SoC03 Kuongeza uwajibikaji katika nafasi za kuteuliwa

Stories of Change - 2023 Competition

Kidaya

Member
Dec 20, 2011
55
49
Utaratibu wa uteuzi kwa jinsi mamlaka husika itakavyoona inafaa huenda ulifaa sana miaka ya zamani kutokana na uhaba wa wasomi na sababu za kiusalama. Kwa miaka ya sasa ambapo mbinu za kiusalama zimekuwa za kisasa zaidi na wanafunzi takriban 100,000 wanajiunga na vyuo vikuu kila mwaka, nchi yetu ina utajiri wa wasomi wa kila aina wanaoweza kufanya kazi kwa weledi na mafanikio katika nafasi za kuteuliwa.

Kwa taasisi za binafsi nafasi za uongozi huwa anateuliwa mtu ambae ni bora zaidi kielimu, ujuzi na uzoefu ili kuwaongoza wengine kufikia malengo ya taasisi kwa muda atakaopewa. Kwa taasisi za umma, nafasi nyingi za uongozi hazina sifa za elimu, ujuzi na kiutendaji wala muda wa kuhudumu bali zinategemea zaidi matakwa ya mamlaka ya uteuzi. Nafasi kama za wakurugenzi wa halmashauri, idara na taasisi, makatibu tawala wilaya na mikoa, wakuu wa wilaya na mikoa, makatibu wa wizara, mawaziri, mabalozi n.k. huweza kuteuliwa mtu yeyote kwa muda fulani kwa kadri mamlaka itakavyoona inafaa wakati mwingine bila ya mteuliwa kuwa tayari kuitumikia nafasi hiyo.

Utaratibu huu una changamoto zifuatazo;

1. Kuwa na mipango na miradi isiyokamilika
Kila mteuliwa anakuwa na mipango na vipaumbele vyake. Mfano, mteuliwa huyu anapoanza kutekeleza kipaumbele chake cha tatizo la elimu, anaweza kuhamishwa na kuletwa mteuliwa yule ambaye kipaumbele chake ni utalii, baadae kidogo nae anahamishwa na kuletwa mteuliwa mwingine ambae kipaumbele chake ni afya. Hii hufanya kuwa na mipango na miradi inayoishia nusunusu (kila kiongozi anaanza upya), badala ya kukamilisha mradi mmoja na kisha kwenda kuanza mradi mwingine kutokana na rasimilimali zilizopo.

2. Mwingiliano kwenye utendaji
Tumewahi kusikia kuwa sababu ya mteuliwa fulani kuhamishwa au kuteguliwa ni hapatani au hashirikiani na mteuliwa mwingine. Sababu huweza kuwa wa chini kumdharau wa juu kwa sababu kuwa kamzidi elimu au wa juu kutaka aonekane yeye tuu ili adumu kwenye nafasi hiyo. Hali hii huzorotesha utendaji kazi wa taasisi kwani badala ya watu kushirikiana kufanya kazi ili kufikia malengo, wanaanza kushughulikiana, kugawa walio chini yao na kuchongeana kwa mamlaka za uteuzi.

3. Kudumaza ubunifu
Mara nyingi tumeona wateuliwa wakifanya na kutetea jambo ili kufurahisha mamlaka ya uteuzi hatakama halina tija. Pia, mamlaka ikisifia jambo fulani kwenye eneo moja, wateuliwa wa maeneo mengine watataka na wao waonekane wakifanya jambo hilo. Hali hii hudumaza ubunifu kwa viongozi hawa katika kutumikia nafasi zao na kujikuta wakifanya jambo kwa kuigana au kusubiri maelekezo.

4. Kujenga hisia za upendeleo
Mamlaka zinapoteua watu wa kushika nafasi fulani bila uwazi wa sifa zinazohitajika, ni rahisi kujengeka kuwa fulani kateuliwa kwa sababu ya kufahamiana, ni ndugu wa fulani au kulipa fadhila. Hali hii huvunja moyo na kushusha morali ya kazi kwa watu wengine kwa kuona kwamba kuipata nafasi fulani sio kwa juhudi na utendaji wako bali sababu zingine za pembeni.

5. Ufanisi mdogo unaopelekea kupata hasara
Taasisi ambazo viongozi wake wanateuliwa bila kuwepo kwa sifa zilizofanywa ateuliwe zimekuwa na ufanisi mdogo kwa viongozi kushindwa kumudu majukumu yao ipasavyo hali inayopelekea kupata hasara kama inavyoripotiwa katika ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG). Wateuliwa wengine huweza kufanya ubadhirifu wa fedha ili siku akitenguliwa awe vizuri kiuchumi.

6. Usumbufu na gharama
Mteuliwa huweza kupangiwa mbali na makazi yake na shughuli zake za kila siku hivyo kulazimika kubadili kuhama na familia yake kwenda kuanza maisha mapya. Baada ya muda mteuliwa huyu huweza kuteuliwa kwenda mahali pengine akalazimika tena kuhamisha familia. Na hatimae mteuliwa huyu anaweza kutenguliwa hivyo kulazimika kurudi kule alipokuwa na makazi kuanza upya maisha kwani atakuta nafasi yake ya zamani imeshachukuliwa na miradi yake imesimama. Hii hupelekea baadhi ya wateuliwa kukataa teuzi baada ya kupima 'risk benefit ration'.

Ili kuongeza uwajibikaji katika nafasi za uteuzi, tuzingatie;

1. Sifa za elimu, ujuzi na utayari

Vigezo vya elimu na ujuzi vinatumika dunia nzima kupima uwezo kiakili wa mtu kumudu majukumu yake. Ni vema nafasi hizi ziwe zinatangazwa zikiwa na sifa zinazotakiwa ili wenye sifa waombe na kati yao walio na uwezo kuliko wengine ndio wateuliwe. Utaratibu huu unaotumiwa na taasisi za binafsi, umekuwa na mafanikio makubwa sana tunayoyaona katika taasisi mbalimbali kama mabenki, makampuni ya simu n.k. Kutozingatia sifa kunapelekea watu kuwa na tabia za kujipendekeza (uchawa) kwa mamlaka ili wateuliwe.

2. Muda wa kushika nafasi
Taasisi nyingi za binafsi zimeweka kipindi kimoja cha muda wa miaka mitatu kwa mteuliwa, na inawezekana kuongezewa muda kutokana na utendaji wake kuwa wa mafanikio. Kipindi hiki angalau kinatosha kupima uwezo wa mtu kwa kumpa muda wa kutosha wa kutuliza akili, kuhimili mazingira mapya na kupanga mipango yake ili kufikia malengo ya taasisi. Kumteua mtu na kumtengua au kumhamisha baada ya muda fulani ni vigumu sana kupata matokeo tarajiwa. Kama madiwani, wabunge na rais tunawapima utendaji wao kwa miaka mitano, kwanini na viongozi wakuteuliwa wasiwe na muda maalum wa kuhudumu kwenye nafasi zao? Ni wazi hili linawafanya wateuliwa kuishi kwa hofu na kujipendekeza ili wasipoteze nafasi zao, hali inayopelekea utendaji hafifu.​

Mtendaji NMB.GIF Taarifa kutoka tovuti ya NMB ikionesha namna mteuliwa alivyopatikana.

3. Kuwapa malengo yanayopimika
Nafasi nyingi za kuteuliwa zimekuwa na utendaji kazi wa mazoea kutokana na wahusika kutowekewa malengo yanayopimika. Mtu anapopewa nafasi tumdai mafanikio fulani baada ya muda fulani, mfano kiongozi wa hospitali apewe lengo kama, baada ya miaka mitatu vifo vitokanavyo na uzazi vipungue kuwa chini ya 25% ya vilivyo sasa, taasisi iweze kujiendesha n.k. Hali hii itamfanya mteuliwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu ili kufikia malengo aliyopewa. Kutokuwa na malengo yanayopimika kunadumaza taasisi na hapo ndio tunaona kuna taasisi ndogo mfano hospitali binafsi zinajiendesha na kulipa kodi wakati kuna taasisi kubwa zenye kila rasilimali (wataalam, ardhi, mejengo, vifaa, teknolojia na ruzuku) zinashindwa kujiendesha.

4. Kuwa na nafasi moja ya kiutendaji kwa wakati mmoja
Kushika nafasi zaidi ya moja kwa wakati mmoja kunamchosha mhusika kwa kumtaka afanye huku na kule, na kunawanyima fursa watu wengine kupata nafasi. Mfano mbunge kuteuliwa kuwa waziri, analazimika kutimiza majukumu ya wizarani, kutimiza majukumu ya bungeni na kuwafikia wananchi wake. Matokeo yake kuna majukumu yatapwaya na kuonekana hana uwezo kumbe ni amepewa mizigo mikubwa isiyoendana na muda uliopo. Angeshika nafasi moja, nafasi nyingine akashika mwingine ingesaidia kuongeza ufanisi kwa kutuliza akili na nguvu eneo moja na kugawana fursa chache zilizopo ili kupambana na tatizo la ajira linalotukabili.

Ni muhimu sana kuzingatia uwazi, vigezo na sifa katika mchakato wa kuwapata viongozi wa kuteuliwa, na kuwapatia malengo yanayopimika na muda wa kutosha unaofahamika kwa utumishi wao ili nafasi za kuteuliwa ziwe na mafanikio yanayokusudiwa.​
 
Inaleta faraja kuona Mhe. Rais anataka kuona mabadiliko ya kiutendaji katika mashirika, taasisi na wakala wa Serikali ili kuongeza tija na waweze kujiendesha kama inavyoonekana katika post ya ukurasa wake wa X (Twitter)
 

Attachments

  • Screenshot_20230819-184653.png
    Screenshot_20230819-184653.png
    24 KB · Views: 4

Similar Discussions

Back
Top Bottom