Magereza watorokwa na mfungwa, mahubusu 12

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125








headline_bullet.jpg
Askari wao aua raia kwa risasi

wafungwa.jpg

Wafungwa


Uzembe wa askari katika Gereza la Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga, umesababisha mfungwa mmoja na mahabusu 12 kutoroka.

Kufuatila tukio hilo, kikosi maalum cha kuzuia uhalifu kutoka Dar es Salaam kimewasili mkoani Tanga kufanya msako mkali wa kuwatafuta katika vijiji vya wilayani Lushoto.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mkuu wa Magereza mkoani Tanga, Editha Mallya, alisema tukio hilo lilitokea Juni 11, mwaka huu majira ya usiku katika gereza la Wilaya ya Lushoto.

Mallya alisema mfungwa huyo na wenzake ambao hakuwa tayari kuwataja majina, walifanikiwa kutoroka baada ya kuvunja ukuta wa choo cha gereza hilo.

Hata hivyo, Mallya, hakueleza walivyoweza kuvunja gereza hilo na kutoroka wakati taratibu zinataka kuwepo na askari Magereza kwa ajili ya kulinda mahabusu na wafungwa wasitoroke.

Pia, Mallya hakueleza ni hatua zipi zimechukuliwa dhidi ya askari waliokuwa wamepangiwa kulinda siku hiyo.

Alitaja makosa yaliyokuwa yakiwakabili mahabusu hao na mfungwa mmoja kuwa ni ya mauaji na kwamba baadhi yao walitakiwa kufikishwa mahakamani jana ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

“Ni kweli tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Jumatatu, lakini mpaka sasa kikosi maalum kimeanza msako mkali kuhakikisha kwamba tunapata taarifa na kuwakamata wahusika hao mara moja,” alisisitiza Mallya.

Kwa mujibu wa Mallya, kikosi hicho kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani hapa kimeanza kukagua njia zote za panya ambazo zinasaidikiwa kuwa huenda wakawa wamezitumia.

Kufuatia hali hiyo, Mallya alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Lushoto na Mkoa wa Tanga kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinazohusika kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwao.

“Kila Kijiji kina uongozi wa serikali, natoa wito kwa wananchi kutupa taarifa kwani watu hawa ni wahalifu, wanaweza kuwa wamejificha maeneo ya karibu wakisubiri hali iwe shwari…asije mwananchi akamficha mtu kwenye nyumba yake kwani hili ni kosa kisheria, bora wajisalimishe mapema kwa vyombo vya dola,” alisema Mallya.

KAULI YA MWENYEKITI KAMATI YA ULINZI NA USALAMA

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Lushoto, Majid Mwanga, amesema serikali wilaya humo imeimarisha ulinzi katika maeneo yote ili kuhakikisha inawatia nguvuni mfungwa na mahabusu waliotoroka katika gereza la wilaya hiyo.

Mwanga mbaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, aliiambia NIPASHE kuwa kamati inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa inawatia mbaroni watuhumiwa hao.

“Hatujalala tangu tukio hili litokee...tumeimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya wilaya na tunawaomba wananchi wasisite kutupa taarifa iwapo wataona kuna sura tofauti kwenye jamii zao, ni imani yetu kuwa watuhumiwa hawa watapatikana,” alisema Mwanga huku akikataa kuwataja majina kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri msako.

Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wameiomba serikali kuhakikisha kuwa watoro hao wanapatikana kwa kuwa wanaweza kufanya vitendo vya uhalifu.

“Mtu ambaye alishakamatwa kwa uhalifu akafungwa au hata kama bado yupo mahabusu, lakisi ni mtuhumiwa sasa kama ametoroka huwezi kujua dhamira yake, akirudi uraiani,” alisema Bakari Zuberi, mkazi wa Lushoto.

ASKARI MAGEREZA AUA RAIA KWA RISASI


Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi Mkoani Singida linamsaka askari Magereza mmoja kwa tuhuma za kumuua fundi ujenzi wa jengo la ofisi za Magereza mkoa, baada ya kumpiga risasi kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo kisha kutokomea kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5:00 asubuhi katika eneo la Bomani, baada ya mtuhumiwa, Koplo Abdalah Kabwe (31), kumpiga risasi fundi ujenzi, Muna Abubakar (37), mkazi wa Mwenge, mjini Singida.

Kamanda Sinzumwa alisema bunduki iliyotumika kufanya mauaji hayo ni SR 1123457 ikiwa na risasi kumi.

“Bunduki hiyo ilikuwa na risasi kumi, baada ya kumpiga marehemu, aliitupa hapo hapo na kwenda zake...tulipofika eneo la tukio tuliikuta ikiwa na risasi tisa tu, ina maana alimpiga risasi hiyo moja,” alifafanua Kamanda Sinzumwa.

Hata hivyo habari zaidi kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo, zinasema kabla ya mauaji hayo, palitokea mabishano kati ya marehemu na mtuhumiwa, yaliyohitimishwa na mlio mkubwa wa bunduki.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Singida, Dk. Suleiman Charles Mutani, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa walimpokea marehemu saa nane mchana, lakini alifariki dunia nusu saa baadaye akiwa katika chumba cha upasuaji.

Dk. Mutani alisema kufuatia jeraha alilokuwa nalo marehemu, ilikuwa vigumu kupona na kufafanua kuwa licha ya kuongezewa uniti tatu za damu, hazikumsaidia kutokana na mshipa mkuu wa damu sehemu ya nyonga kukatika, hali iliyochangia damu nyingi kuvuja.

Imeandikwa na Lulu George, Dege Masoli, Tanga na Elisante John, Singida.



CHANZO: NIPASHE


 
Back
Top Bottom