Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Sisi binaadamu tunajipenda sana, katika kujipenda kwetu ndio maana tuko tayari kuwaona wengine wakiumia ili sisi tuone raha, yaani kuna watu wengine hufurahi sana kuwaona wengine wakiumia kihisia.
Kwa kujipenda kwake binadamu anataka aone kuwa yeye peke yake ndiye anafanikiwa maishani, yeye peke yake ndiye anayepata sifa na yeye peke yake ndiye anayepewa heshima. Ili hayo yatimie ni lazima binadamu wengine wawe chini yake, kwa maana kwamba wasifanikiwe, kwani kufanikiwa kwao kutakuwa na maana ya kumzidi yeye.
Wote tunajua maana ya chuki, ingawa kuna uwezekano mkubwa wengi wetu hatujui ni kwa kiasi gani chuki dhidi ya wengine hutuharibia maisha yetu na kutufanya kila siku kubaki katika hali duni tuliyomo.
Hebu jaribu na wewe kufanya utafiti mdogo. Ni mtu au watu gani ambao wewe unawafahamu vizuri kuwa wana chuki dhidi ya watu wengine?
Ninaposema chuki nina maana ya watu ambao wenzao wakipata wao hujisikia vibaya, wenzao wakifanikiwa wao huponda na kudharau mafanikio yao, wenzao wakijitahidi kupanda kimaendeleo wao huwashusha, wenzao wakisifiwa kwa jambo zuri wao hujitahidi kuwaharibia majina na tabia nyingine za namna hiyo.
Hebu waangalie watu hao ambao wana tabia kama hizo, halafu uangalie au upime kiwango cha maendeleo yao, unaweza ukapima pia aina ya maisha wanayoishi. Bila shaka utagundua kwamba kwa kiwango kikubwa ni watu ambao wana maisha duni siku zote na ni watu ambao maisha yao yanaonekana yamejaa nuksi na hawana furaha katika maisha.
Sisemi hata hivyo kwamba watu wote wasio na kitu wana chuki, au sisemi kuwa watu wote wenye uwezo hawana chuki, hapana. Kuna watu wenye chuki lakini ambao wana uwezo, ingawa uwezo huo kwa kawaida huzongwa na mikosi tele na kukosa amani ya nafsi.
Kuna watu wasio na kitu ambao hawana chuki hata asilani, lakini hawa maisha yao siku zote yamejaa matumaini na furaha ya kweli. Chuki kwenye maisha ina kazi moja tu, nayo ni kuhakikisha kwamba anayeifuga hata siku moja hapandi juu kimafanikio, na anaishi kwenye fadhaa, wasiwasi na kukosa furaha siku zote.
Chuki hupoteza muda wetu, hutuharibia mahusiano na watu, hutukosesha bahati na baraka, sasa kwa nini mtu usiamue kubadilika?
Ukianza kuondoa chuki moyoni au rohoni mwako ni wazi utaanza kujisikia mwepesi zaidi kimwili na kiakili na ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba utaanza kuona mabadiliko kwenye shughuli na mambo yako.