Je, Hekima ni Uhuru? Tafakuri ya Mijadala kutoka UDSM; Kigoda cha Mwl. Nyerere na IGA

Msafiri Haule

Member
Aug 6, 2018
28
18
Na Msafiri Egno Haule,

Chuo kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na historia nzuri ya kuchombeza mijadala yenye kuvutua alaiki ya watanzania wengi. Hii inakuja baada ya wachagizaji wa mada hizo wengi wao kuwa ni wanazuoni wenye kujadili hoja vile zilivyo na si vile wao walivyo. Kwa muktadha wa watanzania wengi wenye kupenda mijadala, ukitaja “Kigoda cha Mwl Nyerere” pasi na shaka haitakuwa mada ngeni kwao. Ukizungumzia ndaki ya Sayansi za Jamii hususani idara mama ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, kwa wapenda mijadala si rahisi kutosema neno la mvuto juu ya uhusikaji wa idara hiyo katika kuyasemea yanayohusu wanajamii kwa lugha rahisi.

Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni, “UDSM” haijapokea sifa maridhawa juu ya mijadala. Badala yake, wanataaluma na wanajumuiya wake kwa ujumla wameonekana kukosolewa mara kadhaa kwa dhana kwamba wamekuwa wakitumika “kupotosha ukweli”, “ubinafsi na unafsi wa kitaaluma” na “kushamili kwa itikadi za kisiasa” nk. Hoja zote zinazotajwa zinaweza kukubaliwa hasa kwa sababu kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi Chuo kikuu cha Dar es Salaam hakijapata mapokeo halisi ya wanajumuiya na washirika wake katika mijadala.

Kama hivyo haitoshi, chuo hicho kimekuwa kikikosolewa mara kadhaa kuwa wanajumuiya wake wanatumia usaliti wa kitaaluma kama njia ya kupokea uteuzi na madaraka ya kisiasa. Japo dai hili laweza kukosa hoja za ushindi ila halipaswi kupotezewa.

Je, Hekima ni Uhuru?
Yamkini isiwe rahisi katika kubaini maana moja na halisi juu ya hekima ni kitu gani kwasababu, ni neno mtambuka lenye kuchochewa na nadharia kadha wa kadha. Mfano, kidini na kijamii. Ila, mitazamo yote inakubaliana kwa pamoja juu ya maana ya hekima yenye kuhusisha Hali ya mtu kuwa na ufahamu na maarifa yenye kuwezesha kutoa tafsiri sahihi ya lipi ni jema na baya.

Na kwa kupitia maana hiyo, tunaweza kukubaliana kwa pamoja kuwa moto wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam kuwa “Hekima ni Uhuru” ulilenga kuwatambua wanajumuiya wake na wote kuwa wenye maarifa na ufahamu, ni rahisi kwao kuyaelewa mambo kwa ukweli wake mtupu pasi na kuegemea upande mwingine maana mara zote Ukweli ni Ukweli. Na hapa tunapaswa kuelewa vilevile, tunahimizwa kuyaelewa mambo vile yalivyo na si kwasababu vile sisi tulivyo.

Yaani, mfano, Karumanzile ni shabiki wa chama cha Walalahoi na ndugu Kipapai ni kidedea wa chama cha Walaliahoi, wote hawa wawili katika mtizamo mama wa “Hekima ni Uhuru” wanashurutishwa kutua vifungo vya ushabiki wa vyama vyao, badala yake washindanishe hoja zao kwa wingi wa nafuu ya kuleta suluhu ya tatizo au changamoto iliyomezani. Na baada ya majadiliano, iwe rahisi kwa ndugu Karumanzile kumpa mkono ndugu Kipapai (au kinyume chake) kwa ushindi wa ujenzi wa hoja zake pasi na kudhuliana.

Kigoda cha Mwl Nyerere
Tarehe 26-27 ya mwezi juni mwaka 2023, kulikuwa na mijadala mbalimbali yenye mada kadha wa kadha. Mijadala hiyo ilikuwa ikichagizwa na wachokoza mada mbalimbali waliokuwa wakiongozwa na waongozaji tofauti tofauti waliogawanywa na waandaaji wa kigoda hicho. Tunaweza kukubaliana kwamba Lengo la kigoda ni kuenzi fikra za Mwl Nyerere katika kustawisha jamii ya sasa. Kwa mujibu wa washiriki wakiongozwa nami, tunakubaliana kwamba mijadala hiyo inaendeshwa katika namna ya weledi mkubwa hasa kwa kuzingatia hadhira iliyo mbeleni yenye kujumuisha watu wa kada mbalimbali zikiwemo; Siasa, Uchumi, Mazingira nk.

Maarifa tunayoyapata katika mijadala ile tena bure kabisa naungana na wengi kuamini kuwa bado Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimebeba moyo wa taaluma/maarifa nchini.

Katika kuelezea mazuri ya kigoda hicho, sifungwi kuyaelewa yale pia ambayo yanaweza kuchafua taswira ya kigoda na na chuo kwa ujumla juu ya dhana mama ya hekima ni UHURU. Mfano; katika mjadala uliowakutanisha wanasiasa na viongozi nguli akiwemo Prof. Tibaijuka, ambapo katika kunawilisha hoja na haja zake alizolenga kufikishia umma wa hadhira ile, kwa hakika na kwa maoni yangu, hakutendewa haki na aliyekuwa anaongoza mjadala ule (Prof. Mukandala). Kwanini? Kwasababu video iliyokuwa ikieleza hoja juu ya mjadala ule iliamriwa kukatwa.

Hata hivyo, hadhira iliyokuwepo pahala pale, kwa maoni yangu, ilikosa kuunganisha mantiki na maana iliyolengwa na mzungumzaji. Sambamba na mwongozaji (Prof. Mukandala), baada ya kuhojiwa na mmoja wa washiriki kusema kwamba, muda ndiyo sababu haswa na Hata hivyo, alikuwa akielezea mada isiyoitishwa nyakati zile. Bado kuna hoja nyingi kinzani, hasa baada ya kile alichokuwa anakisema Prof. Tibaijuka kuwa na maslahi ya taifa kwa kipindi cha hivi karibuni (Sakata la Mkataba wa Bandari kati ya Tanzania na emirati ya Dubai).

Kinachosikitisha zaidi pia, Prof. Mukandala alimjibu muuliza swali kwa jazba, aliamulu kipaza sauti chake kinyang’anywe na hata hivyo kiu ya kusikia maswali zaidi kutoka kwa mzungumzaji yule ilikoma. Sasa, kwa kitendo kama kile, kufanywa na mtu aliye wa hadhi kama yake, katika muktadha kama ule wenye kuwaleta pamoja watu tofauti tofauti wenye kuamini HEKIMA NI UHURU, nahoji kwamba, Haikuwa sawa, haivumiliki na wala haikubaliki hususani katika taasisi inayosadikika kuwa na uvumilivu wa kitaaluma. Kwa hali ilivyokuwa na kwa kufikiria kuwa kuna wageni kutoka mataifa mbalimbali, ni rahisi kufikiri kwamba taasisi za kielimu nchini hazipo huru katika mijadala na taaluma kwa ujumla, wakufunzi wake huweza kutumika kudumaza na kuzika hoja na haja juu ya maoni ya umma vile vile wanaweza kuhoji kwamba uvumilivu wa kitaaluma ni kiulizo nchini.

Kiu yetu washiriki ilikuwa inalenga kufahamu ni kwa namna gani Prof. Tibaijuka aliweza kuunganisha mchango wa raia wanaoishi nchi za nje (Diaspora) katika kuchagiza maendeleo ya nchi yetu hasa kwa kutumia sakata la mkataba wa bandari, sasa isivyo bahati, na kwa nia ambayo haiwezi kueleweka kama ilikuwa njema, tumekosa wazo lake la pamoja.

Hivyo basi, kwa madhumuni mapana ya kunawilisha taasisi zetu za kitaaluma kama Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam chenye moto usemao Hekima ni Uhuru, hatuwezi kujenga kizazi chema cha kesho chenye mawazo ya hofu na woga. Daima tukubaliane kuwa Ukweli ni Ukweli na mara nyingi ukweli huwa na kawaida ya kujirudia.

Tuweke kando mawazo yetu ya kiitikadi linapofika suala la taaluma. Tusiwe wasaliti katika kuyanena yaliyo kweli, kweli zetu zitatufanya tuwe huru Daima.

Mjadala juu ya Mkataba wa Makubaliano kati Nchi ya Tanzania na Emirati ya Dubai juu ya Bandari.

Tarehe 28/06/2023 iliitishwa tukio hili, na katika wito huo, ilielekezwa kama ni mwendelezo wa semina katika ndaki ya Sayansi za Jamii, Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, katika kipeperushi ilielezwa kwamba “mlumbi” wa mjadala huo ni Dr. Richard Mbunda (Mhadhiri kutoka idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma).

Kwakuwa kulikuwa na maswali mengi yenye kuniumiza akili, porojo nyingi nisizo zielewa, matamko mengi yenye nia ya kutetea itikadi fulani, tabaka, dini, asili na hata fani, nikajipa muda nami niweze kuwasikiliza WENYE HEKIMA.

Nilitamani kuwasikia wanataaluma wakichagiza jambo juu ya huo mjadala. Kwa sasa umekua na hoja nyingi nyingine hata zenye kutweza utu na imani yake. Kuna siku nilipata kuandika katika kurasa zangu za kijamii nikihoji kwanini Chuo kikuu cha Dar Es Salaam wakiongozwa na idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma hawajaandaa mjadala huru wa kitaaluma juu ya sakata hili lenye maslahi ya taifa, na kwa hakika, siku kadhaa mbele walinijibu kwa vitendo. Hili niwe muwazi nilipendezwa nalo sana.

Ushiriki wangu uliongezwa chachu hasa baada ya kumwona gwiji wa Sheria, Prof Issa Shivji, akiwa miongoni mwa Walumbi wa mjadala huo. Kwa tafsiri na maoni yangu, mjadala ule ulitoa maana halisi ya HEKIMA NI UHURU.

Ukiongozwa na Dr Kamata, wachangiaji walionekana kuridhishwa si tu kwa kile walichokisikia kutoka kwa walumbi, bali hata wao kupata muda wa kutosha kuelezea uelewa na kutaja vifungu vyenye kuleta shaka na hofu juu ya mkataba huo wa bandari.

Dkt. Richard Mbunda
Alianza kwa kututolea mashaka tuliokusajyika eneo lile, baada ya kusema anachokifanya pale kimepewa heshima zote na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ibara ya 27. Vile vile, kwa kuelewa muktadha wa sakata lenyewe, kwa kuhusianisha na nadharia mbalimbali kama vile za kulielezea jambo hilo kwa Mfano, alitaja muktadha wa kiuwekezaji, kisiasa na hata kisheria.

Msisitizo uliwekwa katika dhana ya uwekezaji ambayo ndiyo inapigiwa chapuo sana na upande wa serikali katika kutetea hoja zake. Katika uwekezaji, Dr Mbunda alisema kuna Uendeshaji, Ubinafsishaji, Ubia na Ukodishaji. Na kwa maoni yake, mkataba unalenga kukodisha bandari kwenda DPW.

Lakini, hakuishia hivyo tu, alitoa hoja katika namna ya kuuliza maswali, kama vile, Je, ni kwa namna gani DPW imefikia makubaliano na Serikali ya Tanzania? Nikimnukuu “Unsolicited Proposal?” au ni “Single Source?”. Vile vile, alishangazwa na kwa nini bunge halikuridhia au kujadili mapendekezo kutoka kwa wataalamu wake “parliamentary secretariat”?

Licha ya kusema mengi ambayo pengine nisiwe na nafasi ya kuyasema hapa yote, bado alitoa siha ya kututoa hapa tulipo na kwenda mbele. Miongoni mwa suluhu alizozitoa ni kwamba, wananchi hawapswi kukaa kimya, badala yake waendelee kuujadili. Hata hivyo, kelele za wananchi hazipaswi kuchukuliwa kama ni uchochezi.

Kushinikiza “host government agreements kuidhinishwa na bunge. Pia, ikibidi, TPA iwe na kampuni, na hivyo mkataba huu uwe ni ubia kati ya kampuni ya TPA na ile ya DPW.

Prof. Issa Shivji, Ni miongoni mwa wasomi wachache nchini, wenye kujizolea umaarufu hasa ifikapo wakati wa kusimama na kusaidia umma kufikia ukweli, hasa katika mambo mbalimbali yanayohusu sheria na siasa.

Akiwa kama mlumbi wa semina, alianza kwa kutanabaisha kuwa atajadili na kutolea maoni zaidi juu ya mkataba wenyewe kuliko muktadha wake.

Hakuonyesha utofauti mkubwa katika hoja za vipengele vya mkataba vyenye kuleta viulizo. Mfano, muda wa mkataba kutowekwa bayana. Kwanini haki zote ziwe upande wa DPW na Wajibu kuwa upande wa Tanzania? Ni nani atakayenufaika na ufanisi? Kuna uhakika wa kiwango gani juu ya ajira zinazotajwa kupatikana baada ya makubaliano hayo,? Na uhakika wa ajira unatoka wapi ikiwa hoja ya ufanisi inatokana na kwamba DPW hutumia zaidi mashine katika utendaji wa shughuli zao? Ajira kwa maana ya “Makuli”?

Hata hivyo, alihoji ikiwa tatizo ni ufanisi, kwanini wasiajiriwe watu kutoka kwa hao DPW na bado Tanzania ikawa na jukumu la kulinda rasilimali hii? Pamoja na yote, alijinasibu kwa kusema kwamba bandari ni miongoni mwa sekta nyeti kama zilivyo sekta za afya, nishati nk ambazo kwa maoni yake hazipaswi kubinafsishwa (nukuu, “bandari ni roho na mishipa ya uchumi wetu”).

Lakini pia, alidokeza kuwa kitendo cha vipengele vya mkataba huo kutotii mamlaka ya katiba na sheria zetu ni kitendo cha kujaribu kudogosha hata mamlaka ya Rais. Dr Kamata, Mwenyekiti wa semina hiyo alichagiza hoja hiyo kwa kusema “Rais amejinyima mamlaka ya ardhi nakadhalika kwa DPW. Vile vile, kuna kipengele kinachojadili hoja za kodi. Ambapo, ni sheria zetu za wakati wa kusaini mkataba huu ndizo zitakazotumika kufanya marejeo; ambapo kwa kusema hivyo na kwa kufahamu sheria za kodi zinatoa mwanya wa kutoa msamaha wa kodi, ni kuendelea kufuta matumaini kabisa kama uwekezaji/ukodishaji huo waweza kuwa na tija kwa taifa.

Pamoja na yote hayo, Prof Shivji, katika kuhakikisha kuwa hekima inasalia kuwa ni uhuru, alitoa mapendekezo ya suluhu ya nini kifanyike ili mkataba huo ukose nguvu ya kisheria (kujitoa):

Mosi, amependekeza kwenda mahakamani kuhoji kuwa azimio la bunge juu ya mkataba ni batili kwakuwa ni kinyume na katiba Kwasababu limelidhia mkataba/ makubaliano ambayo ni kinyume na katiba pia.

Pili, bunge linaweza kupokea msukumo/shinikizo kutoka kwa wananchi, wakishinikiza kuondoa azimio lililowekwa juu ya kuridhia mkataba huo. Na katika hili, jukumu la vijana ni kubwa mno, akiwaasa kuwa tayari katika utetezi wa rasilimali za nchi.

Katika yote haya, ilinichukua muda wa takribani masaa manne, kusikiliza, kuandika, kujifunza na hata kuhoji pasipo eleweka au penye uhitaji wa kufafanuliwa zaidi. Kwa nafasi yangu, kama mdau wa mihadhara ya kitaaluma, semina, midahalo na hata mikutano, nilijisikia fahari na heshima kuwa pahala pale (COSS BOARDROOM).

Palijawa na taarifa zilizo zidi sifa. Hapakuwa na kashfa zaidi ni maarifa. Kwa hadhira iliyoshiba ufahamu hatukukoseshwa hamu. Na kwa kuhitimisha kiulizo cha andiko hili (Je, Hekima ni Uhuru?), hoja yangu ni;; Kama kutakuwa na mwendelezo wa semina za namna ile, mkutano/ warsha/ mjadala wenye kushirikisha wadau kwa kiwango kile, uhuru wa namna ile basi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinasawili moto wake kuwa HEKIMA NI UHURU.

Msafiri Egno Haule
0758059818
msfrhaule@gmail.com
 
Jifunze kuandika Kwa kuacha nafasi, kuzingatia aya, alama za nukta, koma na mshangao

Nasubir waumoderate nitarudi kusoma uzi wako
 
Back
Top Bottom