SoC01 Maboresho ya Nyanja za Uchumi kwa Maendeleo

Stories of Change - 2021 Competition

Manventure

Member
Jul 16, 2021
10
4
MABORESHO YA NYANJA ZA UCHUMI KWA MAENDELEO

Maendeleo ya jamii au taifa lolote huchochewa na watu wake, mifumo ya utendaji na uchapakazi. Mabadiliko na udhibiti wa utendaji ni moja ya silaha kubwa katika kuchochea maendeleo na ufanisi ndani ya Taifa. Katika nchi yetu Tanzania kuna haja ya kufanya mabadiliko na maboresho kwenye nyanja mbalimbali ili kufikia uchumi imara na maendeleo kiujumla. Kwa serikali na wadau wote wa maendeleo, ili kuendeleza taifa kuna mambo kadhaa yanaweza kufanyiwa kazi.

Uwasilishaji ripoti za ukaguzi kwa wakati sahihi. Nchini Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG) ndiyo hutoa tathmini ya mapato na matumizi ya fedha na miradi katika Serikali na taasisi zake. Lakini ripoti hii huwa inatolewa muda mrefu tangu mwaka wa fedha husika kuisha. Mfano, “mwaka wa fedha 2019/20 ripoti ilikabidhiwa Machi 28, 2021”1 . “ripoti ya 2018/19 ilikabidhiwa Machi 26, 2020.”2. n ahata 2012/13 ilikabidhiwa Machi 31, 2014. Hii inaonesha ndiyo ilivyo. Bali ripoti hizi zikikabidhiwa ndani ya muda mfupi itasaidia kukabiliana na upotevu wa fedha ambazo hazijapewa ufafanuzi wa kina na kasoro nyinginezo pia.

Serikali iundwe na chama cha siasa zaidi ya kimoja. Tugusie zaidi Baraza la Mawaziri nchini ambalo kwa muda mrefu huundwa na wajumbe kutoka chama tawala pekee. Hii itasaidia kueneza demokrasia, uwazi, uwajibikaji na pia kutoa nafasi kwa wananchi wa vyama pinzani kuonesha uwezo na uzoefu wao katika kutumikia taifa la Tanzania. Tukitizama “Baraza la Wawakilishi Zanzibar awamu ya 2020-2025 kuna jumla ya wawakilishi wa CCM 69, ACT-Wazalendo 6, na TADEA 1”3 ilhali Tanzania kuna vyama vya siasa 22 hadi Machi 20204. Idadi hii inadhihirisha hata Baraza la Mawaziri litakuwa ni chama tawala. Hivyo ili kuleta maendeleo sawa nchi nzima, vyama pinzani vipewe nafasi katika kuunda Baraza la Mawaziri.

Kuwa na mitandao ya kijamii ya ndani ya nchi. Katika ulimwengu huu wa utandawazi, mitandao ya kijamii imekuwa inachukua nafasi kubwa sana katika kuchochea maendeleo, maelewano, elimu. Pia hata migogoro na uchochezi vinachangiwa na mitandao ya kijamii. Hivyo kuwe na mitandao ambayo imebuniwa ndani ya nchi ili siri, mikakati na mipango ya ndani isiingiliwe. Mfano, haileti picha nzuri kwa viongozi wa nchi na serikali au wakuu wa vyombo vya ulinzi kuwa na makundi (groups) kwenye mitandao kama WhatsApp kwa sababu wameshikilia mikakati ya Taifa. Uwepo wa mitandao kama Facebook, Twitter ni vyema kwa sababu watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii wapo “takribani watu milioni 5.40 hadi Juni 2021 sawa na 8.9% ya watu wote nchini.”5 Kwa idadi hiyo taarifa za ndani ni rahisi kupenya nje ya mipaka. Hivyo, Wizara husika inaweza kuweka mikakati ya kuunda mitandao itakayotumika ndani ya nchi pekee.

Kuhimiza uzalishaji na uuzaji wa mazao ya chakula. Kwa kiasi kikubwa mazao ya biashara ndiyo yanaonekana kupewa kipaumbele sana kwa sababu yanachangia sana pato la taifa. Lakini mazao ya chakula nayo ni muhimu pia kwani hali ya sasa wakazi wa dunia wanahitaji sana chakula kutokana na athari za janga la Uviko 19. Kwa nchi na wananchi wake fursa ya mazao ya chakula ikitumiwa kutakuwa na ongezeko la mapato. Takwimu zinaonesha mpaka sasa mazao ya chakula

yana bei ndogo sana kulinganisha nay a biashara. Mfano, “matunda (bei ya chini chungwa- Tsh 100 na bei ya juu tikiti maji- Tsh. 1500), nyanya (sado 3500), nafaka Tsh. 800/kilo.”6 Angali mazao ya biashara yanauzwa bei nzuri zaidi katika masoko. Mfano, “pamba (Tsh. 1050/ kilo), korosho (Tsh. 4128/kilo), kahawa (Tsh. 4000 hadi Tsh 5610) kwa kilo.”7 Mapendekezo kwa mamlaka husika ni kuwekea msisitizo na kuongeza hamasa katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwani kipindi hiki cha janga la ugonjwa kuna soko kubwa sana.

Pia, kuwa na mamlaka moja ya usimamizi wa biashara. Nchini Tanzania biashara kutoka sekta rasmi na zisizo rasmi zimekuwa na mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya mwananchi na taifa kwa ujumla. Changamoto inaanzia kwenye usimamizi na udhibiti wa mapato katika biashara. Lengo na pendekezo ni kukusanya mapato kwa ufanisi na sehemu moja kuliko kutawanya mamlaka za ukusanyaji mapato. Kwa mfano, mapato na kodi za biashara hukusanywa na halmashauri pia Mamlaka ya Mapato (TRA). Lakini pia kuna taasisi kama Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambao hukusanya baadhi ya mapato kutoka kwa wawekezaji. Mfumo huu unapelekea ukusanyaji usiende sehemu moja hivyo kuna mapungufu. Badala yake Serikali inaweza kuweka mfumo wa ukusanyaji (centralized) kama TRA kuwa mkusanyaji mkuu. Pia usimamizi wa hizi biashara uwe chini ya mamlaka moja kama ni TanTrade au taasisi nyingine.

Ingawaje kuna jitihada nyingi ambazo Serikali na mamlaka husika zinachukua katika kuleta mabadiliko chanya nchini, njia zilizotajwa zinaweza pia kuwa na mchango. Katika maendeleo au kubadili mifumo ili kuchochea maendeleo, ushirikishwaji wa wananchi na sera bora pia ni nguzo muhimu.


Kumbukumbu na nakili:
7www.rungwedc.com
 
Back
Top Bottom