BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,015
Kikwete, Membe na hipokrisis!
Lula wa Ndali-Mwananzela Julai 9, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
KUNA watu wanafiki na wapo waigizaji. Kuna mambo ya kinafiki na mambo ya kizugaji. Katika yote mawili (unafiki na uigizaji/uzugaji) lengo ni kutoa picha au taswira isiyo ya kweli kuhusu mtu au kitu.
Katika lugha ya Kigiriki maneno haya mawili mwigizaji na mnafiki yanahusiana. Kimsingi neno la asili hipokrisis ndilo ninalotupa neno hypocrisy katika lugha ya Kiingereza ambalo tunalitafsiri kama mnafiki.
Lakini neno hili mnafiki ambalo tumelichukua kuwa ni la Kiswahili ni neno la Kiarabu ambalo kimsingi linahusu mtu ajifanyaye ambavyo sivyo alivyo. Linahusiana na uigizaji ule ule lakini lina maana ya kidini (Surat Al-Munafiqun Sura 63.) ambapo wanafiki ni wale ambao wanajifanya/wanaigiza kuwa wana imani kumbe wameiacha imani hiyo.
Ndio maana katika Uislamu, kwa mfano, mnafiki ni mtu wa hatari sana hata kuliko mtu asiyeamini. Kwa nini? kwa sababu Qurani Tukufu inasema Wanapo kujia wanafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo (63:1)
Hili la wanafiki kupingwa kwenye vitabu vya dini siyo suala la Qurani tu bali pia katika Biblia. Tunaambiwa katika maandiko matakatifu kuwa Yesu alisema Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, Wanafiki! Mmekuwa kama makaburi yaliyopakwa chokaa, kwa nje mnapendeza lakini ndani ni mifupa mitupu na uchafu (Mathayo 23:27).
Sasa utaona kuwa tofauti kubwa ya mwigizaji na mnafiki katika maana ya leo hii ni kuwa mwigizaji tunajua anaigiza kwa lengo la kuburudisha, kufundisha n.k lakini sisi sote tunajua kuwa yeye ni nani mwigizaji. Mnafiki kwa upande mwingine lengo lake ni kupotosha watu juu yake au mambo yake kiasi cha kuwafanya waamini kitu fulani ambacho yeye anajua kuwa si kweli.
Mnafiki kweli ni mtu wa hatari, kwani lengo lake laweza kumpatia faida kubwa mbele za watu kwani watu wanaweza kuamini kile anachokifanya.
Ndugu zangu, vitendo na maneno ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Bw. Bernard Membe mwishoni mwa juma kuhusu Zimbabwe, maneno ambayo yalielezea msimamo wa Tanzania na nchi za SADC kuhusu uchaguzi wa Zimbabwe, naamini ni maneno ya kinafiki.
Tulichoshuhudia wiki iliyopita si maneno ya ujasiri (kama nilivyoandika kwenye makala kuhusu serikali yetu na Mugabe) bali ni maneno ya kundi la watu ambao wanataka tuamini kitu fulani juu yao wakati wao wenyewe wanajua kuwa si kweli.
Ninachosema ni kuwa msimamo wa SADC na wa serikali yetu na hasa sababu zilizotolewa za kutomtambua Bw. Mugabe na uchaguzi wa picha wa Zimbabwe ni msimamo wa kinafiki.
Huu unafiki unatokana na mtazamo waliojijengea watawala wetu kuwa wao wanaweza kusimama katika kiti cha hukumu kutoa hukumu kwa haki. Kwa maneno mengine wanataka ulimwengu uamini kuwa wao ni bora kuliko Mugabe na kutokana na ubora huo, basi, wanaweza kutoa hukumu ya haki.
Nikipanua kidogo hoja ni kuwa wanataka tuamini kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake linapokuja suala la uchaguzi wao ni bora kuliko ZANU-PF na serikali yake kwenye swala hilo hilo. Huu ni unafiki.
Matumizi ya vyombo vya habari
Wanafiki wetu waliosimama kumhukumu Mugabe wanataka tuamini kwamba Mugabe aliwanyima wapinzani nafasi huru na sawa kwenye vyombo vya habari vya serikali yake, kitu ambacho wao (watawala wetu) hawakifanyi. Kwamba wao wanatoa nafasi sawa, na huru kwa vyama vya upinzania katika radio, televisheni na magazeti ya serikali hivyo wana uwezo wa kumhukumu Mugabe. Je hii ni kweli?
Mara nyingi imekuwa kawaida kwa Rais (tangu Mkapa) kuwa na hotuba ya mwisho wa mwezi kwa Taifa. Mara kadhaa Rais alipotoa hotuba hiyo amefanya hivyo akitumia pia nafasi yake kama Mwenyekiti wa CCM. Mfano mzuri ni hotuba yake ya mwezi wanne aliyoitoa kwa Taifa kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo alizungumza kupitia viongozi wa jumuiya za CCM. Na hata kabla ya hapo Rais ametumia hotuba zake za mwisho wa mwezi kunadi chama chake.
Cha kushangaza ni kuwa hakuna hata mara moja ambapo vyama vya upinzani vimepewa nafasi ya kujibu hotuba hiyo ya Rais kana kwamba mwenye haki ya kuzungumza na kuuza sera za chama chake kwa Taifa ni Mwenyekiti wa CCM tu. Huko Marekani kila Jumamosi (siyo kila mwezi) Rais wa Marekani anatoa hotuba kwa radio kwa Taifa, haijalishi yuko wapi na anafanya nini (wanaweza kuirekodi kabla). Mwisho wa hotuba hiyo kinachofuatia ni hotuba ya majibu ya upinzani. Hili linafanyika bila kujali Rais ni Republican au Democrat.
Mtindo wao huu wa kutoa nafasi kwa chama cha upinzani hauiishii Jumamosi tu. Kila mwaka mwanzoni, Rais wa Marekani hutoa hotuba yake maarufu ya Hali ya Muungano ambayo anatakiwa kuitoa kikatiba (Ibara ya Pili, kipengele cha tatu cha Katiba ya Marekani).
Kwa muda mrefu hotuba hii ambayo imekuwa ikifanyika mfululizo sasa kuanzia 1939 ilikuwa haifuatiwi na hotuba ya upinzani hadi mwaka 1966 ambapo chama kilichoko upinzani kimekuwa kikifuatia hotuba ya Rais na mtindo huo kuendelezwa hadi kwenye hotuba za Jumamosi au hotuba yoyote ile ambayo Rais wa Marekani atatumia masafa ya Taifa kuzungumzia sera au jambo lolote muhimu.
Sasa hivi imekuwa ni utaratibu kuwa Rais akizungumza basi upinzani nao lazima upewe nafasi ya kujibu.
Chombo chochote cha habari kilichobeba hotuba ya Rais kwa Taifa kinatakiwa nacho kibebe hotuba ya upinzani. Je CCM na serikali yake kama walimu wa Demokrasia kwa Zimbabwe wanaweza haya? Hebu fikiria siku ambayo tunamuona Rais Kikwete amemaliza kutoa hotuba yake kwa Taifa halafu sekunde chache baadaye Prof. Ibrahim Lipumba anatoa majibu ya upinzani!
Hili siyo kwenye masuala ya hotuba tu bali pia katika mchakato wa uchaguzi. Mojawapo ya malalamiko ambayo yamekuwepo Tanzania mara nyingi wakati wa uchaguzi ni kuwa wapinzani hawapewi nafasi sawa kwenye vyombo vya habari vya walipa kodi wa Tanzania.
Hili si suala la Bara tu bali pia Visiwani. Leo hii Rais wa Zanzibar anaweza kuzungumza jambo lolote bila upinzani Zanzibar kupewa nafasi sawa ya kujibu hoja hizo. Wakati wa uchaguzi vyombo vya habari hasa TV za Taifa na Radio za Taifa zimekuwa zikibeba ujumbe wa mgombea wa chama tawala na kumpa upendeleo wa aina ya pekee kulinganisha na vyama vingine.
Sasa leo wanasimama bila haya kumhubiria Mugabe juu ya nafasi sawa ya kutumia vyombo vya habari kwa upinzani? Kama huu siyo unafiki tuupatie jina gani?
Kitu kingine kinachoonesha unafiki ni pale SADC na serikali yetu wanapokumbatia ripoti ya waangalizi wa uchaguzi wa SADC kama msingi wa maamuzi yao ya kutomtambua Mugabe. Hivi wanafikiri sisi ni wasahaulifu hivi? Si waangalizi kama hao walitoa taarifa kuhusu Kibaki na uchaguzi Kenya? Si waangalizi hawa walitoa ripoti kama hii kwenye chaguzi za Zanzibar na tukazitolea nje ripoti zao?
Iweje leo ripoti ya waangalizi iwe imebeba ukweli katika Zimbabwe ambacho chini ya watu 100 wameuawa lakini ripoti hiyo isiwe na uzito kule Kenya ambako karibu watu 1000 waliuawa?
Hivi kweli serikali ya CCM inataka kutuambia kuwa sasa hivi imeongoka na inaamini kuwa taarifa za waangalizi zina ukweli? Au zina ukweli zinapohusu nchi nyingine lakini ikija kwa Tanzania ni maoni yao tu. Kama huu si unafiki tuupe jina gani?
Leo hii serikali yetu inajaribu kumshawishi Mugabe aunde serikali ya Kitaifa, maneno ambayo yamerudiwa na Rais Kikwete kwenye mkutano wa G8 huko Japan. Yaani hivi kweli tuamini kwamba Rais Kikwete ameona mwanga wa kuona haja ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zimbabwe lakini mwanga huo unazimika inapokuja Zanzibar?
Ndio, najua jibu lao litakuwa hivi: Mazingira ya Zanzibar yana tofauti! Hivi watu wa Zimbabwe wameumbwa na damu ya ubuyu? Hivi wananchi wa Zimbabwe wameumbwa kutoka sayari ya Zebaki au Zuhura?
Hivi wanataka tuamini kwamba CCM ina tofauti sana na ZANU-PF katika haja ya kukamata na kukumbatia madaraka yake na dola? Kama wana tofauti kwa nini walibadilisha Katiba na kumfanya Rais wa Tanzania awezekane kuchaguliwa na kura chache kabisa?
Kwa nini hadi leo hii bado wameweka uwezekano wa Rais kutangazwa usiku wa manane ili kuharakisha kumuapisha kama ilivyotokea Zimbabwe na Kenya. Ni kitu gani kinaweza kumzuia Rais kuapishwa barabarani kwa haraka haraka kama alivyofanyiwa Kibaki?
Leo ndugu zetu watawala wanataka tuamini kwamba wao wanaheshimu sana sheria na hawapendi vurugu kutokea nchini? Kwa nini basi wanakwepa kutengeneza uwezekano wa marudio ya kura kama Zimbabwe? Si angalau Zimbabwe kura zisipotosha wanaweza kurudia uchaguzi, lakini Tanzania hakuna kitu kama kura kutotosha!
Wapinzani mbalimbali wakigawana kura kwa asilimia sabini na CCM ikapata kura 30 mgombea wa CCM atatangazwa Rais usiku wa manane na kuapishwa kabla chapati hazijapikwa! Leo wanathubutu kumnyoshea kidole Mugabe cha kutomtambua? Nikiita unafiki nitaambiwa ninawakejeli?
Kuna mambo mengine mengi ambayo naweza kusema lakini nitaawachia wengine waseme. Kikubwa ninachosema ni kwamba msimamo wa SADC na wa serikali yetu kuhusu Mugabe ni wa kupuuzwa kwani misingi yake haina ukweli.
Ni mpaka pale nchi za SADC na serikali ya Tanzania zitakapoweza kusafisha uchafu wao kwenye mambo yao ya uchaguzi ndipo kwa haki wataweza kumnyoshea kidole mtu mwingine.
Vinginevyo, kwenye nchi ya wanafiki, kikombe wanachowanywesha wengine, wao wenyewe hawanywi. Lakini wataimba nyimbo na kupiga panda wengine wanywe. Kwa nini? Kwa sababu wanafiki ni waigizaji.
Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk