Kanuni mpya ya TFF kuzuia udhamini kwa wachezaji inakandamiza maslahi ya wachezaji

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Kanuni mpya ya TFF kuzuia udhamini kwa wachezaji inakandamiza maslahi ya wachezaji.

Wiki iliyopita tuliona taarifa ya maboresho ya Bodi ya Ligi Tanzania yanayozuia au kuweka marufuku kwa mchezaji kuingia mkataba binafsi wa udhamini na mshindani kibiashara wa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ambaye kwa sasa ni Benki ya NBC.

Aidha, maboresho hayo ya kanuni yametaja adhabu endapo mchezaji atakiuka marufuku hayo. Imeeleza mchezaji atakayekiuka atafungiwa kwa kipindi cha kati ya mwezi mmoja na mitatu. Taarifa hii iliwaibua wadau mbalimbali wa michezo kwa kutoa maoni, mitazamo na mapendekezo. Licha ya malalamiko na maoni yaliyotolewa na wadau hatujaona TFF au Bodi ya Ligi ikijitokeza kutoa Mwongozo au ufafanuzi ama kuchukua hatua zozote katika kujibu hofu iliyopo.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia kwa Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta (Baraza Kivuli la Mawaziri) baada ya kupitia kanuni ya 16:1.2 ambayo imeongezwa maneno yafuatayo. “Hairuhusiwi kwa mchezaji kuingia mkataba binafsi wa udhamini na mshindani kibiashara wa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu.

Atakayekiuka atafungiwa kwa kipindi cha kati ya mwezi mmoja na mitatu.” Tumeshangazwa sana kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kupitia bodi ya Ligi kukubali kuingiza masharti haya katika wakati ambao nchi ina mapambana kuona michezo inaenda kuinua maisha ya vijana wengi kwa kutoa ajira na kukuza maslahi ya wachezaji. Tunaungana na wadau wengine kupinga maboresho hayo ya kanuni kwa sababu zifuatazo.

i. Kanuni hii inawanyima wachezaji uhuru na haki binafsi katika kujitafutia kipato. Mchezaji ni raia wa kawaida anayeweza kushiriki kwenye matangazo binafsi na kampuni au taasisi yoyote ambayo haikiuki haki za kipekee (exclusive rights) za Mdhamini Mkuu wa Ligi.

ii. TFF katika kununi ya 16 (1.4, 5,6) imeweka makatazo na utaratibu wa matangazo yasiyokuwa ya Mdhimini Mkuu ambapo vifungu vyote vimezuia maeneo ya uwanja pamoja na matumizi ya nembo ya mdhamini Mkuu kwenye vifaa vya kuchezea vya timu husika. Ni wazi kwamba haki zote kwa mdhamini mkuu zimeorodheshwa kuongeza kifungu hiki ni kukandamiza maslahi ya wachezaji.

iii. Maboresho ya kanuni hayajatoa tafairi ya shughuli zitakazo chukuliwa kuwa ni kuingiliana na zile za Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu. Hii inaweza kutoa tafsiri tofauti tofauti au inaweza kutumika vibaya kuzuia matangazo kwa wachezaji.

iv. Kanuni imekuja bila kuchukua uozefu kutoka maeneo mbalimbali duniani katika kusimamia haki na maslahi ya wachezaji linapoja suala la udhamini. Uzoefu wa wachezaji wakubwa duniani wamekuwa wakiingia mikataba binafsi na kampuni tofauti tofauti ambazo zina mgongano wa kimaslahi wa karibu. Mdhamani Mkuu hawezi kupewa haki ya Uhodhi hata kwa maisha ya wachezaji. Hii haikubaliki.

Hivyo basi, ACT Wazalendo kupitia kwa Msemaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tunaitaka TFF na Bodi ya Ligi kuondoa marekebisho haya mapya ili kulinda maslahi ya wachezaji hususani kutumia fursa ya matangazo kuongeza kipato.

Pili, tunaitaka kuwepo kwa ushirikishaji katika masuala yote ya michezo yanayohusu pande mbalimbali. TFF na Bodi ya Ligi haipaswi kufanya peke yao bila kushirikisha wadau wengine ambao wanaguswa na maamuzi wanayoyafanya.

Mwisho, Sekta ya michezo ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa vikapu na ngumi imetoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri. Kutokana na hatua ambayo Tanzania imeshafika katika sekta ya michezo hususani mpira wa miguu ni muhimu kila hatua itakayochukuliwa na vyombo vilivyopewa mamlaka ya usimamizi kufikiria hatua ya kuboresha maslahi ya vijana hawa kuliko hatua za kuwarudisha nyuma kwa kuweka taratibu, kanuni na miongozo kandamizi.

Ndg. Monalisa Joseph Ndala
Twitter: @Monalisandala1
Naibu Waziri Kivuli wa Utamaduni, Sanaa na Michezo
ACT Wazalendo.
22 Agosti, 2023
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom