tena kwa makusudi.
 
Back
Top Bottom