Mahusiano ya Tanzania na Marekani

mr mkiki

JF-Expert Member
Sep 22, 2016
5,583
11,659
Baada ya ubalozi wa Marekani kutoa taarifa ya kuguswa na hali ya mbinyo wa demokrasia nchini, nimeona vema tufahamu kwa kiasi fulani, mahusiano yetu na Marekani. Hii ni sehemu ya kwanza.

Agosti mwaka huu wa 2018 ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa tamko la kuguswa (Statement of concerns) kuhusu chaguzi ndogo za marudio zinazoendelea nchini. Kuna mambo kadhaa ambayo Marekani kupitia ubalozi wake wa Tanzania wameyataja kama mambo yanayokiuka misingi ya demokrasia.

Moja ni kitendo cha mamlaka ya tume ya taifa ya uchaguzi kukataa kuwasajili wagombea wa upinzani, na kupelekea wagombea wengi wa CCM kupita bila kupingwa.
Pili ni vitendo vya uonevu vilivyofanywa na jeshi la polisi dhidi ya wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa isipokuwa CCM.
Tatu ni vitendo vya kuwanyima wapinzani nafasi ya kufanya siasa kwa uhuru kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, kuwakamata na kuwatia nguvuni bila sababu za msingi.
Tamko hilo linaongeza kwamba vitendo hivyo tajwa vinakiuka haki za msingi za kikatiba kwa raia wa Tanzania, na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi na maeneo jirani.

Kabla ya tamko hilo la ubalozi wa Marekani, Seneta anayewakilisha jimbo la New Jersey, Bw. Robert Mendes alipeleka hoja katika bunge la Marekani (Congress) kuhusu vitendo vinavyokiuka misingi ya demokrasia nchini Tanzania, na kupendekeza mabadiliko ya nafasi ya balozi wa Marekani nchini Tanzania. Katika hoja yake hiyo, Mendes alitaja vitendo kadhaa vinavyoashiria kubinywa kwa demokrasia, na kuongeza kuwa nafasi ya ubalozi nchini Tanzania ipo ‘tupu’.
Huku nchini, Tume ya taifa ya uchaguzi, imejikosha kwa kutaka Ubalozi wa Marekani uthibitishe madai hayo, na kwamba ueleze ni kwa namna gani taarifa za ‘uovu’ wa tume hiyo zimefika ubalozi wa Marekani.
Wasichokijua, au wanachojifanya kutokujua watu wa Tume ya taifa ya uchaguzi ni kwamba, Marekani hawashindwi kujua wanachotaka kujua ndani ya Tanzania. Rostam Azizi, aliyewahi kuwa mweka hazina wa CCM, na mwezeshaji wa kupatikana kwa Urais wa Jakaya Kikwete, anatajwa kuwa wakala wa CIA aliyewezesha kupatikana kwa siri nyeti za nchi na kuzifikisha kwa Wamarekani. Katika serikali iliyosheheni wasakatonge kama Tanzania, si jambo la ajabu kuwapo kwa viongozi wengi wanaovujisha siri za nchi kwa mataifa ya nje, ili “kujipatia riziki”. Ni ujinga kuhoji namna Marekani wanavyoweza kupata taarifa za chaguzi ndani ya nchi yoyote duniani. Raia wote wa marekani wanapotembelea nchi zingine, hupatiwa taarifa kutoka katika balozi zao juu ya hali ya nchi wanayotembelea, mahali wanapotakiwa kufikia, hoteli za kutumia, mitaa ya kuishi na mitaa wanayopaswa kuepuka nk. Wanapataje taarifa za maeneo hayo?

Maswali ambayo watu wengi wanaweza kujiuliza ni Je! Kwanini Marekani? Kwanini Marekani watoe tamko la kuguswa na mbinyo wa demokrasia ndani ya Tanzania? Wao ni nani? Tanzania inawahusu nini? Kwanini isiwe Sweden, Norway, Kenya, au India? Kwanini Wachina wasitoe tamko lenye mtazamo kinzani na tume ya uchaguzi?

Ukiwaulliza watu kwanini Marekani inaingilia mambo ya nchi zingine, wengi watajaribu kuhusisha Marekani na ubeberu, ubabe na uonevu. Majibu ya hivi yanaweza kuwa habari tu, lakini si lazima yawe sahihi. Ni vema kujua kuwa Marekani sio mtu, bali ni Taifa lenye watu wengi wenye maono, chimbuko, itikadi, maslahi na mambo mengi tofauti. Isipokuwa, tofauti zote hizo zinakusanywa katika lengo moja, kuifanya marekani kuwa Taifa kubwa kiuchumi na kijeshi duniani. Lengo moja tu.
Tofauti za kimtazamo haziwafanyi wamarekani kusahau lengo lao moja na kuu. Kwahiyo, ikitokea chombo kingine huko Marekani kikasifu amani na utulivu ndani ya Tanzania, na kupongeza juhudi za viongozi wa Tanzania katika kuboresha demokrasia, tusishangae. Mitazamo yao tofauti, lakini lengo moja, sisi ambao hatujielewi, tutaendelea kuchinjana wenyewe kwa wenyewe.

Kuna msemo mmoja maarufu unaoweza kutetea hoja hii ya wamarekani kuingilia mambo ya nchi zingine; “Injustice anywhere is a threat to justice everywhere” (Ukiukwaji haki popote duniani ni hatari kwa haki duniani kote). Yapo matukio mengi yanayoweza kutetea kauli hii, mfano moja; mauaji ya mfalme wa Austria, Franz Ferdinand, mnamo mwaka 1914 yalipelekea moja kwa moja kuibuka kwa vita vya kwanza vya dunia, baina ya Ujerumani na marafiki zake, dhidi ya Uingereza na Marafiki zake. Mauaji ya Franz Ferdinand hayakuwa na lengo la kuibua vita ya dunia. Mauaji hayakufanyika Ujerumani wala Uingereza, lakini si tu Ujeruimani na Uingereza walipoteza watu wengi na mali nyingi, bali hata Afrika, ilipoteza watu wengi waliokufa kwa kupigania Wakoloni. “Injustice anywhere is a threat to justice everywhere, a threat to peace and tranquility everywhere”. Hiyo ni sababu moja inayofanya wamarekani wakemee mambo wanayoona hayafai hata kama yanafanyika katika nchi zingine, kwa sababu mambo hayo yanaweza kusambaa mahali pengine duniani na kuharibu hali ya usalama na amani. Panapo amani na utulivu, ndipo Marekani anaweza kutawala kwa kushawishi, hadi hapo atakaposhindwa kushawishi ndipo anaweza kuruhusu kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo husika.

Hata hivyo, ni vigumu kujua kama Ubalozi wa Marekani unakemea kubinywa kwa demokrasia kwa sababu za kibinadamu au kwa maslahi ya Marekani, yote yanawezekana. Vyovyote vile, kukemea uovu ni jambo sahihi.

Historia ya mahusiano ya Tanzania na Marekani.

Uhusiano rasmi wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani unaanzia mwaka 1961, wakati huo, Tanganyika ikipata uhuru. Frank Charles Carlucci, jasusi wa CIA anayetajwa kufanikisha mauaji ya waziri mkuu wa kwanza wa Congo, Patrice Lumumba, kwa amri ya Rais Dwight Eisenhower, ndiye aliyekuwa mwakilishi wa Marekani nchini Tanganyika. Carlucci anatajwa pia katika kumlaghai Rais wa Tanganyika/Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili afanikishe muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mawakala wa CIA waliofika kabla, pamoja na jasusi mwingine wa Mossad ya Israel aliyeitwa David Kimche, aliyejifanya mwandishi wa habari kutoka Uingereza, walisaidia mbinu na baadhi ya vitendea kazi kwa waswahili waliopindua utawala wa Sultan huko Zanzibar, kwa kushirikiana na Nyerere. Ndipo Frank Charles Carlucci alipokuja kumshawishi Nyerere kuanzisha muungano wa Tangannyika na Zanzibar, lengo ambalo Nyerere hakulijua lilikuwa kudhibiti wimbi la ukomunisti visiwani humo. Baada ya Mwalimu kugundua kuwa alitumiwa bila kujua, alimtimua Frank Charles Carlucci. Jasusi huyu, badaye alishika vyeo mbalimbali ikiwa ni pamoja na waziri wa Ulinzi (1987 -89), Mshauri wa masuala ya ulinzi na usalama (1986-87), Naibu waziri wa Ulinzi (1981-82), Naibu mkurugenzi wa CIA (1978-81). Frank Charles Carlucci amefariki Juni 3, 2018.

Kabla ya Muungano, Mwalimu Nyerere alikuwa rafiki mkubwa wa rais wa Marekani, wakati huo John F Kennedy (JFK). Nyerere alimtembelea JFK mnamo Julai 1963 na kuweka mikakati kadhaa ya maendeleo, kabla ya kuuawa kwa JFK Nov. 22, 1963. Moja kati ya mashirikiano ya mwanzo kati ya Tanganyika/Tanzania na Marekani ni pamoja na ‘Peace Corps’, yaliyolenga kuboresha elimu hasa upande wa sayansi na hesabu, pamoja na huduma za afya, teknolojia na utunzaji mazingira. Mahusiano mengine yalihusisha misaada ya kibinadamu kupitia USAIDS.

Lakini ghafla, baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na Nyerere kumtimua Frank Carlucci, Tanzania ikajiunga kivitendo na ukomunisti, huku Rais Nyerere akitangaza kwa maneno kutofungamana na upande wowote. Mwaka 1965, Mwalimu Nyerere aliwafukuza watumishi 300 wa ‘Peace Corps, raia wa Marekani. Hii ilikuwa ni baada ya Marekani kuilaumu Tanzania kwa kushirikiana kijeshi na Uchina. Angalau kwa miaka 10 tangu nchi nyingi za Afrika zipate uhuru, Marekani hawakuwekeza nguvu kubwa katika kupambana na Ukomunisti barani Afrika, kama walivyofanya huko Ulaya Mashariki.Hata ilipofika miaka ya 1970, Urusi na Uchina walizidi kupata nguvu zaidi ndani Afrika. Urusi ilikuwa tayari imezishika Somalia na Guinea, Huku wachina wakizishika Tanzania na Zambia. Mataifa ya Afrika kaskazini yalikuwa tayari yanajiweza, Afrika Magharibi walikuwa washirika hasa wa Ulaya, hususani Uingereza na Ufaransa. Nchi nyingi za kusini mwa Afrika hazikuwa zimepata uhuru (Zimbabwe, Angola, Namibia, Msumbiji, South Afrika*) lakini kwa sababu ya mazingira ya kisiasa katika nchi hizo, Ukomunisti ulikuwa unapiga hodi.

Marekani, pamoja na kukosa ushirikiano kutoka nchi hizo, pia haikuwa na mpango wa kutumia mikakati kamambe ya kijeshi na/au kijasusi ili kupambana na Urusi na Uchina katika maeneo ya Afrika, badala yake iliendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa faida ya baadae.

Ieleweke kwamba, Canada, kupitia mpango wake wa Canadian Armed Force Advisory and Training Team Tanzania (CAFATTT) ndio waliojenga jeshi la wananchi la Tanzania (JWTZ) kutoka katika utoto wake mwaka 1965 hadi ukomavu wake mwaka 1970. Canada iliandaa pia majeshi ya Ghana (1961 – 68), Zambia (1965) na Nigeria (1963/68-70). Ujenzi wa jeshi la Tanzania na Ghana ulikuwa wa kimkakati zaidi, tofauti na Zambia na Nigeria ambapo kulikuwa na hali za dharura. Lengo la Canada lilikuwa kupata msaada wa kijeshi kutoka Afrika ili kupambana na Sovieti (Urusi) na Uchina endapo vita baridi ingebadilika na kuwa moto, vita kuu ya tatu ya dunia. Vyombo vya Kijeshi vya Urusi na China viliisumbua Canada ndani ya Tanzania kwa michezo yao ya vita baridi, kitendo kilichopelekea Canada kusalimu amri na kuondoka mwaka 1970. Mpango wa kuifanya Tanzania kuwa mshirika wa Magharibi ukashindwa. Hiyo ilikuwa sababu ya nyongeza ya Marekani kushindwa kushirikiana na Tanzania katika eneo la ulinzi na usalama. Hata hivyo mahusiano mengine yaliendelea ingawa kwa kusuasua. Wakati huo Canada ikipunguza mashirikiano ya kijeshi, ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kuwa kambi la vikundi vya ukombozi kusini mwa Afrika, huku Urusi na Uchina wakitoa msaada mkubwa wa kijeshi.

Miaka ya 1980, Marekani kupitia USAID walifanikisha mpango wa Ugatuzi wa madaraka (Decentralization) nchini Tanzania, ili kutoa madaraka zaidi kwa umma, kama moja ya misingi ya demokrasia. Mwaka 1982 kuliibuka mgogoro wa kifedha nchini Tanzania, na kuifanya nchi kushindwa kulipa mikopo. Jambo hilo lilipelekea kusitishwa kwa huduma za USAID hadi mwaka 1987 zilipoanza tena. Wakati huo USAID ikianza kushika kasi upya, kukawa kumeibuka janga la UKIMWI. Na hapo majukumu ya USAID yakaongezeka na kujumisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Wakati wote huo, kwa sababu kuu ya vita baridi, mahusiano ya kidiplomasia yalikuwa ya kusuasua, mahusiano ya kijeshi ni kama hayakuwepo, isipokuwa tu mahusiano ya kijamii (elimu, afya, kilimo na biashara)
Vita Baridi iliisha mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya uchumi wa Sovieti kuparanganyika. Na huo ukawa mwisho wa ukomunisti.

Mahusiano ya kijeshi, ulinzi na usalama baina ya Tanzania na Marekani yaliibuka kana kwamba yalikuwa yamefichwa, mnamo Agosti 7, 1998 baada ya kulipuliwa kwa balozi za Marekani mjini Dar ES Salaam na Nairobi.
Itaendelea....

mr mkiki.
FB_IMG_1534854844537.jpg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kifupi katika nchi ambazo hazipo consistent kwenye diplomacy ya kimataifa marekani ni namba moja.Toka tupate Uhuru more than 50 years ago rafiki ambaye ni consistent kwa Tanzania na Africa wa kwanza ni Mchina wa pili mjapani Na Toyota zake.The most inconsistent and unreliable in long term on international relationship ni mmarekani.China and Japan don't change colors like Americans depending on weather.Anyway China business and Japanese vehicles will continue to dominate Africa because they are reliable consistent friends of Africa and Tanzania come rain come sunshine. Waafrika kimila Na kitabia hupenda long term relationship kwenye friendship mchina Na mjapani ndio pekee wanaielewa Africa Na Tanzania.
 
Asante mleta uzi, nimejua mambo kadhaa ambayo sikuyajua kabla. Na nyie mnaoletaga thread za kipuuzi humu mjifunze kuleta mambo ya maana kama haya. Hasa nyie watumishi wa Lumumba, mnashusha hadhi ya jukwaa.
 
Back
Top Bottom