Je, Serekali inajua uonevu na unyonyaji huu wa NOKIA-VODA kwa wahandisi hawa?

secyb

Member
Nov 4, 2012
5
10
JE SERIKALI INAJUA UONEVU NA UNYONYAJI HUU WA NOKIA– VODACOM KWA WAHANDISI HAWA?

KWAKO WAZIRI MWENYE DHAMANA YA VIJANA NA AJIRA:
Mheshimiwa waziri pole na majukumu ya ujenzi wa Taifa,
Awali ya yote tungependa kufahamu ikiwa wizara yako inafahamu kuhusiana na uonevu na unyonyaji unaoendeshwa na kampuni ya NOKIA inayosimamia mitambo ya kampuni ya mtandao wa simu ya VODACOM-TANZANIA ikishirikiana na kampuni ya kizalendo ya Northern Engineering Works Limited (NEWL) kwa wahandisi waajiriwa wa NEWL wanaofanya kazi NOKIA.
Lakini kama wizara haifahamu basi tungependa kukufahamisha kupitia waraka huu na pengine tuombe ufumbuzi wa haraka maana haki za wafanyakazi zinanyongwa na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi yetu zinazohusu masuala ya kazi yaani haki na wajibu wa Mwajiri na Mwajiriwa. Kwanza Kampuni ya NOKIA inafanya kazi zake kwa kutumia wahandisi waliogawanyika katika makundi mawili ambayo ni;
INTERNALS
Hawa ni wale wafanyakazi ambao awali walikuwa waajiriwa wa moja kwa moja wa kampuni ya VODACOM na ambao walihamia NOKIA baada ya Outsourcing ya idara ya ufundi (Technical department) yaani wakati VODACOM ikikabidhi mitambo yake kwa NOKIA, hawa walihama na mikataba yao ambayo ni open-ended (isiyo na ukomo) na haki zote zimeendelea kuzingatiwa kama ilivyokuwa wakati wakiwa VODACOM. Kwa kiwango kikubwa hawa hawasumbuliwi na NOKIA kwakuwa mikataba yao inawalinda na hata mikataba yao ina stahiki zote zikiwemo Overtimes, Likizo zinazoeleweka na masuala yao yote yanayohusu rasilimali watu yanasimamiwa vizuri zikiwemo likizo za ugonjwa na hata masuala kama kufariki ama kupata ulemavu kazini yameelezwa kwa uwazi katika mikataba yao. Hawa pia wana haki ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki kutokana na aina ya mikataba yao na kwakuwa wamesaini mikataba na NOKIA ambao wana sera za kudhamini wafanyakazi wanapokuwa wanahitaji mikopo.

EXTERNALS
Hawa ni akina sisi, lile kundi ambalo limeajiriwa baada ya outsourcing yaani wafanyakazi walioajiriwa baada ya VODACOM kukabidhi mitambo yao kwa NOKIA. Sisi wote tumeajiriwa na NOKIA kwa maana kuanzia usaili, majukumu yetu na kila kitu kinachohusu ajira yetu kimapatano kimefanywa na NOKIA lakini mikataba imetolewa na kampuni ya kitanzania ya Northern Engineering Works Limited (NEWL) kwa maana nyingine 3rd Part. Majukumu yetu yote yanapangwa na NOKIA na tunaripoti NOKIA isipokuwa pale tunapokuwa tuna madai flani basi huambiwa mwajiri wako ni NEWL na mara tunapoenda NEWL basi NEWL wanakuwa hawajui lolote zaidi ya kusema ongea na managers wako ambao wako NOKIA na mwisho huishia kukata tamaa. Waraka huu hasa unahusu namna aina hii ya pili ya wafanyakazi tunavyonyanyaswa na kukosa haki zetu.
Baada ya utangulizi huo wa aina ya wafanyakazi/wahandisi labda nikupeleke moja kwa moja kwenye lengo la waraka huu, kama ilivyotanguliwa kusemwa hapo juu ni kuwa hasa waraka huu unahusu unyanyasaji tunaoupata sisi EXTERNALS kama ilivyofafanuliwa hapa chini.
MIKATABA YA MUDA MFUPI ISIYO NA ONGEZEKO LA MASLAHI
Sisi Externals mara zote hupewa mikataba isiyozidi mwaka mmoja, mara ya mwisho mikataba iliisha oktoba mwaka jana (2015) lakini cha kushangaza badala ya kupewa mikataba ya muda mrefu tulitumiwa barua na kutakiwa kuzisaini. Barua hizo zilikuwa za ukurasa mmoja zilizoeleza kuwa mikataba yetu imerefushwa kwa muda wa miezi minne ikiwa na maslahi sawa sawa na ile tuliyokuwa tumesaini awali (oktoba 2014). Hivi unaposoma waraka huu, mikataba yetu kwa maana kama ilivyosemwa katika barua hizo inaisha February 2016 yaani mwezi huu na hatuna matumaini ya kupatiwa mikataba ya muda mrefu angalau inayozidi mwaka mmoja. Huko awali tulipata kutaka kukataa kusaini lakini kama ujuavyo ukosefu wa ajira umekuwa unatumiwa vibaya na waajiri kwa manufaa yao huku ikiacha vilio kwa wafanyakazi, iliishia kuitwa wachache wenye ushawishi wakaongezewa maslahi na kusaini na wengine kujikuta tukitishwa na tukalazimika kusaini. Mikataba hii mara zote imekuwa haina ongezeko la maslahi yaani Salary Review, maslahi yamebaki hayohayo kwa miaka yote ya ajira bila ongezeko lolote. Mh Waziri, mikataba hii ya muda mfupi si tu kwamba inatufanya tufanye kazi kwa wasiwasi lakini pia inatunyima fursa ya MIKOPO na huku kampuni yenyewe ya NEWL ambayo ndo tunaingia nayo mikataba na kwahiyo kuwa kama mwajiri wetu ikiwa haina sera ya kudhamini wafanyakazi wanapohitaji mikopo benki. Huu ni unyanyasaji mkubwa ikizingatiwa wenzetu ambao tunafanya kazi moja ambao wanajulikana kama INTERNALS wanapata haki zote za mikopo na nyongeza ya kila mwaka ya mishahara kutokana na mikataba yao ya muda mrefu na inayowapa haki zao kama ilivyokuwa wakati wakiwa VODACOM.

UKOSEFU WA UTARATIBU WA LIKIZO, UHAMISHO, FIDIA ZA AJALI NA KIFO NA HAKI ZINGINE

LIKIZO NA POSHO ZA SAFARI:
Mh. Waziri, wakati internals wakiwa wanajaza likizo zao kwenye system inayoeleweka sisi Externals tumekuwa tunaambiwa tuwasilishe mpango wa likizo wa mwaka kwa mkuu wa idara ya ufundi(HOD) ambaye anajulikana kwa jina la Shahid Butt. Huyu ndo mwenye mamlaka ya kusema sasa hakuna likizo na sasa wawezaenda likizo kwa siku anazopanga yeye ilhali mikataba inaonyesha kuwepo kwa siku 28 za likizo kwa kila miezi 12 ya kazi. Akisema huyu hakuna wa kumpinga. Kinachosikitisha ni kuwa hata kampuni mwajiri yaani NEWL ambao ndo hutoa mikataba yetu haina sauti kwa huyu mtu. sasa katika mikataba inasemwa kuwa ikifika miezi 12 hujaenda likizo basi inakuwa imefutwa isipokuwa uwe na maandishi ya kuwa likizo yako imeahrishwa kutoka kwa mwajiri (all unserved leaves are forfeited unless stated by employer). Kwa utaratibu huu ikiwa mkuu huyu wa idara (HOD) amekukatalia kwenda likizo na mwajiri wako NEWL kwakuwa hana sauti na wala anakuwa hajui kama umekataliwa kwakuwa likizo unaomba kwa huyu HOD badala ya HR manager wa NEWL ambaye kisheria ndo mwajiri, likizo nyingi huishia kufutwa na wafanyakazi kumaliza mwaka bila likizo na kuingia mikataba mipya mwaka unaofuata, likizo inakuwa imepotea. Mkuu wa idara huyu ana sauti sana hata katika masuala ya posho za kulala nje ya kituo cha kazi, asipopitisha huyu basi hata kama umesafiri NEWL hawakulipi na mara nyingine Mamanager wa kanda (Regional Operation Manager-ROM) wanakuwa wamepitisha safari na sababu ziko wazi lakini ni hadi ajisikie ndo atapitisha ndo ulipwe kwahiyo unajikuta umetumia hela yako na haulipwi kwa wakati.

FIDIA ZA AJALI NA VIFO:
Mikataba hii pia haionyeshi haki za mfanyakazi ikiwa atapata tatizo akiwa kazini kama ajali akapata kilema ama akifariki familia yake inafaidika na nini. Yaani ni kurasa mbili bila kiambatanisho cha company policy wala codes za kampuni. Hii ni hatari hasa ukizingatia kuwa tunafanyakazi kwenye mazingira hatarishi na hata kuendesha magari kwa muda na umbali mrefu na sehemu zenye milima na barabara mbaya kwakuwa minara mingi imewekwa sehemu zenye miinuko.

UHAMISHO:
Mikataba hii pia haionyeshi haki za kuhamishwa na matokeo yake inapotokea mtu anahamishwa anapewa tu 500,000/- fixed bila kujali kama ana familia ama hana. Na hili limepelekea kila kunapokuwa na upungufu wa mfanyakazi/mhandisi mahali na mhandisi mwingine akatakiwa kwenda kuziba nafasi yake kwa muda basi NOKIA huagiza NEWL wamhamishe mtu mmoja kwenda huko, hapa hutasikia Internal akihamishwa maana haki zake zipo kwenye mikataba waliyotoka nayo VODACOM na kwahiyo wanaogopwa. Sasa imekuwa tabia hata kama ni mtu anatakiwa kwenda kukaa miezi 2 basi badala ya kupewa posho ya malazi ya kila siku unaambiwa hamia kwa muda na unapewa 500,000/- basi imetoka, sasa familia unaiachaje? Huko unakoenda unapanga kwa nani kwa miezi 2? Huu ni unyanyasaji mkubwa.

MIKATABA ISIYO NA OVERTIME, HARDSHIP/RISK ALLOWANCES:

Mh.Waziri, NEWL kwa kushirikiana na NOKIA wamekuwa wakitoa mikataba kwa wafanyakazi/wahandisi ambayo haina haki ya Overtime wala Risk allowance. Ifahamike kuwa mikataba yao inasema siku za kazi ni Jumatatu hadi Ijumaa (masaa 8 kwa siku) na Jumamosi ( saa 2 hadi saa 7-masaa matano) ambayo ni zaidi ya masaa 40 kwa wiki yaani masaa 45 kwa wiki. Lakini kutokana na aina ya kazi hizi za mitandao ya simu, kazi nyingi zinazohusisha kuzima mitambo kwa ajili ya matengenezo basi hufanywa usiku ambapo watumiaji ni wachache lakini pia mara zote unakuta upo kazini kwa maana ikitokea hitilafu kwenye mitandao hata kama ni baada ya saa za kazi ama ni Jumapili au sikukuu basi unalazimika kufanya kazi. Kwa makusudi haki hii ya Overtime ipo kwa wale wafanyakazi wa NOKIA internals tu lakini wale Externals ambao tunapewa mikataba na NEWL hakuna Overtime na hata wale ambao tunafanya kazi kwenye maeneo hatarishi hatupewi hardship allowances, tunaomba hili liangaliwe na ikibidi wote tuwe na haki sawa bila kubagua Internals wala Externals.

KUPANDISHWA VYEO:
Hapa pia Mh. Waziri hakuna usawa yaani hutakuja kusikia external amepandishwa cheo hapa kwetu, mfano ni kama sasa wakati wafanyakazi wengi hasa mikoani wakiwa wale wa tabaka la Externals yaani wale waajiriwa wa NEWL lakini Managers wa kanda wote ni Internals na mara zote inapotokea nafasi ni hawa tu wanaoangaliwa. Tunahitaji kuona usawa katika hili.


USHUGHULIKIWAJI WA MAKOSA YA KINIDHAMU KAZINI:
Mh.Maziri; hapa ni mahala pengine ambapo pamekuwa na uonevu wa kupindukia, inapotokea External akafanya kosa la kinidhamu mfano kuzidisha mwendo kasi wa gari (100kph) basi huitwa kupewa onyo ama kufukuzwa kazi. Mara zote anayekuita ni NEWL kama mwajiri lakini ukifika makao makuu ya NEWL Arusha hutakutana na mtu wa NOKIA ambao ni wakusanyaji wa ripoti zote ikiwemo kuangalia utendaji wako na mambo mengine ya kinidhamu. Unaishiwa kusomewa mashitaka na kuambiwa adhabu kama ni kufukuzwa ama kupewa barua ya onyo. Hapa hata kama ungejieleza vipi huwezibadilisha hukumu maana Director wa NOKIA (Janik Pawel) anakuwa ameshatoa maelekezo na NEWL hawana mamlaka ya kupangua alichopanga yeye. Huyu ndo kila kitu na ndo anayempa mamlaka Shahid Butt(HOD) yule mpanga likizo na posho. Hakuna haki katika namna Hearings zinavyoendeshwa maana NEWL kama third part anapokea malalamiko toka kwa NOKIA lakini wakati wa kusomewa mashitaka na kupewa hukumu NOKIA anakuwa keshatoa mwongozo na hayupo, ilipaswa kuwepo mshitaki na anayeshitakiwa halafu NEWL kama mwajiri kisheria ndo awe mwamuzi kulingana na maelezo na utetezi wa mwajiriwa. Adhabu isipangwe kabla ya kusikilizwa na kufanya usikilizwaji kuwa kama suala la kutimiza wajibu tu na matakwa ya sheria za kazi.

TOFAUTI YA MISHAHARA KATI YA WAGENI NA WAZAWA PAMOJA NA UCHELEWESHWAJI WA MISHAHARA KWA EXTERNALS.

Mh. Waziri, katika mambo yanayotusononesha na kutukatisha tamaa mojawapo ni tofauti kubwa ya mishahara kati ya wafanyakazi wazawa na wale wa kigeni. Wakati wahandisi na wafanyakazi wengine wanaotoka nje wakiwa wanafanya kazi zilezile tunazofanya sisi huku wanalipwa mishahara mikubwa na kupangishiwa kwenye mahotel makubwa, mishahara ya wahandisi wazawa ni ya chini, haina posho za makazi na haina uwiano kabisa na wageni hawa ilihali kazi tunazofanya zinafanana. Huu ni unyanyasaji na ubaguzi ambao haupaswi kuendelea katika nchi yetu.
Lakini pia jambo jingine linaloumiza zaidi hasa EXTERNALS ni namna mishahara inavyocheleweshwa tena bila maelezo yoyote. Mara nyingi imekuwa inatokea mishahara ya mwezi uliopita mnaipata hadi tarehe 5 ya mwezi mpya na hakuna maelezo yoyote kutoka NEWL wala NOKIA yanayotolewa. Wakati INTERNALS mishahara yao ikichelewa sana haipiti tarehe 25 kwa upande wa EXTERNALS hali ni tofauti kwani ni mara chache mishahara inaingia katika tarehe iliyowekwa kwenye mikataba yaani tarehe 28. Kimekuwa kilio cha siku nyingi na tungependakuona wizara na serikali yetu inatusaidia kuondoa uonevu huu.

Mh. Waziri wewe ndo tumaini letu na tunaomba ofisi yako iwashinikize NOKIA na NEWL kuweka wazi namna haki za mfanyakazi zinavyopaswa kusimamiwa, ifahamike nani mwenye sauti katika lipi na zaidi NEWL kama mwajiri asimamie haki za wafanyakazi ambao wako chini yake hata kama wanafanya kazi za NOKIA. Masuala kama likizo, uhamisho, kuugua, misiba, Overtimes na Perdiems ziangaliwe na mwajiri ambaye kisheria ni NEWL. Ama la wafanyakazi wote tupewe mikataba ya NOKIA.

Tunaomba masuala haya yashughulikiwe kwa uharaka maana huu ndo mwezi wa mwisho na ndo mwezi ambao wataanza kutoa mikataba mipya na kwakuwa tunafahamu wapo wenzetu wanaoshawishika kirahisi, itakapofika muda wa kusaini mikataba mipya mambo haya yawe yamezingatiwa ili kusiwepo na muendelezo wa masuala ya unyonyaji na unyanyasaji kwetu NOKIA Externals maana kukosekana kwa umoja kunatunyima haki kwa kiwango kikubwa kwakuwa waajiri hawa wanatumia Divide and rule principle kuhalalisha unyonyaji wao.

Tunatanguliza shukrani zetu kwako na tuna imani na wewe pamoja na Serikali nzima ya Rais JPM kuwa inadhamira ya kukomboa watanzania ikiwa ni pamoja na kuwalinda raia wake dhidi ya wawekezaji wanyonyaji.

Asante,
Wako katika ujenzi wa Taifa;
NOKIA EXTERNALS.
 
Si ndio ume wajulisha au ulisha taarifu kabla?, pengine walikuwa hawajui wape muda maana ina hitaji wakati wa kutosha kusoma huu utenzi, kuwa na subira ila ni habari ni ya kusikitisha, poleni.
 
Back
Top Bottom