SoC03 Mambo haya yaingizwe kwenye katiba mpya; yataimarisha demokrasia, utawala bora na uwajibikaji

Stories of Change - 2023 Competition

tpaul

JF-Expert Member
Feb 3, 2008
21,850
18,260
Ni wazi kuwa katiba ya sasa imepitwa na wakati kwa sababu kuu mbili. Kwanza, katiba ya sasa ina chembechembe za ukoloni. Na kama tujuavyo ukoloni ulijaa ukandamizaji, unyimaji wa haki na utawala wa mabavu. Pili, katiba ya sasa imejaa viraka vingi ambavyo viliingizwa kwa mihemko au kwa ajili ya kukidhi matakwa finyu ya kikundi cha watu wachache. Mambo yafuatayo yakiingizwa kwenye katiba mpya yatasaidia kuimarisha demokrasia, utawala bora, haki na usawa:

1. Kumpunguzia Rais idadi ya watendaji wa kuteuliwa
Rais amerundikiwa madaraka makubwa mno ambayo sina uhakika kama hata yeye anapenda nayo. Nadhani anakubali tu kuwa katiba inamruhusu. Kwa upande wa kisiasa, katiba inampa Rais mamlaka ya kuteua kila mtu kwenye serikali yake, kuanzia waziri mkuu hadi katibu tawala wa wilaya.

Nashauri uwezo wake upunguzwe hadi kwenye uteuzi wa Waziri Mkuu na mawaziri tu. Nafasi nyingine zilizobaki zijazwe kupitia usaili au kupigiwa kura na wananchi. Kufanya hivi kutawapa haki raia wengine wenye uwezo kuomba nafasi hizo badala ya kutegemea vetting inayofanywa na watu ambao wakati mwingine wanachomekea watu wao wasiokuwa na uwezo. Ndio maana kila kukicha Rais anahangaika kutengua, kuteua upya au kuwapangia kazi nyingine wateule wake. Hii ni ishara kwamba madaraka haya yamemlemea.

2. Wananchi kumpigia mbunge kura za kutokuwa na imani naye
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, mbunge akiashachaguliwa na wananchi hakuna mtu yeyote anayeweza kumg’oa hadi apigiwe kura tena baada ya miaka 5. Kwa kuwa uzoefu unaonesha wabunge wa aina hii wana uhuru wa kutowajibika kwa wananchi na wanaweza kufanya mambo ya ovyo bila kumuogopa mtu yeyote, katiba mpya ije na kipengele ambacho kitawapa wananchi haki ya kumng’oa mbunge kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye pale anaposhindwa kuwahudmia ipasavyo au pale anapokengeuka na kuanza kuwadharau wapiga kura.

Hii itasaidia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa wabunge kwa kuchelea kung’olewa kabla ya miaka 5 kuisha. Ikiwa hili litafanikiwa, huwezi kuona mbunge akisinzia bungeni, kuunga mkono kila hoja au kufanya ujinga wowote unaorudisha nyuma maendeleo ya wapiga kura wake.
1685471913981.png

Wabunge wakiuchapa usingizi bungeni wakati mijadala ikiendelea
Chanzo: mtandao

3. Baadhi ya kazi za kitaalamu zijazwe kupitia mchujo wa usaili
Viongozi wanaopatikana kwa kuteuliwa na Rais kama vile mwanasheria mkuu wa serikali, jaji mkuu, jaji kiongozi, wakurugenzi wa mashirika ya umma na wakuu wengine wa taasisi za umma, wapatikane kwa kuomba kazi hizo na kusailiwa ili kuwapa nafasi watanzania wenye uwezo kutuma maombi ya kazi.

Kwa mfano, utakuta hakimu wa kawaida ana uwezo wa kuwa jaji mkuu lakini anabaniwa nafasi hiyo kwa kuwa Rais amepewa mamlaka ya kuwateua majaji tu. Au labda unakuta mtu yupo mtaani amesomea sheria na uongozi wa mahakama lakini hawezi kuomba kazi hiyo kwa kuwa katiba inambana.

Vilevile kwa wasomi wengine waliopo mtaani au wanaofanya kazi za kujitegemea wanashindwa kupata nafasi za aina hiyo kwa kuwa tu Rais anapoteua anaangalia wale waliopo kwenye mifumo ya kiserikali (sytem). Hii sio haki na haifai hata kidogo. Kazi hizi sharti zitangazwe ili kila mtanzania mwenye uwezo aombe na awe na nafasi sawa ya kuajiriwa. Kenya wameweza sisi tunakwama wapi?

Na pia kazi hizi zifanywe kwa mkataba wa muda mfupi, kwa mfano miaka 2, 3 au 5. Watakaofanikiwa kuajiriwa wapewe malengo wanayopaswa kuyatimiza ili waongezewe mkataba. Ikiwa mtu atashindwa kufikia maelengo, baada ya mkataba wake kuisha, atupiliwe mbali na usaili uitishwe tena kwa ajili ya kutafuta mtu mwingine mwenye uwezo kuziba nafasi hiyo. Kufanya hivi kutaongeza uwajibikaji na kupunguza wizi, rushwa, uzembe na umangimeza. Kuna baadhi wa wakuu wa taasisi wakishateuliwa kwenye nafasi hzi hujifanya miungu watu.

4. Wakuu wa mikoa na wilaya wapatikane kwa kupigiwa kura na wananchi
Hivi ni baadhi ya vyeo vyenye mwelekeo wa ukoloni. Ni mara nyingi tunashuhudia wakuu wa mikoa na wilaya wakiwafanyia ubabe wananchi bila sababu za msingi kwa sababu tu wananchi hao hawana namna ya kuwawajibisha. Ukichunguza kwa umakini zaidi utagundua ukuu wa wailaya na mkoa hauna tija yoyote kaika nchi hii licha ya kugharimu fedha nyingi kulipa mishahara minono, kununua mashangingi na kulipa posho nyingine kedekede.



Chanzo: Jamiiforums Youtube Channel

Kwa kuwa viongozi hawa wanafanya kazi kwa kujisikia na bila hofu yoyote, katiba mpya iruhusu wapigiwe kura na wananchi kila baada ya kipindi cha miaka 5. Uchaguzi wao ujumlishwe kwenye uchaguzi mkuu kama ilivyo kwa wabunge na madiwani.

Lengo la kufanyya hivi ni kuongeza uwajibikaji kwa namna mbili. Mosi wengi wa viongozi hawa hutokea kwenye mikoa ya mbali hivyo hawana uchungu na maendeleo ya wananchi wa mikoa au wilaya wanazozitawala. Pili, baadhi yao huishi kwa matumaini wakiwa wamejawa na hofu ya kutumbuliwa wakati wowote, kitendo kinachowapotezea umakini wa uwajibikaji kwa wananchi.

Baada ya kuanza kuchaguliwa na wananchi na kwa kuwa watakuwa wakazi wa mikoa husika, wataongeza kiwango cha uwajibikaji na watakuwa utu kwa wapigakura na uchungu wa maendeleo kwenye mikoa au wilaya zao.

5. Ubunge wa viti maalumu utupiliwe mbali
Kila siku watetezi wa haki za wanawake wamekuwa wakipambana kutafuta usawa. Mimi nipo kinyume na utetezi huu kwa sababu kuu mbili. Mosi, kuwateua wanawake kujaza nafasi bungeni ni matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.

Hii haijengi demokrasia wala uwajibikaji kwa namna yoyote ile. Kitendo cha kumteua mwanawake kukalia kiti maalumu ni sawa na kumbagua kwa kumuona kuwa ni kiumbe dhaifu kinachodharaulika na kisichoweza kusimama chenyewe kwenye majukwa ya kisiasa na kujipambania.

Pili, mbunge sharti awajibike kwa watu waliomchagua. Mara nyingi wabunge wa kuteuliwa huwajibika kwa chama kilichowateua badala ya wananchi. Kila jimbo lina mbunge wa kuchaguliwa ambaye anawajibika moja kwa moja kwa wapiga kura wake. Sasa hawa wabunge wa viti maalumu wanakuwa wanamuakilisha nani zaidi ya kula mishahra ya bure inayotokana na kodi za walalahoi? Ili kuongeza uwajibikaji na kumpunguzia mwananchi mzigo wa matatizo, katiba mpya ituondolee upuuzi huu.

7. Nafasi za ukurugenzi wa halmashauri, RAS na DAS zirejeshwe kwenye taaluma kama ilivyokuwa awali
Kabla ya serikali ya awamau ya 5 kuingia madarakani, vyeo tajwa hapo juu vilikuwa ni vya kitaaluma. Kwamba ili mtu uweze kujaza nafasi hizo sharti uwe umepitia kwenye nafasi za chini za utumishi wa umma na kupanda taratibu hadi kufika huko. Kwa mfano, wakurugenzi wa halmashauri walikuwa wakitokana na wakuu wa idara wabobezi walioiva katika nyanja mbalimbali za utumishi.

Ghafla, awamu ya tano ilipoingia madarakani ikavigeuza vyeo hivi kuwa vya kisiasa. Basi kiongozi wa wakati huo akawa anawaokota makada kutoka kusikojulikana na kuwapachika vyeo vya ukurugenzi kama njugu. Matokeo yake hawa wateuliwa sasa wamekuwa mizigo ofisini. Hawawajibiki tena kama walivyokuwa watumishi wa umma.

Ili kuongeza uwajibikaji, haki na utawala wa sheria, vyeo hivi vifutwe kwenye katiba ijayo na utaratibu wa kuwapandisha vyeo watumishi wa umma hadi kufikia nafsi hizi, urejewe.

Kwa mwenye swali, nyongeza, ushauri au kuhitaji ufafanuzi, tafadhali usikose kuniandikia.

Asante.
 
Back
Top Bottom