Kanuni mpya za Mafao ya Wastaafu ni dhulma: Serikali Irudishe 50% ya Mafao ya Mkupuo kwa Wastaafu - J K Maganja ACT Wazalendo

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,883
Kanuni mpya za Mafao ya Wastaafu ni dhulma: Serikali Irudishe 50% ya Mafao ya Mkupuo kwa Wastaafu.

- Kauli ya ACT Wazalendo Juu ya Kupunguzwa kwa Mafao ya Mkupuo ya Wastaafu

Ndugu Wanahabari

A. UTANGULIZI:

Juzi jumamosi, Disemba 1, 2018, Ngome ya Wazee ya Chama chetu ilifanya kongamano la mashauriano ya Wazee wa ACT Wazalendo hapa jijini Dar es salaam, nilipata heshima ya kufungua kongamano hilo ambalo lilijikita katika kujadili changamoto za wazee nchini, hasa wastaafu.

Pamoja na kongamano hilo, nchini kwa sasa upo mjadala mkubwa juu ya suala la kanuni za mafao yatokanayo na mifuko ya hifadhi ya Jamii kwa wastaafu, kanuni zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kanuni ambazo zimesababisha malipo ya mkupuo kwa wastaafu (Lumpsum) kupungua kwa zaidi ya 50%, kutoka 50% ya Mapato yote ya pensheni iliyokuwa awali, mpaka 25% tu ya malipo yote ya Pensheni.


Jambo hili limezua mjadala mkubwa nchini, hasa malalamiko kutoka kwa wafanyakazi ambao ndio waathirika. Kwetu ACT Wazalendo tunaosimamia Ujamaa wa Kidemokrasia, Hifadhi ya Jamii ndio jambo kuu la kisera.

Kwetu ACT Wazalendo Hifadhi ya Jamii ni haki ya msingi kwa wananchi wote, ni nyenzo ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa uhakika wa matibabu kwa wote (Universal Health Care) kwa kupitia Fao la Matibabu, ni njia rahisi ya kupata mikopo na kuongeza mtaji kwa biashara za wananchi, na ni akiba ya mafao kwao na wategemezi wao. Kwa ACT Wazalendo, Hifadhi ya Jamii sio tu ni Uwezeshaji bali ni Ukombozi kwa Wananchi. Hivyo basi tumeona tunao wajibu wa kutoa kauli ya kina juu ya suala hili.

B. PENSHENI:

Pensheni, kwa tafsiri rahisi ya hapa Tanzania, ni bakuli la Fedha za akiba ambalo kila Mtanzania aliyeko kwenye Sekta Rasmi ya Ajira anaweka, yeye na mwajiri wake. Kwa sasa Nchini mwetu kuna watanzania Milioni 2.1 wanaofanya kazi katika Sekta rasmi ya Ajira, ambao moja kwa moja wanaguswa na suala hili la pensheni. Hivi sasa Wazee Wastaafu kwenye Utumishi wa Umma wakiwa wastani wa watu takribani 120,000 na wale wa kwenye sekta binafsi wakiwa ni wastani wa watu 4000 (wengi wao wakiwa ni wanachama wa NSSF).

Kapu hili hatimaye hutumika kulipa watu Mafao wanapostaafu ikiwemo ya kila mwezi na yale ya mkupuo. Mafao hulipwa kwa kanuni maalumu ama kikokotoo. Lengo la pensheni ni kumfanya aliyekuwa mfanyakazi kutoanguka kwenye umasikini baada ya kupoteza nguvu. Pensheni humwezesha mstaafu kuishi maisha ya kawaida na yenye stara hata kama sio ya kula bata. Ifahamike kuwa Watanzania wengi sana Hivi sasa ambao ni Wazee wanaishi maisha ya shida sana kwa sababu nchi yetu haina pensheni kwa wote.

C. KIKOKOTOO:

Mjadala mkubwa wa sasa umejikita kwenye kanuni maalum inayotumika kukotoa Mafao ya wastaafu wetu, kanuni hiyo ndiyo huitwa KIKOTOO. Wastani wa mishahara ya miezi 36 ya mwisho anayolipwa mfanyakazi anayekaribiq kustaafu ndiyo inayotumika kukotoa pensheni yake kwa ujumla. Kisha asilimia flani (zamani ilikuwa 50%) ya jumla ya mafao yake ndio hutolewa kama mafao ya mkupuo (Lumpsum), na kinachobaki hulipwa kama pensheni ya kila mwezi.

Kwa kiasi kikubwa mjadala wa sasa unatokana na hatua ya Kikotoo cha sasa - Kitokanacho na Kanuni zilizotungwa na SSRA kama takwa la Marekebisho ya mwaka 2018 ya Sheria ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kikotoo cha sasa kimepunguza mafao ya jumla ya mkupuo ya mstaafu kwa 50%, kutoka 50% aliyokuwa anapewa zamani mpaka 25% ya sasa.

D. ATHARI:

Sheria zote za zamani zinazohusu mafao ya Pensheni ya Wastaafu (kabla ya Julai 1, 2014) kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii zilikuwa na KIKOKOTOO cha malipo ya Mafao ya Pensheni ya 50% kwa Mkupuo wa kwanza. Hata baada ya marekebisho ya Sheria ya mwaka 2014 bado mpaka iliyokuwa mifuko ya PSPF, GEPF na LAPF ililipa wastaafu wake 50% ya jumla ya Mafao yao kwa Mkupuo.

Mfuko pekee ambao ulilipa 25% baada ya Sheria ya mwaka 2014 ni NSSF, jambo ambalo lilipingwa na Vyama vya Upinzani Bungeni wakati huo, lakini watu waliamua kufumba macho kwa sababu ni jambo lililowahusu wastaafu 3000 tu wa Sekta Binafsi, jambo ambalo lilizalisha ubaguzi kati ya wastaafu.

Tulitarajia kanuni mpya ziwainue hawa wastaafu wachache wa Sekta Binafsi kutoka kupata Mafao ya Mkupuo ya 25% mpaka 50% ambayo wastaafu wengi walikuwa wanapata, lakini hata wale waliokuwa wanapata 50% nao wamepunjwa na kupewa 25% sasa. Malaika anafanywa shetani.

Mfano zamani kama jumla pensheni ya Mfanyakazi wakati wa kustaafu itakuwa ni Shilingi 11 milioni, zamani kwa kutumia Kikokotoo mfanyakazi huyu angepewa 50% ya mafao yake yote, ambayo ni Shilingi 5.5 milioni kwa mkupuo wa kwanza mara tu pale anapostaafu. Na Shilingi 5.5 milioni, 50% zilizobaki angepewa kidogo kidogo kila mwezi kwa maisha yako yote atakayobaki hai.

Kwa sasa, kama jumla pensheni ya Mfanyakazi wakati wa kustaafu itakuwa ni Shilingi 11 milioni, zamani kwa kutumia Kikokotoo mfanyakazi huyu anapewa 25% ya mafao yake yote, hivyo atapewa shilingi 2.75 milioni kwa mkupuo wa kwanza mara tu pale anapostaafu. Na 75%, Yaani Shilingi 8. 25 milioni zilizobaki angepewa kidogo kidogo kila mwezi kwa maisha yako yote atakayobaki hai.

E. KIFO:

Makadirio ni kuwa Mtanzania anaishi kwa muda wa Miaka 15.5 mara baada ya kustaafu, muundo wa mafao ya sasa umejengwa katika msingi huo. Lakini ikitokea Mfanyakazi huyu wa sasa, akifariki dunia baada ya Miaka miwili tu tangu kustaafu (akiwa tuseme amepokea mafao 30% ya Pensheni yake - 25% ya Mkupuo na 5% kidogo kidogo kwa Miaka miwili) warithi wake hawatapewa Ile 70% ya Pensheni iliyobaki, bali watapokea tu kile kiwango alichokuwa mstaafu anakipokea kwa mwezi kwa muda wa miaka mitatu tu.

FAIDA YA 50%: Faida ya Mfanyakazi kupewa 50% ya Mafao ya Pensheni yake ni kwamba ikitokea akifariki mapema mno kabla ya Ile miaka 12.5 ya baada ya kustaafu, fedha ambazo zitakuwa amepoteza na kubaki kule kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii ni chache kuliko zile alizopokea. Na hivyo kwa kiasi kikubwa atakuwa amefaidika na jasho lake, tofauti na akipewa tu 25%.

F. RAI YA ACT Wazalendo:

1. Kwa sasa mstaafu anapopokea 25% ya mafao yake zile 75% ya fedha zake zinazobaki Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii haikai nazo tu bila kuzifanyia chochote, inaziwekeza. Serikali inafanyia Biashara hela za wastaafu, Si jambo baya hili. Ni RAI yetu sisi ACT Wazalendo kuwa badala ya Serikali kufanyia Biashara 75% ya fedha za Wastaafu wetu na kuwapa kwa mkupuo 25% tu ya mafao yao, basi ibadili kanuni na wafanyakazi wapate kiwango cha 50% ya mafao ya Mkupuo. Na Serikali ibaki na hiyo 50% ambayo itawapa kidogo kidogo wastaafu kila mwezi.

2. Utaratibu wa kuwapa 50% ya Mafao yao kwa mkupuo, uliwawezesha Wafanyakazi kuweza kukopa Mikopo ya Nyumba iliyo na thamani ya mpaka 25% ya jumla ya mafao, na hivyo walipostaafu kuweza kupokea 25% ya jumla ya mafao yao iliyobaki huku 50% ya mafao wakilipwa kama kipato cha kila mwezi. Jambo hili lililowawezesha Wastaafu kuwa na uhakika wa makazi, pamoja na ustawi wa maisha, na liliwaondolea usumbufu wa kuanza kujenga au kununua nyumba mara baada ya kustaafu. Kuyapunguza Mafao yao ya mkupuo mpaka 25% ni kuwaondolea haki hii ya kuweza kuwa na Mikopo ya Nyumba. Ni RAI yetu ACT Wazalendo kuwa mafao ya mkupuo yarudishwe kuwa 50% kwa mifuko yote miwili sasa ili kuwawezesha watumishi wa Umma na wale wa Sekta Binafsi kuweza kupata mikopo ya nyumba kupitia akiba ya mafao yao.

3. Wigo wa Pensheni nchini ni mdogo mno, mpaka mwaka 2015 nguvukazi ya Taifa (watu ambao wanaweza kufanyakazi) ilikuwa ni watu 22 milioni, lakini walio kwenye Hifadhi ya Jamii ni watu 2.1 milioni, kama 10% tu ya nguvu kazi ya Taifa. Jambo hili litasababisha Taifa kurithi 90% ya wazee wasio na pensheni katika miongo miwili au mitatu ijayo. Rai yetu ACT Wazalendo ni kuishauri Serikali kufanya juhudi za makusudi ya kupunguza hali hii ya 90% ya nguvukazi ya Taifa kutokuwa katika Hifadhi ya Jamii kwa angalau ifike 50% ndani ya Miaka Mitano ijayo.

4. Tunarudia tena rai yetu kwa serikali kuanzisha fao la bei kwenye mfumo wetu wa hifadhi ya jamii, Fao hili la bei litatumika kulinda makundi ya Wavuvi, Wakulima na Wafugaji pale bei ya bidhaa zao inaposhuka (Price Stabilization). Fao hili litatumika kama kichocheo cha kuyavutia makundi hayo ambayo yanawahusu 75% ya Watanzania kuingia kwenye hifadhi ya jamii na hivyo kuongeza wigo wa Nguvukazi ya Watanzania walio kwenye hifadhi ya jamii kutoka 10% ya sasa.

Yeremiah Kulwa Maganja
Mwenyekiti wa Chama, ACT Wazalendo
Disemba 3, 2018
Dar Es Salaam
 
Sawa sawa lakini naona hili kama limeshapita, hakujakuwa na kelele za kutosha
 
Zitto,ha ha ha eti kazi na bata...
Hivi naibu umeliona tu hilo la kazi na bata kwenye uzi huo? Nikidhani ungekuja na hoja mbadala wa kuonyesha kuwa nawe linakuuma kumbe kwenu wanasiasa haliwahusu! Usisahau kuwa hii nchi siyo ya wanasiasa tena uchwara kama wewe usiye na mission wala vision za kulisaidia taifa lako! Kiuhalisia huna tofauti na mnyonyadamu ambaye anaishi kwa jasho letu halafu hana tija! Ipo siku mtazitapika nawaambia!
 
Kanuni mpya za Mafao ya Wastaafu ni dhulma: Serikali Irudishe 50% ya Mafao ya Mkupuo kwa Wastaafu.
.....
C. KIKOKOTOO:
............ Kisha asilimia flani (zamani ilikuwa 50%) ya jumla ya mafao yake ndio hutolewa kama mafao ya mkupuo (Lumpsum), na kinachobaki hulipwa kama pensheni ya kila mwezi.

Kikotoo cha sasa kimepunguza mafao ya jumla ya mkupuo ya mstaafu kwa 50%, kutoka 50% aliyokuwa anapewa zamani mpaka 25% ya sasa.

D. ATHARI:
Sheria zote za zamani zinazohusu mafao ya Pensheni ya Wastaafu (kabla ya Julai 1, 2014) kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii zilikuwa na KIKOKOTOO cha malipo ya Mafao ya Pensheni ya 50% kwa Mkupuo wa kwanza. Hata baada ya marekebisho ya Sheria ya mwaka 2014 bado mpaka iliyokuwa mifuko ya PSPF, GEPF na LAPF ililipa wastaafu wake 50% ya jumla ya Mafao yao kwa Mkupuo.

Yeremiah Kulwa Maganja
Mwenyekiti wa Chama, ACT Wazalendo
Disemba 3, 2018
Dar Es Salaam
Bw. Zitto,
moja ya mbinu ya kupambana na adui ni kuhakikisha kwamba hufanyi makosa ili asianze na kukukosoa. Ktk taarifa hii unayoiita ya ACT, basically ni ya kwako na ukiwa mbunge ulitakiwa ufahamu nini kiliendelea kabla ya kikokotoo kipya.
Naanza na bahati mbaya kabisa ya kudandia hoja kama hii iwe ni mtaji wa kisiasa. Hilo linaweza kuwa ni tatizo linalokuondolea uangalifu maana wanasiasa wetu tunawafahamu uzembe wenu kwenye mambo yasiyohusu mafao yenu.

Je, unafahamu kwamba kuna PPF ilikuwa na kikokotoo hicho cha 25% kabla ya sheria mpya? Nahisi unafahamu maana naona mifuko iliyokuwa na 50% unayoitaja, PPF haipo. Unafahamu kwamba wana PPF walihangaika kwa miaka mingi kutaka hiyo ibadilishwe lakini haikuja mapema? Kama unafahamu hilo na kama uliwahi kusikia juu ya PPF ulichukuwa hatua gani kwa miaka yote hiyo?

Wana PPF tulifahamu tunaumia kuwaona wenzetu wakipata 50% lakini kila wakati Mkurugenzi mkuu, Erio alibebwa na uhusiano wake na Rais Mkapa na kuamua kukataa tu kutofanya lolote na akasifiwa eti anajua kazi. Akitumia hata pesa za PPF kunyamazisha vyombo vya habari. Wabunge nao hamkutoa msaada wowote, labda kwa kuona idadi ya wana PPF haikuwa mtaji kwenu. Sasa hivi idadi ya wafanyakazi imekuwa kubwa naona munaibeba na kuufanya ni mtaji wa kisiasa. Ulikuwa wapi wakati sheria hii ikipitishwa kizembe?

Haitoshi kusema ni wana CCM, tunachofahamu ni wabunge wote hamukutenda haki kwa wananchi. Kwa umoja wenu tunastahaili kuwaondoa wote Bungeni tuingize watu wapya kila palipo na uwezekano.
 
Hivi naibu umeliona tu hilo la kazi na bata kwenye uzi huo? Nikidhani ungekuja na hoja mbadala wa kuonyesha kuwa nawe linakuuma kumbe kwenu wanasiasa haliwahusu! Usisahau kuwa hii nchi siyo ya wanasiasa tena uchwara kama wewe usiye na mission wala vision za kulisaidia taifa lako! Kiuhalisia huna tofauti na mnyonyadamu ambaye anaishi kwa jasho letu halafu hana tija! Ipo siku mtazitapika nawaambia!
Huyu Zitto na wabunge wenzake ni wanafiki tuu!
 
Back
Top Bottom