Luhaga Mpina aanika Bungeni Ufisadi wa Trilioni 1.7 Mkataba wa SGR Tabora - Kigoma

Shakari

Senior Member
Jul 6, 2022
157
440
Mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Joelson Mpina (Mb) akichangia kuhusu taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Kilimo Mifugo na Maji kwa kipindi cha Januari 2022 hadi Januari 2023 Bungeni Dodoma tarehe 31 Januari 2023

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili ingawa nitaongezea maazimio kwa kamati husika.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Miundombinu imewasilisha taarifa yake huku ikilalamikia miradi kutokamilika kwa wakati, miradi kujengwa chini ya viwango, miradi kutelekezwa, gharama za ujenzi kuwa juu kuliko uhalisia, uwezo mdogo wa wakandarasi nk.

Mheshimiwa Spika, ni lazima Bunge lichukue nafasi yake ya kuisimamia Serikali mapema mikataba inapoingiwa badala ya kusubiri miradi kuharibika na kuliingizia taifa hasara kubwa. Lakini kama hatua zitachukuliwa mapema kutakuwa na nafasi ya kufanya marekebisho ikiwemo kuvunja mkataba na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika. Nitatoa mfano

MKATABA WA TRC NA KAMPUNI YA CCECC YA CHINA

Mheshimiwa Spika,
Mkataba baina ya TRC na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuhusu ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha Tabora-Kigoma (Km 506) kwa gharama ya Tsh. Trilioni 6.34

Baada ya Mfumo wa TANePS (Tanzanian National e-Procurement System) tarehe 4 Aprili 2022 kuonyesha Mkandarasi Kampuni ya CCECC amepewa zabuni ya ujenzi wa SGR Tabora-Kigoma kwa Tsh Trilioni 6.69 kwa njia ya Single Source, wabunge walitoa tahadhari juu ya uwepo wa dosari za kimanunuzi kwenye mchakato wa manunuzi.

Lakini Serikali ilipuuza tahadhari hiyo na kusaini mkataba huo baina ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya CCECC tarehe 20/12/2022 wa ujenzi wa kipande cha SGR Tabora-Kigoma Kilometa 506 kwa gharama ya Dola za Marekani Bilioni 2.7 sawa na Tsh Trilioni 6.34 na ujenzi huu unatarajiwa kuchukua miezi 42.

Mheshimiwa Spika, Changamoto ya mkataba baina ya TRC na Kampuni ya CCECC ni namna mkandarasi alivyopatikana na gharama za mradi zilivyofikiwa:

(i) Kutumia njia ya manunuzi ya Single Source kwa mradi mkubwa wa Tsh Trilioni 6.34 badala ya njia ya ushindani inayotoa nafasi ya wazabuni mbalimbali kushindana kwa bei na kwa ubora na kuondoa mianya rushwa na upendeleo kama Sheria na Kanuni zake zinavyotaka.

(ii) Kampuni ya CCECC imeingia mkataba wa Lot Na. 6 Tabora -Kigoma (Km 506) kwa gharama ya Tsh Trilioni 6.34 ikiwa tayari inatekeleza mradi wa Reli ya SGR Lot. Na. 5 kutoka Isaka- Mwanza (Km 341) kwa gharama ya Tsh Trilioni 3.12 ambapo utekelezaji wake ulikuwa 4% tu na kuifanya kampuni hii kupewa jumla ya Kilomita 847 za ujenzi wa SGR kwa gharama Tsh. Trilioni 9.46 kwa wakati mmoja.

(iii) Kampuni ya CCECC haijawahi kujenga hata kipande cha kilomita 1 cha SGR hapa nchini na kukamilika na hivyo sio rahisi kuthibitisha juu ya uwezo na ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya aina hiyo.

(iv) Kipande cha Tabora - Kigoma kimekuwa na gharama kubwa ikilinganishwa na maeneo mengine. Wastani wa gharama ya ujenzi kwa Kilomita 1 ni Tsh bilioni 9.1 kwa miradi ya SGR inayoendelea maeneo mbalimbali nchini (Lot. Na. 5) lakini wastani wa gharama kwa kilomita 1 ni Tsh bilioni 12.5 kwa kipande cha Tabora-Kigoma ambayo ni zaidi ya Bilioni 3.4 ikilinganishwa na maeneo mengine kwa kila kilomita ya SGR. Na hivyo kupelekea malipo yenye mashaka katika mkataba huu kuwa Tsh. Trilioni 1.7

(v) Kabla ya kutangaza Zabuni Serikali ilifanya usanifu na upembuzi yakinifu wa kujenga kipande cha kilomita 514 cha SGR kutoka Tabora-Kigoma kwa gharama ya Tsh Trilioni 4.89 (wastani wa Tsh Bilioni 9.5 kwa kilomita 1 ya SGR) Lakini amekuja kupewa Mkandarasi CCECC kwa gharama ya Tsh Trilioni 6.34 (wastani wa Tsh Bilioni 12.5 kwa kilomita 1 ya SGR) tofauti ya Tsh. Trilioni 1.45 ya usanifu uliofanywa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, njia ya manunuzi ya Single Source iliyotumiwa na Wizara ya Uchukuzi na TRC katika kumpata Mkandarasi CCECC ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake za Mwaka 2013 na marekebisho yake ya Mwaka 2016 katika utoaji wa zabuni kwa njia ya zabuni zisizoshindanishwa (single source) ambapo masharti yake yamewekwa katika Kanuni ya 159, 160 na 161.

Mheshimiwa Spika, Njia ya manunuzi ya zabuni zisizoshindanishwa (single source) inatumika kwa mazingira maalum ambayo yamewekwa wazi kwenye kisheria. Manunuzi kwa njia ya Single Source yasipozingatia matakwa ya Sheria yaliyowekwa inaweza kuwa kiini cha rushwa, upendeleo kwa baadhi ya wazabuni, mradi kutekelezwa chini ya kiwango, gharama za mradi kuwa juu kuliko uhalisia, pamoja na kupata wazabuni wenye uwezo mdogo wa kazi.

Mheshimiwa Spika, kuingiwa kwa Mkataba huu kunaleta maswali mengi nini kiliwasukuma Wizara ya Uchukuzi na TRC kukubali kumpata Mkandarasi kwa njia ya Single Source wakati miradi mingine yote ya SGR ilitangazwa kwa uwazi. Lakini pia cha kushangaza zaidi Wizara ya Fedha na PPRA kuruhusu mkataba kusainiwa huku wakijua kuwa taratibu za manunuzi zimekiukwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa kuwa, kuna mashaka ya namna mkandarasi alivyopatikana, gharama za mkataba zilivyofikiwa na namna TRC na Wizara ya Uchukuzi walivyojiridhisha juu ya uwezo wa Kampuni CCECC kupewa mkataba wa ujenzi wa Kilomita 847 za SGR kwa wakati mmoja.

Na kwa kuwa, Mamlaka za Usimamizi Wizara ya Fedha na PPRA zimeruhusu Mkataba kusainiwa licha ya kuwepo dalili za ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi na Kanuni zake ambao unapelekea kuwepo kwa malipo yenye mashaka ya kiasi cha Tsh. Trilioni 1.7. Hivyo Basi, Bunge liiagize Serikali kufanya yafuatayo:-

(i) Kuwasilisha bungeni taarifa ya mchakato wa manunuzi kuanzia kutangaza zabuni, tathmini na utoaji wa zabuni ya SGR kipande cha Tabora-Kigoma Kilomita 506 (Kamati ya Miundombinu na Kamati ya Katiba na Sheria zifanye uchambuzi kwa niaba ya Bunge na kuwasilisha taarifa bungeni)

(ii) CAG, TAKUKURU na PPRA wafanye ukaguzi maalum katika mchakato wa manunuzi na kuingia mkataba wa TRC na CCECC wa ujenzi wa SGR kipande cha Tabora-Kigoma Kilomita 506 na taarifa iwasilishwe bungeni ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.

USIMAMIZI WA RASLIMALI ZA UVUVI NCHINI

Mheshimiwa Spika,
nimezipokea taarifa za Utafiti kuhusu kupungua kwa samaki katika Maziwa, Mabwawa na Mito kwa masikitiko makubwa ambapo Kamati inabainisha kuwa imesababishwa na usimamizi hafifu wa raslimali hizo.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa Samaki aina ya Sangara wamepungua kwa 50% na samaki wazazi wamebaki 0.4% katika Ziwa Victoria. kiwango hiki ni cha chini sana kubaki katika ziwa na kama hatua stahiki hazitachukuliwa haraka ziwa hili litabaki kuwa swimming pool. Tafiti za kitaalamu zinaeleza kiwango cha chini cha samaki wazazi katika Ziwa Victoria walau kisiwe chini ya 3%.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilishapiga hatua kubwa sana katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi, kwa takwimu za kuishia Disemba 2020, uvuvi wa mabomu ulipungua kwa 100% na uvuvi haramu wa maji baridi ulipungua kwa 80%.

Mheshimiwa Spika, Samaki wazazi katika Ziwa Victoria waliongezeka na kufikia 5.2% kutoka 0.4%, huku samaki wanaofaa kuvuliwa walifikia 32% kutoka 3.3% na samaki wachanga kupungua hadi 62.8% kutoka 96.6% na urefu wa Sangara uliongezeka kutoka urefu wa sentimita 16 hadi sentimita 25.2 huku uagizaji samaki kutoka nje ya nchi ulibaki sifuri. Mauzo ya Samaki nje ya nchi yaliongezeka kutoka Bilioni 379 mwaka 2015 hadi Bilioni 692 mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, Kamati imebainisha madhara makubwa kwa taifa kutokana na kushamiri kwa uvuvi haramu ambapo ajira zinaendelea kupotea, viwanda vya samaki kufungwa kwa kukosa malighafi, umasikini mkubwa katika ngazi ya familia, Serikali
kukosa mapato. Wizara hii mapato yanayotokana na mifugo na uvuvi yameporomoka kwa kasi.

Mheshimiwa Spika, lakini swali kubwa la kujiuliza nini chanzo cha usimamizi hafifu wa uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi wakati Mamlaka zilizopewa dhamana zote zipo kazini zikifanya kazi ya kulinda raslimali hizo usiku na mchana, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali za Mitaa hadi kwa VEO na vitongoji, Vyombo vya Dola na mamlaka za utoaji haki zote ziko kazini.

Mheshimiwa Spika, Pendekezo la Kamati kwamba Serikali idhibiti uvuvi haramu kwa kutumia njia sahihi ambazo hazitwezi utu wa wananchi lakini zinaleta matokeo chanya nakubaliana nao lakini naongezea mapendekezo mengine mawili.

(i) Bunge liitake Serikali kuwasilisha bungeni chanzo cha usimamizi hafifu wa raslimali za uvuvi ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.

(ii) Bunge liitake Serikali kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi katika maeneo yote kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
Nawasilisha,
……………………………………………….
Luhaga Joelson Mpina (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Kisesa
 

Attachments

  • MPINA_MIUNDOMBINU_KILIMO_ JAN 2023.pdf
    157.3 KB · Views: 10
Bandiko gumu sana nimekopi kingele cha sgr waziri na wataalamu wengine wasaidie majibu ya uelewa
 
Back
Top Bottom