Kumbe Ngeleja alilikoroga Sengerema: Sasa CCM wamkataa Katibu wa wilaya aliyempandikiza

Zak Malang

JF-Expert Member
Dec 30, 2008
5,404
234

CCM Sengerema si shwari, wamkataa Katibu wao



HALI ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza si shwari, baada ya kile kinachodaiwa Kamati ya Siasa ya CCM kumkataa Katibu wa chama hicho wilayani humo, Rahel Washa, kwa tuhuma za kuanza kupanga safu ya viongozi wa kambi ya kigogo mmoja wa chama, kwa lengo la kutafuta ushindi wa Ubunge mwaka 2015; Imeelezwa.

Inadaiwa kwamba, Katibu huyo wa CCM wilaya ya Sengerema, ameonekana dhahiri kuanzisha makundi ya kukigawa chama kwa maelekezo ya kigogo huyo (jina na nafasi yake ya uongozi tunalo), na kwamba hali hiyo hawaikubali maana imelenga kukibomoa chama na kutoa nafasi kubwa kwa wapinzani hasa Chadema kushinda kwenye Uchaguzi mwaka 2015.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM wilaya ya Sengerema zinaeleza kwamba, Katibu Washa (53), alikataliwa na wajumbe wanane kati ya 12 wa Kamati ya siasa ya wilaya hiyo Januari 7 mwaka huu, mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya chama hicho mkoa wa Mwanza, walipokutana kwenye kikao cha usuluhishi mjini Sengerema.

“Wajumbe wanane kati ya 12 waliohudhuria kikao walisimama na kutaka Raheli Washa aondoke Sengerema. Walisema haya tena mbele ya katibu wa mkoa na wajumbe wa kamati ya maadili ya chama mkoa.

“Mimi nilihudhuria kikao hicho nikiwa kama mjumbe….na ninachokisema ni kweli. Huyu Raheli kaletwa Sengerema na (akamtaja jina), ili amsaidie kupanga safu ya kumwezesha kugombea na kushinda ubunge 2015. Kwa hiyo sisi kamati ya siasa tumemkataa kabisa aondoke hatakisaidia chama”, kilisema chanzo cha habari.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kamati ya Maadili ya mkoa ilifuatana na Katibu wa CCM mkoa huo, na kwamba kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 12 wa kamati ya siasa ya wilaya, huku wajumbe wengine wanne wakiwa na udhuru hivyo kushindwa kuhudhuria kikao hicho.

Taarifa zinaeleza kwamba, Washa amehamishiwa Sengerema kutoka wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga kwa ushawishi wa kigogo huyo, ikiwa ni lengo la kwenda kumsaidia kupanga safu zake za ushindi wa ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2015, na kwamba tayari ameshaanza kutekeleza majukumu hayo kwa kuanza kujenga hoja ya kutaka kupangua waweka saini wa chama wilaya.

Inadaiwa kwamba, Katibu huyo wa CCM wilaya ya Sengerema anataka kumwondoa kwenye nafasi ya kuweka saini uchukuwaji wa fedha za chama Katibu mwenezi wa chama hicho wilaya, Masumbuko Bihemo, ili aweke mtu aliyependekezwa na kigogo huyo anayedaiwa kumwendesha kama ‘rimot’.

Vyanzo vya habari vinadai kwamba, baada ya wajumbe hao wa kamati ya siasa wilaya ya Sengerema kumkataa Katibu huyo mbele ya kamati ya maadili ya mkoa, kigogo mmoja wa CCM ngazi ya mkoa alisimama na kusema: “Katibu Washa usihofu kelele za hawa watu, fanyakazi zako vizuri, fagia fagia uchafu wote. Maana hawa watu wa kuchaguliwa mshahara wao ni makofi, kufunga na kungungua vikao”.

Alipoulizwa leo kuhusu tuhuma hizo za kukataliwa na kamati ya siasa, Washa alisema: “Taarifa hizo si za kweli, ni uongo mtupu. Ni kweli kamati ya maadili mkoa ilikuja na kukutana na kamati ya siasa ya wilaya, lakini mimi sikukataliwa”.

Alisema, mwanzo hadi mwisho wa kikao hicho hakuna mjumbe aliyesimama na kumtuhumu kwa hayo mambo, badala yake walizungumzia mgogoro uliopo kati ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sengerema, Jaji Tasinga Gabanyaga na mbunge wa Buchosa, Dk. Charles Tizeba.

“Unajua mwandishi, ukweli wajumbe wa kamati ya siasa hawakunikataa na maandishi yapo. Ila niliona kila anayesimama ananishambulia na kuniingiza kwenye mgogoro huo. Sina makundi ndani ya chama wala sitaki kuegemea upande wowote, mimi ni kuchapa kazi tu niliyotumwa na chama”, alisema Katibu Washa kwa kujiamini.

Hata hivyo, walipotafutwa mwenyekiti Tasinga na mbunge wa Buchosa kuzungumzia suala la mgogoro wao kama ulivyotajwa na Katibu huyo wa CCM wilaya hiyo ya Sengerema, hawakupatikana, na juhudi za kuendelea kuwatafuta bado zinaendeleo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.


Chanzo: Fikra Pevu Blog
 
Back
Top Bottom