Maeneo 9 yaliyoguswa na Sera Mpya ya Elimu Tanzania

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Baada ya mchakato wa muda mrefu hatimaye maboresho ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la 2023 yamekamilika na hatua za utekelezaji wake zitaanza mwakani na kukamilika rasmi mwaka 2027.

Novemba 2, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasilisha bungeni taarifa ya kukamilika kwa maboresho hayo ya sera sambamba na mapitio ya mitalaa kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari pamoja na vyuo vya ualimu.

Hatua hii ya uboreshaji sera na mitalaa ilianza muda mfupi baada Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani na kutoa maelekezo kuwa, kuna haja ya kuitazama upya mitalaa na kuiweka katika mfumo utakaowezesha wanafunzi kupata ujuzi.

Kama ambavyo imekuwa ikielezwa lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha mitalaa inawajengea wanafunzi ujuzi stahiki katika soko la ajira kipaumbele kikiwa mafunzo ya amali.

Kwa mujibu wa Majaliwa, kuna maeneo tisa yamefanyiwa mabadiliko katika sera hiyo ya 2014 na mabadiliko hayo yapo kwenye toleo jipya la 2023.

Elimumsingi

Maeneo yaliyoguswa ni muda wa elimu ya lazima ambapo Serikali imepitisha utakuwa miaka 10 badala ya miaka saba ya sasa. Hapa mwanafunzi atasoma elimu ya msingi kwa miaka sita na sekondari kwa miaka minne.

“Utekelezaji wa pendekezo hili utaanza kufanyika mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba, badala yake itaanza kufanyika tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari,”anasema Waziri Mkuu.

Swali la wengi ni kipi kinatangulia baada ya maboresho hayo kufanyika na Serikali kukamilisha mapitio ya Sera na mitaala kama ilivyoelezwa bungeni na Waziri Mkuu Majaliwa?

Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili Septemba mwaka huu Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda alifafanua kuwa kila mwanafunzi atasoma elimu msingi kwa miaka 10 na baada ya kumaliza kidato cha nne kutakuwa na mikondo miwili, elimu ya kawaida na mafunzo ya amali ambayo yote itakuwa na michepuo mbalimbali.

“Sasa endapo pendekezo letu litapita tutakachoanza kutekeleza mwakani ni kurudisha mkondo wa amali katika ufundi, michezo na kilimo. Haya yanaenda kufanyika katika shule ambazo zilikuwa zikitoea elimu ya ufundi na tayari tumezitembelea hizi shule na kuangalia miundombinu itakayowezesha elimu hiyo kutolewa mfano karakana.

“ Zile shule ambazo zilikuwa zinafundisha kilimo tunaenda kuzifanya rasmi shule za amali kwenye kilimo mwanafunzi akitoka pale anakuwa ameiva kwenye eneo la kilimo”.

Elimu ya amali

Mabadiliko mengine ni hatua ya kuongeza fursa ya elimu ya amali ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza kutoa fursa kwa wanafunzi kupata ujuzi katika fani mbalimbali ikiwemo kilimo, ujasiriamali, ufundi, michezo na nyinginezo.

Ualimu

Eneo lingine lililoguswa katika mabadiliko hayo ni elimu ya ualimu, sera mpya inaelekeza kuwa elimu hiyo itaanza kutolewa kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuendelea tofauti na ilivyo sasa hata wale wa kidato cha nne walikuwa na fursa ya kusomea ualimu.

Si hivyo tu katika sera mpya, suala la ubora wa walimu limeangaliwa kwa kiasi kikubwa, na kwamba mafunzo ya ualimu yatahusisha mwaka mmoja wa uangalizi baada ya kumaliza mafunzo tarajali hatua inayolenga kuwapata walimu wanaokidhi viwango.

Hatua hii itakwenda sambamba na uboreshaji wa mfumo wa ajira za walimu, wakufunzi na wahadhiri kwa kuhakikisha wenye sifa na viwango stahiki ndiyo wanaajiriwa.

Katika eneo hili Profesa Mkenda alisema hatua mojawapo ya mageuzi ni kuboresha ubora wa elimu hivyo umakini mkubwa unapaswa kufanyika katika kuwapata walimu.

“Tunaandaa walimu na kupitia mkakati huu wa mageuzi kutakuwa na mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu waliopo kazini. Ukiachana na hao waliopo kazini kwenye mapendekezo ya sera, mwalimu ataajiriwa baada ya kufanya mtihani kama ilivyo kwa kada nyingine muhimu. Ili uwe mwalimu haitoshi wewe kusoma na kuwa na cheti ni lazima ufanye mtihani ili tuweze kukuajiri.

