Kambi ya Upinzani yasusia Bunge, watoka nje ya ukumbi

RingaRinga

JF-Expert Member
Jul 10, 2015
1,038
505
Wabunge wa upinzani wametoka nje kwa madai kuwa serikali ya awamu ya tano hadi sasa haina 'mwongozo wa kuiongoza nchi' haujatolewa, kwamba hadi sasa serikali inatumia mwongozo wa awamu ya nne.

Pg-1c-300x200.jpg

Madai mengine ni kupinga ubadilishwaji wa matumizi ya fedha kwa kigezo cha kubana matumizi bila kushirikisha bunge, hivyo wamesusia hotuba ya Waziri Mkuu.

======================

KUTOKA DODOMA.!

Wabunge wote upinzani wametoka nje ya ukumbi wa Bunge kususia kujadili budget ya Waziri mkuu kwa sababu 3;

#Mosi; Serikali haina dira inayoiongoza. Hadi sasa hakuna mpango wa maendeleo wa serikali. Yani serikali inaendeshwa bila dira jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa nchi. Hakuna mpango mkakati unaotumika kuongoza serikali. Yani Rais Magufuli anataka Tanzania ifike mahali ambapo hata yeye mwenyewe hajui ni wapi. Washauri wake wameshindwa kumpa dira (Vision/ Focus).

#Pili; Waandishi wa habari kuzuiwa kuingia Bungeni ni ukiukwaji wa haki za msingi za wananchi kupata habari na waandishi kuripoti habari. Na pia ni ukiukwaji wa katiba. Kwa mijubu wa Katiba ya nchi ibara ya 18 na 19 haki ya mtu kupata habari.

#Tatu; Kupinga maamuzi ya Ofisi ya Spika kupunguza matumizi ya bajeti ya Bunge na kurudisha fedha serikalini bila kushirikisha bunge. Hata kama Spika alitaka kupunguza bajeti ya Bunge alipaswa kushirikisha bunge kwanza ili wajadili na kufikia makubaliano, sio kujiamulia kibabe.!

HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI (KUB) MHESHIMIWA FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17.

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Januari, 2016
_________________________________


1. SHERIA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA MAWAZIRI (MINISTERS – DISCHARGE OF MINISTERIAL FUNCTIONS – ACT, 1980.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.

Inasomeka ifuatavyo: Nanukuu “the President shall from time to time by notice published in the Gazette, specify the departments, business and other matters and responsibility for which he has retained for himself or he has assigned under his direction to any minister and may in that notice specify the effective date of the assumption of that responsibility…….” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji wake na kazi kwa wizara mbalimbali. Hii ina maana kwamba Serikali inafanya kazi kwa kauli za Rais na Mawaziri bila kufuata mwongozo wowote wenye msingi na uhalali wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila Wizara (Instrument) unaotumika ni ule uliochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 494A la tarehe 17/12/2010. Kwa mujibu wa Instrument hiyo, majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni:
 Coordination of Government Business
 Leader of Government Business in the National Assembly
 Link between Political Parties and Government.
 National Festivals and Celebration of Management of Civic Contingencies (relief).
 Facilitation and Implementation of Plans for the Development of Dodoma as Capital of Tanzania.
 Coordination and Supervision of Transfer of the Government to Dodoma.
 Government Press Services.
 Investment, Economic Empowerment, Public-Private-Partnership (PPP), Poverty alleviation Policies and their Implementation.
 Facilitation of the Development of Informal Sector.
 Performance Improvement and Development of Human Resources under this Office
 Extra – Ministerial Department, Parastatal Organisations, Agencies, Programmes and Projects under this Office.

REGIONAL ADMINISTRATION AND LOCAL GOVERNMENT:
 Decentralization by Devolution (D by D), Rural Development, Urban Development Policies and their Implementation.
 Regional Administration.
 Primary and Secondary Education Administration
 Dar Rapid Transit – DART.
 Performance Improvement and Development of Human Resources under this Office.
 Extra-Ministerial Departments, Parastatal Organisations, Agencies, Programmes and Projects under this Office.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa Mwongozo wa 2010 ina maanisha kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale yaliyochapishwa mwaka 2010, kwa sababu gazeti hilo la Serikali halijafutwa.

2. UVUNJWAJI WA KATIBA NA SHERIA ZA NCHI KUHUSIANA NA BAJETI UNAOFANYWA NA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, hili ni Bunge la Bajeti ambalo kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepewa mamlaka ya kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaaka wa Bajeti kwa madhumuni ya kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya Serikali , kifungu cha 41(1) cha Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 kinaelekeza kwamba: “ Serikali itawasilisha Bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa”.

Mheshimiwa Spika utaratibu huu unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma wa mwaka 2001( Public Finacne Act, 2001)ambapo kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka Serikali kuleta Bungeni bajeti ya nyongeza ( mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huo wa kisheria umekuwa ukivunjwa na Serikali kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge jambo ambalo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha jambo hilo, kwa mfano bajeti ya maendeleo iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilikuwa ni shilingi bilioni 883.8 ambapo kati ya fedha hizo, fedha za ndani zilikuwa ni shilingi bilioni 191.6

Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza ni kwamba hadi kufikia mwezi Machi 2016 Wizara ilikuwa imeshapokea kutoka hazina shilingi bilioni 607.4 ikiwa ni fedha za ndani.

Mheshimiwa Spika, ukitazama takwimu hizo utaona kuwa kuna ongezeko la fedha zilizotolewa na hazina hadi kufikia mwezi Machi 2016 ukilinganisha na fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, hakuna bajeti ya nyongeza iliyoletwa Bungeni na Serikali kwa ajili ya kupata idhini kutokana na matakwa ya Sheria ya Bajeti ya 2015 au sheria ya Fedha ya 2015.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kuamua kufanya re-allocation ya bajeti bila kupata idhini ya Bunge ni dharau kwa bunge lakini mbaya zaidi ni uvunjaji wa Katiba na Sheria.

3. UHURU NA MADARAKA YA MHIMILI WA BUNGE

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalitaja Bunge kuwa ndicho chombo kikuu katika Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. Katika hali isiyo ya kawaida, kifungu hiki cha Katiba kimevunjwa na badala yake Serikali imelipoka bunge madaraka yake na Bunge kwa maana ya uongozi wake wanaonekana kushiriki na kukubali kupokwa huku kwa madaraka na uhuru wake.

Mheshimiwa Spika, Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, na wananchi wana haki ya kujua Bunge lao linavyofanya kazi ili wawe na uwezo wa kuwawajibisha wawakilishi wao iwapo hawafanyi kazi inavyostahili.

Katika hali isiyo ya kawaida, Serikali na uongozi wa Bunge, imewapoka wananchi haki yao ya kupata habari za Bunge kwa kuzuia mijadala Bungeni kurushwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa na vyombo vingine vya habari vya kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, Jambo hili pia ni uvunjwaji wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inasema kwamba kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, katika Mazingira kama hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiko tayari kuendelea kushiriki uvunjaji wa Katiba Sheria na haki za msingi za wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani haitakuwa tayari kuwasilisha hotuba yake katika mazingira haya na inaushauri uongozi wa Bunge kupata ufumbuzi wa haraka wa kadhia hii ili kurejesha heshima ya Bunge na haki za msingi za wananchi. Hivyo basi Kambi bado inatafakari kwa kina na makini hatua za kufuata.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Freeman Aikaeli Mbowe (Mb)

KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI NA
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU
22 Aprili, 2016.


Binafsi naona swala hili linaleta tafsiri tofautitofauti katika mustakabali wa siasa za Tz kwa siku hizi;

Moja- Kwa mustakabali wa kihistoria ktk kuweka kumbukumbu sawa lazima bunge liendelee kuisimamia serikali na kuhakikisha sheria kwa mujibu wa katiba ya nchi zinafuatwa. Hii inasaidia kuirudisha serikali katika mstari pindi inapoenda kinyume cha katiba, ingawa kwa kufanya au kutokufanya hivyo mambo mawili yote yanawezekana,
aidha rais atakuwa ametenda jambo jema la manufaa zaidi kuliko kusubiri taratibu za kisheria hasa kwa mambo ya dharula au anaweza kufanya jambo lenye kuleta uharibifu kwa taifa na kuturudisha nyuma. Ili kujenga utamaduni wa kuisimamia serikali ni muhimu kwa wabunge kuprotest katika mambo ambayo yanaenda kinyume na sheria, aidha kwa kuikumbusha tu au kupambana hadi kieleweke.

Pili- Kwa upande mwingine bunge lazima lifahamu kuwa huku nje ndiko hasa kuna mabwana wakubwa waliowatuma bungeni kwenda kuwakilisha maoni na vilio vyao. Hawa
muda wote wanataka kuona 'a right action at a right time' haijalishi maamuzi yametoka wapi. Hapa ndipo credit za kisiasa hujengwa, na ni swala la timing tu, anaewahi ndie anaepata
point, pia ukijua kuitumia nafasi ya aliyewahi unakula point pia.
Kwa nchi zetu za dunia ya tatu zilizochelewa ambazo wananchi wake wengi tunaishi Kwa dharula, ni vyema wanasiasa wetu wakajua kucheza na reality, haikufaa kujumuisha mambo yote hayo na kuyachukulia uamuzi unaofanana, ilifaa kumkumbusha tu rais umuhimu wa kushirikisha bunge kwenye kubadili matumizi ya fedha bila kusahau kupongeza kazi iliyofanyika. Siku nyingine jamii itaelewa vizuri pale litakapotokea jambo lisilofaa linalohitaji kupingwa lipingwe Kwa nguvu zote iwe Kwa kuprotest au kufanya chchte halali na wananchi watawaelewa na kiwaunga mkono.

Kwa hiyo basi;-
Kwa hoja zilizotolewa jana na KUB kwa mwananchi wa kawaida (80%+) ya
Watanzania hawawezi kukunwa na hoja hizo sanasana itaonekana upinzani kazi yao ni kupinga kila kitu na hiyo ni hatari kwa ustawi wa kambi ya
upinzani. Kimsingi katika mazingira ya sasa KUB ingetoka bungeni kwa hoja moja tu yakushinikiza mwongozo wa uongozi wa awamu ya tano, kwamba ilikuwa haiwezekani kuendelea mbele bila kuwa na mwongozo huo wananchi wangeelewa kuwa hayo ni mambo ya mjengoni wala sio hoja kwao tena wasingejishughulisha na swala hilo.Kwa siasa za Tz ambazo ni za kutafuta credibility kwa hoja na matukio, binafsi nilishaona JPM alikuwa anaijenga kambi ya upinzani Kwa kuwa mambo mengi waliyoyapigia kelele wapinzani yanafanyiwa kazi na rais severely hadi kufikia mahali wanasema anatekeleza ilani ya UKAWA. Sasa wanaanza kuipoteza credit hiyo, maana mwisho wa siku unaangalia 2020 utapanda au utashuka?
 
Wabunge wa upinzani wametoka nje kwa madai kuwa serikali ya awamu ya tano hadi sasa haina 'mwongozo wa kuiongoza nchi' haujatolewa, kwamba hadi sasa serikali inatumia mwongozo wa awamu ya tank. Madai mengine ni kupinga ubadilishwaji wa matumizi ya fedha kwa kigezo cha kubana matumizi bila kushirikisha binge, hivyo wamesusia hotuba ya waziri mkuu.
Habari zaidi zitafahamika hapa

Mie nadhani upinzani ni jicho la tatu na ni vizuri kuonyesha hayo mapungufu.lakini kususia siyo suruhu. Kama wanashirikiana na uongozi uliopo kwa mambo mbalimbali iweje sasa ukatae kuendelea kujadili budget kwa kisingizio cha kuwa mwongozo wa serikali ni wakizamani
 
Sijaelewa hapo unaposema hadi sasa serikali inatumia mwongozo wa awamu ya tano ,kwani tupo awamu gani ?
 
Naunga mkono kutoka kwao kwani nchi onaongozwa kwa matamko na sio sheria na taratibu kwa sasa. Najua wapo wanaojifanya viziwi na vipofu wanaoongozwa na ushabiki zaidi ya uhalisia watapinga hili. Na bado tutashuhudia madudu mengi kuliko haya. Ni muda tu utatuamua.
 
Back
Top Bottom