Mambo 10 ya kujifunza kuhusu fedha na utajiri kutoka kwenye orodha ya mabilionea ya mwaka 2018

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Fedha ni muhimu sana kwenye maisha yetu, kwa yale mambo yanayohusu fedha. Na kwa kuwa karibu kila kitu kwenye maisha yetu kinahusu fedha, basi fedha ina umuhimu mkubwa.

Sitaki nianze kukuambia kwamba ili afya yako iwe imara unahitaji fedha kwenye kula vizuri, kwenye kujikinga na magonjwa na hata kwenye kupata matibabu mazuri pale unapokutana na changamoto za kiafya.

Kadhalika sina haja ya kukuambia kwamba ili wewe upate maarifa bora, elimu nzuri na hata watoto au unaowalea wapate elimu bora, fedha zinahitajika. Hivyo fedha siyo tu ni muhimu, bali ni muhimu sana.

Kila mwaka, jarida linaloongoza kwa kuandika mambo yanayohusu fedha linaloitwa Forbes huwa linatoa orodha ya matajiri duniani. Orodha hii huwa wanaitengeneza kwa kuwafuatilia watu na mali zao, kuanzia mali wanazomiliki, biashara wanazomiliki na uwekezaji wanaofanya, kisha kuja na namba ya utajiri wao.

Ukweli ni kwamba, orodha hii ya Forbes siyo halisi sana kwenye utajiri halisi wa watu, kwa sababu wapo watu wenye fedha nyingi lakini haziwezi kuelezewa zimepatikanaje. Kwa mfano baadhi ya viongozi wa nchi, wanasemekana kuwa na utajiri mkubwa, lakini hauendani na vipato vyao halisi, hivyo hawaingii kwenye orodha hii. Lakini pia ni orodha sahihi ya kutumia hasa kwa wale ambao tunapenda kujifunza na kufikia uhuru wa kifedha, kwa sababu inaonesha zile njia halali ambazo watu wametumia kutengeneza utajiri mkubwa kwenye maisha yao.

Yapo mambo mengi ya kujifunza kwenye orodha ya mabilionea kwa mwaka huu 2018, lakini leo nimekuchagulia yale kumi muhimu, ambayo unaweza kujifunza na kuondoka na kitu cha kufanyia kazi ili uweze kupiga hatua kifedha.

Kabla sijaingia kwenye orodha hii ya mabilionea, nikukumbushe kwamba malengo yangu makubwa mawili kwenye maisha yangu ni KUWA BILIONEA na KUWA RAISI WA TANZANIA MWAKA 2040. Haya ni malengo ambayo sijawahi kuwa na wasiwasi kwamba nitashindwa kuyafikia, kwa sababu nayafanyia kazi kila siku. Hivyo orodha kama hizi za mabilionea zinapotoka, huwa nahakikisha najifunza vitu ninavyoweza kufanyia kazi.

Siyo lazima utake kuwa bilionea ndiyo ujifunze kutoka kwa mabilionea, kwa kuwa tunakubaliana fedha ni muhimu, basi tunapaswa kujifunza kutoka kwa wale ambao wamezipata kwa wingi.

Yafuatayo ni mambo kumi niliyokuandalia ya kujifunza kutoka kwenye orodha ya matajiri wa dunia ya mwaka 2018.

1. Utajiri wa dunia unaongezeka.

Wapo watu ambao wamekuwa wanafikiri kwamba linapokuja swala la fedha, basi ili watu fulani wapate, lazima wengine wakose. Kwamba matajiri wanawanyang’anya masikini fedha zao, watu wanaamini kwamba watu wengi ni masikini kwa sababu matajiri wachache wanamiliki fedha zote.

Kama hili lingekuwa kweli, ina maana kwamba kiasi cha fedha duniani kingekuwa kile kile wakati wote. Lakini sivyo mambo yalivyo, kwenye orodha ya mwaka huu ya Forbes, inaonesha kwamba kwa mwaka mmoja tu, utajiri wa matajiri wa dunia umeongezeka kwa dola trilioni 9.1 sawa na ongezeko la asilimia 18 ukilinganisha na utajiri wa mwaka jana.

Kama utajiri wa dunia unaongezeka, hizi ni habari njema kwa kila mmoja wetu, kwamba utajiri siyo mchezo wa kupata na kukosa, bali ni mchezo wa kila mtu kupata kulingana na thamani anayozalisha.

2. Tajiri namba moja ndiyo bilionea wa kwanza kuvuka bilioni 100.

Jeff Bezos, mmiliki wa kampuni kubwa inayojihusisha na uuzaji wa vitu kwa njia ya mtandao wa intaneti ya Amazon ndiye tajiri namba moja duniani kwa mwaka 2018. Yeye ndiye tajiri namba moja ambaye amevuka utajiri wa dola bilioni 100. Akiwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 120, ndiye anayeongoza, akifuatiwa na Bill Gates ambaye ameshika nafasi ya kwanza kwa muda mrefu.

Kwa tajiri namba moja kuvuka dola bilioni 100, inaonesha kwamba fursa ya kufika utajiri wa juu zaidi zipo, na zipo wazi kwa kila mmoja wetu.

3. Kulala masikini na kuamka tajiri inachukua miaka zaidi ya 20.

Tajiri namba moja duniani, Jeff Bezos, kwa mwaka mmoja, tangu 2017 mpaka 2018, utajiri wake umeongezeka kwa asilimia 59, yaani kwa mwaka mmoja tu kipato chake kimeongezeka kwa dola bilioni 39.2, hili ni ongezeko kubwa la utajiri kuwahi kutokea kwa mwaka mmoja.

Ukiangalia hivyo ni rahisi kuamini kwamba wapo watu ambao wanalala masikini na kuamka tajiri, watu wenye bahati, ambao dunia inawapendelea.

Lakini sasa unapokuja kuiangalia safari halisi ya utajiri wa tajiri namba moja duniani, haikuanza mwaka huo mmoja, badala yake imemchukua miaka zaiid ya 20 mpaka kufika hizi ngazi za utajiri wa kidunia.

Kampuni yake ya Amazon aliianzisha mwaka 1994, kama stoo ndogo ya kuuza vitabu na alifanyia kila kitu nyumbani kwake. Lakini kuanzia hapo amekua akikua kidogo kidogo mpaka sasa imekuwa stoo kubwa ya mtandaoni ambayo inauza kila kitu, kila kitu unachojua basi kinaweza kupatikana kupitia Amazon.

Hivyo kwa wale ambao wamekuwa wanaota kwamba ipo njia ya mkato ya kutajirika, angalia jinsi inavyowachukua watu muda.

4. Mabilionea wengi wameanza bila ya kitu kabisa na kutengeneza utajiri mkubwa.

Wapo watu ambao wamekuwa wanajiambia kwamba kama wangerithi mali kutoka kwa wazazi wao basi maisha yao yangekuwa bora kabisa. Japo ni rahisi kufikiria hivyo, huo siyo uhalisia. Zaidi ya nusu ya mabilionea wote duniani wameanza wakiwa hawana kitu kabisa. Walikuwa na ndoto kubwa za mafanikio, wakiwa na kitu ambacho kinatoa thamani kwa wengine na kisha kujipa muda huku wakiweka juhudi kubwa.

Hata waliorithi mali za wazazi wao, wameweka kazi kubwa sana kuhakikisha wanapiga hatua. Kwani ipo mifano ya waliorithi mali lakini wakafilisika.

Hivyo hata kama huna pa kuanzia kabisa, usiwe na shaka, hujatengwa na dunia kwamba huwezi kufanya makubwa. Jua ni wapi unakwenda, jua ni namna gani unakwenda, halafu anza safari kama wanavyosema kwamba safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja.

5. Fani tano zinazoongoza kwa kutoa mabilionea wengi.

Mabilionea wanatoka kwenye kila aina ya fani na kazi au biashara zinazoweza kufanywa na watu. Kuanzia teknolojia, uzalishaji mpaka uuzaji wa reja reja. Lakini zipo fani tano ambazo zimezalisha mabilionea wengi.

Moja ni fedha, hii inaongoza kwa kuzalisha mabilionea, hasa wale ambao wanatoa fedha zao kwa wengine kupitia mikopo au uwekezaji kwenye masoko ya mitaji kama hisa, hatifungani na njia nyingine za kuwekeza fedha kama kununua hisa kwenye makampuni binafsi.

Mbili ni mitindo na urembo, hili ni eneo ambalo limetengeneza mabilionea wengi pia. Kupitia makampuni ya nguo na bidhaa za urembo, watu wengi wameweza kutengeneza utajiri mkubwa.

Tatu ni uwekezaji wa mali (real estate), umiliki wa majengo kibiashara umekuwa njia kubwa ya kuzalisha mabilionea wengi, hasa kwa nchi zinazokua kiuchumi na zenye watu wengi kama China na hata Marekani.

Nne teknolojia, hii imezalisha mabilionea wengi sana, kuanzia kwenye uzalishaji wa vifaa mbalimbali mpaka kwenye utengenezaji wa programu zinazotumiwa sana na watu kama Facebook na nyinginezo, teknolojia imezalisha mabilionea wengi.

Tano ni michezo, kwenye michezo pia mabilionea wengi wamezalishwa.

Fani hizi tano siyo pekee zinazotoa mabilionea, kila aina ya fani inatoa mabilionea, lakini hizo zimetoa mabilionea wengi. Hivyo kama unaweza kutumia moja ya fani hizo, fursa zilizopo ni kubwa.

6. Ukomunisti unashindwa na ubepari.

Watu wamekuwa wakiaminishwa kwamba ukomunisti ni bora kuliko ubepari, hasa wanapoangalia madhaifu ya ubepari. Ukweli ni kwamba ubepari siyo mfumo bora kabisa wa kiuchumi, lakini ukilinganisha na ukomunisti, ubepari ni mfumo bora zaidi. Kwa sababu kwa asili yetu sisi binadamu, ni vigumu sana mfumo wa kikomunisti kujiendesha kwa mafanikio.

China ni taifa kubwa ambalo limekuwa na mfumo wa kiuchumi wa kikomunisti, lakini ndiyo taifa la pili kwa wingi wa mabilionea, taifa hilo lina mabilionea 476 nyuma ya Marekani yenye mabilionea 585. Kwa tunakoelekea, China utakuwa taifa linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mabilionea.

Sina haja ya kuanza kukushawishi kwamba, kama nchi inakuwa na mabilionea wengi binafsi basi hatuwezi kuiita tena ni ya kikomunisti, maana kwenye ukomunisti hakuna utajiri binafsi, bali utajiri wa jamii nzima.

Tuuelewe na kuutumia vizuri ubepari, ndiyo njia bora ya kutengeneza utajiri huku ukitoa huduma kwa wengine.

7. Uongozi siyo sehemu ya kutengeneza utajiri.

Watu wengi wamekuwa wakifikiria kwamba kuwa kiongozi mkubwa wa nchi, kama raisi basi ni njia ya kutengeneza utajiri. Labda kama ni kwa njia zisizo halali, kitu ambacho pia hakitahesabiwa kama utajiri. Lakini kwauhalisia, na orodha ya Forbes ya mwaka 2018 inadhibitisha hili, uongozi siyo sehemu ya kutengeneza utajiri.

Donald Trump, raisi wa marekani, kwa kipindi cha mwaka mmoja, utajiri wake umepungua kwa dola milioni 400, akitoka kuwa mtu wa 544 kwa utajiri duniani mpaka kufika mtu wa 766 kwa utajiri kwa mwaka huu 2018.

Hivyo tukumbuke kwamba uongozi ni sehemu ya huduma lakini siyo sehemu ya kutengeneza utajiri.

8. Afrika inakua kwa kasi kwa utajiri.

Kwa kipindi kirefu, Afrika imekuwa inaonekana kama bara lenye matatizo mengi na hivyo kuwafanya watu wake kushindwa kupiga hatua. Lakini kwa sasa mwanga mkubwa unaonekana, kwenye orodha ya Forbes ya mwaka 2018, inaonesha mabilionea Africa wameongezeka, kutoka mabilionea 21 mwaka 2017 mpaka mabilionea 23 mwaka huu 2018.

Pia jumla ya utajiri wao imeongezeka pia, kutoka dola bilioni 70 mpaka kufika dola bilioni 75.4. Hii ni dalili nzuri kwamba uchumi wa Afrika unakua, na fursa za kukua zaidi zipo.

Dangote anaendelea kuwa bilionea namba moja Afrika kwa mwaka wa 7 mfululizo, huku pia historia yake ikiwa ya kuchukua miaka zaidi ya 30 mpaka kufika alipofika sasa.

Afrika Kusini ndiyo taifa linaloongoza kwa mabilionea Afrika, likiwa na mabilionea 8.

9. Mohammed Dewji kutoka Tanzania ndiye bilionea mdogo Afrika.

Mohammed Dewji, bilionea pekee kwenye orodha ya Forbes anayetokea Tanzania, ndiye bilionea mdogo kuliko wengine wote Africa. Akiwa na umri wa miaka 42, Dewji anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola bilioni moja na nusu.

Forbes wanaeleza kwamba Mohammed Dewji aliridhi biashara za baba yake na kuweza kuziendesha na kuzikuza kwa mafanikio makubwa. Biashara ambazo ameorodheshwa kumpa mafanikio ya kifedha ni viwanda vya nguo na mafuta ya kula.

Hizi ni habari njema kwetu watanzania, kwamba tuna mwenzetu ambaye ameingia kwenye orodha hii ya mabilionea wa dunia, akitengeneza utajiri huu hapa hapa Tanzania. Hivyo kama tutaweka juhudi kwenye kuzalisha vitu vyenye thamani kwa wengine, mlango upo wazi kwa kila mmoja wetu kufanikiwa zaidi kifedha.

10. Mapenzi yana mchango mkubwa sana kwenye kufikia ubilionea.

Ukiangalia orodha ya mabilionea wote wa dunia, kitu kimoja unachokiona ni mapenzi kwenye kile ambacho mtu anafanya. Wengi hawafanyi kwa sababu ya fedha, bali wanafanya kwa sababu ndiyo kitu wanachopenda kufanya, wanafanya kwa sababu wanaona mbali zaidi kuliko fedha.

Mabilionea wengi wangeweza kulala na fedha zao zikawatosha kuendesha maisha yao mpaka watakapokufa, lakini ukiwaangalia ndiyo wafanyaji wakubwa wa kazi.

Hili ni funzo kwetu, hasa wale wenzetu ambao wakipata fedha kidogo tu wanaona kama wameimaliza dunia, mtu akipata faida kubwa kwenye biashara basi siku inayofuata hafungui kabisa, au akiongezewa kipato kwenye kazi basi anajisahau na kuacha kuweka juhudi, na kuona ameshakuwa bosi. Katika mabilionea karibu wote, wanafanya kazi kuliko hata watu waliowaajiri.

Nyongeza; ajira siyo njia sahihi ya kufikia ubilionea.

Kwenye orodha ya mabilionea, wanaoongoza ni wale walioanzisha kampuni zao wenyewe na kuzikuza, au waliorithi biashara za familia na kuzikuza zaidi. Hata wachache ambao waliajiriwa, ni wale waliofika nafasi za juu sana za ukurugenzi na pia wakawa na hisa kwenye kampuni wanayoongoza.

Lakini kwa ujumla, ajira siyo njia sahihi ya kuelekea kwenye ubilionea. Hivyo kama unawaza kuingia kwenye ubilionea, lakini umeajiriwa, anza kufikiria njia mbadala za kufikia lengo lako hilo. Uzuri ni kwamba haimaanishi leo uache kazi kabisa, bali unaweza kuanza kidogo pembeni na kuendelea kupiga hatua.

Haya ndiyo mambo kumi na nyongeza tunayoweza kujifunza kutoka kwenye orodha ya mwaka 2018 ya mabilionea wa dunia. Kama nilivyoeleza awali, orodha hii inaweza isiwe sahihi kwa asilimia 100, lakini haimaanishi hakuna cha kujifunza kabisa. Pia haimaanishi uwe na malengo ya kuwa bilionea ndiyo ujifunze, kwa kuwa fedha ni muhimu, basi tunapaswa kujifunza.

Jua wapi unapokwenda, jua njia ipi itakufikisha unapokwenda, anza safari na jipe muda wa kutosha, huku ukipenda unachofanya na kuweka juhudi sana. hiyo ni sentensi moja ambayo ukiielewa na kuifanyia kazi, hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Karibu ujifunze zaidi kwa makala za biashara, mafanikio na hamasa kwenye mtandao wa www.amkamtanzania.com
 
Umenifurahisha unapo sema una malengo ya kuwa bilionea mkubwa. Na kuwa rais wa tanzania mwaka 2040 na umesema hauna mashaka juu hilo.
 
Halafu akaongeza kuwa Kiongozi sio kigezo cha kua Tajiri
Nitakuwa bilionea kabla sijawa rais,
Na urais siuchukulii kama sehemu ya kutengeneza kipato, bali sehemu ya kutoa kile kilichopo ndani yangu kwa ajili ya taifa langu, kwa ngazi kubwa.
 
Nitakuwa bilionea kabla sijawa rais,
Na urais siuchukulii kama sehemu ya kutengeneza kipato, bali sehemu ya kutoa kile kilichopo ndani yangu kwa ajili ya taifa langu, kwa ngazi kubwa.
Ukitaka usiwe Tajiri kua Kiongozi labda uwe fisadi. Trump amedrop sana Tangu aingie madarakani
 
Ukitaka usiwe Tajiri kua Kiongozi labda uwe fisadi. Trump amedrop sana Tangu aingie madarakani
Sasa unamfundisha mwandishi, na wakati yote kayaelezea kwenye andiko lake.

NB:Kasema anataka kuwa billionaire au rahisi, na sio awe billionaire na raisi
 
Back
Top Bottom