Magereza, Polisi wana hali ngumu sana: Wabunge

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,320
33,125
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, amependekeza Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu wake wawekwe gerezani kwa muda wa miezi sita ili wapate uzoefu wa hali ilivyo mbaya kwenye magereza mbalimbali nchini.

Aliyasema hayo jana wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliyowasilishwa bungeni na Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi.

Filikunjombe alisema iwapo mawaziri hao watawekwa gerezani basi wawe kwenye magereza ya Ludewa ambayo yanahali mbaya sana ili wakitoka wajue hali halisi inayozungumzwa na wabunge.

Filikunjombe alisema mawaziri wa wizara hiyo kabla ya kuteuliwa wawekwe magerezani angalau kwa miezi sita hali itakayowawezesha kujua hali mbaya iliyoko magerezani na kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.

“Waziri akifungwa naomba afungwe gereza la Ludewa ili ajue mazingira magumu ya kule maana inafika wakati huwezi kutofautisha mfungwa ni yupi na askari magereza ni yupi, mheshimiwa Spika hali ni mbaya sana magerezani, sitaunga mkono hoja hii hadi nipate maelezo ya kuridhisha,” alisema.

Kuhusu Jeshi la Polisi, mbunge huyo ambaye aliwahi kufanyakazi katika jeshi hilo, alisema lina vifaa duni na halina uwezo wa kukabiliana na wahalifu ambao wanatumia teknolojia ya kisasa kutekeleza uhalifu wao.

“Nilikuwa askari nayajua fika mazingira ya jeshi hilo, hawana vifaa vya kutosha, vifaa vingi walivyo navyo ni virungu tu sasa sijui kwa ajili ya kuwapiga wanafunzi wa vyuo vikuu wanapoandamana au kuwapiga Chadema,” alisema.

Alisema ni heri kuwa na Jeshi lenye askari wachache lakini wenye tija kuliko kuwa na jeshi kubwa linalojiendesha kizamani na ambao wanashindwa kupambana na wahalifu.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema ndani ya Jeshi la Polisi kuna mtandao mkubwa wa uhalifu na ana ushahidi wa baadhi ya askari walioko kwenye mtandao huo.

Lugola ambaye alianza kwa kutangaza kutoiunga mkono bajeti hiyo, alimtaja askari Fadhil Kweka kuwa mmoja wa wanamtandao huo na amekuwa akiwasaidia majambazi kwa kuwatajia majina ya wananchi wenye silaha ili wakawapore.

Alisema udhaifu wa utendaji wa polisi unachangiwa sana na vifaa duni na kwamba angalau vifaa vingi ambavyo jeshi hilo wanavyo ni filimbi na virungu.

“Mheshimiwa Spika wahalifu ni wadau wakubwa sana wa wizara hii, hivi sasa wanasikiliza kwa makini tunapanga bajeti kiasi gani kwa ajili ya kupambana nao, wao wanajipanga kufanya uhalifu kwa teknolojiaa ya kisasa, sisi jeshi letu la filimbi na virungu hatuwezi kufika,” alisema.

Alishauri viwekwe vifaa vya kisasa zikiwemo kamera kwenye miji mikubwa ya Dar es Salaam ili askari wazitumie kuangalia mwenendo wa matukio ya uhalifu.

Wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo walieleza namna ambavyo Polisi wanafanyakazi katika mazingira magumu ikiwemo ukosefu wa nyumba za kuishi pamoja na vifaa.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom