Hotuba ya Msemaji wa kambi ya Upinzani, Wizara ya katiba na Sheria 2015/2016

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2015/2016


(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
Kwa vile huu ni Mkutano wa Ishirini na wa mwisho katika maisha ya Bunge hili la Kumi, hii ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kwenye masuala ya Katiba na Sheria. Ni matumaini yangu kwamba katika miaka hii mitano, nimelitendea haki Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla kwa kutoa Maoni yaliyojengwa kwenye msingi imara wa utafiti.

Katika maisha yake, Mwenyekiti Mao alipendelea kusema ‘no investigation, no right to speak', yaani, ‘bila utafiti, hakuna haki ya kuzungumza.' Katika miaka hii mitano ya maisha ya Bunge lako tukufu, nilitofautiana na Serikali hii ya CCM na Mawaziri wake watatu wa Katiba na Sheria na Wanasheria Wakuu wa Serikali wawili karibu kwa kila jambo lililoletwa mbele ya Bunge lako tukufu kwa mjadala. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, sidhani kama yupo mmoja kati ya Mawaziri na Wanasheria Wakuu hao anayeweza kusema, kwa haki kabisa, kwamba msimamo wangu haukuwa based on solid research and factual data. Sina shaka kwamba watakaoandika historia ya Bunge la Tanzania ya kipindi hiki wataona tofauti kati ya Msemaji huyu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Wasemaji waliomtangulia.

Mheshimiwa Spika,
Kwa vile hii ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kwa Wizara hii, naomba nichukue fursa hii kufanya mambo mawili. Jambo la kwanza, kwa kupitia Wenyeviti wa Vijiji arobaini na saba kati ya hamsini wa Jimbo la Singida Mashariki ambao leo hii wako ndani ya Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu, niwashukuru wapiga kura na wananchi wangu kwa moyo wangu wote kwa kunipa heshima kubwa ya kuwatumikia wao na Watanzania wengine katika Bunge lako tukufu.

Kwa sababu ya heshima hii kubwa waliyonipatia, miaka hii mitano imekuwa ni miaka yenye maana kubwa sana katika maisha yangu binafsi na, ninaamini, katika maisha ya wapiga kura na wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki. Kwa kiasi kikubwa, tumekuwa huru. Hii, kwa maoni yangu binafsi, ndio tafsiri sahihi ya ushindi mkubwa tulioupata katika Uchaguzi wa Vijiji na Vitongoji wa Desemba ya mwaka ambako tuliiachia CCM Wenyeviti wa Vijiji vitatu tu! Kabla ya Uchaguzi huo, CCM ilikuwa na Wenyeviti wa Vijiji arobaini na tano na sisi wa UKAWA tulikuwa na Wenyeviti wa Vijiji watano. Sasa tunawasubiri mahasimu wetu hawa mwezi Oktoba ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika,
Jambo la pili ni hoja iliyopo mezani. Kwa vile hotuba hii inahitimisha kazi yangu ya miaka mitano kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu katika Wizara hii, naomba kwa ruhusa yako nifanye rejea ya masuala muhimu ya kikatiba na kisheria ambayo tumeyazungumzia katika kipindi hiki. Kwa maneno mengine, Mheshimiwa Spika, Maoni haya ni post mortem ya Serikali hii ya CCM katika masuala ya katiba na sheria katika mitano ya maisha ya Bunge la Kumi. Kwa sababu za wazi kabisa, napendekeza kuanza na mchakato wa Katiba Mpya.

KATIBA MPYA IMEKWAMA!!!


Mheshimiwa Spika,
Tarehe 31 Disemba, 2010, Rais wa nchi yetu, Mheshimiwa Profesa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete alilihutubia Taifa na kuwaahidi Watanzania kwamba itakapofika tarehe 26 Aprili, 2014 – wakati wa Golden Jubilee ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – nchi yetu itapata Katiba Mpya. Miezi miwili na nusu baadae, yaani tarehe 11 Machi 2011, Serikali hii ya CCM ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Gazeti la Serikali. Tarehe 18 Novemba ya mwaka huo, Muswada huo ulipitishwa na Bunge lako tukufu na kuwa Sheria, ambayo ndio iliweka msingi wa kisheria wa kutekeleza ahadi ya Rais Profesa Dokta Kikwete kwa Watanzania.

Siku hiyo ya tarehe 18 Novemba, 2011, nilisema yafuatayo mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya uliokuwa unaanza rasmi: "Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana." Kwa ushahidi wa miaka minne iliyofuatia, ni wazi kwamba ushauri wetu juu ya haja ya kutafuta muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya ulipuuzwa. Na hukumu ya historia imekuja haraka kuliko pengine tulivyotarajia, lakini imekuwa kali kama tulivyoitabiri.

Mheshimiwa Spika,
Golden Jubilee ya Muungano wetu, yaani tarehe 26 Aprili, 2014, ilipita bila ya nchi yetu kuwa na Katiba Mpya iliyoahidiwa na Profesa Dokta Kikwete. Baadaye tarehe 2 Oktoba ya mwaka huo, ‘Bunge Maalum' lenye wajumbe wa chama cha waliohusika na EPA, Richmond/Dowans, Tegeta Escrow, Operesheni Tokomeza Wafugaji na Operesheni Kimbunga dhidi ya Watanzania waishio mipakani, kilipitisha Katiba Inayopendekezwa, baada ya kura iliyopigwa na wafu waliokuwa wametangulia mbele ya haki, mahujaji waliokuwa wanampiga shetani mawe katika Mlima Ararat, Makka nchini Saudi Arabia, wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini India na wajumbe wengine wasiojulikana kwa majina wala walikokuwa wakati wa kura hiyo!

Na baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa katika sherehe iliyofanyika hapa Dodoma na kususiwa na viongozi wote wa taasisi kubwa za kidini hapa nchini, yaani Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Masheikh na Maimam wa taasisi mbali mbali za Kiislamu, pamoja na vyama vyote vikuu vya kisiasa nchini (UKAWA) na mashirika ya kiraia na wawakilishi wa ofisi za kibalozi zilizopo Tanzania, Rais Profesa Dokta Kikwete aliwaahidi Watanzania – kwa mara nyingine tena – kwamba Katiba Inayopendekezwa na chama chake itapigiwa kura ya maoni mnamo tarehe 30 Aprili, 2015.

Ahadi hiyo ilirudiwa rudiwa na kila kiongozi wa CCM na Serikali yake ndani na nje ya Bunge hili tukufu. Hata hivyo, tarehe 30 Aprili ilipita na kura ya maoni iliyoahidiwa na Profesa Dokta Kikwete haikufanyika. Leo ni wiki ya tatu tangu tarehe ya kura ya maoni ipite bila kura hiyo kufanyika na watu wale wale wa chama kile kile kwa maneno yale yale wanatuahidi kwamba kura ya maoni itafanyika katika tarehe ambayo hawaitaji.

Mheshimiwa Spika,
Wahenga wetu walisema ‘wajinga ndio waliwao.' Kwa sababu hiyo, Mtanzania yeyote atakayeamini ahadi hewa za watu hawa na chama chao asije akashangaa wala kulalamika atakapoliwa tena. Kwa kifupi, Mheshimiwa Spika, hakuna uhakika wowote kwamba kutakuwa na kura ya maoni ili kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa na CCM. Badala yake, uhakika pekee tulio nao ni kuwa Rais Profesa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete ataondoka madarakani bila Katiba Mpya aliyowaahidi Watanzania takriban miaka mitano iliyopita. Ndio kusema kwamba, kwenye signature issue ya utawala wake, yaani Katiba Mpya, huyu ni Rais aliyeshindwa. Hii ni Serikali iliyoshindwa. Na kwa vile imekuwa fashionable kwa upande wa pili kusema kwamba sisi wa UKAWA ‘tuliweka mpika kwapani na kuondoka uwanjani', wale waliobaki uwanjani peke yao, yaani CCM na washirika wao, CCM ni chama kilichoshindwa. Tunaomba kufafanua zaidi.

Katika Taarifa yake mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria wiki chache zilizopita, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria alizungumzia ‘Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba' kwa aya tatu tu, kati ya aya hamsini na mbili za Taarifa yake! Mheshimiwa Waziri alisema yafuatayo kuhusu Katiba Inayopendekezwa: "... [N]i matumaini yangu kuwa wananchi watatumia muda uliopo kwa kuisoma na kuielewa Katiba Inayopendekezwa na hatimaye kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kushiriki katika kura ya maoni kuhusu Katiba hiyo."1 Swali analotakiwa Mheshimiwa Waziri kulijibu ni lini kura hiyo ya maoni itafanyika na kwa Sheria ipi?

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, hata kama Tume ya Uchaguzi itakamilisha jukumu lake la kuandikisha wapiga kura nchi nzima, bado hakuna – na hakutakuwa na - uhakika wa kufanyika kwa kura ya maoni kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa. Tatizo la msingi hapa ni matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni, 2013.2 Sheria hiyo imeweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa kura ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani kuahirishwa wala kuongezewa muda.

Kwa mfano, ndani ya siku kumi na nne tangu tarehe ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, Rais anatakiwa – kwa Amri iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali na baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar – kuielekeza Tume ya Uchaguzi kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa.3 Amri ya kura ya maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura hiyo ya maoni inatakiwa kufanyika.4 Rais Kikwete alikwishatoa Amri kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kura ya Maoni.

Rais hana mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria hii, wa kutengua Amri yake au kutoa Amri mpya ili kuwezesha kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine tofauti na tarehe iliyotangazwa kwenye Amri ya kwanza.

Pili, ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, Tume inatakiwa kuandaa swali la kura ya maoni na kulichapisha katika Gazeti la Serikali.5 Na ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapisha swali hilo, Tume inatakiwa kutoa Taarifa ya kufanyika kwa kura ya maoni, itakayoeleza kipindi cha kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya kura hiyo na siku ya kura ya maoni.6 Na kila msimamizi wa kura ya maoni anatakiwa, ndani ya siku ishirini na moja baada ya kuchapishwa kwa Taarifa ya Tume, kuwajulisha wananchi katika Jimbo lake la Uchaguzi kuhusu utaratibu wa kufanyika kwa kura ya maoni.7 Aidha, Tume inatakiwa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa muda wa siku sitini tangu Katiba Inayopendekezwa ilipochapishwa.

Tume ilikwishaandaa na kuchapisha swali la kura ya maoni na ilikwishatoa Taarifa ya kura ya maoni na ratiba yake nzima. Tume haina mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, ya kutengua Taarifa yake na kutoa Taarifa nyingine, au kuweka ratiba nyingine badala ya ratiba iliyokwishatolewa. Vile vile, Tume haiwezi kujiongezea muda wa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa; au kujipa muda mwingine kwa vile muda uliowekwa na Sheria haukutumika ipasavyo. Kwa upande wao, wasimamizi wa kura ya maoni hawana mamlaka yoyote kisheria ya kuongeza au kuongezewa muda wa kutoa taarifa kwa umma chini ya kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Kura ya Maoni.

Mheshimiwa Spika,
Tume ya Uchaguzi haina mamlaka yoyote kisheria kuongeza muda kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuendesha elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa baada ya muda wa awali uliowekwa kwa ajili hiyo kupita.9 Kwa kifupi, Mheshimiwa Spika, hakuna uwezekano kisheria wa kurudia tena hatua zozote muhimu ambazo zilikwishachukuliwa kwa ajili ya kufanyika kwa kura ya maoni iliyokuwa imepangwa tarehe 30 Aprili, 2015. Hakuna uwezekano kisheria wa kuongeza muda kwa hatua zozote ambazo muda wake ulikwishapita. Kwa sababu hizi, hakuna uwezekano wa kufanyika kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni kama ilivyo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika,
Tume ya Uchaguzi yenyewe imeshatangaza kwa maandishi kwamba kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa katika mazingira ya sasa ya kisheria. Katika Randama ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2015/16, Tume imesema kwamba "Sheria ya Kura ya Maoni ina maeneo ambayo hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja. Eneo ambalo linaweza kuleta utata ni uhesabuji wa kura ya maoni na utangazaji wa matokeo."10 Tume inasema kwamba ‘Suluhisho la Changamoto' hiyo ni "Sheria ya Kura ya Maoni ifanyiwe marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya moja."11

Hadi sasa, Serikali hii ya CCM haijaleta Muswada wowote wa marekebisho ya Sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni siku za usoni. Kama ilivyokuwa kwa ahadi ya kupata Katiba Mpya ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014; kama ilivyokuwa kwa ahadi hewa ya kufanyika kwa kura ya maoni ya tarehe 30 Aprili, 2015, Serikali hii ya CCM inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na kura ya maoni katika mazingira ya sasa ya kisheria. Kwa sababu hiyo, huyu ni Waziri aliyeshindwa!

FEDHA ZA MAHAKAMA NA UHURU WA MAHAKAMA

Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yangu ya juu ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/12 nililiambia Bunge lako tukufu kwamba "... tatizo kubwa linalozikabili mahakama zetu sio uhaba wa uwezo wa kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili yao, bali ni uhaba wa fedha zenyewe! Pili, tatizo la uhaba wa fedha ... linasababishwa ... na ukosefu wa uelewa wa mahitaji halisi ya Mahakama. Tatu, tatizo la ukosefu wa uelewa wa mahitaji halisi ya Mahakama ... linasababishwa na ukosefu wa watu wanaoelewa mahitaji hayo serikalini au ukosefu wa wafanya maamuzi ya migawanyo ya fedha wanaofahamu mahitaji halisi ya Mahakama."

Mwaka huo huo wa 2011, wakati nawasilisha Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama, nilirudia tena hoja hiyo kwa kusema kwamba moja ya matatizo makubwa yanayokabili mahakama zetu nchini ni "... vipaumbele vyake kutozingatiwa katika migawanyo ya bajeti za Serikali za kila mwaka." Mwaka uliofuata nilirejea hoja hiyo kwa mara nyingine tena: "... [T]ishio kubwa kuliko mengine yote kwa uhuru wa Mahakama za Tanzania ... sio tu kuingiliwa na wanasiasa na watendaji wakuu wa Serikali. Tishio kubwa zaidi ni lile la Serikali kutumia udhibiti wake wa hazina ya taifa kuinyima Mahakama rasilmali za kuiwezesha kutimiza wajibu wake kikatiba."

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu haikuchoka kuzungumzia matatizo ya kibajeti ya Mahakama ya Tanzania. Mwaka 2013/14 nilisema, kwenye Maoni ya Kambi, kwamba "... Mahakama ya Tanzania imeshindwa kutekeleza wajibu wake huu wa kikatiba kwa sababu ya kunyimwa fedha na vitendea kazi vingine na Serikali hii hii inayodai kwamba dira yake ni ‘haki kwa wote na kwa wakati'!" Niliyarudia maneno haya verbatim katika Maoni yetu ya mwaka jana.

Nilipendekeza, katika Maoni hayo ya mwaka jana – kama nilivyopendekeza katika mjadala wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama miaka mitatu kabla - kwamba "... badala ya Mahakama kutegemea ukomo wa bajeti unaowekwa na Hazina, sheria ielekeze – kama ilivyo kwa Bunge na vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni na nchi jirani ya Kenya - kwamba bajeti ya Mahakama ya kila mwaka isiwe pungufu ya asilimia 3 ya bajeti ya kila mwaka ya Serikali ili kuiwezesha Mahakama kuwa na uhakika wa fedha zake na kuiwezesha kupanga mipango yake kwa uhakika zaidi." Pendekezo langu lilitokana na ukweli kwamba "utaratibu wa sasa wa kutegemea mgawo wa Hazina hauwezi kutatua matatizo ya fedha ya Mahakama ya Tanzania."

Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano ya maisha ya Bunge lako tukufu, Serikali hii ya CCM haijawahi kuipatia Mahakama ya Tanzania fedha za kukidhi mahitaji yake kwa mujibu wa vipaumbele vyake. Ukweli ni kwamba Serikali hii ya CCM haijawahi kukana jambo hili. Wimbo wake ni ule ule wa miaka yote: ‘ufinyu wa bajeti.' Hivyo, kwa mfano, kwenye Taarifa yake ya mwaka huu Waziri amesema kwamba kumekuwepo na changamoto zifuatazo katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2014/2015: "Upungufu wa watumishi; ufinyu wa bajeti na fedha kutokutolewa kwa wakati; na uhaba wa majengo na vitendea kazi."12

Mheshimiwa Spika,
Katika Maelezo ya Wizara yake kuhusu utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2013/14, Waziri huyu huyu alilalamikia "‘bajeti finyu isiyokidhi majukumu ya Mahakama'", na '"fedha kutokutolewa kadiri ya mpango wa kazi ... wa mwaka na kwa wakati."' Aidha, Waziri alilalamikia '"upungufu wa vitendea kazi kama vile magari, kompyuta, uduni wa mazingira ya kazi na nyumba za kuishi watumishi hususani majaji, mahakimu na watumishi wengine wa umma."' Vile vile, Waziri alikiri mwaka jana, '"hali ya majengo ya Mahakama haijaridhisha kiasi cha kutosheleza mahitaji (kwani) kiasi cha fedha za maendeleo kinachotolewa na Serikali ni kidogo sana ukilinganisha na idadi na hali halisi ya majengo ya Mahakama hapa nchini."'

Mheshimiwa Spika,
Hali ilikuwa hiyo hiyo katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2012/2013. Katika mwaka huo, mtangulizi wa Mheshimiwa Waziri wa sasa, yaani Mheshimiwa Mathew Chikawe, alilalama kwamba: "... Wizara yangu bado inakabiliwa na changamoto nyingi katika vyombo vyake vya utoaji haki nchini (ikiwa) ... ni pamoja na uwezo mdogo wa Serikali kifedha na rasilimali watu katika vyombo vyake vya utoaji haki kwa wananchi wake na kusababisha kuendelea kuwepo kwa mlundikano wa mashauri ya jinai na madai kwa kiwango kikubwa...."

Aidha, Mh. Chikawe alikiri kwamba licha ya idadi ya watumishi wa kada mbali mbali wa Mahakama kuongezeka, "... bado uwezo wa Serikali kifedha ni mdogo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika utoaji wa haki hapa nchini. Pia Wizara yangu ina upungufu wa nyenzo za kufanyia kazi kama magari, ofisi, samani, na nyumba za watumishi. Changamoto hizi zinaathiri utekelezaji wa azma ya Serikali ya upatikanaji wa haki kwa wote mapema na kupunguza tija ya Taasisi mbali mbali zilizoko chini ya Wizara." Malalamiko ya mtangulizi wa mtangulizi wa Mheshimiwa Dkt. Migiro, yaani Mheshimiwa Celina Kombani, kuhusu ‘ufinyu wa bajeti' nayo yako on official record ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Athari za Serikali hii ya CCM kushindwa kutoa fedha kwa mujibu wa mahitaji na vipaumbele vya Mahakama ya Tanzania zimekuwa nyingi, kubwa na zimezungumzwa katika miaka yote mitano ya maisha ya Bunge lako tukufu. Kwa mfano, kwa sababu ya kutopatiwa fedha za kukidhi mahitaji halisi ya utoaji wa haki, Mahakama ya Tanzania imeshindwa kabisa kutatua tatizo la mlundikano mkubwa wa kesi na mashauri katika ngazi zote za Mahakama. Kwa sababu hiyo hiyo, '"uhaba wa watumishi wenye sifa zinazotakiwa bado unaendelea kuwa tatizo. Maslahi yasiyokidhi hali ya utendaji katika Mahakama inapelekea baadhi ya watumishi kuacha kazi."'

Mheshimiwa Spika,
Aidha, Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imeendelea kufedheheka kwa kuwa mdeni mkubwa na sugu wa majaji na watumishi wengine wa Mahakama, watoa huduma, wenye nyumba za kupangisha majaji, wajenzi na wazabuni mbali mbali. Kama Jaji Mkuu Mstaafu Augustino S.L. Ramadhani alivyowahi kusema juu ya madeni ya majaji: '"Ni vigumu sana kwa Jaji anayeishi katika nyumba inayodaiwa kodi kuweza kusikiliza na kutoa hukumu katika kesi za mwenye na mpangaji au kesi yoyote ya uvunjwaji mkataba. Lazima Jaji atoe boriti kwenye jicho lake ili aweze kutoa (sic!) kibanzi kwenye jicho la mwingine."'

