Hotuba ya Paul Makonda kwa Madereva; Awasaidia madereva kujiunga na Chama Cha Wafanyakazi

lumumba the son

JF-Expert Member
Jun 16, 2011
207
60
MKUTANO WA VIONGOZI WA MADEREVA NA WAANDISHI WA HABARI
TAREHE: 26. 6. 2015
MAHALI: ROMBO GREEN VIEW


1.0 UTANGULIZI
Naamini sisi sote tuliopo hapa na watanzania kwa ujumla tunakumbuka kuwa mnamo tarehe 4 mwezi wa tano mwaka huu madereva wote nchini, tuliingia kwenye mgomo mkubwa wa kitaifa uliohusisha madereva wa vyombo mbalimbali vya usafiri na hivyo kufanya shughuli nzima za usafirishaji kuwa ngumu kwa kipindi cha siku za mgomo. Ukweli ni kwamba, tulifanya mgomo huu huku tukitambua wazi juu ya athari zake, lakini bado tulichukua maamuzi haya kwasababu ya ukubwa na msongamano wa matatizo ya madereva ambayo kwa muda mrefu yamekuwepo bila kutatuliwa na hivyo kuanza kuzaa matatizo makubwa zaidi ambayo si tu yaliishia kuwaumiza madereva bali jamii ya watanzania kwa ujumla wake.

2.0 MATATIZO YA MSINGI
2.1 Wingi wa siku na saa za kazi.

Kimsingi madereva hawana idadi kamili ya siku wala saa za kufanya kazi, mara zote madereva wamekuwa wakifanyishwa kazi saa nyingi sana ambazo hazizingatii uwezo wa binadamu wa kawaida kumudu kiwango cha saa hizo za kufanya kazi kabla ya kuchoka na ufanisi wake kupungua. Kimsingi, jambo hili haliwagusi madereva peke yao bali pia wananchi wanaotumia vyombo vyetu vya usafiri, kwani ajali nyingi tu zimekuwa zikitokea kwasababu dereva anaendesha gari akiwa amechoka na hivyo kujikuta akisinzia.

2.2 Kutozingatiwa kwa afya za madereva

Katika moja ya swala ambalo lilipelekea mgomo ni wamiliki wa vyombo vya usafiri kutojihusisha kabisa katika suala la afya za madereva, hivyo ilikuwa ikitokea dereva yeyote akiumwa ilikuwa ni juu yake kuhangaika apate fedha, suala ambalo lilikuwa likiwagharimu madereva wengi na hata kupelekea wengine kushindwa kabisa kupata matibabu na hasa ukizingatia kuwa, madereva hawana bima ya afya kama ilivyo kwa waajiriwa wengine kwenye sekta binafsi na serikalini.

2.3 Kutohusika kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kwenye misiba ya madereva

Ukweli ni kwamba ilikuwa hata dereva akifariki achilia mbali akifiwa, wamiliki wa vyombo vya usafiri ama waajiri wao walikuwa hawajihusishi kabisa katika kutoa msaada wa aina yoyote ile, kuna wakati ilifikia hata ajali ya chombo cha usafiri imejitokeza, mmiliki husika wa chombo cha usafiri akifika kwenye eneo la tukio anafanya kazi ya kutoa tu chombo chake bila kujishughulisha kabisa na taratibu za mazishi ya dereva wake na wafanyakazi wengine wa chombo chake wanaokuwa wamepoteza maisha.

2.4 Kukosekana kwa utaratibu rasmi wa kulipa mishahara.

Utaratibu wa kulipa mishahara kwa muda mrefu umekuwa wa kiholela na wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekulipa wakilipa mishahara kwa namna wanavyojisikia bila kuzingatia muda wa malipo, utaratibu wa malipo hayo huku wengine wakienda mbali zaidi kwani, kuna miezi ambayo baadhi ya wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wamekuwa wakiamua tu kukaa kimya bila kuwalipa kabisa madereva wao.

2.5 Ukosefu wa Bima

Mpaka leo hii hakuna dereva mwenye bima ya aina yoyote ile, hata bima ya afya ambayo tunaamini kila mtu anajua ukubwa wa umuhimu wake kwa kila mmoja wetu. Na kila mnaposikia ajali imetokea basi ni kawaida kushuhudia abiria na wamiliki wa magari wakilipwa na makampuni ya bima lakini kwa madereva imekuwa tofauti kabisa, huwa tunaondoka tu na majeraha yetu bila kuzingatiwa na yeyote yule.

Kimsingi ni kwamba, mchanganyiko ama mlundikano wa matatizo haya ndio uliotufanya madereva wa nchi nzima kusimamia uamuzi wakugoma ambao ulilenga kuishinikiza serikali kuwalazimisha wamiliki wa vyombo vva usafiri kutoa haki za msingi kwa madereva na kuendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria hasa zile zinazotoa maelekezo juu ya kazi na ajira.

Sasa kabla sijaeleza mwisho wa safari yetu ya maridhiano umekuwaje, kwanza tuwakumbushe tena kuhusu mwanzo wa safari hiyo iliyoanza tarehe

5 mwezi wa tano mwaka huu, ambayo ilikuwa ni siku ya pili ya mgomo wetu, ambapo Mh. Paul Makonda, mkuu wa wilaya ya Kinondoni alikuwa kiongozi wa kwanza wa serikali kufika Ubungo kutusikiliza kwa umakini ambapo pamoja na mengineyo alibaini kuwa madai yetu yalikuwa ni ya msingi na kutamka mwenyewe kuwa, hayawagusi madereva tu bali wananchi kwa ujumla. Na jambo hili likamfanya asaini mkataba na madereva, mkataba uliosema ya kwamba, kama matatizo yetu hayatofanyiwa kazi basi angegeuka kuwa kiongozi wa mgomo wetu hadi madai hayo yatakaposhughulikiwa.

Na tuseme tu kuwa kwa namna ya kipekee sana tunamshukuru kwa ujasiri wake, ambao haukuishia kwenye kumaliza mgomo na kusababisha magari yarudi barabarani, bali alikwenda mbali zaidi kwa kuunganisha uozngozi mzima wa madereva na ofisi ya waziri mkuu na mawaziri wa wizara ya mambo ya ndani, wizara ya uchukuzi na ya fedha kupitia naibu waziri wake. Na kwasababu hizi uongozi wa madereva uliamua kumuandikia barua Mh. Paul Makonda ya kumuomba kuwa mlezi wa umoja wa madereva Tanzania na msimamizi wa haki za madereva kwenye kamati ya kudumu ya madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri, ambayo imeweza kufanya mambo yafuatayo kama sehemu ya harakati zake za kutafuta majawabu ya kudumu ya mgogoro uliojitokeza.

3.0 MUAFAKA
3.1 Kutolewa kwa mikataba ya ajira kwa madereva.

Kupitia kamati ya kudumu ya madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri iliyoundwa na waziri mkuu ambaye Mh. Paul Makonda alitukutanisha nae, tumeweza kuafikiana na wamiliki wa magari juu ya kutengenezwa kwa mikataba bora ya madereva inayozingatia haki zote za msingi za madereva, ikiwemo, saa za kazi kutozidi nane na ikitokea, basi mmiliki wa chombo cha usafiri analazimika kumuongezea dereva saa nyingine tatu tu za kazi ambazo zitakuwa na malipo ya ziada yaani "overtime", mikataba ya ajira kuwa ya kudumu ili pia ajira za madereva ziweze kulindwa kisheria na sio mmiliki wa chombo cha usafiri kuwa na uwezo wa kumfukuza kazi dereva wakati wowote na kwa namna anavyojisikia, wamiliki wa vyombo vya usafiri kulazimishwa na mikataba katika kuhusika kwenye kushughulikia za misiba ya madereva pindi ikitokea, madereva kulipwa posho kwa pesa za kigeni (USD) pindi wanapovuka mipaka kwenda nje ya nchi wakiwa kwenye shughuli za udereva, kupatiwa bima muhimu hasa bima ya afya na siku za kufanya kazi kwa wiki zibaki kuwa sita.


3.2 Kupatikana kwa usajili wa chama cha Madereva Tanzania

Kwa ushirikiano wa karibu sana na mlezi wetu Mh. Paul Makonda tumeweza kufanikiwa, kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Tanzania tokea uhuru wake kusajili chama cha madereva wote Tanzania kinachojulikana kama Tanzania Drivers Workers Union (TADWU) ambacho pamoja na majukumu mengineyo kitakuwa kikifanya kazi ya kudumu ya kutetea haki za msingi za madereva wote nchini kuanzia wa bodaboda mpaka wa magari makubwa. Kimsingi, mipango ya mbeleni ya chama hiki ni kufungua matawi nchi nzima sambamba na kusajili wanachama pamoja na kumiliki miradi mbalimbali mahususi kwa ajili ya kuwakwamua madereva wenyewe.

4.0 Hitimisho

Shukrani za kipekee zimwendee Mh. Gaudensia Kabaka, waziri wa kazi na ajira, Mh. Samwel Sitta, waziri wa uchukuzi na mlezi wetu Mh. Paul Maonda kwa hekima zilizotumika kutushauri na kutufikisha hapa. Ombi letu kubwa ni kwamba, kamati ya kudumu iliyoundwa na waziri mkuu iendelee kushughulikia kwa nguvu zote changamoto zote za msingi zinazowahusu madereva na sekta ya usafirishaji kwa upana wake.

11539631_1604618346459345_8100162936545697513_n.jpg
 
Back
Top Bottom