“Hali ilivyo sasa zinapotangazwa nafasi za kazi za ualimu, watu wanapanga foleni kwa wabunge wao na vimemo kibao sasa hatuwezi kuajiri kwa namna hii katika fani nyeti kama ualimu. Hatutaki kufanya mchezo kwenye ualimu.Ilifika mahali mtu akikosa kazi anahangaika mzazi anamwambia umeshindwa hata ualimu sasa hatuwezi kuruhusu ualimu uwe chaguo la mwisho,”alisema Profesa Mkenda.

Upimaji na tathmini

Mabadiliko mengine yanayotarajiwa kuanza kutekelezwa kwenye sera mpa ya elimu, ni mfumo wa upimaji na tathmini kwa kuzingatia mahiri zinazohitajika katika kila ngazi kwa lengo la kuwa na upimaji endelevu na matumizi ya mbinu mbalimbali za upimaji ya matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana.

Kitabu kimoja

Waziri Mkuu amelitaja eneo lingine liliguswa na mabadiliko hayo ni upatikanaji wa kitabu kimoja , katika eneo hili alisema Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada katika elimu ya msingi na sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana.

Utekelezaji wa hili tayari umeshaanza, Novemba 3 Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ilitoa taarifa ya kukamilika kwa maandalizi ya vitabu vya kiada kwa madarasa yote yanayotarajiwa kuanza kutekeleza sera na mitalaa mipya.

Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk Aneth Komba anasema, “Kwa mwaka 2024 tunatarajia darasa la awali, la kwanza na la tatu kwa elimu ya msingi wataanza kutekeleza sera na mitalaa mipya ya elimu na tayari vitabu vya kiada na ziada tumeshaandaa. Upande wa sekondari tutaanza na mkondo wa elimu ya amali ambao pia vitabu vyake vimeshaandaliwa”.

Vipaji maalumu

Uendelezaji wa wanafunzi wenye vipaji maalum ni eneo lingine litakaloenda kutiliwa mkazo kwenye sera mpya ambapo Waziri Mkuu, anasema Serikali itaweka utaratibu wa kuwabaini na kuwaendeleza wanafunzi wenye vipawa mbalimbali vinavyojitokeza miongoni mwao.

Gharama za elimu

Eneo la mwisho ni kuhusu gharama za elimu, hapa Waziri Mkuu anabainisha kuwa pamoja na kuendelea kutoa elimu bila ada katika elimumsingi kwa shule za umma, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa elimu na mafunzo wenye vyanzo anuai katika ngazi zote.

Si hivyo tu Serikali itahakikisha katika taasisi zisizo za umma, ada na michango katika ngazi mbalimbali za elimu inazingatia hali halisi ya uchumi, huduma zinazotolewa katika taasisi, misingi ya elimu bora na endelevu ya uwekezaji katika sekta ya elimu.

Maoni ya wadau

Mhadhiri wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Amos Mbaruk anasema sera hiyo mpya inahitaji ushirikiano kutoka kwa wizara na wadau wote husika ili kufanikiwa.

"Ni hatua kubwa inayohitaji uvumilivu. Sasa tunahitaji fedha, rasilimali watu na elimu kwa umma ili kuwezesha mafanikio ya sera hii," anasema.

Hata hivyo, anasisitiza umuhimu wa utekelezaji wa vipengele vyote vya sera ipasavyo, kwani sera za awali zilikumbwa na kutokamilika kwa utekelezaji licha ya uwezo wake.

“Utekelezaji huu uende hatua kwa hatua ili tusirudi tulipotoka, hii ni fursa kwa wadau wengine na sekta binafsi kuchangia ili elimu yetu iwe na tija,” anasema Dk Mbaruk.

Mkuu wa programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Martha Makala, anasema mashirika ya elimu nchini kupitia mtandao huo, yameshiriki kikamilifu katika mapitio ya sera na mitalaa kwa kuwa sehemu ya vikao vya kujadili maboresho hayo, ambayo wana hakika yataenda kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya elimu.

“Kuna mambo ambayo mtandao wa elimu tuliyapendekeza na tumeyaona yametokea kwenye sera mojawapo ni eneo la upatikanaji wa elimu kwa mtoto wa kike na toleo hili la sera limegusia kuwarudisha shuleni watoto wa kike wanaokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito.

