Kaburi lililokuwa jirani na kaburi langu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,341
51,907
KABURI LILILOKUWA JIRANI NA KABURI LANGU

Na, Robert Heriel

Kulikuwa na giza. Sikuweza kuona. Giza lilizidi uwezo wa mboni zangu. Giza totoro, Jepesi mwororo. Giza la Kaburi, lenye jeuri na kiburi. Hivi ndivyo Ilivyokuwa;

Niite Taikon wa Fasihi, Maiti ndani ya kaburi.

Sikumbuki nilifikaje, wala ilikuwaje mpaka nikafika mahali pale. Muhimu niseme; nilijikuta kwenye kiza totoro nikiwa nimelala chali kama kifo cha mende aliyeuawa na sumu kali. Puani nilikerwa na vitu nisivyokuwa navijua, vilikuwa ni nini? Hapo nikahisi jambo baya, na kabla sijapata jibu, mkono wangu wa kulia ulikuwa umeshafika kwenye matundu ya pua yangu, Masikini Taikon! Zilikuwa ni pamba! Pamba za maiti. Maiti ndani ya sanduku.

Inamaana nimekufa? Nikajiuliza swali la mauzauza kwani tangu lini mtu aliyekufa aweze kuuliza.

Taharuki na kiwewe kikanishika. Hima nikataka kuamka. Lakini siweza, nilipata pigo baya la kujigonga. Kumbe nilikuwa ndani ya Jeneza. Hapo moyo wangu ukapoteza mapigo, ukawa unapiga bila mpangilio ngudu! ngudu! kudu! kudu! Ngudu! kwa Pupa bila kusita. Huku maimivu kwa paji la uso yakisambaa kwa uchungu mwilini mwangu.

Tayari nimezikwa au bado? Nilijiuliza huku wasiwasi ukizidi kunikumbatia. Nilikata tamaa pale nilipokumbuka habari za kufukiwa kaburini na mchanga. Nilijua kuwa endapo nimefukiwa na mchanga, basi ni wazi kuwa habari yangu ndio ingekuwa imeisha. Ningesubiri kufa polepole kwa mateso ya njaa. Lakini nikajipa moyo kuwa siku hizi makaburi mengi hayafukiwi na mchanga bali huzibwa na zege kama kisima. Hapo matumaini yakawepo kidogoo. Ingawaje nilijua shida ya kupasua zege lililosiriba kaburi langu.

Basi nikaanza kuhisi joto kali ndani ya lile jeneza. Ukichanganya na yale marashi ya maiti niliyokuwa nimepuliziwa ndio tabu kabisa. Basi nikapeleka mkono kwenye sehemu ya kichwa, nikasukuma kwa nguvu bila mafanikio. Nikasukuma tena na tena, kwa bahati kifuniko cha jeneza kilichopo sehemu ya kichwa kikafunguka. Hooo! Nilivuta pumzi huku jasho likinitoka, nikiigombea hewa niliyoikuta nje ya jeneza lakini ndani ya jeneza. Ilikuwa ni hewa mbichi yenye harufu ya saruji. Nafikiri harufu ile ilitokana na zege lililokuwa limewekwa kwa juu.

Bila shaka nilizikwa masaa machache yaliyopita. Nilifikiri.

Bado kulikuwa na giza hata nisione Rangi la jeneza langu wala nguo nilizokuwa nimevalishwa. Nilijitoa ndani ya jeneza, kisha nikakaa juu yake. Nikasimama kisha nikashika paa la kaburi langu ambalo lilikuwa la zege. Looh! Bado lilikuwa bichi kabisa. Nilishika cement iliyochanganywa na kokoto.

Nikapiga akili nitafanyaje nitoke mule ndani ya kaburi. Basi nikavua kiatu kimoja, kisha nikaanza kubomoa lile Zege na kile kiatu nilichokuwa nimekivua. Nilifanya hivyo kwa muda wa nusu saa, nikaanza kusikia joto tena, nafikiri ni kutokana na damu kuchemka. Nikaongeza jitihada lakini wapi.

Niliwalaumu mafundi walioweka ile zege. Iweje waweke Zege Quality kwa kiwango kile. Yaani wameweka Zege kama wamefukia mali ya Mjerumani ndio ile Rupia. Mimi sio Rupia bhana mpaka wawekee kaburi langu Zege kama lotee! Nilijiwazia mambo hayo kwa hasira. Hata hivyo nisingesahau kuwashukuru kwa kuweka zege kwa maana kama ingekuwa ni kufukiwa na mchanga walahi leo hii nisingeandika mambo haya.

Nikachoka, nikakaa. Kiu nayo ikanisaliti, koo lilikauka kama nyama ya mgogo. Hapo nikaanza kukumbuka siku ya mwisho na mambo yaliyonikuta. Nilijikuta natoa machozi ya buriani na kukata tamaa. Pengine niseme; niliona ni muda wa kuyafanya machozi yangu maji ili niyanywe yakate kiu yangu iliyokuwa inanikaba kooni ikitaka kuniua. Looh! Machozi yalikuwa na chumvi, hayakuweza kukata kiu zaidi ya kuongeza.

Nikaamka tena, mara hii nikiapa kuwa ndio mara ya mwisho, nikachimbua chimbua ile zege hasa ile sehemu niliyoiona nimeichimba sana nikitegemea nitafika juu kabisa nje ya kaburi. Nikachimba! Nikachimba! Chimba wee!

Punde si punde nikashangaa maji yananimwagikia kutoka juu pale nilipochimbua. nnhooo! Niligugumia kwa ubaridi wa maji yale. Maji yalizidi kuingia na kupanua zaidi lile shimo. Sasa sikuwa na muda wa kupoteza, niliyafakamia maji yale nikiyanywa kama Kiliwanzoki. Jamani nilikuwa ninakiu, maji yale yalikuwa matamu licha ya kuwa yalikuwa na harufu ya saruji. Nilipotosheka kunywa maji, bado maji yakiendelea kuingia kwa kasi ndani ya lile kaburi. Tayari yalikuwa yamejaa na kufika usawa wa magoti.

Pale maji yanapoingilia tayari lilikuwa shimbo kubwa linalotosha kichwa kupita lakini isionekane nafasi ya kuona nje. Sikutaka kupoteza muda, nilishika kwenye lile shimo yanapoingilia maji upande huu na upande huu nikipabomoa zaidi ili pazidi kuwa papana nipate sehemu ya kutoka. Waaa! Nilifanikiwa.

Sasa nikashika huku na huku kwa mikono yangu iliyokuwa inatetemeka nikajivuta mpaka nje ya kaburi nikatoka.

Nilipokelewa na matone makubwa ya mvua huku giza la usiku likinitazama. Ilikuwa ni usiku mnene nilipofanikiwa kutoka ndani ya kaburi langu huku mvua kubwa ya mambwa na mapaka ikinyesha. Nikasimama juu ya kaburi langu nikiyatazama yale maji yaliyokuwa yakiingia ndani ya kaburi langu.

Radi na vimulimuli vikimulika mulika kila mara na kufanya nione nisione eneo lile la makaburi. Kumbe Mkononi nilivalishwa saa ya mshale yenye rangu ya Dhahabu. Nilipoitazama ili kuona ni saa ngapi, niliikuta imepoteza majira, nafikiri ni kutokana na kulowa maji. Hata hivyo muda wa mwisho kabla haijapoteza majira ilisomeka ni saa nane na nusu. Nikiri kuwa kama kusingekuwa na vimuli muli vya zile radi basi nisingeweza kusoma majira ya saa ile kutokana na giza la usiku ule.

"Bila shaka sasa hivi ni saa tisa" Nilijisemea kimoyo moyo huku matone ya mvua yakinichapa usoni hali iliyopelekea nifumbe macho kidogo na kujilamba lamba midomo kila saa.

Nikauona msalaba wa kaburi langu, nikausogelea huku nguo nilizovaa zikiwa tepetepe kwa kulowa na mvua ile ya kutisha. Mvua ya makaburini.

Bado mvua iliendelea, radi ikipiga. Msalaba wa kaburi langu ulisomeka majina yangu matatu, siku niliyozaliwa, siku niliyokufa, Kuhani aliyeendesha mazishi yangu na idadi ya waliokuja kunizika. Hayo yote niliyasoma kwa msaada wa vimuli muli vya radi. Maandishi yalikuwa yakionekana na kupotea kwa kadiri radi ilivyokuwa ikimulika. Ikimulika niliona, ikizima sikuweza kuona.

Hapo nikaona Makaburi manne yaliyokuwa yamezunguka kaburi langu. Yaani hawa ndio waliokuwa majirani zangu huko makaburini nilipokuwa nimezikwa.

Kaburi la kwanza lilikuwa upande wa kulia wa kaburi langu. Kaburi hili lilikuwa la vigae, pia lilikuwa na msalaba. Kaburi hili lilionyesha dhahiri shahiri lilikuwa la mtu mkubwa aliyekuwa na cheo au pengine tajiri enzi za uhai wake. Kaburi hili lilikuwa la zamani lakini bado lilionekana ni jipya. Kaburi hili halikuwa limebomoka wala maji ya mvua hayakuweza kuingia ndani alipohifadhiwa huyu jirani yangu. Bali maji ya mvua yalimwagika kwa pembeni na kutiririka kwenye maporomoko.

Mtu huyu niliposoma jina lake nilishtuka, lilikuwa jina kubwa sana, jina mashuhuri. Pia alizikwa na Kuhani mwenye jina kubwa hapa nchini. Loooh!

Kaburi la Pili, Lilikuwa upande wa kushoto wa kaburi langu. Hili lilikuwa kaburi la mchanga, likiwa limeunda mashimo yaliyoingiza maji ndani ya jirani yangu huyu. Kaburi hili lilikuwa limechoka ingawaje lilikuwa la juzi juzi tuu. Hatukuwa tumepishana mwezi na jirani yangu huyu. Nilipoangalia kuhani aliyemzika jirani yangu huyu, nilishangaa sana.

Wala hakuwa kuhani bali mtu wa dini tuu asiye na wadhifa wowote. Maji yote yaliyotoka kwenye kaburi la upande wa kulia(Kaburi la Vigae) yaliingia kwenye kaburi la kushoto ndilo kaburi la mchanga. Baadhi ya mifupa ya jirani yangu ilitolewa na maji na kubebwa kwenda kwenye maporomoko ambapo niliwaona mbwa wakiishambulia na kujipatia kitoweo. Looh!

Kaburi la Tatu, Lilikuwa upande wa Juu wa kaburi langu ambapo msalaba wa kaburi langu ulikuwepo. Kaburi hili lilikuwa ni la saruji lenye mashada na vitabu vya dini, vitabu vya sheria na vitabu vya nyimbo. Tofauti na makaburi yote, kaburi hili lilikuwa na kengele iliyofungwa na mnyororo ambayo upepo ukivuma kengele ile inajigonga na kutoa sauti. Niliposoma jina lake. Nilistaajabu sana. Alikuwa ni yule kuhani aliyemzika jirani yangu wa kaburi la kulia(Kaburi la Vigae).

Naye maji ya mvua hayakuweza kuingia ndani ya kaburi la kuhani. Bali yalijaa na kusomba mashada, baadhi ya vitabu na kuvipeleka kwenye kaburi la chini lililokuwa jirani yangu.

Kaburi la nne na la mwisho, Lilikuwa ni kaburi la chini ambapo kaburi langu liliielekeza miguu yangu huko. Kaburi hili lilikuwa na mashimo matatu yaliyokuwa yanaingiza maji ndani ya hili kaburi. Vitabu vyote vilivyochanika vilivyoletwa na maji yaliyotoka kwenye kaburi la tatu, ndilo kaburi la kuhani vilifanya kaburi hili kama jalala. Lilikuwa kaburi lenye makaratasi yaliyochanika chanika. Hakukuwa na kitabu hata kimoja kilichokuwa kizima kisichokuwa kimechanika ndani ya kaburi hili la mwishio, kaburi la chini.

Nikaenda kusoma jina la jirani yangu huyo wa nne aliyeupande wa chini wa kaburi langu. Lilisomeka jina moja tuu "Muumini"
Nalo lilikuwa ni kaburi la udongo kama lilivyokuwa kaburi la mkono wa kushoto.

Basi nikaona mifupa ya Muumini ikizuia yale makaratasi ya vile vitabu vilivyochanika chanika. Mifupa ya Muumini haikutaka hata karatasi moja ya vitabu vile vilivyochanika kubebwa na maji.

Basi nikaligeukia kaburi langu na kulitazama, kisha nikatazama mavazi yangu, kumbe nilikuwa nimevalishwa suti yenye rangi nyeusi. Nikavua suti niliyokuwa nimevaa nikabaki na nguo ya ndani. Kisha nikaiweka ile suti kwenye lile shimo la maji lililokuwa kwenye kaburi langu.

Nikaondoka na kurudi mjini nikiwa na kifua wazi na nguo ya ndani, mbua ikiendelea kunyesha.

Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa habari ya makaburi yaliyokuwa jirani na kaburi langu.

Acha nipumzike sasa. Mwenye swali anaweza kuuliza. Ila majibu yangu yatamtatizo.

Ulikuwa nami:

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Awam ya kwanza
Awamu ya pili
Awamu ya tatu
Awamu ya nne
Awamu ya tano

Huyo aliyefufuka kwenye kabuli lazima mzee wa kupigwa risasi nyingiiiii akapona.
 
Back
Top Bottom