Haya yanatokea Bunge lako tukufu lilikwishatunga Sheria ya Malipo na Mafao ya Majaji (Judges (Remuneration and Terminal Benefits) Act) ya mwaka 2007. Sheria hiyo inaweka masharti kwamba majaji wanastahili kulipiwa – nje ya mishahara yao – nyumba yenye samani ya Daraja A; gharama za matibabu kwa ajili yao wenyewe na familia zao; gari ya Serikali pamoja na dereva. Tumewahi kusema siku za nyuma kwamba "fedheha hizi kwa majaji wetu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania zinaonyesha sio tu ukiukwaji makusudi wa sheria tajwa bali zinathibitisha jinsi gani ambavyo mfumo wa utoaji haki na uhuru wa Mahakama haujawa kipaumbele cha Serikali hii ya CCM."
Mheshimiwa Spika,

Mheshimiwa Spika,
Hali ya miundombinu ya mahakama zetu imekuwa mbaya na ya kusikitisha katika miaka hii mitano ya maisha ya Bunge lako tukufu. Randama ya Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/16, Fungu 40, Mfuko wa Mahakama, inataja mojawapo ya ‘changamoto' za Mahakama ya Tanzania kuwa ni "hali mbaya ya miundombinu ya Mahakama kutokana na uchakavu na uhaba wa majengo ya Mahakama."13

Na kama ambavyo tumewahi kusema siku za nyuma, katika kipindi cha zaidi ya nusu karne ya uhuru wetu, "Kanda nane kati ya kumi na tatu za Mahakama Kuu ya Tanzania zimeendelea kutumia majengo yaliyorithiwa kutoka dola ya kikoloni. Kanda nne kati ya tano zilizobaki na Divisheni tatu za Mahakama Kuu, yaani Divisheni ya Biashara, ya Kazi na ya Ardhi zinatumia majengo yaliyoazimwa au kuchukuliwa kutoka taasisi nyingine za umma! Ni Kanda moja tu ya Mahakama Kuu ya Tanzania – Kanda ya Bukoba – ambayo imejengewa jengo jipya ya Mahakama katika kipindi cha miaka hamsini ya utaifa wetu. Na hata hilo moja halijakamilika hadi leo!"

Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania haijawahi kuwa na jengo lake yenyewe tangu kuanzishwa kwake mwaka 1979 na kwa miaka kumi iliyopita, imekuwa mpangaji wa iliyokuwa Hoteli ya Forodhani. Sasa, yapata miaka thelathini na sita tangu Mahakama ya Rufani kuanzishwa, Randama inasema kwamba "zoezi la kusafisha kiwanja ... katika Mtaa wa Chimala limekamilika. Kazi ya uchambuzi wa kumpata Mshauri elekezi ... zimekamilika na Mshauri kapatikana. Mkataba wa mshauri elekezi umesainiwa na mshauri ameanza kazi na kuwasilisha inception report kwa majadiliano.

Mheshimiwa Spika,
Tangu tupate uhuru mwaka 1961, Mikoa ya Kigoma, Mara, Singida, Lindi, Morogoro, Manyara, Geita, Njombe na Simiyu haijawahi kuwa na Masjala za Mahakama Kuu. Sasa, kwa mujibu wa Randama ya Fungu 40, "Mshauri elekezi ... amekamilisha na kuwasilisha rasimu michoro ya Architectural Drawings, makisio cost estimates." Aidha, tunaambiwa kwamba "michoro ya mwisho (detailed architectural, structural and service drawings) inakamilishwa sambamba na kuandaa makisio (cost estimates) na rasimu ya makabrasha ya zabuni (tender documents)." Kwa rekodi ya Serikali hii ya CCM, tutasubiri kwa nusu karne nyingine wakati mchakato wa ujenzi wa majengo hayo unaendelea! Kwa kifupi, sera za utoaji haki za Serikali hii ya CCM hazijawahi kutekelezeka na hazitekelezeki.

HALI YA HAKI ZA BINADAMU


Mheshimiwa Spika,
Sehemu hii ya Maoni imechukuliwa, kwa kiasi kikubwa, kutoka katika Maoni yetu ya mwaka jana. Sababu ya kufanya hivyo ni moja tu: tuliyoyasema mwaka jana yameendelea kufanyika katika mwaka huu wa fedha. Ukweli ni kwamba kuna kila dalili za kuonyesha kwamba tuliyoyapigia kelele mwaka, badala ya kupungua, yameongezeka. Kwa kifupi, hali ya haki za binadamu katika miaka mitano ya maisha ya Bunge lako tukufu inatisha na imezidi kuwa mbaya. Mauaji na mashambulio dhidi ya viongozi wa kidini na waumini wao na sehemu zao za ibada yaliyotokea kati ya mwaka 2012 na 2013 hayajatatuliwa hadi leo. Hakuna mtu yeyote ambaye ameadhibiwa kwa mauaji ya padre mmoja wa Kanisa Katoliki Zanzibar. Hakuna aliyeadhibiwa kwa shambulio la risasi na la tindikali dhidi ya mapadre wengine wawili wa Kanisa hilo huko huko Zanzibar wala kwa shambulio la tindikali dhidi ya Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar.

Hakuna aliyetiwa hatiani wala kuadhibiwa kwa kuhusika na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki Olasiti Arusha lililoua watu watatu na kujeruhi wengine wengi. Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni juu ya wahusika wa mauaji na mashambulio hayo na sababu zake. Mauaji na mashambulio ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine kama madaktari yaliyotokea kati ya 2012 na 2013 hayajatatuliwa pia. Maafisa wa Jeshi la Polisi walioamuru mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi hawajachukuliwa hatua yoyote. Badala yake, aliyekuwa kamanda wa polisi hao amepandishwa vyeo na kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Huu ni ushahidi wa wazi kabisa kwamba mauaji hayo yalipangwa na/au yalifanywa kwa maelekezo ya Serikali hii ya CCM.

Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na wa Jeshi la Polisi waliohusika kumteka nyara na kumtesa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka hawajakamatwa hadi leo licha ya majina yao kujulikana. Raia wa Kenya aliyebambikiziwa kesi ya kumteka Dk. Ulimboka amekwishaachiliwa huru na mahakama. Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni kuhusu jambo hili. Huu ni ushahidi wa kuhusika kwa Serikali hii ya CCM katika shambulio hilo.

Hakuna aliyekamatwa wala kuadhibiwa kwa kumteka nyara na kumtesa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda. Serikali hii ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni kuhusu shambulio hilo linalofanana na shambulio dhidi ya Dk. Ulimboka. Serikali hii ya CCM ina wajibu kisheria na kisiasa wa kulinda maisha ya Watanzania na mali zao. Imeshindwa kutekeleza wajibu huo kwa Watanzania.

DEMOKRASIA KITANZINI!

Serikali hii ya CCM imeitia demokrasia kitanzini na inatishia kuinyonga na kuiua. Mikutano halali ya vyama vya siasa vya upinzani imeshambuliwa kwa mabomu na risasi za moto na Jeshi la Polisi. Watu wengi wameuawa katika mashambulizi hayo. Wengine wengi wamejeruhiwa. Viongozi, wanachama na hata wapita njia tu wamepigwa, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa kushiriki mikutano halali ya vyama vya siasa vya upinzani.

Tunavyozungumza ni jana Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa taarifa rasmi kwamba Jeshi la Polisi lilikiuka haki za binadamu na sheria za nchi yetu wakati wa kuwakamata viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) mnamo tarehe 27 Januari, 2015. Na jana hiyo hiyo, Jeshi la Polisi limeripotiwa kuua raia mmoja na kujeruhi mwingine baada ya kudaiwa kukutwa wakinywa pombe baada ya saa nne usiku Mjini Njombe. Matokeo ya mauaji hayo, siku nzima ya jana Mji wa Njombe umefuka kwa moshi wa mabomu ya machozi na kurindima kwa milio ya risasi baada ya wananchi wa Njombe kupinga mauaji hayo kwa maandamano.

