Makongamano ya aibu na makongamano ya haiba

Rosh Hashannah

JF-Expert Member
Sep 13, 2017
3,415
2,042
(sehemu 1)

Kwa mada hii nilikuwa na vichwa vingi vya kumwaga. Kwa mfano, ningeliweza kuiita “WAAFRIKA HATUKO SAWA NA WENGINE” au “WAAFRIKA WAMOJA, HATUVAI MBILI.” Vichwa vyote hivyo vingeliweza kuwa muhtasari sahihi wa maudhui ya mada hii.

Ninasema kwa jinsi tunavyofikiri, kuamua na kutenda, sisi Waafrika hatuko sawa na wengine: Wamerikani, Wazungu na Waasia. Polepole sijatukana. Najieleza.

Sisi tunafikiri, kuamua na kutenda kitoto zaidi kuliko watu wa mabara mengine. Ndiyo maana linapokuja suala la IQ ya jamii sisi ni wa mwisho karibu ya mataahira. Huu ni ukweli wa kuudhi, lakini heri tuuanike hadharani huenda vizazi vijavyo vitaamka na kuwa tofauti na sisi. Hivyo ninaposema hatuko sawa na wanadamu wengine simaanishi masuala ya maumbile yetu, au kuzaa na kula. Katika haya tunaweza kusema tuko sawa.

Tusipo sawa ni pengine. Ni katika namna tunavyofikiri, kuamua na kutenda. Tunaona sasa hivi habari za makongamano. Siku hizi kuna hatua za kufanya makongamano kukabiliana na matatizo yetu.

Hapa tumepotea njia ya watu wazima. Badala yake tumeanza kwenda njia ya watoto wachanga.
Nisikilize vizuri. Sisi Afrika tunafanya makongamano ya aibu wakati wenzetu wanafanya makongamano ya haiba. Yaani makongamano yetu ni ya kutia haya ya uso, ya kijinga, ya kitoto, ya aibu, wakati wenzetu wanafanya ya kuweledi, ya kiutu uzima, ya haiba, yenye kuheshimisha. Ona! Sisi eti tunafanya makongamano tupeane akili ya Kinjikitile na kutoana mapepo tukimwomba Mungu atutoe kwenye roho za ujane, umaskini, na maradhi kama ukimwi, asthma, ukoma, presha, kisukari, kuota ndoto mbaya, kuwaona wachawi usiku na kadhalika.

Ndipo eti tunajikusanya watu wazima na watoto wetu tumwombe Mungu atuauni katika matatizo ya kukosa ajira, kukataliwa, kurogwa na watu, “kulaaniwa na wazee wetu”, kukosa ustawi, kupagawa na mapepo, kupandwa na majini (maruhani), kuota ndoto za ajabu, nyumba kutembelewa na bundi, vyumbani kuingia popo, kuchukiwa na majirani, kutopendwa, pesa kutokukaa, kukojoa kitandani, kuumwa na nyoka na kadhalika. mbona wenzetu hawalalamiki kuhusu haya? Kweli tunasikitisha mno na kwa haya tunatembea katika ujinga mkubwa.

Halafu? Dawa tunayoichukua katika makongamano hayo kutibu matatizo yetu eti ni kuanguka, kuweweseka, kulia, kusali kwa sauti ya juu, kufunga kavu, kukesha, kutoana mapepo, kukata miti ya ukoo inayotusababishia laana na kutiana moyo kwamba kwa jina la Yesu wa Nazareti wachawi hawatatuweza tena na tukilala hatuona tena maruweruwe.
Eti tunamtupia kazi Yesu, tukiita kwa kelele nyingi, “ Hakuna Mungu kama wewe!” “Hakuna Mungu kama wewe!” “Yesu anaweza!” “Yesu anaweza!” Ha, Mungu atusaidie katika utoto wetu? Yesu atusaidie katika mambo ya kipuuzi hayo? Ujinga mtupu!

