KUTOROKA 'MWAMBANI' - Kinachokuzuia si kuta ndefu, bali akili yako.

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,629
24,532
KUTOROKA MWAMBANI - kinachokuzuia si kuta ndefu, bali akili yako.


Awali ya yote nashkuru sana kwa watu wote ambao wamekuwa wakifuatilia simulizi zangu na hata mikasa mbalimbali ambayo narusha ndani ya ukumbi huu, nawashukuru kwa kila ‘like’, ‘comment’ na hata ‘pm’ zenu, hakika zanitia moyo katika namna kubwa. Kuna siku mtu mmoja aliwahi niuliza, unawezaje kuandika mavitu marefu hivi, hauchoki? Unawezaje? Yani mimi siwezi kabisa! Sikushangazwa sana na maswali lake maana sisi binadamu, kama ilivyokuwa kwa maumbo ya vidole vyetu mkononi, hatufanani.

Kuandika ni ‘passion’ yangu. Ni kitu ambacho kama nisipokifanya kwa muda basi nahisi kupungukiwa na jambo maishani hivyo kuna muda nafanya kutimiza tu haja ya moyo wangu. Kwa wale ninaowakera, samahani, na kwa wale wafurahiao, basi karibuni jamvini.

Nisiwachoshe sana

Nadhani kuna baadhi ya mambo tumezoea kuyaona kwenye runinga. Tunaamini kwenye maisha halisia hayawezi kutokea kwahiyo tunatazana kufurahia tu ubunifu wa watu na uwezo wao wa kuvaa uhusika.

Kuna mambo tunaamini ni ya kwenye ulimwengu wa tamthilia tu. Mambo ambayo yanaaminika kuwezekana nyuma ya kioo cha televisheni tukiwa tumeketi vitini na kula popcorn. Zaidi tukitoka hapo tukawahadithie marafiki, majamaa na washkaji vijiweni.

Tunaweza tukaliona hilo kwenye moja ya tamthilia kama vile PRISON BREAK ambapo wafungwa kadhaa hupanga, kuazimia na hata kutekeleza mpango wao wa kutoroka dhidi ya gereza gumu walilomo. Tulifurahia tamthilia ile, na kuipenda pia. Kuna wengine bado huifuatilia hata sasa lakini ni wazi ni wachache wanasadiki kitu kama hicho kinawezekana. Watu kuwa na akili vile? Kupanga mambo kama yale? Na hata zaidi kuwa na ngekewa kama ile? Ah - ah! Hapana, haiwezekani.

Pengine tukisoma mkasa huu, tunaweza tukabadili mawazo yetu hayo. Na hata kuafiki kuwa muda mwingine binadamu akiamua kutumia akili yake yote na ‘determination’ ya hali ya juu, aweza kufanikisha lolote. Hata kama ni uhalifu basi yapasa kumpongeza.

Karibu…

Alcatraz ilifunguliwa kama gereza lenye ulinzi mkali (Maximum security prison) mnamo mwana 1934 ambapo hapo awali katika eneo hilo kulikuwapo na kambi ya jeshi. Kwa utani gereza hilo lilikuwa likienda kwa jina la ‘the rock’(mwamba), jina ambalo lilipatikana kipindi hicho wakati bado likiwa ni eneo la kambi ya jeshi na eneo hilo liliitwa hivyo kwasababu ni kweli ndivyo lilivyokuwa, yaani mwamba ambao ulikuwa umejitenga kwa takribani maili moja na robo toka fukwe ya San Francisco. Na kwasababu hiyo basi, yaani kuwa mwamba, ikawalazimu wanajeshi kuuleta udongo kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya kupanda bustani.

Basi kutokana na sababu hii, yaani gereza kuwa kisiwa cha mwamba kilichojitenga kwa umbali fulani toka kwenye ulimwengu mwingine, ikasadikika kuwa eneo hilo ni salama zaidi kwa kuweka wafungwa. Zaidi ya hapo, maji yanayozunguka kisiwa hiki yalikuwa ni kati ya nyuzi joto 8°c mpaka 12°c kwa mwaka mzima, maji ya baridi kabisa kwa binadamu kuweza kuogelea mpaka aweze kufika nchi kavu. Na kama haitoshi maji hayo ya baridi yanaambatana na mkondo mkubwa wa bahari uelekeao mbali zaidi na nchi kavu, yaani baharini zaidi.

Hivyo basi kutokana na sababu hizo ilileta mantiki kuwa eneo hilo ni eneo sahihi kabisa kwa wafungwa hatarishi. Endapo wakiwekwa hapo basi watatumikia kifungo chao vema pasi na haja ya kuhofia juu ya uwepo wao.

Hapo nyuma kuliwahi kutokea na wafungwa waliothubutu kutoroka kwenye gereza hilo, kwa idadi ni thelathini na moja ndani ya miaka 29 tangu Alcatraz ipate kuanzishwa, lakini wote hao hakuna hata mmoja aliyefanikiwa. 23 walikamatwa, sita wakadunguliwa na risasi na kuuawa na wawili wakazama kufa ndani ya maji.

Kuna mfungwa mmoja aliyekuwa anaitwa John Paul Scott yeye alifanikiwa kutoroka ndani ya gereza na akaogelea kwa umbali wa kama maili 2.7 lakini akaja kupatikana fukweni akiwa amedhaniwa amekufa. Taarifa ilipotolewa, bwana huyo akatambuliwa ni mtu aliyetoroka gerezani hivyo akakamatwa na kurejeshwa tena gerezani.

Muda ukiwa unaenda zaidi, gereza hilo likaanza kupata hitilafu za matengenezo na bajeti ya kurepea ikawa haikidhi mahitaji, hili likawa ni moja ya nyenzo muhimu sana kwenye kusaidia kutoroka kwa wafungwa. Lakini hilo lilisitusahaulishe ya kwamba bado mazingira hayakuwa rafiki kabisa kwa mfungwa yeyote kutoka katika eneo hilo, ama tuseme hakuna afisa ambaye angeliwaza kuwa kuna mfungwa anaweza kutoka kwenye mikono yao, na atakapopatikana wa kufanya hivyo basi ataishia kujifia tu baharini!

Mungu si athumani, watu hao wakapatikana. Watu wenye akili za mafikirio, mioyo ya kujaribu na mikono ya kutenda. Watu ambao mpaka leo hii wamebaki kwenye historia ya kutenda yale yaliyokuwa yanahisiwa kutowezekana kutendeka kwenye macho ya binadamu wengine.

Watu hawa hawakujali historia ya kutisha kuhusu mahali hapa.

‘F*ck the history, we gonna make our history!’


KIKUNDI CHA WATOROKAJI.

Mosi, walikuwa ni wadugu wawili wa damu, bwana John William Anglin na kaka yake Clarence Anglin (Anglin brothers) ambao wote walikuwa kwenye miaka ya kati ya thelathini. Mabwana hawa tunaweza tukawatambua kama ndugu katika uhalifu (relatives in crime), walikuwa ni wadugu walioshibana tangu utotoni. Na kwa mujibu wa rekodi zao walikuwa ni waogeleaji wenye ujuzi usio wa kawaida wakiwashangaza ndugu zao kwa kuweza kuogelea kwenye maji ya baridi ya ziwa Michigan ambalo lilikuwa likielelea barafu.

Rekodi ya uhalifu ilianza kwenye miaka ya 1950 wakivamia mabenki haswa yakiwa yameshafungwa kwa dhamira ya kutowaumiza watu. Kwa mujibu wa maelezo yao wadugu hawa wawili katika mavamizi yao yote ya mabenki waliwahi kutumia silaha mara moja tu, tena toy. Walikamatwa mnamo mwaka 1956 na wote wakahukumia miaka 20 jela katika gereza la Florida, Leavenworth na kisha Atlanta. Kwasababu ya kujaribu mara kadhaa kutoroka kwenye gereza la Atlanta, basi ndipo wakahamishiwa kwenye ‘gereza la wagumu’, mwambani, Alcatraz. Joh akipewa namba AZ1476 na Clarence nambari AZ1485.