Pia suala la elimu ujuzi tulikuwa tukilishauri kwa muda mrefu na lenyewe limepewa msisitizo mkubwa kwenye sera mpya. Vijana sasa hawatakaa kusubiri kuajiriwa bali watapewa jicho la kuziona rasilimali zinazowazunguka na kuzitumia kuweza kujiajiri,”anasema Martha.
 
Ila bado muda wa Elimu yamsingi ni mkubwa sana ilitakuwa kuwa miaka saba tuu au nane ! Sijaona mabadiliko yeyote hapa ..ilitakiwa kuanzia la kwanza hadi la nane iwe imecover hadi form four au la kwanza hadi la 10 iwe imecover hadi form six hivyo akitoka hapo ana kwenda chuo au ufundi! Maana yake tungefata mfumo wa Kenya!

Halafu bado tuna shida kwenye lugha ya kufundishia na lugha ya kuwapima watu au kuwasaili ! Nilitegemea Wizara ichukue uamuzi Mgumu kuanza kutumia lugha ya kingereza kufundishia mashuleni halafu kiswahili liwe somo la lazima!

Halafu nilichopenda ni kada ya Ualimu kuchukuliwa kwa Userious mkubwa sana sana…..kwani ni vyema walimu wapatikane kwa kupimwa kama Kada nyingine zozote…..! Walimu naoa wafanyiwe usaili kama wengine
 
Si tumekubaliana kingereza kianzie shule ya awali..

Au sio ndugu zangu...

Uzi wa member
keisangora

 
Wamecheza tu na akili lakini hakuna jipya ...bado ni kupotezeana muda tu bila sababu za msingi.
 
Kiingereza kiingereza kiingereza kama lugha ya kufundishia kipo wapi?
 
Waache kupokea rushwa kutoka shule za English medium kuuza mitihani na kisha hiyo mitoto kwenda special schools wakiwa hawajui lolote
 
Ila bado muda wa Elimu yamsingi ni mkubwa sana ilitakuwa kuwa miaka saba tuu au nane ! Sijaona mabadiliko yeyote hapa ..ilitakiwa kuanzia la kwanza hadi la nane iwe imecover hadi form four au la kwanza hadi la 10 iwe imecover hadi form six hivyo akitoka hapo ana kwenda chuo au ufundi! Maana yake tungefata mfumo wa Kenya!

Halafu bado tuna shida kwenye lugha ya kufundishia na lugha ya kuwapima watu au kuwasaili ! Nilitegemea Wizara ichukue uamuzi Mgumu kuanza kutumia lugha ya kingereza kufundishia mashuleni halafu kiswahili liwe somo la lazima!

Halafu nilichopenda ni kada ya Ualimu kuchukuliwa kwa Userious mkubwa sana sana…..kwani ni vyema walimu wapatikane kwa kupimwa kama Kada nyingine zozote…..! Walimu naoa wafanyiwe usaili kama wengine
Syllabus nyingi duniani ni miaka 12 toka msingi mpaka sekondari yote
 
Bila mtu kufika kidato Cha Sita, asiruhusiwe kudahiliwa chuo chochote kiwe Cha kati au chuo kikuu
 
Ila bado muda wa Elimu yamsingi ni mkubwa sana ilitakuwa kuwa miaka saba tuu au nane ! Sijaona mabadiliko yeyote hapa ..ilitakiwa kuanzia la kwanza hadi la nane iwe imecover hadi form four au la kwanza hadi la 10 iwe imecover hadi form six hivyo akitoka hapo ana kwenda chuo au ufundi! Maana yake tungefata mfumo wa Kenya!

Halafu bado tuna shida kwenye lugha ya kufundishia na lugha ya kuwapima watu au kuwasaili ! Nilitegemea Wizara ichukue uamuzi Mgumu kuanza kutumia lugha ya kingereza kufundishia mashuleni halafu kiswahili liwe somo la lazima!

Halafu nilichopenda ni kada ya Ualimu kuchukuliwa kwa Userious mkubwa sana sana…..kwani ni vyema walimu wapatikane kwa kupimwa kama Kada nyingine zozote…..! Walimu naoa wafanyiwe usaili kama wengine
Ndio ushangae swala la lugha ya kufundishia halipewagi kipaumbele kabisa. Infact tunapaswa kuwa na sera ya lugha peke ake. Yenye malengo na madhumuni yake. Ila sasa nikama vile hili swala halina maana sana wakati ndo linabeba mustakabadhi mzima wa elimu
 
Back
Top Bottom