Leonard Rwizandekwe: Mtanzania pekee aliyethubutu kumuondoa Nyerere madarakani Kikatiba

WilsonKaisary

JF-Expert Member
Apr 4, 2017
392
946
Mzee Leonard Rwizandekwe aliwashangaza Watanzania mwaka 1965 kwa kukiomba chama cha TANU kimpendekeza kwa wananchi awe mgombea pekee wa urais badala ya Mwalimu Nyerere, akiwa kijiji kwake Katendaguro Wilaya ya Misenye Mkoa wa Kagera alipofanyiwa mahojiano na Elisa Muhingo na Mathias Byabato, Bukoba, anasema wakati huo ilikuwa ni nadra na vigumu mtu yoyote kutaka kugombea nafasi hiyo kwa kuwa wananchi wengi walidhani kuwa hapakuwepo mtu mwingine zaidi ya Mwalimu Nyerere ambaye angeweza kuwa Rais wa nchi.

Alizaliwa tarehe 14 juni mwaka 1929 katika kijiji cha Katendaguro na kusoma shule ya msingi ya Rukurungo na baadae alipelekwa katika jumba la Mugorola lililokuwa Bunge la jadi ambapo hapo alikaa humo akilelewa na wazee ikiwa ni pamoja na kufundishwa maadili, utii, na uwajibikaji.

Mwaka 1948 alichaguliwa kujiunga na shule ya Serikali Ihungo iliyopo Bukoba kwa masomo ya Sekondari ambapo baada ya kuhitimu aliajiriwa katika idara ya mahesabu katika Wilaya ya Buhaya.

Rwizandekwe aliamua kujisomea mwenyewe masomo ya sheria na alipofanya mtihani wa Chuo cha Kibete cha nchini Uganda alifaulu vizuri na baada ya kupata cheti aliajiriwa katika sekta mbalimbali serikalini ambapo juni 1 mwaka 1959 aliteuliwa kuwa Hakimu wa Mahakama ya Rufaa ya Buhaya.

Mwaka 1960 alichaguliwa kama mtumishi bora kutoka Halmashauri ya Buhaya kwenda kuhudhuria semina ya sheria za Afrika nchini Uganda ambapo kupitia huko alichaguliwa pia kuhudhuria masomo ya shahada ya sheria za mila za Afrika katika Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza.

Aliporudi nchini mwaka 1963 alikuwa Msomi mzuri tu na kwaajili hiyo aliajiriwa kama Mkurugenzi msaidizi wa Halmashauri ya Buhaya ambapo baada ya muda mfupi Mwalimu Nyerere alimuhamishia Makao Makuu ya Wizara ya sheria alipoajiriwa kama mshauri mkuu wa sheria za mila za Serikali.

Rwizandekwe ,wazo la kugombea nafasi ya urais lilimjia mwaka 1965 baada ya kubaini kuwa mambo ambayo alikuwa amekubaliana na Mwalimu kuwa angeyafanya baada ya kupata Uhuru yote yalikuwa hayakufanyika.

Akiwa nchini Uingereza mwaka 1961 alikutana na Mwalimu Nyerere katika Hotel ya Minsure, ambapo Mwalimu alikuwa amekwenda kumuona Malkia wa Uingereza kuhusu Tanganyika kupata Uhuru wake. " wakati wa chakula cha Usiku nilimuomba Mwalimu kuwa iwapo tungefanikiwa kupata Uhuru basi A-afrikanishe mali za umma , ataifishe mashule na majumba ,ahakikishe kunakuwepo na mlingano kati ya shule za wakristo na waislamu kwani wakati huo asilimia 70 ya shule zote zilikuwa ni za wakristo asilimia 27 zilikuwa za serikali na asilimia tatu tu ndizo zilikuwa shule za waislamu."

" Nilimwambia kuwa iwapo ata-afrikanisha rasilimali za nchi na kuweka mlingano wa shule waislamu Wengi wangesoma", Mwalimu alimshukuru kwa mawazo hayo na alimuomba ampatie kwa maandishi na alipofanya hivyo alimuhakikishia kwamba angeyatekeleza yote baada ya kupata Uhuru.
Hata hivyo ,Mwalimu hakufafanua hiyo na kwa ajili hiyo alimwandikia Waziri Mkuu wa wakati huo Mzee Rashidi Mfaume Kawawa barua ya karatasi 42 kuhusu aliyokuwa amekubaliana na Mwalimu Nyerere pamoja Ku-afrikanisha rasilimali na kuwa na shirikisho la Afrika.

"Nilisubiri mwaka 1962 na 1963 Mwalimu hakutekeleza maazimio yetu na mwaka 1964 nako hakutekeleza hadi hali ikiwa mbaya sana mpaka wanajeshi wakataka kuleta machafuko ". Rwizandekwe alipoona hali inakuwa hivyo mwaka 1965 aliamua kugombea nafasi ya urais akitaka achaguliwe yeye ili aweze kutekeleza mambo hayo ambayo aliona Mwalimu Nyerere yalikuwa yamemshinda au alikuwa akiogopa mikataba fulani fulani.

Wakati wa kuomba urais kipindi hicho, mgombea alikuwa anawasilisha karatasi za maombi na siyo kuchukua fomu kama sasa, " Mimi peke yangu kwa nchi nzima niliwasilisha maombi ya karatasi 25 hapo Lumumba kwa Katibu mkuu wa TANU wakati huo Oscar Kambona na walizipokea"

Katika waraka wake huo alikuwa ameeleza mipango yake ya baadaye iwapo angepitishwa kuwa mgombea urais na hatimaye kuwa Rais badala ya Mwalimu Nyerere.

Watu Wengi walikuwa wanamuona Mwalimu kama yesu na kuwa walikuwa wakimshangaa kuona anathubutu vipi kugombea nafasi waliyoiita ni ya Mwalimu Nyerere. "Mimi Nilikuwa najua sheria na Katiba ya nchi. Nilikuwa najua kwamba hayo hayakuwa makosa mtu kutumia demokrasia kugombea nafasi yoyote ikiwemo ya urais ".

Hakuweza kupitishwa kuwa mgombea badala yake Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa mgombea na hatimaye Rais wa nchi, lakini mafanikio ni kuwa baada ya muda mfupi tangu awasilishe maombi hayo Mwalimu Nyerere alitekeleza yote ambayo alikuwa ameyaweka katika barua ya maombi ya kugombea nafasi ya urais.

" Baada ya kutopitishwa sikuleta chokochoko bali nilikubali kwani haikuwa lazima nipitishwe bali niliendelea na kazi yangu pale Wizara ya sheria ambapo watu walianza kuniona kama mtu wa ajabu, Nakumbuka kuna wakati tulikwenda kumpokea Mwalimu uwanja wa ndege lakini mimi nilikaa kando ya uwanja kwani Sikuwa na umuhimu wa kwenda kumshika mkono Rais.

"Hata hivyo Rais mwenyewe alipotupa jicho na kuniona aliwapita wote na kuja kunisalimia na tulishikana mikono na akanieleza kuwa mambo yako tumeyafanyia kazi ,kwa kweli tangu siku hiyo watu waliniheshimu sana.

ILANI YA UCHAGUZI YA RWIZANDEKWE ILIYOZAA AZIMIO LA ARUSHA


ILANI hiyo aliipeleka kwenye Mkutano Mkuu wa TANU na Afro Shirazi Agosti mwaka 1965 akiomba chama kimpendekeze kuwa mgombea pekee wa Rais badala ya Mwalimu Nyerere, Rwizandekwe anaamini ilani hiyo ndiyo iliyotumiwa na Mwalimu kuunda Azimio la Arusha.

Leonard Rwizandekwe
c/o Justice Division
P.O. Box 2481
Dar es salaam.
Agosti 5, 1965

Waheshimiwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TANU na Afro Shiraz wa kuteua Mtanzania atakayegombea urais wa Jamhuri ya Tanzania katika uchaguzi Mkuu ujao.

Mabwana,

KATIKA nchi zinazohubiri na kuamini demokrasia kuwa ndiyo ngao ya kutawala vizuri zaidi na kuleta maendeleo kwa upesi ,watu wake ambao wanataka kugombea urais na uongozi Mkuu wa namna hiyo, yapaswa wajitokeze ili wenye mamlaka ya kuchagua waweze kuwa kwenye hali nzuri zaidi ya kuchagua kiongozi shujaa na shupavu wa kuongoza nchi yao.

Kwa hiyo ,mimi ambaye najiamini kwamba naweza kuongoza Tanzania vizuri zaidi iwapo nikichaguliwa kuwa rais ,naona sina budi nijitokeze ili nigombee uongozi, kwa kuwa ni kawaida katika nchi nyingi za ulimwengu kuwa wagombea urais na uongozi mkubwa wa namna hiyo hutoa hotuba kueleza maoni yao juu ya siasa ya nchi yao, kuhusu mambo ya ndani ( ya nchi yao) na yale yahusuyo nchi za nje,naona sina budi nitoe hotuba fupi ambayo iwawezeshe kunipima na kunichagua nigombee urais.

Mimi ni mwanachama wa NUTA ,na mwanachama wa chama cha kahawa na ni mlimaji na mwenye nyumba, nilikuwa mwanachama wa chama cha Bukoba Society Council ambacho kimesaidia watu Wengi katika wilaya ya Bukoba na Karagwe kuanzisha Credit Society yaani vyama vya kuweka akiba na kutoa mikopo kwa bei nafuu. Nilikuwa kwenye kamati yake ya utendaji na nilikuwa mkaguzi wa mahesabu ya chama hicho.

Nilikuwa Acting President wa chama cha kuzungumza ( Discussion Group) juu ya mambo yaliyohusu nchi kwa ujumla . chama hicho kilipokea wanachama wa mataifa yote watoe mawazo yao, Viongozi mashuhuri wa nchi hii kwa mfano ,Mheshimiwa Rais wa Tanzania ,Mwalimu Julius Nyerere, waliweza kuhutubia na tukawauliza maswali mbalimbali kuhusu nchi yetu ,Niliacha uongozi wa chama hicho nilipokwenda Ulaya mwaka 1960.

Nikiwa katika shule ya Sekondari Nyakato, nilikuwa scout na mtunza vitabu wa shule(School Librarian) na nilikuwa nakimbia mbio za maili nyingi hata Nilikuja kuwa mshindi wa kwanza katika mwaka 1952. Zaidi ya hayo yote ni mwanachama halisi wa TANU hata kabla ya kuingia chamani nilikuwa nahudhuria Mikutano yake na kutoa maoni ambayo yalisaidia viongozi .Niliingia kwenye chama mwaka 1956 tarehe 14 ,Oktoba kadi Namba 149883.

Kuhusu siasa ya chama kimoja ,natumaini mimi ni mmoja wa watanzania wa kwanza wa kufikiria na kuamua kwamba Serikali ya chama kimoja ni nzuri iwapo Katiba zake Zimetungwa na kuhakikisha kuwa haki za binadamu na demokrasi zitahifadhiwa.

Mwanzoni mwa mwaka 1962 nikiwa mafunzoni Uingereza ,nilimwandikia Mheshimiwa Waziri Mkuu ,nakala kwa Mheshimiwa Rais wa TANU nikitoa mapendekezo yangu ili tuitoe Tanganyika katika mamlaka ya Malkia wa uingereza na kuifanya jamhuri tuanzishe Serikali ya chama kimoja.

Pia nilishauri juu ya kuunganisha mahakama na kuifanya jinsi ilivyofanywa tangu tarehe 1---7--1964 na nilishauri kufanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa na Serikali, na kuzitafsiri katika lugha ya Kiswahili sheria zote zilizoandikwa Katika lugha ya kiingereza. Pia nilishauri kuharakisha kuwapandisha wakuu wa Majeshi na Polisi na Magereza nilieleza hatari ambazo wakoloni huleta mara kwa mara nchi zinazoendelea iwapo wanacheleweshwa vyeo na mishahara katika majeshi na polisi.
Mpaka sasa mambo yote niliyosema hapo juu yamekwisha tokea.

Pamoja na hayo ,katika taarifa hiyo yenye kurasa 42 nilieleza naamini pia kuwa sio kwa matajiri au na wakoloni au sio kuhamia kwenye siasa ya Mashariki au Magharibi watakaokomboa nchi yetu kutoka kwenye minyororo ya kunyonywa utajiri wetu, ufukara na kudharauliwa ,bali kuokoka kwetu kutategemea jitihada zetu.

Moyo mgumu na ushujaa na ushupavu na haki kwa kufanya Mikataba ya kuuza mali na mazao yetu, ushupavu katika kuagiza mali kutoka nchi za nje kutoa bei nafuu na ushupavu wetu wa kupokea mikopo isiyo na masharti na kufyonza utajiri katika kutuinua. Hotuba yangu naomba kuitanguliza kwa kichwa kizuri kama hiki;

KIAPO CHA KUHARAKISHA ZAIDI UKOMBOZI WA ELIMU, HESHIMA NA UTAJIRI WA TANZANIA

Kiapo cha kuharakisha zaidi ukombozi wa elimu, heshima na utajiri wa Tanzania , watu Wengine wanaweza kusema kuwa mradi TANU na Afro Shiraz zimekwisha eleza au kukubali siasa ya ujamaa ambayo hakuna mtu au hata na rais wa Tanzania awezaye kuibadili, hakuna haja tena ya wagombea "Urais" kutoa hotuba wakati wa kuwateua ,Lakini kwa kuwa Rais aliyechaguliwa na watu ana mamlaka makubwa ,hasa kufuatia Katiba yetu jinsi ilivyo, na kwa kuwa marais hao wangezaliwa mama mmoja au wangezaliwa mapacha juu ya ukoloni ambao ulikuwa bado kuondolewa katika mambo ya uchumi na elimu ya nchi na namna ya kuuondoa .

Sina shaka mawazo yangu yalitumiwa na Waheshimiwa viongozi, kwa kuwa mimi ni mwamini wa Serikali ya chama kimoja majuzi nimezidi kutaka Mheshimiwa Rais wa jamhuri ya Halmashauri kuu ya TANU mawazo juu ya taarifa ya tume na namna ya kuiimarisha demokrasia katika chama kimoja, Mawazo hayo pia yamesaidia kwa kutengeneza na kuthibitisha katiba mpya ya Serikali na TANU.

Mimi babu zangu wote walikuwa mashujaa wa kupigana vita, waliwekwa katika mpaka wa nchi yao ili waendelee kulinda na kutandika maadui na kuwashinda au kufa wala sio kujitolea. Walijulikana sana sio kutoka Buhaya tu bali na katika nchi nyingine kama Rwanda ,Biharamulo na Uponda.

Walifanywa majemedari wakuu na watawala wa nyakati zile na walitetea utajiri na jeshi la nchi yao. Na mimi katika maisha yangu ndivyo nataka kuifanyia Tanzania, lakini jinsi babu zangu walivyowapa Maziwa na vyakula mateka ambao waliwateka kwenye vita, ndivyo na mimi nitashauri Tanzania iwafanyie maadui iwapo itakuwa lazima tupigane na kuwateka wasioweza kulingana nasi, kwa ushujaa ,ushupavu ,mapenzi ,uvumilivu na kugawana na kutaka kutafsiri siasa ya nchi na kutimiza utendaji wao, naona ni bora maoni ya wagombea Urais yatolewe tena katika siku ya kuchagua jinsi kama baadhi ya nchi zifanyavyo.

Natumaini Waheshimiwa wajumbe watapenda kusikiliza sauti za wagombea urais kabla ya kutumbukiza kura zao za uteuzi katika sanduku la kura. Kwa kuwa watumishi au wafanyakazi naweza kuwalinganisha na gari Moshi ambalo husafirisha abiria na kuburura mizigo kufuata jinsi reli ilivyotengwa naona siwezi kuepuka kuwaambia waziwazi kuwa kufaulu kwa nchi hii, kukirimiwa kwa nchi hii au kuanguka kwake iwapo kupo kutategemea au kutatokana na viongozi zaidi ambao ndio wanajua siasa ,ndio wanakataa maazimio ambayo yanakabidhiwa na raia na watumishi ili yatimizwe.