Niwaambieni kitu? Ningelikuwa Mungu ningelivamia makongamano ya Waafrika na kuwatawanya kwa mateke ya matumboni na ngumi za usoni! Yesu “aliwafanyia hivyo” wabadili pesa na wauza njiwa na wanyama hekaluni. Hakika hapa naielewa hasira ya Yesu (Mk 11:15-19).

Sikilizeni Waafrika wenzangu. Tunafanya mambo kinyume na mategemeo ya Mungu mwema. Sawa na watu wengine, Mungu alitupa akili na utashi tuvitumie kutatulia matatizo yetu na yeye aje kubariki na kufanyia wepesi jitihada zetu tu (Zab 90:17). Usinibishe. Ndiyo kisa Mungu alituagiza tufanye kazi siku sita kati ya siku saba za juma. Sisi tunafanya kinyume chake, tunatumia siku sita kusali na kufanya mikutano na makongamano ya kijinga na kufanya kazi kwa shingo upande labda siku moja kwa juma. Hapo Mungu atusaidie kwa sababu gani? Tunafanya kinyume na alivyotupangia, tutampendezaje hata atujali? Sisi ni wa kupuuzwa tu, maana “hatunazo kichwani”.

Sasa sikiliza. Wakati sisi tunafanya makongamano hayo ya aibu, au ya kijinga katika majimbo yetu, parokia zetu na mitaa yetu, wenzetu Wamarekani, Wazungu na Waasia wanafanya makongamano ya haiba, ya kujipanga kiutu uzima, ya kiuchumi.

Nakukumbusheni. Tumesikia habari, kwa mfano, ya Kongamano la Kiuchumi la Singra-La, Kongomano la Kiuchumi la St. Petersburg, Kongamano la Kiuchumi la Qatar, Mkutano wa G7, Mkutano wa G20 na kadhalika.

Wenzetu wanajikusanya katika makongamono hayo wapange namna ya kufanya biashara kati ya nchi zao, makampuni yao yajulishane fursa za uwekezaji mitaji yao, jinsi ya kufanya biashara na nchi maskini za Afrika na Amareka ya Kusini, jinsi ya kutengeneza ajira kwa watu wao na jinsi ya mabilionea wao kuingia katika kushamirisha huduma za jamii kama elimu, afya na mahitaji kama umeme na gesi na mafuta.
Sasa hebu linganisha na makongamano ya kwetu. Ya wenzetu ni ya akili tupu, ubongo unatumika na suluhu zitakuwa zenye mapato ya kweli na ya kudumu. Kinyume chake, sisi tunaishia kudumazana na kulialia kama watoto wanywa uji wa chekechea. Je, hapo tupo sawa nao kweli? Mwogope Mungu, useme ukweli!

Sababu za Matatizo Yetu
Chanzo cha makongamano yetu ni ya aibu. Ni sababu za matatizo yetu tulizokosea. Eti sisi tumejiaminisha kwamba sababu ya matatizo yetu ni kurogwa, laana, mikosi, mapepo, majini na kadhalika. Jamani hizi ni sababu za kitoto, za kitaahira, za kujidumaza, za mtu kuwa chini ya viwango vya kuwa sura na mfano wa Mungu. Yaani ni sababu za chini ya mtu. Kinyume chetu ni wenzetu. Wenzetu huishi kwa utafiti na kujijali na kujihesabu kama wenye uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi hata magumu kabisa. Wenzetu wanajisikia kuwa “makamu wa Mungu” wakati sisi tunajiona kama hayawani fulani tu (Zab 8:3-8). Kutokana na kujitambua kwao, wenzetu wamekataa sababu za matatizo yao kuwa kurogwa, laana, mikosi, mapepo, majini na kadhalika. Katika kuyasoma mazingira na kutafiti wenzetu wameona sababu za matatizo yao ni pamoja na kutindikiwa rasilimali, mabadiliko ya tabia nchi, elimu isiyotosheleza mahitaji ya kisasa, teknolojia ndogo na magonjwa tandavu kama saratani na COVID -19. Kinyume chao, sisi ndiyo hizo sababu za kijinga.

Tunadai Tunajua hata Pasipo Utafiti
Kwa bahati mbaya, Waafrika hatufanyi utafiti kujua sababu halisi ya matatizo yetu isipokuwa tunarukia majawabu kumbakumba: kurogwa, laana, mikosi, mapepo, majini na kadhalika. Kwa huruma, hapo mwaka 2009, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alitusaidia kutufahamisha moja ya sababu ya uduni wetu na akatupendekezea suluhu baada ya Sinodi II ya Afrika. Ajabu lakini, pamoja na msaada huo, hatutilii maanani alichosema na wengi sana wala hatuna habari na alituambia. Ni hivi, katika jukumu lake la kutuchunga hata Waafrika Baba Mtakatifu Benedikto XVI alituandikia akidokeza imani katika uchawi kati ya sababu zinazotudumaza akisema:
“Uchawi, ambao msingi wake ni dini za jadi, kwa hivi karibuni hutiwa tena nguvu. Woga wa zamani unaibuka tena na unatengeneza pingu poozeshi za kutojiamni. Wasiwasi kuhusu afya, ustawi, watoto, hali ya hewa, na kujikinga na pepo wabaya mara nyingine husababisha watu kukimbilia kwenye mazoezi fulani ya dini za jadi za Kiafrika ambayo hayapatani na mafundisho ya Kikristo. Tatizo la ‘kujisajili kuwili’ – kwenye Ukristo na kwenye dini za jadi za Kiafrika – linabaki ni changamoto. Kwa njia ya katekesi na utamadunisho wa kina, Kanisa huko Afrika linahitaji kuwasaidia watu kugundua ukamilifu wa tunu za Injili. Ni muhimu kuweka wazi maana ya kina ya mazoezi haya ya ushirikina kwa kuainisha mambo mengi ya kiteolojia, kijamii na kiuchungaji yanayohusu janga hili” (Africae Munus 93).

Mzigo wa Suluhu za Ovyo
Wataalamu wanasema, “Wrong diagnosis, wrong prescription”, yaani “Ubainishaji ugonjwa uliokosewa, utoaji dawa uliokosewa.” Tunavyong’ang’ania sisi ni suluhu za ovyo tu. Kwa kuwa tulishakosea sababu ya matatizo yetu, tunachong’ang’ania kama suluhu ni bure: eti kwenda kwa waganga wa kienyeji, kwenda kwa wachungji na manabii, kufanya makongamano ya Roho Mtakatifu, maombi kwa Mungu na kwenda kuomba nchi za nje.

Tunakwenda kwa waganga wa kienyeji watusaidie kupata mali, kupata ajira na kuponywa maradhi yetu. Wao, kama wajinga wenzetu, wanatupatia hirizi na kututoza mbuzi, kuku, ng’ombe na pesa taslimu. Wanatufilisi ndiyo maana sisi tunabaki pale pale. Hawajui chochote hao ndiyo maana hawana tofauti na sisi wenyewe. Sisi maskini na wagonjwa kama wao pia. Hayupo aliyempita mwenzake hasa, hali yetu moja tu.

Tukitoka kwa waganga wa kienyeji, tunakwenda kwa wachungaji, manabii na mitume watuombee. Tunaombewa kwa sauti za kupasua anga, tunapigwa mateke ya upako, tunanyweshwa maji waliyooga wao, tunanunulishwa chumvi za upako, maji ya upako, chupi za upako, kunyonywa matiti, “kujambiwa ushuzi” na kadhalika eti tupate utajiri na matatizo yetu yakome. Wajinga sisi!

Tukitoka hapo, kila mwaka tunatengeneza “Makongamano eti ya Roho Mtakatifu” eti tumwombe Mungu tupate ajira, majumba, pesa, visa za kwenda Marekani au Ulaya na kadhalika. Hapo napo tunafanyiana mambo ya kitoto kutoana pepo, kuwingana majini, kukata mizizi ya laana na kadhalika. Papo hapo tunamtania Mungu, tukisali, kufunga na kukesha, kukemea, kupayuka payuka na kadhalika. Jamani, haya tunayong’ang’ania ni mambo ya kitoto ndiyo kisa hayatutatulii lolote; maradhi yapo pale pale, kukosa ajira kuko pale pale, ufukara upo pale pale. Ndiyo kisa wagonjwa wetu wapo pale pale. Ukosefu wa ajira unaendelea. Umaskini unaendelea na kadhalika. Mkinibisha niambieni kwa takwimu tangu shughuli za makongamano ya Wapentekoste, Walokole na Karismatiki zianze ni ajira ngapi zilizopatikana nchini? Mbona maelfu wanatafuta ajira bado? Au tuseme, kwa mfano, je, Karismatiki wetu wote wana ajira? “Wanaowabomu” pesa watu si wao pia? Wagonjwa wangapi waliopona, Karismatiki wenyewe hawaumwi? Hivi hawapo pamoja nasi katika foleni za hospitalini? Viwete wangapi wanaotembea? Bubu wangapi wanaosema? Viziwi wangapi wanaosikia? Wakoma wangapi waliotakaswa? Wafu wangapi waliofufuliwa? Bila shaka hakuna. Kama wapo, ni wa kuwasingizia kwa usanii tu. Ni aibu! Ndiyo maana hata “wajanja na mabingwa wa miujiza” waliokuwa wanatudanganya wenzao kwamba wana uwezo wa kutufanyia miujiza wengine wamekufa, wamezikwa na wameoza makaburini mwao. Wenzao wala hawakuwaponya wasife na hata walipokufa hawakuwafufua. Je, niwataje kwa majina? Orodha yao ninayo hapa mezani pangu.

Kulia ndiyo kutia uchafu wa kunuka sebuleni kwetu Waafrika. Ni aibu kubwa. Wanaume wazima wanatumaini kulia kutatulia matatizo yetu! Akina mama wetu wazima wanatumaini kulia kutatulia matatizo yetu. Vijana wazima wanatumaini kulia kutatulia matatizo yetu. Ndipo basi watoto wetu watakuwa malofa hivyo hivyo maana mtoto wa kakakuona ni kakakuona. Hii ni aibu kubwa kabisa kwa bara letu. Hivi bara gani lingine duniani ambalo watu wazima wanalia ili kutatua matatizo yao, kama si Afrika peke yake? Hivi ni watu wa ngozi gani nyingine duniani ambao watu wazima wake wanalia ili kutatua matatizo yao kama si watu weusi na machotara wetu? Hivi watu gani wengine wanaomtwisha Mungu kazi ya kuwatunza na kuwalisha kama ndege kama si watu weusi na machotara wetu? Ndipo aibu hii ni ya hapa Afrika, Kusini mwa Sahara, na Amerika ya Kaskazini na Kusini walipo jamaa zetu weusi na vizalia vyetu. Ni aibu kweli kweli. Ndiyo maana wasiotutakia mema wanatuona sisi nusu masokwe au chimpanzee. Unadhani wanatuonea? Hapana. Tunayayoyatenda kwenye makongamano yetu ndiyo yanayotustahilisha kutukanwa huko. Hebu tuamkeni jamani!

Mzee wetu Pd. Titus Amigu
 
(sehemu 2)

Wenzetu hawajikusanyi eti walie. Akili yao inakataa kabisa. Wenzetu wanakabiliana na matatizo yao ana kwa ana tofauti na sisi. Historia yao yote inasema hivyo. Nawakumbusheni. Wenzetu walipopata tatizo la malighafi walikaa chini, wakaamua watukamate watufanye watumwa tuwazalishie pamba, sukari na kadhalika bure. Walitukamata utumwa takribani miaka 341 (yaani rasmi tangu 1526 mpaka 1867), wakituvusha Bahari ya Atlantiki na kutushusha kwanza huko Brazili kabla ya kutawanyishiwa sehemu zingine. Ukiwaona watu weusi huko Amerika ya Kaskazini na Kusini ujue ndio vizalia vyetu. Katika udhalili wetu walitukamata watumwa milioni 12.5 lakini walioweza kufika Amerika walikuwa milioni 10.7, kwa maana kwamba wenzetu milioni 1.8 walikufa wakisafirishwa. R.I.P. Amen.
Kwa upande wa Bahari ya Hindi, Waarabu nao wakatukamata na kutuuza utumwani, kama samaki, tangu mwaka 1861 hadi 1895, mamilioni mengine tukawa wahanga pia. Tukawazalishia karafuu na nazi zao na tukawafanyia kazi za majumbani mwao kwa vipigo.

Baadaye kwa miezi mitatu na nusu (yaani tangu 15.11.1884 – 26.2.1885), Wazungu wakakaa chini, kwenye Mkutano wa Berlin, wakagawana bara letu na kisha wakaja kututawala mchana kweupe. Leo wenzetu wanakaa makongamano na kupangia mikakati jinsi ya kulifanya bara letu na jinsi ya kutufanya sisi wenyewe. Eti wenyewe hatuna habari! Yaani mambo ni kama vile mfuga kuku anavyokaa na mkewe au mumewe na kupitisha maamuzi jinsi ya kulitenda banda na kuku wake pia. Tusidanganyike! Yaani hata tuwasikie wakipigana Marekani, NATO na Ukraine dhidi ya Urusi, akili yao haijapotea katika kulitumia bara letu na kututumia sisi kutatulia matatizo yao. Nisikilize tena. Katika matatizo yao yoyote, wenzetu kanuni yao ni hii: “AFRICA MUST BE PART OF THE SOLUTION” yaani “AFRIKA LAZIMA IWE SEHEMU YA SULUHISHO” lao. Haya bwana, sisi tulazane tu usingizi wetu wa pono kwenye makongamano yetu ya aibu! Haya tuendelee tu na akili yetu ya Kinjikitile!

Kuna methali ya kale isemayo, “Aliyelala usimwamshe, ukimwamsha utalala wewe.” Basi, kumbe wenzetu wakijua kwamba sisi tunachukua hatua za kitoto katika kutatua matatizo yetu, hatuwaoni Wahindi wala Wazungu wa kweli kwenye makongamano yetu. Wanatuachia wenyewe ujinga wetu. Wanatuachia wenye ulofa wetu. Wanatuacha tuendelee kudumazana kwa akili yetu ya Kinjikitile. Narudia. Wenzetu walishagundua tangu karne 6 zilizopita kwamba suluhu za matatizo yao ni elimu, sala na kazi ndiyo maana walijitoma katika mradi wa kuvumbua dunia na walipotukuta Waafrika tumelala, kwanza wakatufanya watumwa na kisha kututawala kwa ukoloni. Na hata sasa tulipopata uhuru wa bendera wanaendelea kututawala kwa ukoloni mambo leo huku wakihodhi teknolojia yote. Wametukanyaga.
Nahoji mambo. Maombi kwa Mungu ndiyo hivyo tena hadi tunamchosha. Watu weusi tunamwomba Mungu kila kitu tena pasipo kujali alichotuambia na wala alichotujalia. Yeye alisema tufanye kazi siku sita huku tukitumia rasilmali na utajiri aliotupatia barani mwetu na siku moja tushike kitakatifu kwa ajili yake. Sisi watu weusi na machotara wetu tunamgeuzia Mungu mambo; tunamwomba kwa siku sita katika juma na kufanya kazi labda siku moja kwa juma. Papo hapo kile alichotupatia hatukitumii alivyokusudia yeye: maji mazuri, maziwa, bahari, madini, ardhi yenye rutuba, hali ya hewa nzuri na kadhalika. yaani sisi tunakuwa kama nyani ambao ukiwapa dola elfu moja na ndizi watachagua ndizi. Mungu hawezi kutujali kwa namna hii maana tumekuwa wapuuzi wa kupuuzwa.
Mahali pengine, Mungu alisema tufanye kazi kisha tumwombe athibitishe kazi ya mikono yetu (Zab 90:17). Sisi hatufanyi hivyo. Badala yake tunaitisha makongamano ya aibu na kwenda mbele yake bila ripoti ya kazi yoyote na kumwomba eti atubariki tu. Hapo tena Mungu hawezi kutujali wajinga siye. Basi, katika ufurufuru huu, Waafrika tunamwomba Mungu makanisani na majumbani mwetu na tunapomwona hatujibu tunamfokea na kumpazia sauti kana kwamba yeye ni punguani na kiziwi. Wapi na wapi! Ndiyo maana katika kumlazimisha atusikilize tunabweka kinyume kabisa na tulivyoagizwa katika Mt 6:5-8 ambapo Yesu alituasa mchana kweupe akisema:

“Mnaposali, msifanye kama wanafiki, wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli, nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango kisha umwombe Baba yako asiyeonekana.Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza. Mnaposali msipayuke payuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza atikwa sababu ya maneno mengi. Msiwaaige hao, Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba” (Mt 6:5-8).

Eti jamani nukuu hii haisemi kitu kwetu? Yaani haisemi chochote kabisa kwetu? Basi, sisi kweli tunatumikishwa na Shetani! Maana ni mtu anayeongozwa na Shetani tu asiyeweza kuelewa wala kujali kilichoandikwa hapa. Aliyevishwa miwani ya mbao na Shetani peke yake hawezi kuona kilichoandikwa hapa. Kauli iliyo wazi kabisa kama hii eti sisi tunaisigina huku tukitaka atusikie katika mafuriko ya maombi na maombezi yetu! Wapi na wapi! Sikiliza. Mimi niliye mwalimu wa kawaida tu hapa nakasirika, je mwenyewe Yesu aliyesema haya? Ndipo nina uhakika, Mungu anaipika dawa yetu, atuoneshe cha mtema kuni kilichomtoa kanga manyoya mwishoni mwa maisha haya. Dawa yetu inachemka. Kwa hili nina hakika ya 100%.

Waafrika Wamoja, Hatuvai Mbili
Acha nihitimishe sasa. Je, Waafrika tunaweza kujikwamua katika utoto wetu? Hivi tunaweza kujitoa huko nyuma tunakopelekana kwa makongamano yetu ya aibu au ya kijinga? Kwa kweli mwenzenu nina mashaka makubwa, maana naona dini na elimu siyo msaada kwetu. Dini na elimu si msaada kabisa. Naona havichangii chochote kwenye mabadiliko chanya ambayo Waafrika na machotara wetu tunahitaji. Sisi dini tumeivaa kama koti tu na hali kadhalika elimu tunakariri tu. Ni kweli tumepokea Ukristo miaka mia kitu iliyopita na hali kadhalika elimu. Lakini kwa jinsi mambo yanavyokwenda halijojo sasa, dini zimetangulia mbele kutudumaza waafrika kwa akili za Kinjikitile na kutubwetekesha katika maombi, kufunga na kusali kwa kishamba. Hivi tunafikiaje fikra ya kutatua matatizo ya umaskini, maradhi na ujinga kwa ujinga? Katika hili, mwenzenu nakata tamaa. Kama dini ilitaka kutuvisha nguo ya sikukuu sisi tunaikataa kimtindo. Inaonekana panapotufaa sisi ni pale pale Ukristo ulipotukuta. Kifupi, inaonekana sisi ni watu wa moja tusioweza kuvaa mbili.

Katika elimu, mambo ni hivyo hivyo ovyo. Elimu ya Kizungu inaonekana kuwa mzigo tu. Nakufikirisheni kidogo. Wewe sikiliza, tuna waalimu wakubwa, madaktari na maprofesa, lakini tupo pale pale na wao wanatembelea akili ile ile ya zamani na hofu zile zile za makabila yao. Ndiposa hospitali zetu ni hoehae. Hazina lolote isipokuwa taasisi kubwa zisizojimudu bali kukaa na kusubiri teknolojia na dawa za kuagiza kutoka Ulaya, Marekani na Asia. Ashakum si matusi, shule na vyuo vyetu ni mikusanyiko mikubwa ya watu wenye kukomea kukariri na kurudia mambo ya wengine tu. Ndiyo maana si ajabu kabisa kusikia mambo ya aibu kitaaluma. Mambo ni sege msege. Ni aibu tu. Ndiyo maana vyuo vikuu vingine badala ya kuchuchumia teknolojia za kisasa zinatafakari jinsi ya kurudi nyuma na kuanzisha vitivyo vya kufundisha imani za uchawi. Nasema tena, ni aibu kwetu.
Sasa hebu nimalizie kwa ashakum si matusi ya pili. Katika dini, tuna masheikh, wachungaji, manabii, maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa na walei lakini hakuna chochote. Badala ya wataalamu, manabii, mitume, masheikh na makleri kuwa walau chongo mbele ya vipofu inaonekana wanakuwa vile vile vipofu na tena waliolala. Pole, simtukani mtu. Kwani kwenye makongamano yetu ya aibu hawahudhurii walimu, madaktari, maprofesa, maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa na walei? Wanaoendesha makongamano hayo ni nani? Si manabii, mitume, maaskofu na mapadre, watawa na walei? Basi, ninalosema si uongo: Sisi Waafrika wamoja, hatuvai mbili sisi.

Mhutasari wa Hoja Yangu
Naomba niseme kwa jedwali dogo. Poa moto, ukilitazama vizuri utaelewa linasema nini. Li rahisi sana.

MUNGU MKUU
Kawaumba wanadamu wote kwa mfano na sura yake akiwapa akili na utashi pamoja na ardhi na rasilmali zake bora (Mwa 1:26-28)

WAAFRIKA
Kufanya makongamano ya kukesha, kufunga kavu, kulialia, kuanguka anguka, kuweweseka, kugaragara chini, kutoana laana, kukata miti ya ukoo, kupungana mapepo, “kutoana majini”, kukemea umaskini na nguvu za giza na kutumainishana kupata ndoa, mali, magari, ajira na utajiri kwa maneno

WANADAMU WENGINE
Kufanya makongamano ya kupanga mikakati ya kazi, kisayansi, kiakili, kutaaluma na kiteknolojia kwa kutumia rasilimali watu na vitu

Nadhani picha hii inaeleweka kwako msomaji wangu. Sasa niambie, kutokana na picha hii, kwa nini Waafrika tusiitwe wajinga? Kwa nini Waafrika tusiwe maskini wa mwisho? Kwa nini Waafrika tusiandamwe na maradhi yote? Kwa nini Waafrika tusiwe watu wa daraja la chini? Kwa nini Waafrika tusiwe na hatia mbele ya Mungu?

Kwa nini wanaoendekeza makongamano ya Kiafrika wasitambuliwe kama maadui wa Waafrika?
Kwa nini watu wanaoendekeza makongamano ya aibu tusiwakemee? Kwa nini tusiwaonye kama watu wanaojidumaza wenyewe na wenzao pia?
Nipeni hoja kwa nini makongamano yetu si ya aibu. La sivyo, tuamkeni hima!

Mzee wetu Pd. Titus Amigu
 
Back
Top Bottom