Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dakta Boniface Kasululu,akiwa ameongozana na mkuu wa mkoa huo Bw Zelote Steven akizungumza kijijini Samazi,amethibitisha kuwa mlipuko huo wa kuhara na kutapika ni ugonjwa wa kipindupindu, na kwamba tayari wametenga mahali pa kuwalaza wagonjwa waliokumbwa na ugonjwa huo kwa ajili ya tiba,huku mkuu wa mkoa huyo akipiga marufuku tiba za kienyeji,na wengine kwa imani zao wakiwaombea wagonjwa na kuwachelewesha kwenda kupata tiba.
Baadhi ya wananchi wakiongea kijijini hapo Samazi,wamesema wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama,na hivyo kulazimika kuyatumia maji ya ziwa tanganyika kwa shughuli zao zote,ambayo sio salama kabisa kwa vile yanachafuliwa mno kwa watu wengi kuligeuza ziwa hilo kuwa choo.
Chanzo: ITV