Kumbe PAC iliazima hoja ya ubinafsishaji wa IPTL kutoka Standard Chartered Bank?

SERGIO

JF-Expert Member
Dec 13, 2012
348
145
Standard Chartered yaliazima Bunge hoja ya ubinafsishaji



Na Prince M. Bagenda


UTAIFISHAJI wa njia kuu za uzalishaji ni hoja mpya ambazo mabepari wameona zinafaa kunusuru mfumo wa ubepari duniani. Wakati wa mtikisiko wa uchumi duniani serikali za Marekani na Uingereza zilitumia mabilioni ya dola na kuziingiza katika benki zilizokuwa zinachungulia kaburi. Kwa miaka kadhaa benki na mashirika ya kiuchumi ya nchi za Magharibi yaliweza kuendelea kufanyakazi kutokana na fedha za walipa kodi na fedha zilizowekezwa kutoka nchi mpya zilizoibuka na kutajirika kama China, India, Uturuki na Brazil kununua hati fungani katika hazina za nchi tajiri za Magharibi.
Mwaka 2009, wakati dunia ilikuwa katika giza nene kuhusu hali mbaya ya uchumi, hapa kwetu Tanzania Benki ya Standard Chartered ikiiga yaliyofanyika Uingereza na Marekani, ilileta mapendekezo kwa kampuni ya kufua, kusambaza na kuuza umeme ya TANESCO ikitaka shirika hilo lipeleke wazo kwa serikali kukubali kutaifisha mali za shirika la IPTL, ikiwemo na mitambo yake ya kufua umeme Tegeta. Sababu ya Benki ya Kibepari kugeukia utaifishaji wa mali ni kwamba ilikuwa inataka kulipwa deni lake ililokuwa imekopesha kwa IPTL iliyokuwa katika mgogoro mkubwa na TANESCO na serikali ya Tanzania kwa ujumla. Katika dunia ya leo, utaifishaji wa mali ya mashirika binafsi ni kitu cha nadra. Sababu kubwa ni kwamba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hawapendi kiwingu kujitokeza kwamba siku moja mali zao zinaweza kutaifishwa.
Hoja ya Benki ya Standard Chartered kutaka IPTL itaifishwe ni hoja ya hatari kutokana kwamba benki hiyo inachofikiria ni madeni yake tu. Haifikirii mustakabali wa uwekezaji nchini Tanzania na pia kuwepo utaratibu unaotambulika kwamba kama ikitokea hali ya kutaka kuwepo kutaifisha mali fulani basi utaratibu utakaofuatwa utakuwa wa namna fulani. Wazo la Standard Chartered la kutaka mali binafsi zitaifishwe, ni wazo linalotokana na tamaa ya kupata fedha kwa njia rahisi na za udanganyifu kwa kufikiria kwamba watu wote ni wajinga na wapumbavu.
Inasikitisha kwamba wako watanzania wenzetu, waheshimiwa na viongozi ambao wamegeuka kuwa mawakala wa wakoloni mamboleo ambao wako tayari kuiuza nchi kwa dinari. Wazo lililotolewa mwaka 2009 na Standard Chartered limekuja kupitishwa kama Azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2014. Je, ni matukio yanayofanana na kutokea nyakati tofauti?
Sauti za watu wachache hazisikiki hasa pale siasa za ushabiki zinapotamalaki. Katika mjadala bungeni kuhusu Ripoti ya Kamati ya Mahesabu ya Serikali kuhusu Akaunti ya Escrow iliyofunguliwa na serikali na IPTL, kuna baadhi ya watu walisema kwamba katika suala la Escrow kuna maslahi ya nchi na mashirika ya nje na pia kuna maslahi ya ndani, hasa katika mfumo wa siasa.
Ni wazi kwamba mapanga yalikwishanolewa na kilichokuwa kimebaki ni kuchinja na kutupilia baharini. Lakini kila kukicha mambo na habari mpya za kuthibitisha nani vinara wa njama za kuhujumu na kutekeleza maagizo ya wakubwa wa ndani na wa nje ya nchi.
Katika sakata la fedha za akaunti ya Escrow, ni wazi kwamba makundi maslahi ya ndani, hasa makundi yanayowania Urais ndani ya chama tawala, CCM yalikuwa yanacheza karata ya mtoano. Wale waliotajwa kuhusika, kwa namna moja au nyingine katika kuchotwa au kunufaika na fedha za Escrow walitakiwa wajiuzulu nyadhifa za uongozi. Waziri Mkuu Pinda, mwenyekiti wa kamati ya sheria na katiba na Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi walilengwa, pamoja na mambo mengine walikuwa wameonyesha nia ya kugombea Urais. Hivyo kuwataka wajiuzulu, ni njia mojawapo ya kupunguza mlolongo wa wanaotaka kugombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bunge lilipitisha maazimio manane. Mojawapo ya maazimio hayo inasema kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua, kutaifisha mitambo ya IPTL. Wazo hili liliwashangaza wengi kutokana na itikadi za wapinzani ambapo zinataka uchumi wa kuheshimu umilikaji binafsi wa njia kuu za uwekezaji na soko huria.
Kwa upande mwingine ni jinsi Bunge lilivyotumiwa kutunga azimio ambalo asili yake inaonekana siyo hapo bungeni bali ni Benki ya Standard Chartered ya Uingereza ambayo imejiingiza kwenye mgogoro wa IPTL kwa kuleta madai ya kutaka kulipwa deni iliyokopesha kwa kampuni ya Mechmar ambayo ilikuwa inamiliki asilimia 70% ya hisa katika IPTL.
katika barua yake ndefu, benki ya Standard Chartered ilitoa mapendekezo matano kuhusu mchakato wa kutaifisha kampuni ya IPTL ambayo inafua umeme.
Azimio la kutaka mitambo ya kufua umeme ni mojawapo ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge baada ya kupitia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kuchotwa kwa fedha za Akaunti ya Escrow.
Hata hivyo hoja ya Bunge kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe ni hoja ya kuazima. Si hoja ambayo imetokana na kufikiria mazingira ya kufanya biashara ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2009, Benki ya Standard Chartered iliyokuwa inataka kumiliki IPTL kwa ujanja, ndiyo ilikuwa ya kwanza kuleta wazo la kutaifisha IPTL kwa barua ya Septemba 22, 2009 iliyoiandikia TANESCO. Iliandika barua kwa TANESCO kwenda kwa Dkt. Idris Rashid, wakati ule akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO.
Barua hiyo ndefu ilikuwa na mapendekezo mengi, yaliyokuwa yanataka serikali itaifishe TANESCO ili fedha ambazo serikali itaifidia IPTL zitumike kulipa deni la Benki ya Standard Chartered.
Kutokana kwamba kulikuwa na kesi mahakamani Standard Chartered ilipendekeza kwamba hoja ya kutaifisha IPTL ianzie na kupitishwa bungeni.
Benki ya Standard Chartered ambayo haikuwa na mkataba wa serikali ya Tanzania au TANESCO, lakini ikijitangaza kwamba ilinunua deni la kampuni ya Mechmar iliyokuwa na hisa ya asilimia 70%.
Mpango wa Standard Chartered ulikuwa haujali kwamba kuna mashauri mahakamani au kwamba kuna mwanahisa mwenye hisa chache 30% VIP Engineering and Marketing ambaye haki na maslahi yake yanapaswa kuheshimiwa.
Hoja kwamba kuna viongozi wanatekeleza matakwa ya makampuni ya kigeni, si hoja za kubuni; kama ushahidi wa hoja ya kutaifishwa kwa mitambo ya IPTL kunavyoonesha
(a) Mchakato wa kutaifisha IPTL upitie bungeni na siyo mahakamani.
(b) Benki ya Standard Chartered ndiyo ilipwe fedha za fidia ya kutaifisha mali ya IPTL kwa sababu ndiyo inamiliki hisa katika IPTL
(c) Benki itakubali mpango huu wa kutaifisha kama mpango wa mwisho. Benki haitalazimisha vipengele vya kutaifisha mali za IPTL kama ilivyo kwenye makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Tanzania na IPTL ya mwaka 1995
(d) Benki haitafungua shauri katika mahakama ya usuluhishi wa mchakato wa kutaifisha mali za IPTL, dhidi ya TANESCO au serikali ya Tanzania kwa jina lake au kwa jina la IPTL, kuhusiana na mambo ambayo yanabishaniwa kisheria
(e) Ikitegemea mambo mengine, kwa jinsi mchakato utakavyokuwa bungeni kuhusiana na mpango wa utaifishaji wa mali za IPTL, utekelezaji wake unaweza kufanyika haraka bila kushirikisha Afsa mfilisi aliyeteuliwa au mahakama.
Mawazo yaliyopendekezwa na Standard Chartered ni mawazo ambayo yanayodhalilisha mfumo wa maamuzi nchini na pia ni kielelezo kwamba makampuni ya nje hayana hofu ya kutoa mawazo ya ovyo kwa sababu kuna wajinga na mafisadi wakimya watayakumbatia na kuyatetea.
 
Hilo linafahamika kuwa akina Zitto hawakuwa free minded. Walikuwa wanaburuzwa na Standard Chatered na Reginald Mengi
 
Back
Top Bottom