Mbinu za kujitambua

Hemedy Jr Junior

JF-Expert Member
Feb 17, 2023
908
1,064
Kwa kifupi naweza kusema kujitambua ni hali ya kuwa na ufahamu wa nini kuhusu wewe.Hali yako,umuhimu wako,malengo yako,hatima yako, changamoto zako, nk, hayo yote yanakuwa wazi kwako kwa kujitambua.
Dhana ya kujitambua kwa zama za sasa imekuwa kama kengele ya kanisa au azana ya msikiti, kwa jinsi ambavyo hutamkwa mara kwa mara.Sasa yatosha kwa jinsi tulivyoisikia,leo nataka tuje na kitu kipya kama kilivyoelezwa katika kichwa cha mada yetu.

Sipendi kukuchukulia muda wako naomba niingie moja kwa moja kwenye mada

1. PIMA UMRI NA KIWANGO CHA FIKRA ZAKO

Sote tunafahamu kuwa hakuna kiwango maalumu cha kufikiri kilichoidhinishwa kimataifa kutoka umri mmoja na mwingine. Bali tunaviwango vya kimataifa vinavyotoa uwiano wa umri wa mtoto na kuandikishwa shule.Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kupima kiwango cha fikra zako kwa kulinganisha na umri wako.

Unaweza kupima fikra zako kwa kutazama ubora wa matokeo ya kila unachoamua kutenda pasipo kusaidiwa na mtu mwingine.Pia unaweza kupima fikra zako kwa kuzilinganisha na ubora wa fikra za watu wenye kiwango cha juu cha fikra katika umri wako. Lakini mwisho wa yote viwango bora kabisa vya kifikra vinalenga juu ya usahii wa wakati katika kutekeleza jambo fulani.

Unaweza kupima jinsi unavyopanga, unavyoamua,unavyotekeleza, na kuendelea au kusitisha maswala fulani fulani katika maisha yako na aina ya matokeo unayoyapata kwa kuzingatia ubora wake.

Kwa kufanya hivyo itakusaidia kuanza kupata picha ya namna gani unajitambua.

2. TAFUTA KUJUA UPEKEE ULIONAO

Hii nayo ni kati ya mbinu bora inayokufanya ujitambue.Watu wengi hupenda kufanana na watu fulani fulani haswa watu ambao wao huwaita role model (mtu wa mfano),Na kusahau kuwa yeye ndiye role model na.1 kwake binafsi.Makosa haya humpelekea mtu huyo kujua zaidi kuhusu huyo role model na.2 na upekee wake kuliko anavyoweza kujifahamu mwenyewe.

Leo imekuwa ni kawaida kumsikia mtu akieleza kwa ufasaa upekee alionao OBAMA na MKEWE lakini ukimuuliza upekee alionao akakujibu kirahisi tuu sijui.Kitu pekee kitakachokuokoa na tatizo hili ni kuamua kufahamu upekee ulionao na si upekee wa mtu mwingine au Role model wako.

Kama wewe ni mwandishi wa vitabu jiulize unatofautiana nini na waandishi wengine, au kama ni mwanafunzi, mwanasayansi, mchezaji, mwanajamii, nk, unatofauti gani na wengine ukiwa na maana uthamani wako uko wapi zaidi.

3. TAFUTA KUJUA CHANGAMOTO ZINAZOKUKABILI

Kama kweli umedhamiria kujitambua unatakiwa kufahamu changamoto au matatizo yanayokukabili. Changamoto hizo zinaweza kuwa ni zile zinazotokana na rika, mazingira, kiwango cha elimu yako,Hali uliyonayo (ulemavu, mahitaji maalumu au uathirika wa magonjwa, ndoa, bila ndoasingle nk. ).

Kama ni rika tambua rika lako linakabiliwa na changamoto zipi.Ikiwa ni mazingira tafuta kujua changamoto za kimazingira ulizonazo. Unaishi kijijini, mjini, shuleni, chuoni, mfanyakazi, kiongozi, mfuasi au vinginevyo ,jiulize katika mazingira hayo unakabiliwa na changamoto gani.

Inawezekana wewe ni teenager (13-19 miaka) au kijana au mzee, jiulize kuhusu changamoto zako. Vivyo hivyo kwa kiwango cha elimu pamoja na hali kama ilivyofafanuliwa katika mabano_Orodhesha changamoto zinazokukabili.

