Sildenafil Citrate
JF-Expert Member
- Jan 29, 2021
- 573
- 2,554
Akizungumza East Africa Radio asubuhi hii, Disemba 12, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo amesema Haki za wananchi zinazopatikana nje ya mtandao zinapaswa kutolewa pia ndani ya mtandao kwa kuwa ni haki za msingi zinazogusa maisha ya watu.
Kuhusu kutokutolewa kwa taarifa za alipokuwa Makamu wa Rais Dkt. Mpango, Melo amesema Makamu wa Rais ni kiongozi wa umma, analipwa kwa pesa za umma. Hata kama alienda kwa kazi maalum ni lazima wananchi waambiwe kwa kuwa analipwa kwa kodi zao. Hata kama hawatasema kaenda kufanya kazi gani lakini wananchi wanapaswa kujua kaenda wapi, kwa siku ngapi.
Akitoa maoni yake kuhusu hatua ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kuwashughulikia waliotoa Taarifa za uzushi kuhusu kifo cha Makamu wa Rais, Melo amesema "Nimesikia Waziri atachukua hatua, ni sawa. Lakini wewe pia ukiguswa sheria hii ichukue mkondo wake, isionekane ipo kwa ajili ya kulinda viongozi pekee. Kuna ushahidi wa matukio mengi yametokea kwa wananchi na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa"
Ameongeza "Sheria ya Makosa ya Mtandao (Kifungu cha 16) inasema anayetoa taarifa za uongo kwa makusudi atashughulikiwa. Kazi ipo kwenye kuprove kama mtu alifanya kwa kusudi, lakini sheria hizi hazitumiki zikivunjwa kwa wananchi wa kawaida lakini zikivunjwa kwa viongozi ndio zinafanya kazi. Kuna "impunity"
Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa kwenye matukio muhimu yanayohusisha viongozi wa kitaifa taarifa sahihi zinapaswa kutolewa. Kama kuna uzushi taarifa sahihi zitolewe kuondoa uzushi huo maana kukaa kimya huendeleza kusambaa kwa uzushi.
Melo aliulizwa pia ni kwa nini habari za uzushi kuhusu afya ya Makamu wa Rais ziliendelea kusambaa hata baada ya Waziri Mkuu kutoa taarifa. Alisema watanzania wana haki ya kutokumwamini Waziri Mkuu, yaliwahi kutokea enzi za Uongozi wa Hayati Magufuli, mazingira ya wakati huo na sasa kwa kiasi fulani yalikuwa yanafanana.