Leseni za udereva 7,072 za Daraja C zafutwa na Jeshi la Polisi Tanzania

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,818
11,994
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) limezifuta leseni za udereva 7,072 za Daraja C kati ya leseni 68,987 zilizohakikiwa hadi kufikia Julai 25, mwaka huu.

Leseni hizo ni za madereva wa malori na mabasi ya abiria ambao wamebainika kukosa sifa ikiwemo kutosomea madaraja hayo. Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Ramadhan Ng'azi alipozungumzia kuhusu tathmini ya uhakiki huo kwa awamu ya pili inayotarajiwa kufikia tamati Julai 31, mwaka huu.

Ng'azi amesema leseni zilizofutiwa madaraja zilionekana kutokidhi vigezo kwa sababu wamezipata visivyo halali na kuwashusha madaraja ya awali. "Hadi sasa asilimia 75 ya madereva wa mabasi na malori wamejitokeza kuhakiki leseni zao na baada ya uhakiki wa hiari kumalizika Julai 31, mwaka huu, madereva ambao hawakuhakikiwa kwa sababu maalumu ikiwemo kuumwa na kuwa nje ya nchi utaandaliwa utaratibu maalumu wa kuhakiki leseni zao," amesema.

Amesema wameanza uhakiki kwa madereva hao kwa sababu wanabeba watu wengi ambapo ikitokea ajali maafa yanakuwa makubwa. Amesema madereva waliofutiwa madaraja watatakiwa kurudi kwenye shule za udereva kupata elimu ya udereva ili kuwaongezea umahiri na weledi katika kazi zao.

Ng'azi amesema baada ya kufanya tathmini ya uhakiki wa hiari itaanza oparesheni maalumu ya uhakiki wa leseni za madereva wa bodaboda na magari binafsi katika muda ambao utapangwa hivi karibuni.

Amesema pia kikosi kitaanza kupambana na upakiaji wa abiria zaidi ya mmoja na wanafikiria kumshitaki abiria wa pili anayening'inia pamoja na dereva.
 
Back
Top Bottom