Kumbuka hata uonevu wa kibinadamu wa kawaida hutokea zaidi kwa watu wasiozingatia kipengele hiki cha ufahamu wa changamoto. Hakikisha unafahamu wapi utakwama kabla hujafikia na kuanza kuchukua hatua mapema iwezekanavyo. Kitendo hicho kitakufanya uwe macho saa zote na kila atakayekuona atakuthamini hivyo kutokuwa na madhara kwako.

4. TAFUTA KUJUA WAJIBU NA MAJUKUMU YA WATU WA RIKA LAKO

Kwa haraka unaweza kufikiri kuwa nataka kufundisha uraia. Utanisamehe kama nitakuwa nimekukumbusha kitu unachoimba au ulichoimba kilasiku shuleni. Lengo langu nataka nikufumbue macho kuhusu wajibu na majukumu kama dhana muhimu katika kujitambua.

Mfano; mama mmoja alikuwa akilia kwa uchungu nje ya nyumba yake huku akijitupatupa chini na kugalagala. Majirani wakaja mbio na kukusanyika kufahamu kilichotokea. Lakini kila walipomuuliza mama alichokua akililia aliwaonyesha kidole katika mlango uliokuwa wazi.

Watu wakakimbilia ndani na kumkuta mtoto wa miaka minne na nusu aliyewekewa kila kikorokoro cha kuchezea lakini hakuna alichokishika wala kukichezea. Walipotoka na kumuuliza mama mbona hatukuona chochote zaidi ya mtoto na vitu,mama akaongeza kilio na kusema “masikini mwanangu asala gani hii! huyu ni mwanangu watatu, wenzake waliotangulia walikufa kwa moto shambani kwasababu hawakuweza kusogea hata hatua moja moto ulipotokea nilipokuwa kisimani kuteka maji. Kinachoniumiza zaidi ni kuona hata huyu naye hagusi chochote nilichomwekea nahisi naye atakufa kifo kama cha wenzake”.

Kwa mfano huo tunapata picha ya mtu asiyetambua wajibu wake anavyoweza kuleta hasara kubwa kwake yeye mwenyewe, kwa familia yake na kwa taifa lake.Mama aligundua kuwa mtoto wake hajitambui kwa kutonyanyua chochote. Majukumu ya msingi ya mtoto wa umri ule ni kucheza. Kutokucheza ilikuwa ni ishara tosha ya kutokujitambua. Jiulize kama wewe ni mmoja wa wale wasiowajibika?.

Piga picha na kuyatazama majukumu yako kama mtoto,kijana,au mzee.
Jiulize kuwa wewe ni Yule mtoto mwenye kila kilicho mbele yake lakini hakuna anachogusa?

Jiulize kuwa umekuwa mtu wa kunyooshea vidole majukumu au umekuwa mstari wa mbele kutumikia?.
Umewahi kushiriki kutatua kero yeyote nyumbani kwako, mtaani kwako au maeneo yaliyokuzunguka?

Jiulize unafanya nini katika kujiandaa kutumia fursa zinazojitokeza duniani?
Nafasi uliyonayo unaitumia kufanya wengine kuinuka au unawadidimiza?
Jiulize kama wewe ukikosekana duniani, dunia itakuwa imepata hasara yeyote?

Wakati unajiuliza maswali hayo ni wazi kuwa utaanza kupata picha ya jinsi ulivyo kwa kupima uwajibikaji wako.Kitendo kicho kitakufanya uongeze uelewa wako juu yako binafsi na kwasababu hiyo utaingia kwenye kundi la watu wanaojitambua.

5. PIMA KUJIAMINI KWAKO
Ili kujitambua inakupasa kuchukua jukumu hili msingi la kupima kujiamini kwako.Hebu jichukue katika fikra zako na kujiweka mbele ya umati mkubwa wa watu wenye uelewa wa kutosha. Jaribu kuwaelezea au kuonyesha kitu ambacho unakifahamu kwa usahihi kabisa hapa duniani.Unahisi unaweza kukifanya kikamilifu bila hofu wala kubabaika.

Unaweza kujikumbusha mambo ambayo yalikuwa yanakufanya ushindwe kujiamini kama bado yapo au la. Pima ubora wa unachofanya kama una nafasi yeyote katika viwango vya kidunia? Kama wewe unajihusisha na sanaa je sanaa yako inaweza kumvutia mtu yeyote duniani?
kama ni huduma je! huduma yako inaweza kumfaa mtu yeyote duniani?
Kama ni mwanafunzi je wewe unaweza kuwa mwanafunzi bora popote duniani au ni hapo kijijini kwako tu?

Unaweza kushindanishwa na mtu yeyote duniani kwa hilo ambalo wewe ni bora sana hapo kwenu au ubora huo ni wa hapo kwenu tu?

Kwa vipimo hivyo vitakufanya uzidi kujitambua na kuchukua hatua ya kuondosha mapungufu uliyonayo na kukufanya uzidi kujiamini.

6. WEKA VIPINDI MAALUMU VYA KUJITATHIMINI

Kitendo cha kujitathimini kitakufanya kujichunguza na kujiweka karibu na wewe binafsi. Tatizo kubwa tulilonalo leo duniani ni kwamba tunawatu wengi ambao wako karibu sana na watu wengine lakini hawako karibu na wao wenyewe. Kifupi ni kwamba wanajua sana kinachoendelea kwa watu wengine kuliko kinachoendelea kwao binafsi.

Wanalaumu watu hawana elimu wakati wenyewe hawana,
Wanatetea unyanyasaji wa kijinsia wakati wao wenyewe wananyanyaswa,
Wanalaumu watu wanaovunja ndoa wakati wao wenyewe wana nyumba ndogo, wanalaumu kuhusu wizi wa viongozi wa umma wakati Wao mwenyewe wanaiba kwenye kampuni zao.

Sasa, kitu ambacho kinaweza kusaidia katika kujitambua ni kufanya tathmini binafsi juu ya mwenendo wako.Kabla hatujaanza kukosoa uzembe wa watu wengine tenga vipindi maalumu ikiwa ni kila baada ya wiki, mwezi au mwaka kutathimini ni uzembe wa namna gani umefanya na matokeo yake. Hata hivyo unaweza kufanya tathimini za kila siku ili kutokuwa na mlundikoano wa tafakuri za muda mrefu kuhusu namna ulivyoishi.

Unaweza kutathimini kiwango cha mafanikio kwa kulinganisha na matarajio,kiwango cha mapungufu kwa kwa kulinganisha na namna ulivyoshindwa. Kama mafanikio hayakufikia malengo basi ni wazi kuwa bidii na mbinu bora zaidi zinahitajika na kama matokeo ni kushindwa basi ni wazi kuwa mfumo mzima wa maisha inabidi ubadilike na mbinu mpya zinatakiwa.

Kiwango cha kujitambua kinaendana na tathimini binafsi. Ni kiwango cha hali ya juu cha kutojitambua kuendelea na kazi ileile au mbinu ileile inayokufanya kilasiku ushindwe kutimiza malengo yako.Kila baada ya tathimini lazima uje na mapendekezo mapya yenye mbinu mpya ,mikakati mipya na matarajio mapya.Kwa kufanya hivyo ni dhahili kuwa kiwango chako cha kujitambua kitakua na kuongeza mabadiliko ya kila siku katika maisha yako.

7. KUBALI KUANZA UPYA

Bila kujali wasifu ulionao unaweza kuonyesha kiwango cha kujitambua kwako kwa kuanza upya mara tu unapobaini kuwa kunamakosa makubwa katika mwenendo wa maisha yako.mtu mwenye kiwango cha chini kabisa cha kujitambua hawezi kuanza upya .kwasababu ya kutojitambua kwake haoni shida kwa lolote limpatalo na kuhisi kuwa amestahili.

Mtu asiyejitambua haoni umuhimu wa kubadilisha mtindo wa maisha kwasababu hufikiri kuwa kufanya hivyo ni sawa na kupoteza wakati. Inashangaza sana kumwona mtu anatumia staili ya aina moja katika kupambana na changamoto ambazo kila siku zinabadilika.

Jenga tabia ya kukubali kuanza upya kila unapoona kuwa hatua ya kiwango cha makosa ulichofikia hakiwezi kurekebishika. Mfano, kama pengine fani unayoitumikia haiendani kabisa na kipaji ulichonacho kubali kuanza kujifunza fani nyingine. Na endapo marafiki ulionao wanakusababisha kushindwa kutimiza majukumu yako, kubali kuanza kutafuta marafiki wapya.

Kitendo cha kukubali kuanza upya kitakufanya kujitambua. Utakapoanza awamu ya pili itakusaidia kubaini makosa uliyoyafanya mwanzo na kwasababu hiyo kuwa mwalimu wa wengine.

Kupitia mada hii bila shaka utakuwa umepata uelewa mkubwa sana kuhusu mbinu ya kujitambua na sasa unaweza kuwa na mchango mkubwa kwako na kwa jamii yako.

Uwe na siku njema. Naitwa Hemedyjrjunior
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom