Kauli ya Rev. Kishoka kwa wapiganaji wa CCM 2009

Rev. Kishoka

JF-Expert Member
Mar 7, 2006
4,526
1,529
Niliandika kipande hiki tarehe 8 August 2009


WARAKA WA REVERAND KISHOKA KWA WA TANZANIA

Nimefuatilia kwa karibu sana kuhusu kile kinachoitwa vita ya ufisadi nchini mwetu inayoendeshwa katika majukwaa ya kisiasa na hata ya kijamii na kusikitika ni jinsi gani jamii yetu inavyozama na kuvutwa pande mbili na karibu kukatika katikati.

Baada ya kufuatilia vita hiyo ya ufisadi inayoendeshwa na wapiganaji kutoka ndani ya CCM binafsi nimejenga mtazamo wangu kuhusiana na hao waitwao Makamanda wa Ufisadi (maana ya kumuita mtu Kamanda wa kitu ina maana yeye ni msimamizi mkuu wa kitu!) au Wapiganaji ambao yawezekana kabisa wapo watakaofikia kunishutumu ama natumiwa na hapo mafisadi ama hata nimi ni mmojawapo wa hao mafisadi wanaopigwa vita kwa hotuba za majukwaani.

Watanzania tunadanganyana na kudanganywa na hivi vita vya nyati wawili ndani ya boma la CCM. Kinachoumia ni nyasi ambao ni sisi Wananchi wa Tanzania bila kujali itikadi wala chama cha siasa tunavyoshabikia ugomvi wa nyati hawa bila ya kutambua kuwa hawa ni nyati na sisi ni majani.

Nimesema hapo awali kuwa Mzee Mwanakijiji, kawaonea haya na kuwauliza maswali mepesi, sitanii na napingana na Mzee Mwanakijiji kwa kuendelea kuwapa nafasi na hata tumaini hawa wanaojiita Wapiganaji wa Ufisadi kwa maana wanalofanya kwa kusema na matendo havisaidii nchi yetu ipate maendeleo.

Kifupi, Wapiganaji au ukipenda uwaite Makamanda wa Ufisadi, ni Wanafiki, Wazandiki na Wabinafsi!

Hawa hawana lengo la kuleta mabadiliko ya kweli yanayotakiwa kwa Tanzania, bali wamechagua kibwagizo kinachonoga, kutetea Uhalali wa wao na kundi lao la kisiasa kuendelea kuaminiwa na kupewa dhamana ya kuwawakilisha Watanzania na hata kuwaongoza ilhali hawathamini wala kuheshimimu matamanio ya watanzania hao ya kutaka kuona mabadiliko ya kweli.

Nasema ni Wazandiki maana wanachagua ni lipi lipendezalo na lililo tamu kusikika masikioni mwa watu na linalofurahisha na kuleta mvuto wa kupewa ukurasa wa mbele wa Gazeti na Maandamano Uchwara na hata ushabiki wa kijinga ambao unaburutwa kisa ni kipenda roho(hula nyama mbichi)!.

Tanzania ina matatizo mengi sana ambayo yanahitaji Wabunge na Wapiganaji makini na hodari ili kuleta Maendeleo na kutuondoa kwenye Umasikini na Unyonge, lakini husikii hata siku moja hawa wanaojiita Wapiganaji wakiongelea lolote la maana ambalo limekuwa machoni mwetu tangu tupate Uhuru ili kutupa Uhuru wa kweli wa kujitegemea.

Sijasikia wakipigia kelele hata kusitisha Bajeti ya Serikali wakilenga kumtetea mfanyakazi wa Tanzania ambaye bado ananyonywa na kukandamizwa serikali yake kwa kupewa ujira hafifu ambao haukidhi wala kukimu mahitaji yake.

Sijasikia wakipiga kelele kila siku, na hata kuiamrisha Serikali kutaka huduma bora za Afya na Elimu zidumishwe ili tuwe na Taifa lenye watu wenye nguvu na afya, walio na elimu na maarifa bora ili kuzidisha juhudi katika kazi na hivyo kuongeza si pato la Taifa pekee, bali kipato cha Mtanzania huyu katika safari yake ya kujitegemea.

Siwasomi wakimpigania kwa nguvu zao zote Mkulima, Mfugaji, Mmachinga, Mwanapolo, Mama Ntilie au Mtanzania yeyote ambaye anahitaji apewe kipaumbele ili aweze kuwa na nguvu za kujitegemea na Uimara wa kutosha aweze kujumuika kwa dhati katika ujenzi wa Taifa letu.

