Maharage: Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unaelekea kufikia 91%, matarajio ya kuanza kuzalisha umeme ni Juni 2024

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
1.JPG

Sehemu ya Mradi wa JNHPP katika Tuta Kuu ambapo ujenzi unaendelea.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya ukaguzi na tathmini ya Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (The Julius Nyerere Hydropower Project - JNHPP) uliopo Rufiji.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo uliofanyika Ijumaa Agosti 25, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema kwanza maendeleo ya Mradi ni kuwa hadi Julai 2023 ujenzi wake ulikuwa 90.19% na wanatarajia hadi utakapomalizika mwezi Agosti 2023 mradi utakuwa umefikia 91%.

Ameweka wazi kuwa tayari mchakato wa kuwapeleka Watumishi wa TANESCO kwa ajili ya kujifunza kuendesha mradi huo unaendelea.
3.JPG

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande akifafanua jambo mara baada ya kufanya ukaguzi kwenye Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere.

2.JPG

Moja ya eneo lenye mitambo katika Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Amesema dalili za awali zinaonesha matarajio ya kuanza kuzalisha umeme hatua ya awali ni Juni 2024, kwa kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kufunga mitambo ambayo inaendelea vizuri.

Amesema “Mwaka jana (2022) mahitaji ya juu kabisa ya umeme Nchini yalikuwa ni Megawatt 1,354 lakini hadi kufikia Agosti 17, 2023 tumeweka rekodi ya kufikia mahitaji ya juu kuwa Megawatt 1,482.7, hiyo inaonesha ongezeko la mahitaji ya juu ni zaidi ya Megawatt 100,” amesema Maharage na kuongeza:

“Hivyo, kuna mashindano makubwa ya kutumia umeme, yanaongezeka kutokana na shughuli za uchumi, nasi tunashindana kuongeza umeme zaidi ili kuendana kukidhi mahitaji ya uchumi, inamaanisha ukamilikaji wa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utatuwezesha kuendana na kasi iliyopo.

“Tunaimani ukamilikaji wa Mradi utatuwezesha kukidhi mahitaji ya uchumi na inawezekana ikawa mwisho wa upungufu wa umeme Nchini.”
5.JPG

Mafundi wakiendelea na ujenzi eneo la mradi.

Aidha, amesema changamoto mbalimbali zipo lakini timu ya TANESCO inaendelea kupambana nazo kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.

Amesema kuwa mpaka Agosti 25, 2023 ujazo wa maji kwenye Bwawa umefikia kwenye Mita 164.6 wakati na maji yanayotosha kuzalisha umeme ni Mita 163.

Ameongeza “Leo kama tungekuwa tumekamilisha kufunga mashine inamaanisha tungeweza kuanza kuzalisha umeme, pia itambulike kuwa Bwawa hili kimo chake ni Mita 190 lakini operation level ni 184.”

MVUA ZA VULI ZINAZOTARAJIWA
Amesema ikiwa mvua zitanyesha kama zinazotarajiwa bwawa litajaa mapema zaidi ya kipindi walichotegemea, pia kama mvua zitakuwa kubwa zaidi wamejipanga kuhakikisha hakuna kitu kinachoharibika.

Amedadavua kuwa Bwawa la Julius Nyerere linahifadhi maji zaidi ya Lita Bilioni 30 na litakuwa msaada mkubwa katika uzalishaji, kwa kuwa pia lina uwezo wa kuhimili muda mrefu kuzalisha umeme bila kuwa na mvua tofauti na vyanzo vingine.
6.JPG

Mratibu wa Mradi wa JNHPP, Mhandisi John Skauki (katikati) akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Menejinenti ya TANESCO, Mhandisi Aboubakar Issa (kulia) na Mhandisi Decklan Mhaiki walipotembelea mradi huo.

KUHUSU BEI BAADA YA MRADI KUKAMILIKA
Maharage amesema “Wakati huu Watanzania na wateja wetu wanahitaji kujua bwawa linakwendaje, pia sisi umakini na Mawazo ni katika kumaliza Mradi, kuhusu bei ni masuala ya mazungumzo, kwa sasa tunaelekeza nguvu kwenye ujenzi kwanza."

VIFAA KWENYE MRADI
Maharage ameeleza matarajio yao ni kuwa kufikia Desemba 2023, vifaa vyote vitakuwa vimefika sehemu ya mradi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.
4.JPG

Ujumbe uliotembelea Mradi wa JNHPP, Agosti 25, 2023

WATUMISHI WA TANESCO WAELEKEA KWENYE MRADI
“Ili mradi uweze kufanya kazi unahitaji Wafanyakazi 221 ambao wanapelekwa kwa makundi kulingana na umuhimu wa uhitaji wao, mfano kuna ongezeko la Watumishi 20 waliojiunga hivi karibuni na wenzao kadhaa ambao tayari wapo katika mradi.

“Kundi la Watumishi lililofika linahusu zaidi umeme wa mitambo kwa kuwa ili mradi uendelee kuna uendeshaji unaotakiwa kufanyika wa mitambo, baadaye wataanza kuja watu wa idara nyingine.”
7.JPG

Wajumbe waliotembelea Mradi wa JNHPP, Agosti 25, 2023
 
Nikikumbuka zile sarakasi za kuzinduliwa kwa safari za SGR, ninapata ukakasi wa kuamini huo mradi utakamilika kwa wakati.
 
Back
Top Bottom