Mbunge atimua mbio kuikwepa Takukuru

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
Frederick Katulanda, Mwanza
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashughulikia wanaotoa rushwa katika uchaguzi, mbunge wa Nyangâwale James Msalika, juzi alinusurika kutiwa mbaroni baada ya kufanya sherehe kwa viongozi wa chama na baadhi ya madiwani wa jimboni kwake.

Katika tukio hilo ambalo lilitokea katika Kijiji cha Bukwimba wilayani Geita Machi 4 mwaka huu, inadaiwa kuwa mbunge huyo aliandaa sherehe hiyo kwa lengo na nia ya kujinadi kwa wapigakura na alichinja ngombe wawili.

Hata hivyo, mbunge huyo amesema Takukuru haijamkamata wala kumuhoji na kufafanua kuwa yeye si muandaaji wa sherehe hiyo bali iliandaliwa na kata moja ya CCM kuadhimisha miaka 33 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Imeelezwa kuwa wakati wakiwa wanaendelea na hafla hiyo, ghafla diwani mmoja alipata taarifa kuwa kulikuwa na gari kutoka wilayani Geita ya maofisa wa Takukuru waliokuwa wakienda kijijini hapo kufuatilia sherehe hiyo hivyo kumwarifu mbunge huyo na wapambe wake wengine kuingia katika gari na kuondoka.

"Muda mfupi baada ya kuondoka walifika maofisa wa Takukuru ambao waliomba kupata maelezo ya hafla hiyo na kuambiwa ilikuwa imetayarishwa kwa ajili ya madiwani kuwapongeza wenyeviti wa serikali za mitaa walioshinda uchaguzi," kilieleza chanzo chetu.

Kutokana na hali hiyo maofisa hao wa Takukuru waliamua kupiga picha sehemu ya masufuria ya wali na nyama ambayo ilikuwa bado haijapikwa na kuondoka kurejea wilayani Geita.

Kamanda wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Christopher Mariba hakutaka kuzungumzia tukio hilo, lakini akadokeza kuwa hajasoma taarifa kutoka wilayani Geita.

"Kikubwa tunaomba ushirikiano kwa wananchi na nyie huku, ili tuendelee kupata taarifa za kufanyia kazi. Sijasoma ripoti ya Geita na hapa niko nje ya ofisi nina wageni sasa siwezi kuwa na maelezo," alieleza kamanda huyo na kuhimiza ushirikiano kwa wananchi.

Akizungumzia hali hiyo, Msalika alisema kuwa alialikwa kwenye sherehe awe mgeni rasmi na alifika hapo kwa lengo na nia ya kusherehekea kutokana na kualikwa na chama hicho, kata ya Bukwimba.

Alisema awali sherehe hiyo ilipangwa kufanyika Februari 5 mwaka huu, lakini walisogeza mbele kutokana na nafasi yake hivyo kufanyika siku hiyo.

"Nilitumia fursa hiyo kugawa vitabu vya kidato cha kwanza hadi cha nne ambavyo tumepata Nyangâwale kama msaada toka taasisi ya Fursa Sawa kwa Wote," alieleza.

Alisema sheria mpya ya fedha za uchaguzi inawachanganya watu, lakini akasema kuwa mbunge anayeshikilia jimbo hazuiliwi kuwa mgeni rasmi katika sherehe na wala kutoa msaada.

"Kwa ajili ya ufafanuzi naomba waulizeni Chiligati ama Makamba juu ya sheria hii, mbunge niliyeko madarakani siwezi kuombwa msaada wa saruji nikakataa eti kwa sababu ya sheria... nitatoa maana huko ni kutekeleza ilani ya chama," alieleza Msalika na kudai kuwa taarifa za sherehe hiyo zimepotoshwa na mmoja wa wagombea anayewania jimbo hilo.
 
Back
Top Bottom