Mbali na wao, kulikuwapo pia na bwana Frank Morris, naye miaka yake ikiwa si mbali na wale wadugu, bwana huyu alitekelekezwa na wazazi wake tangu utotoni akiwekwa kwenye sehemu za mahifadhi na kutoroka na akiwa na rekodi ya kuzama na kutoka jela tangu akiwa na miaka kumi na mitatu.

Inaripotiwa kuwa bwana huyu alikuwa ni miongoni mwa watu wenye uweledi mkubwa kwenye mambo ya utumizi wa akili akiunda asilimia mbili za watu wa juu kabisa kwenye ulimwengu wa intelijensia ambapo kwa mujibu wa vipimo vyake vya uwezo wa akili (IQ) alikuwa na IQ ya 133.

Alitumikia kifungo kwenye gereza la Florida na Georgia kisha gereza la Louisiana ambapo alitoroka akiwa anahudumia kifungo cha miaka kumi kwa uvamizi wa benki. Alikuja kukamatwa mwaka baadae na ndipo akapelekwa gereza la wagumu, Alcatraz, chini ya namba AZ1441.

Mhusika wa mwisho wa kundi alikuwa anajulikana kwa jina la Allen West, mwanaume aliyekuwa na miaka 31 wakati akiingia Alcatraz. Bwana huyu naye alikuwa na rekodi ya kuwekwa gerezani tangu alipokuwa na miaka 14 akiwa amepitia na kuhudumia magereza kadhaa. Maishani ana rekodi ya kukamatwa mara 20.

Bwana huyu alikamatwa kwa kuiba gari mwaka 1955, akafungwa gereza la Atlanta na kisha Florida. Baada ya kufanya jaribio la kutoroka pasipo mafanikio huko gereza la Florida ndipo naye akahamishiwa kwenye gereza la wagumu chini ya namba AZ1335.

Bwana huyu, tutakuja kuona vema baadae, ndiye mtu pekee kwenye kiku hiki ambaye hakufanikiwa kutoroka gerezani.

Sasa kikundi kilikuwa kimekamilika. Tuanze kuangazia tukio la kutoroka…


TUKIO LA KUTOROKA.

Inasemekana kuwa bwana West ndiye aliyemfuata bwana Frank Morris kuhusu mpango wao wa kutoroka mapema mnamo mwaka 1960 japo pia ikiaminika kuwa utorokaji huu ulikuwa chini ya uongozi wa bwana Morris. Ni wazi walikuwa wananufaika na uwezo mkubwa wa akili yake.

Bwana West alikuwa anafahamu kuhusu mlango mdogo wa chemba kwenye Bloku B ambao hakuwa umefunikwa na saruji vizuri. Kwahiyo basi kama ni kweli kuhusu hilo, mlango huo utawawezesha kwenda kwenye paa ya gereza wakitokea ndani.

West pia akaendelea kupembua na kufanyia uchunguzi wa kina kwenye mwonekano na mpangilio wa jengo hilo la gereza ili apate kutambua udhaifu wake zaidi.

Kuelekea mwezi wa tisa mwaka 1961, wale wadugu, bwana John na Clarence, Morris na pia West wote wakatuma maombi ya kuwekwa kwenye vyumba vinavyofuatana kwa ukaribu huko kwenye Bloku B, chini ya eneo lile lenye mlango dhaifu. Bahati maombi yao yakakubaliwa.

Pengine tunaweza kusema kuwa hili lilikuwa ni mojawapo ya makosa makubwa ambayo maafisa wa gereza hili walilifanya. Lakini kwanini wasifanye hivyo ingali wanajiamini hakuna lolote litakalotokea? Na si tu wao wakiamini hivyo bali hata wale walio nje ya gereza hilo. Wafanye tu wanachokitaka, kwani kutakuwa na madhara gani? Hawakuona haja ya kuhofia.

Lakini katika moja ya makosa makubwa unapokuwa kwenye uwanja wa ‘vita’ basi ni kum- ‘underestimate’ adui yako. ‘don’t look down on your enemy, and don’t give him your back.’ Walikuwa wanaenda kufundishwa somo hilo adhimu.


MPANGO WA KUTOROKA.

Hatua ya kwanza ya mpango (Ulaghai).

Katika gereza hili shida si tu kuvuka kuta zake ndefu na ngumu bali pia namna utakavyoweza kufikia ardhi kavu ambayo ipo umbali wa maili moja na robo pasipo kukamatwa. Umbali ambao umemezwa na maji ya bahari tena ya baridi kupita kiasi na kujazwa na mkondo mkubwa wa maji.

Kwahiyo basi ili kulikamilisha hilo na mipango yao mengine ipate kwenda kama walivyoazimia, wakakubaliana kuwa wanahitaji ‘Ulaghai’. wanahitaji kuwapumbaza maafisa wa gereza ilhali wao wakiwa wanatekeleza kusudi lao la kutoroka. Iliwalazimu watafute namna ambayo itawakawiza walinzi kujua kama wapo ndani ya gereza.

Watalifanyaje hilo?

Basi kwasababu kulikuwa na utaratibu wa kukagua vyumba vinavyowatunzia wafungwa kila baada ya muda fulani, watorokaji hawa wakaafiki kuwa hilo ndiyo jaribu lao la kwanza wanalotakiwa kulishinda. Kwahiyo basi jamaa hawa wakatengeneza midoli ya vichwa vya binadamu kwa kutumia mchanganyiko wa sabuni, vumbi la saruji, dawa ya meno, toilet paper na nywele halisi za binadamu!

Walipomaliza kazi hiyo, wakaviweka vichwa hivyo kitandani na kuvifunika nusu kwa shuka ili kuwapumbaza walinzi

Basi ikiwa ni June 12, walinzi bado wakatambua kuwa watorokaji wale wapo kitandani wamelala. Ilikuwa vivyo mpaka pale mlinzi mmoja aliyejawa na mashaka alipoingia ndani ya chumba cha Morris na kusukuma kichwa kilichopo kitandani, akatahamaki kinadondoka chini! Puh! Hapo ndipo wakajua kuna kitu hakipo sawa, lakini wakiwa tayari wameshakawia sana.

Mpaka leo hii mdoli huu wa kichwa umehifadhiwa tena ukiwa na uharibifu wake wa upande mmoja kama ulivyodondoka baada ya kuguswa na mlinzi.

Haijulikani ni nani aliyesuka mpango huo, lakini ilikuwa inafahamika kuwa bwana Clarence alikuwa ni kinyozi hapo gerezani hivyo ndiye mtu mwenye uwezo wa kupata nywele kwa urahisi.

Lakini pasipo kujali hayo, hatua hii ya kwanza ilifanikiwa!

Hatua ya pili (kuvunja).

Baada ya kuweka midoli ile vitandani, jamaa hawa wakaanza kushughulikia namna ya kutoka kwenye vyumba vyao. Kwenye kila chumba kulikuwapo na kijimlango mdogo wa nyavu mahususi kwa kuingiza hewa. Kwa upana ilikuwa ni inchi tano na kwa urefu inchi tisa na nusu.

Pengine kwenye upembuzi wake wa jengo hilo, bwana West alibaini kuwa ukuta uliokuwa umeshikilia milango hiyo midogo ulikuwa hauzidi upana wa inchi sita hivyo inawezekana kwa kila mtu kuuathiri ukuta huo ili wapate kutengeneza sehemu ya kupitishia mwili wa mtu mzima.

Basi kwa mwezi mzima, kila mtu akawa anachimba mashimo madogo madogo yanayofuatana kandokando ya kijimlango hicho, wakitumia nyenzo kama vile vijiko walivyokuwa wanaiba jikoni, na kifaa kimojawapo chenye ncha walichokinyofoa kwenye mashine ya kufanyia usafi.

Kwasababu uchimbaji wa mashimo hayo ungesababisha kelele ambayo ingeliwashtua watu, basi kila walipokuwa wanafanya vivyo, bwana Morris akawa anapiga muziki kwa kutumia kifaa chake cha ‘accordion’ kuzalisha melodi za kumeza kelele.

Mashimo hayo madogomadogo mwishowe yakaja kuwawezesha kuondoa kijimlango kile na msingi wake kabisa hivyo kupata nafasi ya kutosha kupita mwili wa binadamu. Na mashimo hayo wakawa wanayaziba kwa kutumia vifaa vya muziki kama vile gitaa na vifaa feki kama vile ‘boards’.

Kwahiyo basi mashimo hayo yatawawezesha kutoka kwenye vyumba vyao na kufikia kwenye korido maalum isiyokuwa na ulinzi. Korido ambayo hutumika kupitishia mabomba ya maji, mabomba yenye nyaya za umeme na kadhalika kwenda maeneo mbalimbali ya jengo, kwa kizungu huitwa utility corridor ama utility tunnel.

Kwa kutumia korido hiyo watakuwa na uwezo wa kuambaaambaa mpaka juu ya paa za vyumba vyao ambapo huko walipafanyia kazi kwa miezi kadhaa.

Baadhi ama watorokaji wote hao walishawahi kupewa ruhusa hapo nyuma ya kuhusika kwenye matengenezo kadhaa kwenye eneo hilo (kumbuka hapo awali tulisema bajeti ya kutunza gereza hili ilikuwa haikidhi mahitaji hivyo kutumia wafungwa ilikuwa ni kitu cha kawaida).

Basi wakiwa kwenye marepeo hayo, bwana West aliwahi kuwaambia walinzi kuwa anahitaji kuweka mashuka kuziba sehemu anapofanyia kazi sababu vumbi lilikuwa jingi na endapo lisipozibwa basi litatapakaa gereza zima, lakini kiuhalisia bwana huyu alikuwa anatumia mashuka hayo kuzibia mambo waliyokuwa wanayafanya huko.

Hivyo basi sehemu hii ikawa ni sehemu maalum kwa wao kufanyia kila kitu walichokuwa wanakihitaji kwa ajili ya kutoroka. Huko ndipo walipotengenezea hata ile midoli ya vichwa waliyotumia kuwapumbazia walinzi, nyenzo na vifaa vingine ambavyo wangevitumia kukamilisha haja yao.

Sasa ulipowadia usiku wa kutoroka, watu wote hao wakafika kwenye eneo lile walipokuwa wanafanyia kazi zao za siri isipokuwa bwana West pekee. Bwana huyu alishindwa kabisa kuvunja lile eneo lenye kijimlango cha hewa ndani ya chumba chake hivyo hakuwa na ‘access’ ya siri ya kufika huko isipokuwa kutumia njia ya kuongozana na walinzi, njia ambayo asingeweza kuendana nayo.

Kwahiyo basi, bwana West akaachwa na wenzake.

Watorokaji, ambao sasa walikuwa watatu mbali na West, wakafanikiwa kufika sehemu ile ya siri walipokuwa wanafanyia kazi zao. Huko wakakwea bomba lililokuwa limepachikwa ukutani, wakapanda kuelekea paa ya juu kabisa, ambapo hapo wakasukuma kijimlango kidogo cha hewa ambacho walishakishughulikia hapo kabla wakiwa wanafanya kazi kwenye lile eneo lao la siri.

Wataalamu wanaamini kuwa sauti iliyosikika kwenye majira ya saa nne na nusu usiku ilikuwa ni ya kijimlango hicho kizito kikiangukia kando.

Watu hao baada ya kufika huko juu kabisa ya gereza wakashuka chini, yani kwa nje sasa ya gereza, kwa kuambaa na bomba lililojishkiza ukutani na kisha wakafanya namna ya kuvuka fensi ya gereza na kujikuta nje kabisa ya uzio. Na hapo ndipo tunaingia hatua ya tatu sasa, wameshatoroka gereza, sasa inafuata kutoroka kisiwa.

Hatua ya tatu (kutoroka kisiwa).

Mabwana hawa walipokuwa kwenye chumba chao walichokuwa wanatumia kutengenezea dhana zao, walipata kutengeneza jaketi za kuwasaidia majini kwa kutumia makoti ya mvua waliyoyapata gerezani, lakini pia walitengeneza boya
kubwa la mpira (rubber bag) ambayo walilitengeneza kwa kutumia malighafi ya makoti ya mvua takribani hamsini.

Makoti hayo wakayashona kwa kutumia mashine zilizomo ndani ya gereza na kisha wakaya - ‘slid’ kabisa wakitumia joto kali la mabomba ya ya kupitishia moshi utokao kwenye moto unachemshia na kupikia ndani ya gereza. Mabomba hayo yalikuwamo kwenye ile ‘utility corridor’.

Boya hilo walilijaza kwa kutumia kifaa cha muziki kinachoitwa ‘concertina’, ambapo huzalisha melodi za kimuziki kwa kukitanua na kukiminya. Vifaa hivi vya muziki vilikuwa vinapatikana ndani ya gereza kwa ajili ya wafungwa.

Kwa mujibu wa maelezo ambayo bwana West alikuja kuyatoa kwa FBI hapo baadae, mpango wao ulikuwa ni kuambaa majini mpaka kwenye kisiwa cha kilichopo kaskazini wa eneo la gereza kisha waambae tena mpaka ardhi ya San Fransisco ambapo huko wataiba gari na mavazi.

Sasa basi kule gerezani baada ya kubainika kuna watu hawapo, vyumba vyote vya gereza vikafungwa msako ukianza. Maafisa wakagundua kuhusu yale mashimo ndani ya vyumba vya waliotoroka, pia wakabaini alama za viatu mpaka kuelekea juu kabisa ya paa la gereza.

FBI walichukua na kusimamia kazi hii wakitangaza msako mkali pamoja na maafisa ulinzi wa pwani (coastguard) pamoja na maafisa magereza lakini waliotoroka kamwe hawakuonekana. Hata kama wanaume hao walifanikiwa kutoroka salama, kilichotokea baada ya hapo bado kimekuwa ni kitendawili mpaka leo hii.

NADHARIA ZA NINI KILITOKEA.

Hapa kuna mawazo mawili juu ya tukio hili, mosi ni kwamba watu hao walifanikiwa na kujiendea zao au walipotelea kwenye safari yao kutafuta ardhi kavu ya San Francisco. Tuanze na hiyo inayoamini kuwa watu hao walipotelea kwenye safari ya kutafuta nchi kavu.

WATOROKAJI WALIFIA MAJINI.

Maji ya mahali hapa kama tulivyoona hapo awali yamejawa na mkondo wenye nguvu ambao ungewazuia watorokaji kufanikisha malengo yao. Na sababu hiyo basi inaaminika kuwa ilikuwa ni ngumu sana kwa watorokaji kutumia boya lao kuelekea kaskazini mwa eneo hilo kama walivyoazimia.

Na zaidi wataalamu wakatengeneza boya kama lile lililotengenezwa na watorokaji wale kisha wakalijaribu na kubaini kuwa lisingeweza kuwabeba wanaume wale watatu, wawili iliwapasa wasilitumie ili kuendelea kutunza upepo uliopo ndani ya boya.

Nyuzi joto ya maji ilikuwa ni 12°c, hivyo basi kama boya lile lingeshindwa kuwabeba na kuwamwagia majini basi wangelidumu kwa takribani masaa mawili tu kabla hawajaanza kupoteza ufahamu.

Mnamo tarehe 12 June, wakaguzi wakaona mapakuo ya kupakulia maji yakiwa yanaelea baharini. Mapakuo haya yalikuwa yametengenezwa kwa mkono tu. Mnamo tarehe 14, mabegi ambayo yalikuwa yamefumwa na makoti ya mvua yakaonekana baharini. Mabegi hayo yalionyesha wazi kuwa yalikuwa yakimilikiwa na wale watorokaji. Ndani kulikuwa na picha za wale wadugu wawili na familia zao, orodha ya namba za watu na barua aliyoandikiwa bwana Clarence akiwa gerezani.

Hivyo kwa shahidi hizi, inafanya iaminike kuwa huenda safari ya watorokaji hawa ilikumbwa na balaa.

Mnamo tarehe 15 June, jaketi la kuogelea likapatikana likiwa linaelea baharini, na jaketi la pili likaja kubainika mnamo tarehe 22 mashariki ya mbali ya kisiwa cha Alcatraz.

Na kwakuwa watu hao walikuwa hawana pesa kabisa ya kujikimu, ilitarajiwa kwamba wakifika kwenye nchi kavu waweza kufanya uvamizi ili wapate chakula, mavazi na usafiri, lakini hakuna taarifa yoyote ya uvamizi iliyoripotiwa kwa muda.

FBI wanakiri kwamba hakuna ushahidi wowote ule aidha ndani ya Marekani ama nje unaothibitisha kuwa watorokaji hao waliishi.

Zikiwa zimepita majuma sita baada ya watorokaji wale kutoroka gerezani, wafanyakazi wa meli kubwa ya mizigo iliyokuwa inatembea baharini ikaona mwili wa mtu mfu ukiwa unaelea lakini hawakutoa taarifa yoyote ile mpaka muda mrefu ulipopita waliporudi San Francisco na mwili ule haukuonekana tena.

WATOROKAJI WALIFANIKIWA KUISHI.

Mosi, miili ya watu waliokufa katika eneo hilo huwa inaelea kwa muda, hivyo basi kama watorokaji wale wangelikuwa wamekufa, kwa msako ule uliokuwa umefanyika, basi ni wazi miili yao ingelionekana.

Lakini zaidi, bwana David Widner, ambaye ni mpwa wa wale wadugu wawili waliotoroka, alisema kuwa kaka mkubwa wa wale wadugu ambaye anaitwa bwana Robert Anglin alikiri kwa dada yake akiwa kitandani akijifia kuwa asihofu kwani ndugu zao wapo salama, amekuwa akiwasiliana nao, hivyo hana haja ya kuhofia.

Na zaidi ya hapo, mpwa huyo alisema kuwa bibi yake, ambaye ni mama wa wale wadugu alikuwa sometimes akipokea maua na kadi zenye sahihi za watoto wake.

Kama haitoshi, ndugu za wale wadugu wawili waliotoroka wanakiri kwamba kwenye misiba kadhaa ya familia walikuwa wanawaona wanawake wawili wasiowafahamu ambao walikuwa wakivalia kofia na kujijaza ‘make up’, hivyo wakidhania kwamba huenda ni ndugu zao wale wawili huja kutoa heshima zao za mwisho.

Bwana West, jamaa aliyeachwa na wenzake huko gerezani, alihusika kuwasaidia FBI kwenye msako huo pasipo mafanikio. Alikuja kuachiwa mnamo mwaka 1967 lakini akadumu uraiani kwa mwaka mmoja tu kabla hajakamatwa mara kadhaa kwasababu za uvamizi. Alikufa mwaka 1978.

Gereza la Alcatraz lilikuja kufungwa March 1963, mwaka mmoja tangu watorokaji watoroke. Nao FBI wakafunga kesi hiyo rasmi mwaka 1979 baada ya miaka 15 ya upelelezi uliokosa mafanikio. Kwa kunukuu walisema,

“Ni moja ya mkasa ambao tungependa kuusuluhisha.”
 
Gereza la Alcatraz
 

Attachments

  • alcatraz 2.jpg
    alcatraz 2.jpg
    9.9 KB · Views: 117
  • alcatraz.jpg
    alcatraz.jpg
    8.6 KB · Views: 91
Akili hukomazwa kwa kufikiri mambo magumu na kutafakari jinsi ya kuyarahisiha na kutenda hasa yale yasiyowezekana kwa macho ya kawaida.
Nadhani mojawapo ya nyenzo kwenye kufanya lolote kwanza ni kuligawa jambo lako katika vipengele vidogovidogo na kila kipengele kukichukulia muda kukitafutia ufumbuzi. Hauweza kulifanya jambo lote kwa pamoja kama lote.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom