Ili tuendelee, tunahitaji Katiba Bora! Tuimarishe Uwazi, Uwajibikaji na Ushirikishwaji

Aug 31, 2010
9
13
Katiba Mpya yenye kuzingatia misingi ya demokrasia na yenye kukubalika na Watanzania wengi ni muhimu sana katika kuondoa umaskini, ujinga na maradhi. Upo uhusiano mkubwa sana kati ya Katiba bora na mafanikio katika vita ya kuondoa maadui hawa watatu ambao tumekuwa tukipambana nao toka tupate uhuru mwaka 1961.

Swali muhimu la kujiuliza: Hivi kuna uhusiano gani kati ya Katiba bora kwa upande mmoja na maisha yenye ustawi kwa upande mwingine? Ni maoni yangu kuwa upo uhusiano mkubwa sana kama ambavyo nitaeleza.

Katiba ni Sheria Mama. Sheria zote za nchi zinatokana na Katiba. Na pale inapotokea kuwa, sheria au kanuni zinapingana na Katiba, basi sheria hiyo au kanuni hiyo huwa ni batili. Hivyo basi, Katiba ni utaratibu ambao unatakiwa kuongoza maisha yetu yote kwa ujumla wake.

Jamii yoyote haiwezi kuendeshwa bila kuwa na utaratibu ambao mmejiwekea ili muweze kuendesha mambo yenu kwa amani na ustaarabu. Utaratibu huu ni Katiba. Pale inapotokea kuna mitazamo tofauti, basi rejea yetu ni Katiba. Na swali tunalojiuliza, ni : Je Katiba katika hili inasemaje? Kwa maneno mafupi sana, Katiba ndio mfumo mzima wa maisha yetu yote.

Ili tuweze kuondoa umaskini tunahitaji nini? Tunahitaji mambo mengi. Hayati Baba wa Taifa alisema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Tunaweza vipi kuyapata haya tukiwa na Katiba ambayo si bora na haikubaliki na wengi? Katiba ambayo ina mapungufu na ilitungwa katika zama ambazo changamoto zake ni tofauti na sasa ? Katiba ambayo ambayo ni mhimili mmoja tu ndio wenye nguvu na huru!

Tunahitaji tuwe na Katiba bora. Katiba bora ambayo itatupa Uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika ili tuweze kupata viongozi wenye maadili, viongozi bora, waliochaguliwa kihalali, wenye uwezo wa kuongoza na waadilifu. Viongozi hawa kwa kuwa wana sifa hizo, wataweza kubuni na kusimamia sera nzuri za kuondoa umaskini, watabuni mipango na mikakati ya kuongeza kipato cha wananchi maskini na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kama vile elimu bora, afya bora, maji safi na salama, miundombinu na nishati ya uhakika.

Hili haliwezi kupatikana bila ya kuwa na viongozi waadilifu, shupavu, wenye uwezo na wabunifu. Viongozi hawa watapatikana tu kwa kuwepo kwa Katiba bora ambayo itahakikisha kuwa Taifa letu linapata viongozi bora kwa njia za haki na si kwa kutumia rushwa, vitisho, uongo, ghilba na hila nyingine.

Katiba ninayoizungumzia, itaweka maadili ya viongozi na uwajibikaji. Maadili ya uongozi na uwajibikaji utaimarisha sana vita yetu dhidi ya umaskini. Hakutakuwa na nafasi ya uzembe, ubinafsi, ufisadi mambo ambayo huongeza umaskini kwa wananchi.

Ili tuweze kupata viongozi waadilifu, tunahitahitaji kuwa na taasisi zenye nguvu, huru, uwezo na zenye raslimali za kutosha. Taasisi hizi ndio zina majukumu ya kusimamia masuala mbalimbali katika Taifa letu, likiwemo jukumu muhimu sana la kutupatia Uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika. Uchaguzi wenye thamani, ambao utawapa sababu za msingi wapiga kura kuacha shughuli zao na kushiriki kikamilifu na kupiga kura kwa uelewa bila vitisho wala hila.

Uchaguzi huu unahitaji Taasisi imara, madhubuti, zenye kukubalika na wadau wote, huru na zenye uwezo wa kiutendaji na rasilimali. Bila kuwa na Katiba bora hatuwezi kujenga Taasisi zenye sifa hizi. Ndio maana, haikuwa jambo la ajabu kwa nchi mbalimbali duniani kukubaliana kuwa moja ya Malengo Endelevu ya Maendeleo ni lengo la kumi na sita (16) ambalo ni ‘Amani, Haki na Taasisi Imara’ (Peace, Justice, and Strong Institutions).

Katiba bora itatupa taasisi imara. Tasisi imara zitasimamia raslimali zetu vizuri ili ziwanufaisha wananchi maskini, lakini pia zitatupa viongozi wanaotokana na maamuzi ya wananchi, viongozi bora waadilifu na wanaowajibika. Viongozi wanaowajibika, hawatatumia nafasi zao kujinufaisha wenyewe, la hasha! bali watawajibika kwa wananchi, watawatumikia wananchi.

Wataingia mikataba na makampuni na mataifa mengine kwa kutazama maslahi ya wananchi, bungeni watatumia muda wao kujadili masuala ya msingi yenye maslahi mapana kwa taifa, watasimamia miradi ya maendeleo, watahakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, watafanya tafakuri ya kina ili kubaini chanzo cha matatizo ya wananchi na kuyatafutia majawabu. Matokeo yake, tutaona miradi, mathalani: ya maji safi na salama ikiboreka na kuongezeka, madarasa yenye viwango yakijengwa, hospitali na zahati zenye viwango zikijengwa, miundo mbinu bora ikikamilika.

Aidha, tutaona sera na mipango mizuri na bora ya kuboresha huduma za elimu na afya. Elimu bora ndio silaha muhimu sana katika kuondoa umaskini. Umaskini utapungua kwa kuwasomesha watoto wetu na hasa watoto wa kike. Haya yote yatawezekana iwapo tutaweza kuwa na viongozi bora, siasa na sera bora na matumizi sahihi na bora ya raslimali zetu.

Hili litawezekana kwa kuwa na viongozi makini na bora ambao wataonyesha njia ya kule tunakotaka kufika. Viongozi hawa watatokana na taasisi imara. Haya yote hatuwezi kuyapata bila kuwa na Katiba bora na inayokubalika na wengi. Katiba itakayoimarisha kuongeza uwajibikaji, uwazi, ushirikishwa na itakayotupa maadili ya uongozi na kuchungana kati ya mihimili mikuu mitatu. Hizi ni nyezo muhimu sana katika vita ya kuondoa umaskini. Tutaweza vipi kujenga uchumi bila kuimarisha uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji na maadili ya uongozi? Wakati ni sasa tuboreshe Katiba yetu ili tuondoe umaskini!
 
Katiba Mpya yenye kuzingatia misingi ya demokrasia na yenye kukubalika na Watanzania wengi ni muhimu sana katika kuondoa umaskini, ujinga na maradhi. Upo uhusiano mkubwa sana kati ya Katiba bora na mafanikio katika vita ya kuondoa maadui hawa watatu ambao tumekuwa tukipambana nao toka tupate uhuru mwaka 1961.
.Tutaweza vipi kujenga uchumi bila kuimarisha uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji na maadili ya uongozi? Wakati ni sasa tuboreshe Katiba yetu ili tuondoe umaskini!
Naunga mkono hoja, Ila wale maadui watatu wa tangu uhuru, adui ujinga, umasikini na maradhi, sasa wameongezeka watatu wengine, rushwa, ufisadi na ubadhirifu.

P
 
Back
Top Bottom