Ninyi mko macho na masikio ya raia waliowachagua mpo na mishipa ya fahamu au hazina kubwa ya nchi , sina shaka mnaona, mnasikia na kufahamu yote yanayotendeka na mliyonunua. Hata na makampuni ya wageni yaliyomo Nchini humu .kwa hiyo mtachagua mtu aliyeumbwa na Mungu kuongoza Tanzania katika mwaka 1965---1970.

Kwa kuwa utawala wa vyama vyetu na serikali ndio chama nitatoa mawazo juu ya mambo ambayo kama ningechaguliwa kuwa Rais ningeyaleta mara kwa mara, mbele yenu na Bunge ili yachunguzwe na kurekebishwa, Mimi ingawa itanibidi nihimize yale mtakayopitisha ,lakini maoni yangu binafsi ningependelea hali ya kuweka watu vizuizini bila hukumu iondolewe ,Mimi kama Mwafrika ,Mtanzania, labda aliyejifunza zaidi sheria za mila za waafrika ambaye pia nimewahi kufundishwa elimu ihusuyo maisha ya watu yaani Sociology naona ni vizuri mtu kusikilizwa kosa lake Kabla ya kumtia kizuizini au kumfunga.

Hata na machifu wetu wa zamani ambao walikuwa na uwezo wa kidikteta hawakuadhibu kabla ya kuhukumu , Nikichaguliwa kuwa Rais nitaweza kueleza zaidi hasara iwezayo kuliletea Taifa na sheria kama hii isipofutwa. Naamini pia binadamu hakuumbika kufanya makosa na dhambi bali hufanya makosa iwapo ameona amebanwa ,ameonewa au anajitetea au ametafsiri Vibaya mazuri. Kwaajili ya magonjwa na ubongo na fahamu zake, na dawa ya kuwatibu ni kuwafundisha na kuwauguza vyema.

Kwa hiyo ,nikiwa Rais nitachunguza mwenyewe kuongezeka kwa wahalifu na wakorodi na sheria zote hasa zinazoweza vina vya adhabu mapema na kuwashauri tuongeze Vyuo vya kuwafundisha na kuwataka na kuwapatia kazi za kufanya ili wapungukiwe nafasi ya kufikiria yale yanayochukiza raia.

Mimi kwa kuwa nilikuwa Hakimu na niliwahi kufunga watu Wengi nilipokuwa London niliiomba Serikali na ilikubali kugharamia safari zangu ili nitembelee Mahabusu za Uingereza na za ulaya ili nijifunze hali za wafungwa , nilitembelea Mahabusu za Uingereza ,Uholanzi na Sweden ,Hizo nchi za Scandinavia na Uholanzi ,zilipunguza adhabu na kuongeza shule na hospitali za kutibu wakosaji ndipo zikapata matokeo bora zaidi.

Utakuta nchi zile ambazo zimeachwa na wakoloni au zilizoshindwa kuendeleza watu kwa upesi na haki ndizo watu wake Wengi wamekuwa kwenye hali ya kufanya makosa na wa nchi kama hizo ,ambazo zimepata ubingwa na nishani za kudhihaki watu. Sisemi kuwa Tanzania imo kwenye Orodha ya nchi zinazosifika kwa kuadhibu lakini ningependelea kuona Tanzania inapunguza haki zinazoweka baadhi ya binadamu katika hali ya kukosa.

Kwa kuwa naamini kuwa watu wote wawe sawa hata na kwa kutia sheria ambazo ndizo zinatufanya pia tuwe na njia fulani ,nikiwa Rais nitakuwa kwenye hali nzuri ya kushauri kuwa kifungu Na. II (I) cha Katiba ambacho kinasema kuwa Rais hawezi kushitakiwa kwa namna yeyote popote kwa kosa la jinai kifungwe, kikifutwa kitafanya marais wajihadhari wasitende makosa, jambo ambalo linatakiwa ,kwa Kiongozi yeyote .

Baadhi ya wafalme wa zamani na watawala Wengine waliweza kufanya makosa mengi kwa sababu walihifadhiwa na sheria kama hii. Maoni yangu Rais kwa kuwa ni binadamu kama watu Wengine ashitakiwe akikosa ,akishindwa alipe fidia Wala siyo kuacha Urais, labda iwapo atafanya kosa kubwa ambalo haliwezi kuepuka kufanywa, kimila na kiafrika wafalme fulani na watawala fulani walipowakosea raia zao, washauri na wataalamu wao walisikiliza shauri na walipokuta chifu ndiye amekosa walimshauri alipe fidia kama ng'ombe ,mashamba hata na mali nyinginezo zilizostahili.

Kwa kuwa wabunge wanawawakilisha raia ambao ndio wanaohusika na ulipaji wa kodi na upindishaji wa mikopo ,nitashauri na kukubaliwa. Kuhusu chama cha TANU nitashauri kuwa makisio ya mapato na matumizi na ripoti za mahesabu za kila mwaka kuhusu mali ya TANU zisomwe na Mkutano Mkuu wala sio kuachia kazi hii Halmashauri kuu,pia nitashauri bidii iongezwe na kukosa mapenzi ya raia ili walipe ada kwa wingi.

Kama wanazidi kuingia chamani lakini inaonekana ada hazilipwi vizuri sana ili TANU iweze kupanua mipango nakulipa mishahara na posho zinazostahili kwa watumishi na viongozi na baadaye ikubaliwe kila wilaya iweze kuwa na mjumbe katika National Executive Committee na kila Mkutano Mkuu wa TANU na wa mikoa ziweze kukutana kila mwaka badala ya miaka miwili.

Kwa jinsi Central committee ilivyo na madaraka makuu ya kuwakilisha Halmashauri kuu ,nitashauri wajumbe wake wote wachaguliwe na Halmashauri kuu yaani wajumbe ambao wanachaguliwa na Rais kwa mujibu wa kifungu Na. 52 (C) wachaguliwe na Halmashauri Kuu.

Nikichaguliwa kuwa Rais nitahimiza TANU na Afro Shiraz viungane na uchaguzi mkuu wa kuchagua wabunge ufanyike kisiwani pia. Kwa kuwa mimi ni mwamini wa demokrasia zaidi nikiwa Rais nitashauri na ikikubaliwa na Regional Commissioners na watu wengine wote ambao wameingia kwenye Bunge bila kupigiwa kura watu hao waondolewe kwenye Bunge na kubaki na kazi zao na nafasi zao kwenye Bunge zitolewe kabisa au miji na wilaya zilizo kubwa ziongezwe majimbo ya uchaguzi na ma-region commissioners na watu Wengine wawe huru kugombea viti hivyo na atakayeshinda ndiye atakayeingia kwenye Bunge.

Katiba iliyopo ya kuingiza baadhi ya watu bungeni bila kupigiwa kura inamwezesha Rais kuingiza kwenye Bunge kiasi cha watu 50 au kiasi kinachokaribia nusu ya wajumbe waliochaguliwa . Huu ni uwezo mkubwa sana ambao haijulikani kwa watawala wa Siku hizi.

Hata na wafalme wengi wenye mamlaka ya namna hii tukiongeza wajumbe wengine10 na hata ambao wanawakilisha vyama vyao ,bila ya kupigiwa kura na watu, karibu wabunge ambao hawakupigiwa kura na watu wanakaribia kiasi cha 60 Kwa kiti cha wajumbe waliochaguliwa. Tusiporekebisha kifungu hiki basi ,kwa upesi tutakuja kushitakiwa na Raia kuwa tunafuata nyoyo za wakoloni na wafalme wa zamani ambao waliwaingiza Kwenye Bunge watu ambao hawakuchaguliwa na watu ili kurudisha mamlaka yao na kupunguza kuhojiwa.

ULINZI NA UUNDAJI WA AINA ZOTE ZA MAJESHI

Ni kweli kabisa kusema kuwa katika ulimwengu huu ambao mpaka sasa sio mkamilifu ,mtu akitaka amani sharti ajitayarishe kwa vita.

Wana-Afrika tunadharauliwa sio Kwamba sisi sio binadamu au sio kwamba hatuamini Mungu. Mijini ili wananchi wasitiliwe na wakoloni bila kujua vyombo vya kupokea na kupeleka habari kwa njia isiyo halali na kwa wasiohusika.

Pia Balozi, maduka na makampuni yaliyomo nchini nitahakikisha kuwa hawana vyombo vya uchunguzi na upelelezi kama kamera ambavyo huwezi kuchunguza majumbani na mitaani kuona watu na kusikia yanayosemwa na ambayo hayastahili kujulikana bila vyombo hivyo kutumiwa na kutenga watu ambao hawapendwi na wakoloni na vibaraka wao,hugonganisha viongozi na watu weusi bila wao kujulikana kwa urahisi.

Vyombo kama hivyo vya ulinzi Serikali yetu ikiwa inavitumia katika ulinzi ni lazima vishikwe na wananchi ,waafrika kama hawakuwepo wakati tulipopata Uhuru natumaini ndio idara iliyostahili kuwa ya kwanza ,ku-afrikanise . Pia ni lazima tu-afrkanise ofisi za kupeleka na kupokea simu za kila aina, mitambo ya kuandika ambayo inaweza kuandika hapa na yakasomeka mikutano ile katika nchi za ulaya na Amerika (teleprinter) ikiwa Kenya na Uganda nazo zitawahi au kuchelewa kuharakisha Afrcanisation katika mambo makuu katika upatikanaji na upelekaji habari basi nitashauri Tanzania ifikirie kurekebisha jambo hili yenyewe katika nchi yake.

Mimi naona kuwa kupinduliwa hatuwezi kukujua mapema na kwa urahisi ili tukwepe ,kuuawa ovyo ovyo na bila kujulikana hatutakuepuka, fedha za kuhonga majasusi hatutajua kwa urahisi zinavyoingizwa Nchini , ili wayaamini kuwa ndiyo ngazi za kuwa matajiri na kupanda vyeo na kuwafanya watu na matajiri ,kutopata maendeleo kutopata maendeleo ya haraka iwapo wakoloni na matajiri wakingali wameweka mikono yao kwenye ulinzi wa nchi za Afrika.

Kwa hiyo ndiyo sababu sababu siridhiki na mpango wa maendeleo ya elimu yetu mpaka mwaka 1980 ndio tutapata waafrika wa kushika kazi zote.

ndiyo sababu siwezi kuridhika na mpango wa Vyuo vikuu vya Afrika Mashariki ambao pia unafanya Tanzania ichukue muda mrefu Kabla ya kuwa kwenye ardhi yake na Vyuo vya kutoa shahada kama uganga wa mifugo ,umakenika wa jinsi zote utaalamu wa ujenzi, utaalamu wa madini, fizikia, na matawi mengine ya uchunguzi wa sayansi.

Mimi nikiwa Rais lazima nishauri kuleta mapinduzi katika elimu ya juu yaani kabla ya miaka mitano Tanzania ianzishe Vyuo nilivyotaja hapo juu na nitawafahamisha sasa hivi namna ya kupata fedha kama nchi nyingine zinavyopata fedha.

UCHUMI WA TANZANIA

Napaza sauti kuwa Tanzania haikuumbwa na Mungu kubaki kuwa mashimo ya wakoloni ya kuchimbua utajiri kufanya biashara na sisi waafrika tukabaki katika machaka ,tukiendelea kutumia majembe kama ya ng'ombe bila kujua elimu ya kuunda mitambo na elimu ya masoko ya dunia ,Almasi zetu wakoloni wanaleta watuuzie na dhahabu wanataka vilevile wao ndio wawe wauzaji na wapiga mnada ,badala yetu.

Wakoloni kutueleza kuwa korosho zetu ni hafifu ,kahawa zetu ni hafifu ,ngozi za ng'ombe wetu ni hafifu, na kuwa eti kutupa bei hafifu na kutusamehe ,wanapozinunua na kuzitia rangi na manukato huzirudisha kuziuza kwa bei ya juu sana

Kwa mfano mlimaji analipwa karibu shilingi moja kwa ratili moja ya korosho lakini ounzi mbili tu za korosho iliyokaangwa eti kitaalamu inauzwa shilingi moja yaani karibu ratili moja yauzwa shilingi 16.

Mkanda wa ngozi wa ng'ombe wa saa ya mkono nimeuziwa shilingi nane na wachuuzi wa Dar es salaam katika ngozi moja ya ng'ombe karibu inaweza kutoa vipande 100 na kujipatia shilingi 800 ,lakini ngozi ya ng'ombe hununuliwa kwa kiasi kisichozidi shilingi 50 nchini Tanzania.

Ripoti za UNO na za mataifa mengine ya ulaya zinasema nchi zetu zinazidi kuwa masikini ingawa zina mali nyingi za asili na ardhi kubwa ya kustawisha mazao kuwa nchi zinazoitwa zimeendelea zinazidi kuwa tajiri nguvu mali ya asili katika nchi zao imepungua.

Mapato ya mwingereza ya wastani kila mtu nakisia ni shilingi,12,000, Mwamerika anazidi hapo, nchi nyingi za ulaya ziko Kwenye kima cha chini cha utajiri kinachokaribia cha Mwingereza, mapato ya Mtanzania ni shilingi 400 kwa mwaka .

Ni wazi hatuwezi kupokea mpango wa namna hii ambao umefanywa makusudi kuhakikisha kuwa nchi zetu zitabaki masikini na nchi fulani zibaki tajiri tu.

FB_IMG_1590889863674.jpg
 
Mkuu kuhusu hiyo Ilani ni vyema ungefanya attachment yake original kama ipo. Ukiandika mwenyewe inapoteza uhalisia. Omission au addition ya maneno inaweza kufanyika na kuishia kupotosha.
 
Mzee alikuwa kichwa na maono ya mbali, karibia vyote alivyopinga mpaka leo vinapingwa.
Kuweka watu kizuizini bila kusikilizwa, Rais kupewa mamla ya kuteua viti maalumu, Raisi kutoshitakiwa nk.

Ipo siku yote haya yatabadilika.
 
" Baada ya kutopitishwa sikuleta chokochoko bali nilikubali kwani haikuwa lazima nipitishwe bali niliendelea na kazi yangu pale Wizara ya sheria ambapo watu walianza kuniona kama mtu wa ajabu, Nakumbuka kuna wakati tulikwenda kumpokea Mwalimu uwanja wa ndege lakini mimi nilikaa kando ya uwanja kwani Sikuwa na umuhimu wa kwenda kumshika mkono Rais.

"Hata hivyo Rais mwenyewe alipotupa jicho na kuniona aliwapita wote na kuja kunisalimia na tulishikana mikono na akanieleza kuwa mambo yako tumeyafanyia kazi ,kwa kweli tangu siku hiyo watu waliniheshimu sana.

Angefanya haya enzi hizi kule nchini 'PORTLAND' angejua nini maana ya GANGNAM STYLE.
 
Maelezo ni mengi sana sijasoma yote isipokua jina la mwisho la huyo bwana wala hakua muhaya wala mnyambo..huyo alikua ni Mhangaza ambaye lazima alitokea Rwanda..so tungeongozwa na mnyaRwanda
 
Wahaya wamemtania sana Mwalimu, mwanzo nilimjua yule wa matofali kumbe yupo na huyu.

Ile era ilikua ni shifting era, kulikua hakuna namna angekabidhiwa kijiti. Na ni kweli hicho kipindi ndicho kipindi hautakiwi kumtaja Rais hovyo, In fact nashangaa kwanini maombi yake waliyapokea bila kumletea shida.

Pengine Mwalimu alipoambiwa kuna mtu anataka kugombea urais halafu akauliza anaitwa nani? Anajibiwa "Leonard Rwinde.." akasema tu "Basi usimalizie muache tu"
 
Mzee alikuwa kichwa na maono ya mbali, karibia vyote alivyopinga mpaka leo vinapingwa.
Kuweka watu kizuizini bila kusikilizwa, Rais kupewa mamla ya kuteua viti maalumu, Raisi kutoshitakiwa nk.

Ipo siku yote haya yatabadilika.
Mkuu kweli kabisa. Imenivutia mpaka nimerudia kusoma mara mbili.Mzee ni kichwa sana
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom