‘Kikwete, Magufuli ni Kusi na Kasikazi’

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Raia Mwema: Kuna ambao wamekuwa wakiwalinganisha, kwa kauli na matendo, Jakaya Kikwete na John Magufuli. Wewe unawafahamu vizuri wote. Tuambie kiasi jinsi unavyowapima?

Kinana: Niseme kwamba nimepata nafasi ya kufahamiana na Jakaya Kikwete kwa miaka mingi. Tangu mwaka 1978 tulipokuwa katika uongozi wa Umoja wa Vijana na kwenye kamati mbalimbali, ikiwamo Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana.

Tumefanya kazi pamoja. Tumekuwa pamoja kwenye Jeshi, kila mmoja kwa wakati wake, na kwa nyakati tofauti tulikuwa tunafundisha Chuo cha Jeshi Monduli. Mimi nilipoondoka, yeye akaja kufundisha pale.

Baadaye tulikutana bungeni, na baadaye tena tulikuwa wote kwenye Baraza la Mawaziri katika serikali. Mimi niliondoka mapema serikalini nikamwacha. Yeye amefanya kazi serikalini kwa muda mrefu zaidi hadi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Tunafahamiana kwa karibu kwa kufanya kazi pamoja na tumeelewana kwa muda mrefu.

La pili, nimemfahamu kuwa ni mtu ambaye ameshika uongozi kwa muda mrefu ndani ya chama na serikali na bahati nzuri mpaka akafikia kuwa Mwenyekiti wa chama chetu na Rais wa Jamhuri.

Nimemfahamu kama muungwana. Mtu ambaye ni rahisi kwa mtu mwingine yeyote kuweza kuishi naye. Ni muungwana na msikivu. Ni mtu ambaye ni rahisi kuelewana na mtu mwingine yeyote wa ngazi yoyote na wa kipato chochote. Ni mtu ambaye ni rahisi kujenga naye uhusiano na urafiki. Ni mtu ambaye anajua mambo mengi sana. Ameshika nafasi za uongozi akiwa kijana mdogo hadi kufika ngazi za juu kabisa.

Nadhani uhusiano tuliokuwa nao tangu tukiwa vijana kwenye chama chetu ulinisaidia sana kuwa karibu na yeye. Ni mtu makini.

Hachukui uamuzi kwa haraka. Inamchukua muda kufanya uamuzi kwa sababu anafanya tathmini na anaomba ushauri kutoka sehemu mbalimbali kabla ya kuchukua uamuzi, na huenda hii imemsaidia kufanya uamuzi mzuri na wenye busara kwa sababu chombo kama chama chetu hakiendeshwi kwa maagizo. Chama kinaendeshwa kwa mashauriano na vikao. Kwa maana hiyo lazima kuwe na majadiliano na maelewano.

Jingine, lazima nikiri kwamba alinipa fursa kubwa sana ya kufanya kazi. Aliniruhsu kufanya mambo mengi ndani ya chama kwa kadiri nilivyoona inafaa ingawa kabla ya uamuzi nilikuwa nikishauriana naye.

Nilipoamua kutembelea mikoani alikubali. Wakati mwingine aliniruhusu kuhamisha watendaji. Alinisaidia pale ambapo nilikuwa naona matatizo katika utendaji. Niliomba ushauri na hata uamuzi wake. Alikuwa tayari kunisaidia kwa sehemu kubwa.

Unajua serikali ya CCM kama ikifanya kazi yake vizuri mambo yanakuwa mazuri zaidi wakati wa uchaguzi na kama isipotenda kazi yake vizuri katika Ilani mambo yanakuwa magumu katika uchaguzi.

Kwa hiyo ni lazima chama na serikali kufanya kazi kwa ukaribu sana kwa kuangalia matendo ya serikali na hata kufanya marekebisho pale tunapoona kwamba vitendo fulani vya serikali vinaweza kuathiri uchaguzi. Kwa maana hiyo nilikuwa nafanya kazi kwa karibu sana naye.

Lakini lazima nikiri kwamba kwa sehemu kubwa ziara zangu za mikoani zilifanikiwa kwa sababu alikuwa ananiunga mkono. Ziara hizo zilikuwa na changamoto kubwa ambazo zilikuwa zinahitaji utatuzi.

Ilibidi wakati mwingine aagize mawaziri, na alimtaka Waziri Mkuu anipe mawaziri niende nao katika baadhi ya ziara ili wakajibu maswali ya wananchi. Pale kwenye madeni (yenye masilahi ya moja kwa moja na wananchi) aliagiza hatua zichukuliwe. Tulifanya kazi kwa karibu na kwa maelewano.

Lakini katika kipindi cha mwisho vilevile yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa mchakato wa kutafuta mgombea urais na tulifanya kazi kwa ukaribu na maelewano makubwa.

Tulifanya kazi hiyo kwa uadilifu na kwa umakini hadi chama chetu kikashinda na yeye kama Rais aliweza kumkabidhi madaraka hayo mgombea wa CCM.

Kwa hiyo ameondoka akiwa ameridhika. Na bila shaka, amefurahi kwamba amemwachia kijiti Rais aliyetokana na CCM kama ambavyo yeye alikipokea kijiti hicho kutoka kwa Rais aliyetokana na CCM.

Nina uhakika katika maisha yake ya kustaafu atakuwa amestaafu kwa raha na amani. Nina uhakika nitakuwa namtembelea mara kwa mara kuchota uzoefu wake na busara zake ili kufaidisha chama chetu.

Raia Mwema: Sasa John Pombe Joseph Magufuli?

Kinana: Kama ambavyo nimekwishakusema, Rais Magufuli ni mchapakazi na mtu ambaye hana uvumilivu na uvivu, uzembe na matumizi mabaya ya mali ya umma na kutowajibika.

Anajulikana kama ni mtu ambaye akipewa kazi, basi kazi ile ataifanya kwa ufanisi.

Hata ukitazama kwa mfano, baadhi ya kaulimbiu zilizowekwa kwenye mabango ya CCM wakati wa kampeni zilieleza kuwa ni mtu mchapakakazi, muwajibikaji na hodari, sifa ambazo Watanzania walikuwa wakimjua nazo.

Ni mtu ambaye ni mnadhimu (disciplinarian). Mara nyingi sana ulimsikia Rais Jakaya Kikwete wakati ule wa kampeni akisema jamani ninyi mlikuwa mnasema mimi nilikuwa mpole, nadhani sasa mtapata mtu mkali.

Sasa ukali ule umeanza kuonekana. Ni ukali mzuri kwa nchi. Tumvumilie. Ndiyo staili yake, ana nia njema na nchi hii. Anajaribu kubadilisha utamaduni wa nchi yetu. Utamaduni wa kuendesha serikali na hata utamaduni wa mazungumzo.

Unajua tumekuwa tukikaa na kuzungumza muda mrefu hata kwa jambo dogo. Tumekuwa na viongozi wanaotaka kumfurahisha kila mtu na wakati mwingine hata kama jambo lenyewe halifai tunatafuta maneno mazuri ya kuliahirisha.

Yeye hayuko hivyo. Kama jambo halifai anasema halifai. Kama jambo liko hovyo anasema ni la hovyo. Nadhani tumuelewe na kumsaidia.

Raia Mwema: Wengine waliomtathmini Rais Magufuli, akiwamo mshindani wake katika uchaguzi wa mwaka jana, Edward Lowassa wameeleza kidogo kuhusu mafanikio lakini wakaonya kwamba yote si kheri. Kwamba, kwa mfano, maisha kwa wengi nchini sasa ni magumu na hali hiyo si mliyoahidi?

Kinana: Nimesoma tathmini ya rafiki yangu Edward Lowassa. Kwanza, tathmini yake haikumtendea haki Rais Magufuli. Lakini vilevile yeye mwenyewe hakujitendea haki na nikikutana naye nitamwambia.

Sidhani kama ni sahihi kutathmini kazi ya Magufuli katika mwaka mmoja kwa nusu ukurasa wa gazeti. Ni kama alikuwa na haraka ya kusema chochote. Mradi tu aseme.

Lakini katika tathmini hiyo fupi, anakiri kwamba Rais Magufuli amefanya kazi nzuri. Hapo angeweza kufafanua. Yapo mambo mengi mazuri aliyofanya Rais.

Amesema kwamba hali ya uchumi ni ngumu. Akagusia matatizo ya wafanyakazi, hana takwimu, hana maelezo ya kina … anatoa tu maelezo ya jumla jumla na kwa kweli ni maelezo ambayo ni rejareja.

Sidhani kama mtu akisoma ule waraka anaweza kuona kwamba kuna umakini wa mtu aliyekaa akafanya tathmini kwa kina. Nadhani kama nilivyosema, yeye mwenyewe (Lowassa) hakujitendea haki kwa kutoa maelezo mafupi kiasi hicho lakini pia hakumtendea haki Rais Magufuli.

Watu hasa wa kutathmini kazi za Rais Magufuli ni Watanzania wenyewe walioko vijijini na mijini … waliompa kura na wasiompa.

Naelewa yako maneno kidogo kuhusu hali ya uchumi, kuhusu kubana matumizi, kuhusu mzunguko wa fedha na mengine, na Rais Magufuli amesema mwanzo utakuwa mgumu. Ni dhahiri mwanzo utakuwa mgumu kwa sababu ni kipindi cha kusahihisha mambo fulani fulani. Kujega misingi mizuri ya kiuchumi na kijamii na utamaduni wa watu kufanya kazi.

Kila mtu aishi kwa jasho lake, na kuna maneno amekuwa akitumia Rais Magufuli, kwamba ni lazima tufanye juhudi kuondoa utaratibu wa kutumia njia zisizo halali kupata mapato, kuwanyima wengine fursa kwa wewe mwenyewe kujipa fursa.

Kwa hiyo kama anavyosema nia yake ni njema, uamuzi anaofanya ni kwa ajili ya wengi, analenga kujenga uchumi utakaofaidia kila Mtanzania na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Hata mimi, kwa mfano, kwenye ziara zangu, baadhi ya maneno niliyokuwa nasema jukwani ndiyo hayo anayotekeleza Rais Magufuli.

Nilikuwa nasema, kwa mfano, kwamba nchi yetu ina sherehe nyingi sana. Na kila sherehe ina matumizi makubwa na wanaotumia na kuhudhuria sherehe hizo na kufaidi ni wale wale kila siku.

Sherehe zenyewe hazina tija sana kwa Watanzania, yeye mwenyewe wakati alipohutubia Bunge alieleza mambo mengi sana, alikosoa matumizi yasiyo ya lazima serikalini na alitoa takwimu kwa mfano kuhusu safari nyingi za nje zisizo na tija.

Na wakati mwingine watu wamekwenda katika nchi ile ile moja mara 10 kujifunza jambo lile lile na wakarudi na hakuna lililobadilika.

Watu wanakwenda kujifunza, namna gani wenzetu wameweza kufanya kile … namna gani wameweza kufanya hiki … namna gani wameweza kujenga reli. Kwenye nchi hizo wamekwenda wabunge wamerudi, wamekweda makatibu wakuu wamerudi, wamekwenda mawaziri wamerudi, wamekwenda wataalamu wamerudi, kila mmoja ameandika taarifa lakini matokeo hatuyaoni.

Sasa Rais Magufuli anasema hapana. Hatuna haja ya kwenda huko nje bila mpangilio, kwamba tukae kwetu tuamue kufanya kazi. Najua wapo watakaonung’unika, lakini ni wachache na ukweli ni kwamba watakoanufaika ni wengi.

Raia Mwema: Kabla ya Mkutano Mkuu Maalumu wa Julai mwaka huu kulikuwa na ishara ya kuwa unataka kuondoka, na kisha uliandika kwa Mwenyekiti mpya akuruhusu wewe na Sekretariati yako muondoke. Kwa nini hukushikilia msimamo wako wa kuondoka?

Kinana: Kwanza lazima niseme kwamba nilipokubali kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu nilitoa maombi yangu kadhaa.

Nilijiambia kwamba nitamsaidia Mwenyekiti na chama changu kufanya kazi na niliahidi kufanya kazi kwa juhudi, kwa maarifa yangu yote. Nilijitolea kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na nguvu zote kwa kuamini kwamba nimekuwa kwenye chama hiki kwa zaidi ya miaka 40.

Niliwaomba wale walionishawishi kuchukua nafasi hii kwamba mara baada ya uchaguzi wa 2015 kumalizika niruhusiwe kupumzika.

Kwanza, kwa sababu nimekwishakukaa kwenye chama na kwenye uongozi kwa muda mrefu. Lakini pia kwamba tayari nimekwishakufanya kazi ya utendaji ambayo mara nyingi nilikuwa nikiikimbia. Lakini pia umri umekimbia.

Kwa hiyo uchaguzi ulipomalizika na Mkutano Mkuu unakuja na kutakuwa na kubadilishana kati ya Mwenyekiti Kikwete na Mwenyekiti mpya Magufuli, nikaona ni wakati muafaka kuandika barua kuwashawishi viongozi wastaafu na wale walionishawishi, nipumzike.

Wakati umefika Mwenyekiti mpya ambaye ni Rais, akaona si wakati muafaka mimi kuondoka. Kwa sababu ana shughuli nyingi za kiutendaji serikalini na kwa hiyo angechukua muda mwingi kufanya kazi za serikalini. Huenda busara zake ndizo zilizomwongoza kwamba nibaki kumsaidia katika ukatibu mkuu.

Kwa nini sikushikilia msimamo wangu? Nadhani ni uungwana tu unapoombwa na Mwenyekiti wa chama na Rais wa Jamhuri, kumkatalia si busara. Naamini anaamua hivyo kwa nia njema ya kusaidia nchi. Katika hali hiyo inakuwa vigumu sana kumkatalia.

Raia Mwema: Unafikiria kustaafu lini, mwakani?

Kinana: Tutaendelea kushauriana na Mwenyekiti na tutaangalia kama nitaweza kumshawishi siku zijazo. Kwa sasa hilo namwachia Mwenyekiti mwenyewe.

Tunajiandaa kufanya uchaguzi mwaka ujao ndani ya chama na kwenye jumuiya, nadhani kwanza tumalize kazi hiyo.

Raia Mwema: Umekuwa kwenye timu za kampeni za urais wa CCM tangu mwaka 1995. Mwaka jana mlitikiswa sana. Ni uchaguzi mwingine upi uliowapeleka mbio?

Kinana: Nimeshiriki kwenye chaguzi zote na nimekuwa kiongozi kwenye chaguzi zote tangu 1995 hadi sasa.

Uchaguzi mgumu sana, lazima nikiri, ni uchaguzi wa mwaka 1995. Kwa nini? Kwa sababu wakati mzee Ali Hassan Mwinyi anaondoka kulikuwa na kelele nyingi sana za rushwa na masuala yanayohusiana na uadilifu na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Na utakumbuka kwamba wakati mzee Mwinyi anangia alikabidhiwa fagio la chuma. Lifagie uoza na rushwa vilivyokuwa vimeanza kukua zaidi japo hapo kabla, wakati wa Mwalimu Nyerere, vilikuwa vya hapa na pale. Na utakumbuka kulikuwa na jambo moja lilikuwa linasemwa sana kipindi hicho . Suala la Chavda.

Hilo lilikuwa moja. Lakini la pili, tulikuwa na kiongozi, huwezi kusema kiongozi bora, aliyekuwa anapeperusha bendera ya Upinzani, Augustine Mrema.

Mrema alikuwa waziri wa mambo ya ndani, na katika kipindi ambacho alikuwa waziri, baadaye nilikuja kugundua katika utafiti wangu, kwamba mambo mengi aliyokuwa akifanya alipokuwa waziri alilenga kuja kugombea uongozi wa nchi.

Sote tulikuwa mawaziri, mimi nikiwa ulinzi. Nilikuwa namhoji nikawa nagundua kwamba mwenzangu alikuwa na safari ya masafa marefu. Alijihusisha sana na masuala yanayohusu wananchi.

Kero za wananchi. Namna ya kuzitatua na kwa sababu alikuwa na wizara ya mambo ya ndani, chombo chenye mamlaka ya kukamata na kufungua mashitaka, kiasi alikigeuza kuwa mahakama na yeye Mrema akawa ni jaji mkuu. Akishakukusema Mrema, ndiyo mwisho.

Nakumbuka siku moja nilimuuliza, mwenzangu mbona kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri sikuoni, vipi? Akasema nyinyi (mawaziri) mkikaa kwenye Baraza la Mawaziri mnazungumza mambo ya serikali, mimi nazungumza mambo ya wananchi huku. Ndiyo maana huwezi kuniona kwenye Baraza.

Alijenga umaarufu mkubwa hadi mzee Mwinyi akamteua kuwa naibu waziri mkuu bila kujua mipango yake mingine ya ziada.

Lakini nadhani baadaye waligundua. Wakampeleka wizara ya kazi na ustawi wa jamii. Wakati huo, tayari alikuwa amekwishakujijengea jina na umaarufu. Amekwishakuitumia wizara ya mambo ya ndani kujijengea heshima kwenye jamii kama mtu anayeweza kutatua matatizo ya wananchi mara moja na kwa haraka na ikajengeka hisia kwamba huyu anaweza kuongoza nchi na kuondoa mambo yote ya hovyo.

Na yeye, nadhani, umaarufu huo ukamwingia kichwani, kwa sababu, unajua mwanasiasa raha yake watu, kupigiwa makofi na sifa sifa nyingine.

Ni rahisi sana ukiwa mwanasiasa, ukawa maarufu sana … ukapigiwa makofi, ukapendwa sana. Ni rahisi sana kuamini kuwa mimi sasa ndiye. Kwamba inawezekana hawa watu wanataka nichukue nafasi kubwa kwa hiyo unaweza kushawishika.

Ulipofika wakati akaachishwa uwaziri kule Dodoma, liliibuka zogo kubwa. Watu walikusanyika wakaandamana, wanamshangilia na kusukuma gari lake. Wengine wanamwonea huruma. Akajiongezea umaarufu.

Wakati ule kwenye CCM aliteuliwa Benjamin Mkapa kuwa mgombea. Mtu makini, mtaratibu, lakini ambaye hakuwa maarufu.

Kwa hiyo, huku upande wa pili kuna mtu maarufu bila kujali kama ni makini au la. Halafu kwetu kuna mgombea ambaye pengine wengi hawakumtarajia, ni kiongozi wa serikali miaka mingi, msomi na makini lakini hana mbwembwe. Hakujijenga ili kutafuta umaarufu.

Kulikuwa na kazi ya ziada ya kumuuza. Ilikuwa kazi ngumu ya kupambana na Mrema. Mrema ndiye mpinzani ambaye alipata kura kwa asilimia kubwa ambayo kwa maoni yangu hakuna kiongozi wa Upinzani aliwahi kupata asilimia nyingi hivyo. Mzee Mkapa alipata asilimia 61 ya kura. Utaona kwamba kwa kura hizo za Mkapa, Mrema alikaribia sana kwenye asilimia 40 hivi.

Raia Mwema: Kama si kuingia ulingoni kwa Mwalimu Julius Nyerere, Mrema angeweza kuwapiga kumbo?

Kinana: Lazima nikiri kwamba ushiriki wa Mwalimu Nyerere katika kampeni za Mkapa ulimtibua Mrema na wafuasi wake na uliongeza kura nyingi sana kwa CCM na kwa Rais Mkapa.

Kuingia kwa Mwalimu kwenye kampeni zile, labda huko mbele ya safari wasomi wa sayansi ya jamii watapenda kufanya utafiti wa hili, lakini kwetu kuja kwa Mwalimu ilikuwa ni factor (kigezo) kubwa sana katika ushindi wa CCM na Mkapa katika uchaguzi ule.

Mwalimu alifanya kampeni katika mikoa 12, kwa jinsi watu walivyokuwa wanamheshimu na kusikiliza kauli yake, aliongeza nguvu sana kwenye mchakato ule. Kila alikopita, alimponda (kueleza udhaifu wa) Mrema na kumsifu Mkapa na kueleza kwamba matatizo tuliyonayo na kero zilizopo mtu anayeweza kuzitatua ni Mkapa. Watanzania wengi walimsikiliza Mwalimu Nyerere, alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wetu.

Uchaguzi mwingine unaoweza kuwa mgumu nadhani ni wa mwaka jana. Kwanza, nadhani CCM tulimwachia Lowassa muda mrefu. Jambo ambalo ni kinyume cha kanuni zetu.

Tuliruhusu akajijenga na kukimega chama. Tumekuja kuteua mgombea wakati tayari yeye amekwishakujijengea nguvu kubwa akitumia mbinu mbalimbali.

Alikwishakwenda mbali sana. Halikuwa jambo rahisi. Mmemuacha yeye, mmemleta Magufuli na mnakwenda kwenye kampeni muda mfupi ujao.

Baadaye naye akaingia Upinzani na wapinzani wakaungana. Labda tungemteua mgombea wetu mapema zaidi huenda isingekuwa ngumu kiasi hicho. Kwa hiyo, hatuwezi kusema uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa uchaguzi rahisi.

Lakini ni dhahiri uchaguzi ule umedhihirisha jambo moja kubwa, kwamba bado Watanzania wana imani na CCM.

Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu hakuna mtu aliyetarajia Magufuli angekuwa mgombea wa CCM. Katika yale majina yote, yeye hakuwa mmojawapo, najua nyinyi ni kati ya wachache sana mliokuwa mkimtaja, lakini umaarufu wake ndani ya chama na ndani ya nchi haukuwa mkubwa sana.

Baada ya kuchaguliwa, ilibidi yeye mwenyewe afanye kazi kubwa, na lazima nikiri kwamba amefanya kazi kubwa sana ya kujinadi mwenyewe. Amepita kila jimbo, tofauti na mgombea wa Upinzani.

Alihutubia mikutano mingi sana, yawezekana hata mara 10 zaidi ya mikutano ya mpinzani wake (Lowassa). Lakini pia taratibu na maandalizi yetu ya kampeni vilikisaidia chama chetu. Kubwa ni kwamba Watanzania wengi bado wanakikubali CCM.
 
Back
Top Bottom