Hawajasimama kidete hata mara moja kutetea haki za Mtanzania wa Pemba, Waislamu wa Mwembechai, Mazeruzeru, Wanafunzi wa Vyuo, Waalimu, Wastaafu na wengine wengi ambao Dola imewadhulumu na kuwanyanyasa kama si kuwapuuza. Haya yote ambayo yamekuwa yakifanyika kwa kutumia mabavu na kuruhusu kikundi fulani kitumie urafiki wao kwa viongozi wasio waadilifu kujipatia wanachotaka.
Nenda Loliondo, Simanjiro, Kilosa na hata sasa Kisarawe, Mtanzania ananyang'anywa haki yake na mali yake ya asili kwa kuzaliwa na kupewa mtu mwingine wao wanakimbilia majimboni kuwahonga wapiga kura na miradi isiyo na uhakika kama VICOBA na mingineyo wakidai ni utekelezaji wa ilani ya kundi lao la kisiasa.

Siwasikii wakitoa hamasa na kuwa mfano wa kuigwa kiutendaji na kiuadilifu katika majimbo, mitaa na kata zao ambapo wananchi waliowachagua wangeanza kupiga hatua za maendeleo kutokana na hamasa kutoka kwa kiongozi wao.

Hawajakaripia Serikali wala kupingana na Serikali kutokana n Serikali kushindwa kutimiza ahadi zake na wajibu wake kwa Mtanzania. Badala yake bila ya haya wanavamia kila kinachoonekana na kukivika rangi ya kijani kuwalaghai watanzania kuwa huo ni utekelezaji wa ahadi za serikali yao.

Sijasikia wakiikalia kooni Serikali na kuiwajibisha kwa matumizi mabaya ya fedha, kuongezeka kwa Umasikini, na Ukosefu wa Ufanisi.

Siwasikii wakitoa hoja kufuta misamaha ya kodi kwa wawekezaji ambao ukweli wamedhihirika kuwa wachukuaji kwa minajili ya kuongezea Taifa kipato ama kufuta posho haramu na malipo yasiyo ya lazima kwao wao na wenzao wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao kama waajiriwa wa wananchi.

Sijasikia hata siku moja, wakipinga na kupiga vita tabia ya Serikali kuombaomba misaada, kukopa na kutegemea kupewa fedha na wahisani, ili kujiendesha huku tuna Rasilimali za kutosha kujitegemea. Hawajaondoa kura, iwe ni Bungeni au kwenye vikao vya chama kupinga tabia chafu ya utegemezi na ombaomba inayofanywa na Serikali yetu na viongozi wake!

Sijawasikia wakiwafundisha Wananchi wao, mbinu bora za uzalishaji mali, elimu ya Uraia, Utu na Uhuru wa kujiamulia ili kujenga jami iliyo na Uhuru wa kweli na yenye kujitegemea?

Siwasikii wakiwaambia Wananchi wa majimbo yao kuwa wana haki kuwasikiliza na kuwakaribisha wapinzani wa kisiasa kujadili yale yaliyo ya msingi bila kuwafanya wao ni maadui au watu hatari kwa Taifa letu!

Wapiganaji hawa, ni maarufu kwa kulikariri na kulitamka Azimio la Arusha, Mwongozo wa Chama na kumuenzi Nyerere, lakini matendo yao hayaendani na kauli na hotuba wanazotoa. Kwao wao haya yote si masuala ya imani ya maendeleo bali ni vibwagizo vya kuhalalisha uzandiki wao.

Ni vipofu wa makusudi kwa kujifanya hawaoni ubovu wa mfumo wa Utawala na Siasa Tanzania hasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambao unaua na kudumaza Demokrasia, Uhuru na Haki za Mtanzania. Wangelipenda wote tuige upofu wao wa kudhani kuwa ufisadi na maovu mengine ni masuala ya watu binafsi na sio mfumo ambao wao ni wadau wake wakuu.

Wao wamedhihirisha kuwa wajibu wao ni kwa CCM na matakwa ya CCM. Lakini wanasahau kuwa matakwa wanayoyafanikisha sasa hivi si ya CCM bali ni ya wachache ndani ya CCM ambao wamekiteka nyara CCM na kukifanya mali yao na hivyo kila aliye ndani ya Chama amekuwa Mtwana!

Hata nikirudi katika nafasi zao za Ubunge na mengi ambayo yanafanyika Bungeni, wote hawa, Mwakyembe, Seleli, Kimaro, Sitta, Sendeka, Limbeli, Kilango walikuwa wapi kumtetea Mbunge na mpiganaji mwenzao Zitto alipoleta hija ya kuhoji mkataba wa Buzwagi kama si wao kujiunga pamoja kama Chama Tawala na kumdhalilisha na kumbeza Zitto na si kusimama kidete na kufuata mkondo wa halali na ulio sawa wa kuchangua hoja na kuifanyia uchunguzi.

Hivyo basi siridhiki na sifa tunazowamwagia hapa kuwa wao ni mashujaa, maana tunafurahia yale tunayoyataka kwa nafsi zetu binafsi na si kwa manufaa ya Taifa. Walichokifanya na kinachotulewesha ni kile walichokifanya Februari 2008 na kulazimisha Lowassa ajivue Uwaziri Mkuu. Lakini Mkataba wa Richmond bado haujatenguliwa, je mbona bado wako mguu pande huku tunaumia kwa bei kubwa za umeme na mbaya zaidi ukosefu wa umeme kutokana na uzembe uliozaa huo mkataba?
Hivi sio hawahawa waliotamka hadharani kwamba kuna mengine mengi waliyowaficha watanzania kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama chao. Imekuwaje tena watanzania tukawa na umuhimu zaidi ya chama chao kama walivyonyesha hapo na pengine pengi.

Vita ambavyo wanavifanya sasa hivi si kwa manufaa yako na mimi au na hata yule, bali ni kwa manufaa yao, ili waendelee kupaka siagi na jibini mkate wao.

Nimesema mara kadhaa, kuwa vita vya Ufisadi na Ufisadi, ni sehemu kiduchu tuu, katika kuangalia matatizo ya Tanzania na kupima Maendeleo ya Tanzania.

Kinachotokea CCM na hizi kambi mbili, ni ndugu kugombea tonge, sawa na Waprotestanti walivyoachana na Wakatoliki au jinsi Shia walivyotengana na Sunni.

Ukiangalia, wote, Waprotestanti, Wakatoliki, Sunni na Shia, kila mmoja wao anatetea lile lililobora machoni pake na kujiita kuwa yeye ni bora na zaidi. Lakini wote hawa wanne, hawamjali yule ambaye si Mprotestanti, Mkatoliki, Msunni au Mshia.

Wapiganaji wa CCM, hawana nia ya kuleta maendeleo nchini mwetu kama ilivyotamkwa katika Azimio la Arusha au Mwongozo wa Chama wa mwaka 1981. Hata Ilani ya CCM ya 2005, hawaipitii na kuhoji utimilifu wake na nguvu za wananchi na Serikali kwa umoja ili kutufikisha japo asilimia 75 ya malengo ya MKUKUTA, MKURUBITA, DIRA 2015 na hata Malengo ya Milenia.

Hawamjali Mtanzania wa pale Kisiju ambaye leo hii, bado anatembea maili kadhaa, kwenda kuteka maji, kukata kuni, kupata tiba, huku akitumia jembe la mkono, akiishi kwenye nyumba ya tembe na watoto wake hawana mahali bora na vitendea kazi bora ili wajielimishe na kuelimika.

Ningewapa heshima, kama wangekuwa na msimamo thabiti hasa ndani ya Chama chao na ndani ya vikao vya Chama kwa kusimama kidete kumtetea Mkulima na Mfanyakazi kama katiba ya CCM inavyosema, jinsi Azimio la Arusha lilivyoagiza.

Ningeamini vita vyao, kama walipokaa Butiama, mwanzoni mwa mwaka 2009, wangesimama na kuwashurtisha watuhumiwa wote wa Ufisadi, wajieleze na wavuliwe Uanachama, la sivyo wao wangejivua Uanachama wa CCM na kueleza umma, ni jinsi gani Chama Tawala kilivyo haribiwa na Takrima na Rushwa na kukumbatia Mafisadi badala ya kuwaadhibu.

Haieleweki machoni mwangu kuwa leo hii, wale walio rudisha nyuma maendeleo ya Taifa letu kutokana na Uzembe, watu kama Lowassa, Chenge, Karamagi, Msabaha, Mramba, Yona, na wengine wengi hata ukiongeza Rostam, bado wana sauti zenye nguvu ndani ya vikao vya Chama na wana ushawishi wa hali ya juu, kiasi kwamba wamegeuza "Wapiganaji" kuwa kunguru mwoga.

MbonaWapiganaji hawakutoa tamko la kulaani kitendo cha watendaji wa Chama na Serikali walioandaa maandamano kuwapokea Chenge na Lowassa watu waliokitia madoa CCM?

Je walipokuwa Dodoma mwezi wa August 2009, mbona hawakufurukuta ndani ya vikao vyao vya chama ili lijulikane moja kwa Taifa na ndani ya CCM kuwa wao ni "Wapiganaji" wa kweli na hawatayumbishwa au kuburuzwa na Uongozi usio makini? Kwa nini waliruhusu Sauti za Mafisadi kunguruma na kutawala vikao vya chama? Waliogopa nini kuropoka ovyo na kuvuliwa Uanachama kama NEC na CC ingeamua kuwatenda hilo?

Nikisoma kauli zao, nikipima matendo yao, bado siridhiki kuwa Wapiganaji, kweli wana nia ya kujitoa mhanga, kulifia na kulitetea Taifa lao.

Leo hii ninaposikia wakitoa vilio kuwa wanafanyia hujuma, lakini hakuna mmoja wao aliyekwenda mahakamani na kutoa ushahidi au kufungua kesi ya kuhujumia, je mnafikiri kuna ukweli kwa wanalosema?

Ikiwa wao kama Wabunge, rasilimali zote, nguvu zote na mamlaka waliyo nayo, wanaendelea kulialia na kulalamika kama mimi Mchungaji na wewe Mlalahoi mwenzangu na hawana hata Ubavu wa kusema sasa basi, ni vipi tuendelee kuamini kuwa wana nia nzuri na kilio chao na kampeni zao eti kupigana na Ufisadi ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa?

Iweje leo waseme fulani na fulani wamefanya makosa na kutumia madaraka vibaya, lakini wao wenyewe wamefanya makosa kama hayo ili kujinufaisha na tunaambiwa walichofanya ni kwa ajili ya kumtetea mlalahoi?

Mimi nawauliza, si wanapigania nini, bali wanampigania vita hii nani? halafu ndipo wajibu wanapigani nini?

Ndio, Siasa ni mchezo mchafu, lakini iweje nao wafanane na wale wanaowatuhumu kuwa ni Mafisadi na wanacheza mchezo mchafu, ikiwa hawasimami kidete kuitetea Haki ya Mtanzania, kutumia Utu na Kweli?

Je ule mwiko na kiapo "Nitasema kweli daima, fitina kwangu Mwiko" ni maneno tuu ya kurudia kama wale wanaoimba Sala ya Bwana "Baba yetu uliye Mbinguni"?

Biblia inatufundisha, Imani bila Matendo ni Haba na Batili.

Wao Wapiganaji, wanatughairi kutuonyesha ni Waumini Safi, lakini matendo yao hayafanani kabisa na hata matokeo ya kazi zao, hazimsaidii Mtanzania, awe ni CUF, CHADEMA, TLP au CCM yenyewe, bali ni wao na vibiongo vyao vya kulemewa na mizigo ya tamaa ya Uongozi na kupenda Umaarufu.

Kama kweli Wapiganaji wangetaka niwaheshimu, wangesimama kidete kutaka Muafaka wa Suala la Muungano, Wangeilazimisha Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya dhuluma dhidi ya kila Mtanzania, iwe ni Waislamu wa Mwembechai, Wapemba wa Unguja, Mazeruzeru au ndugu zetu wanaonyang'anywa mali na ardhi ili kumnufaisha Mwekezaji na Bepari.

Wangekuwa ni Wapiganaji kweli, wasingeweka matumbo yao mbele na kujiongezea vipato na kupewa posho, huku kima cha chini hakijaongezea, Bei za Mazao zinadidimia, Wastaafu wananyimwa mafao yao, Wanafunzi wananyimwa ada na mikopo, Wauguzi na Waalimu wanadanganywa kuhusu mishahara yao, Polisi na Wanajeshi wetu wanaishi maisha duni yanayosababisha wajiingize katika vitendo vya utovu wa nidhamu na kuvunja sheria.

Wapiganaji hawa, hawana Sera, Msimamo, Itikadi au mwelekeo.

Bali ninavyowapima, vita vyao ni kugombea Madaraka na mianya ya kujiongezea kipato binafsi na umaarufu, dhidi ya lile kundi la Kifisadi ambalo limedhamiria kumnyonya Mtanzania abakie mifupa mitupu.

Vita vyao, vingeleta maana kama vingekuwa ni vishirikishi vya Watanzania wote kwa kudai Uwajibikaji kutoka Serikali na Chama chao, ili kutimiza ahadi za Uchaguzi, kuibana Serikali kutokana na ukosefu wa nidhamu katika matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuishurtisha Serikali ijenge upya mchakato wa Demokrasia ya kweli (Katiba Mpya kwa manufaa ya Watanzania si CCM pekee) ulio huru na shirikishi ili haki na utu wa Mtanzania uimarike naye aweze kushiriki kikamilifu kulijenga upya Taifa lake.

Sikatai, vita dhidi ya Ufisadi ni muhimu, lakini kitendo cha wao kuamka miaka mitatu baadaye tangu vita vilipoanza ni kuonyesha wazi kuwa hawana nia kupiga vita ufisadi. Zaidi kitendo cha wao kupiga kelele eti kwa minajili ya kuhakikisha hawamuachii Zitto na Slaa tu kupiga kelele hizo kama alivyowahi kutamka bungeni Mpiganaji Anne Kilango kinaonyesha dhahiri kuwa upiganaji wao sio wa dhati bali ni usanii waliouzoea.

Kilichotokea Bungeni Februari 2008, ni wazi ndio kichocheo cha mfarakano ulioko ndani ya CCM, na si ukweli kuwa wanachokifanya ni utashi wa kulinda maslahi ya Mtanzania na hazina ya Taifa letu.

Kama kweli hiyo ni nia yao, mbona hawakusikiliza, kutafakari na kufanyia kazi kelele, mayowe na vilio vyetu kila siku tulipong'amua kuwa tunahujumiwa? Hata la EPA, RICHMOND na mengine, kama si sisi kulizungumza na kuhoji tunachokisoma magazetini na kutoka kwenye mikutano yao, wasingejipukutisha na kukifanyia kazi. Kama Slaa asingeileta ile listi ya Mafisadi, ambayo iliorodhesha "Wabaya" wao, wasingeamka na kumlazimisha Rais aunde tume kuichunguza BOT!

Buhemba wanaathirika na Sumu, lakini hamjaitaka Serikali isitishe mkataba wa Barrick. Buzwagi ilifanyika kiharamia, aibu yenu ya kumtukana Zitto, imewafanya mfumbie macho makosa ya Mkataba na hivyo Taifa kuendelea na mkataba ambao ni wazi kuwa ni batili!

Labda niwaulizeni, je katika majimbo yenu, ambako mnadai wanaandaliwa makuwadi wa Mafisadi kuwanyang'anya tonge, mmefanya nini la maendeleo kuwa Wananchi wa Majimbo yenu hata hizo rushwa za Mafisadi hazitawababaisha nao watawachagua nyinyi tena?

Tukitaka kupima mafanikio na maendeleo tangu muwe wawakilishi na Wabunge wa wilaya zenu, tunaweza kuona Ufanisi katika Uzalishaji mali, Uadilifu katika Uongozi, na mipango bora inayotokana na Siasa safi?

La mwisho ambalo limenifanya niongee kwa ukali kuliko Mzee mwenzangu Mwanakijiji, ni kitendo chenu cha kuhalalisha Takrima na Rushwa.

Leo hii mmeshindwa kuwafundisha Wananchi wa Tanzania na hasa majimbo yetu, utu, uwajibikaji na uadilifu kwa kuhimiza wapokee hongo zitokazo kwa Mafisadi na hao mnaowaita Mafisadi kwa kisingizio kuwa hizo pesa ni haki yao, ni marejesho ya walichodhulumiwa.

Spika Sitta na Mwakyembe wamelisema hilo wazi katika mikutano ya kunadi dhamira ya Wapiganaji.

Mnachofanya ni kuruhusu Mtanzania aendelee kushangilia Takrima na kunogewa na kipato cha ziada kitokanacho na Rushwa. Kwa kifupi mnahalalisha ufisadi huohuo mnaodai kuwa mnaupiga vita.Ndio maana tunahoji ninyi mnapigana vita ya ufisadi ama vita dhidi ya ufisadi.

Ningekuwa mimi nyie, ningewaambia na kuwakumbusha Watanzania wote, kuwa Rushwa ni Adui wa Haki na watakapomuona yeyote anayeleta hongo, wasipokee, bali wawakamate watu hawa na kuwapeleka Polisi na Serikali iwe ya Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa au Taifa hata TAKUKURU ili sheria ifuate mkondo wake kupiga vita Ufisadi.

Mlichofanya ni kuwaambia Wananchi kuwa ni Ruksa kupewa hongo, na waitumikie vizuri, kama aliyewapa ni mzungumzaji mzuri kama nyie mnavyojifanya kuwa ni Wapiganaji.

Kwa hilo la kuhalalisha haramu ya Rushwa, Takrima, Kidogodogo na Hongo, mmelitia aibu Taifa letu, mmekiuka kiapo chenu kupita Katiba zote, anzia Katiba ya Jamhuri na hata Katib yenu ya CCM.

Je tuwaamini vipi basi kuwa nyinyi mna lengo la kuleta mabadiliko Tanzania yatakayoamsha Uwajibikaji, Ufanisi, Ushindani, Haki, Utu, Juhudi na Maarifa ili kujenga Taifa linalojitegemea na linaloshinda (si kupiga vita kwa maneno na maandishi tuu) Umasikini Ujinga na Maradhi, ikiwa mnachokipiga vita sasa hivi Ufisadi ambacho ndio msingi mkuu wa Rushwa, mnauhalalisha kwa kuwataka Watanzania wapokee hongo kutoka kwa "Mafisadi" na kuwapigia kura nyinyi?

Kama kilio chenu ni cha kweli na mnaamini Uongozi Mkuu wa Chama chenu CCM na Serikali yake haufai, mbona hamuutii Uongozi huu matumbo joto kama Mafisadi wanavyowafanyia nini?

Ni nani kati yenu yuko tayari kuwa Kondoo wa Zaka na kumwambia Mwenyekiti wenu wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa ameshindwa kazi, hawezi na kuongoza Tanzania katika kuleta maendeleo na hana nia ya kupiga vita Umasikini, Ujinga, Maradhi na Ufisadi?

Msimtegemee Slaa, Mrema, Lipumba, Mtikila au Zitto kuwatatulia tazizo mlilo nalo ndani ya Chama chenu ambacho ndicho mnalialia na kunung'unika.

Fanyeni kweli na aliye mwanaume na mpiganaji wa kweli kati yenu, akaze kende na atikise Kiberiti na kuutaka Urais wa Tanzania kupitia CCM kupingana na Kikwete , ili vita vyenu vilete maana na tuone kama mkipata hayo mamlaka, kama mtaleta maendeleo kwa Taifa letu na kuushinda Ufisadi!
 
Mkuu wangu katika hili nadhani trumejadili huko Twiter karibu siku nzima tukipishana juu ya mtazamo. Binafsi yangu naamini kabisa ADUI yetu mkubwa ni UFISADI na huwezi kufikiria kuijenga nchi wakati wa Vita hata kidogo kwanza pigana vita umshinde adui kisha ndipo utazame utafanya nini. Ufisadi ni zao la maskini wa hali (akili) ule ulodi Lofa kutothamini UTU.. utawezaje kuwajengea maisha bora ikiwa umeshapoteza UTU.

UFISADI unaua maendeleo ni kama ndoo yenye tobo.. Huwezi kufikiria kuijaza ndoo maji kabla ya kufiikiria kuiziba tobo laa sivyo hutabakia na maji huko uendako. Mimi naamini kabisa sababu kubwa na kielelezo cha - KWA NINI WATANZANIA NI MASKINI? jibu lake linaanza na UFISADI wa viongozi wake! Tulichonacho sisi ni Mirija, wale walopewa madaraka hunyonya kila kinachongia hivyo ujazo wa ndoo yetu kamwe hauwezi kupanda!

Ni mara ngapi kambi ya Upinzani imepinga bajeti ya serikali kwenye ELIMU na AFYA? mara ngapi kambi ya Upinzani imepinga bajeti ya serikali kuwa kubwa katika matumizi ya kawaida (recurrent Expenditure) Kuliko bajeti ya Maendeleo na wakashinda? Mara ngapi kambi ya Upinzani wametaka mikataba ya serikali iwe wazi wasifanikiwe? Kumbuka Meremeta, Kagoda, IPTL, Rada, Richmond, Nyumba za serikali, Bomba la gas, Buzwagi, Bulyanhuru, misamaha ya kodi isolazima na kadhalika haya yote yanachangia sana katika umaskini wetu. Leo hii watu wanataka kuyakubali kama yalopita tugange yajayo!

Mkipuuza tobo hili la Ufisadi kwa kulipamba na maua ya waridi na mizeitun ya kwamba sii hoja basi mtaendelea kubeba ndoo tupu za maji kwa miaka mingine 50. nambie kwa nini hadi leo hatuna Umeme wakutosha japo tuna gas kuliko nchi yeyote Afrika, Leo hatuna maji wakati tuna maziwa kuliko nchi yeyote Afrika! unadhani kwa sababu ya bajeti?..

Naamini kabisa hatuwezi kufuta kabisa UFISADI lakini kama crime nyinginezo, hii ya KUHUJUMU UCHUMI hata kama mtajenga hoja gani pasipo kuiharamisha na sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya kuhujumu Uchumi basi tumekwisha..Ikiwekewa mkazo kama enzi ya Sokoine, wahalifu watakuwepo lakini wataogopa kuyafanya ya Ufisadi kama ndio mila na sehemu ya maisha ya kila Mtanzania.

Labda nikuache na list ya viongozi wa Canada walowajibishwa kwa scandal mbali mbali nyingine ndogo kabisa lakini wa sababu wana wajibu juu ya misingi ya miiko na maadili katika Uadilifu wa kiongozi wamewajibishwa tena wengine walikuwa wanafanya vizuri sana kazi zao. Jambo moja tu likawaondoa madarakani na kupoteza sifa zote walizojenga kama viongozi. BOFYA. Haya kwetu yanawezekana? kama hayawezekani tujiulize kwa nini viongozi wanakuwa juu ya sheria!
 
Mkuu wangu katika hili nadhani trumejadili huko Twiter karibu siku nzima tukipishana juu ya mtazamo. Binafsi yangu naamini kabisa ADUI yetu mkubwa ni UFISADI na huwezi kufikiria kuijenga nchi wakati wa Vita hata kidogo kwanza pigana vita umshinde adui kisha ndipo utazame utafanya nini. Ufisadi ni zao la maskini wa hali (akili) ule ulodi Lofa kutothamini UTU.. utawezaje kuwajengea maisha bora ikiwa umeshapoteza UTU.
!

Ufisadi pamoja na kuwa ni silika ya mtu, jinsi ulivyoshamiri Tanzania ni matokeo si ya umasikini, bali matokeo ya kukosekana uongozi imara, it is that simple!

Kama tungekuwa na uongozi imara, wenye uthubutu, usio na woga kuukabili umasikini na kutoyumbishwa yumbishwa na wageni na wenyeji wenye tamaa, tusingefika hapa tulipo.

Umeongelea ya watu kupiga kelele bungeni, lakini je wamewahi kuandika sheria mpya na kanuni na kuziwasilisha na zikakataliwa kwa kura na hivyo kuwakilishwa kwa wananchi kuwa jitihada na kazi zao zimeshindikana kutokana na kukataliwa na chama kingine chenye mamalaka na dola?

Narudia tena na tena kuwa tatizo kubwa ni uongozi, ufisadi ni matukeo ya uongozi dhaifu unaorubunika na kulainishwa kiurahisi na kununuliwa!
 
Rev. Kishoka salute.

Watanzania wameshindwa kuuliza maswali magumu kwa wale wanaotaka uongozi. Mtu anasema ataendesha nchi bila misaada, wananchi wanashindwa kuuliza inakuwaje wewe unasema hivyo wakati - moja umeneemeka na kupora mashirika ya umma, then inakuwaje unanunua nyumba Ulaya kwa pesa za walipa kodi na unasema unataka kuiondoa nchi hii kwenye umasikini. Are you joking or what?

Wakati huo huo ndio hawa hawa viongozi ambao waliunga mkono Azimio la Zanzibar la kuwafanya wajitajirishe isivyo halali kwa kutumia fedha za walipa kodi. Je wanaweza kutuhabarisha mbinu utakazotumia kuwaondoa wananchi kwenye umasikini?
 
Back
Top Bottom