Wakati sisi wa UKAWA ndani ya Bunge lako tukufu tulipolazimisha mjadala wa dharura kuhusu vitendo viovu dhidi ya viongozi na wanachama wa CUF tarehe 28 Januari, wapo Wabunge – wa CCM pekee – waliojaribu kuutetea au kuukosha udhalimu huu wa Jeshi la Polisi. Sasa Tume ya Haki za Binadamu - iliyoteuliwa na Rais na Mwenyekiti wao, Profesa Dakta Jakaya Kikwete – imewaumbua. Sasa na wajitokeze hadharani na kulitetea Jeshi la Polisi kwa ujasiri ule ule waliouonyesha tarehe 28 Januari.

Mheshimiwa Spika,
Sio viongozi na wanachama wa CUF peke yao ambao wamepata chungu ya ‘element za kifashisti' katika Jeshi la Polisi. Kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na viongozi na makada wa CCM, Jeshi hilo limewabambikizia viongozi na wanachama wa CHADEMA kesi za uongo za ugaidi. Wengi wameteswa kwa ukatili mkubwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa katika vituo vya polisi katika kesi hizi. Hadi sasa Serikali hii ya CCM haijasema chochote juu ya kufutwa kwa kesi za uongo za ugaidi walizofunguliwa viongozi na wanchama wa CHADEMA kama vile Wilfred Lwakatare na Henry Kilewo. Walioshiriki kutunga mashtaka hayo ya kidhalimu hawajachukuliwa hatua yoyote.

Kwa miaka mingi, sisi wa UKAWA tumelalamika kwamba Jeshi la Polisi linatumiwa na CCM kukandamiza wapinzani wa kisiasa wa chama hicho kichovu. Ushahidi ni mwingi. Mwenyekiti wa CCM, Profesa Dakta Kikwete mwenyewe, aliwaambia wanaCCM wenzake wafanye kazi ya siasa badala ya kutegemea nguvu za Jeshi la Polisi. Tume ya Haki za Binadamu, katika uchunguzi wake wa mauaji ya mwandishi habari Daudi Mwangosi, ililishauri Jeshi la Polisi "... waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo ... CCM walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar...."

Mheshimiwa Spika,
Licha ya Tume ya Haki za Binadamu kusisitiza katika Taarifa yake juu ya mauaji ya marehemu Mwangosi kwamba "demokrasia ya mfumo wa vyama vingi iheshimiwe na kulindwa", Jeshi la Polisi limebaki kiziwi. Halisikii. Jeshi la Polisi limeendelea kutumia visingizio vile vile dhaifu vya miaka yote, yaani kile kinachoitwa ‘taarifa za kiintelijensia', kujaribu kuhalalisha vitendo vyake vya kihalifu dhidi ya haki za binadamu. Hivi, kwa mfano, ndivyo Naibu Kamishna wa Polisi S.N. Sirro wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam alivyojaribu kuhalalisha kuzuia mkutano na maandamano halali ya CUF tarehe 28 Januari ya mwaka huu: "Kutokana na taarifa za kiintelijensia zilizopo maandamano hayo/mkutano huo kama utafanyika kuna kila dalili za kuwepo vurugu na hatimaye uvunjifu wa amani."

Uongo kama huu uliofichuliwa jana na Tume ya Haki za Binadamu umerudiwa wiki iliyopita na Jeshi la Polisi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida. Tarehe 14 Mei, 2014, CHADEMA Wilaya ya Iramba ilitoa taarifa ya mikutano ya hadhara katika maeneo kadhaa ya Wilaya hiyo kwa lengo la ‘ujenzi wa Chama.'14 Siku iliyofuata, yaani tarehe 15 Mei, Mkuu wa Polisi Wilaya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Juma W. Majula, aliijulisha CHADEMA Wilaya kwamba ‘taarifa (yao) imepokelewa kwa ‘masharti' kwamba wazingatie tarehe, muda na maeneo ya mikutano yao; "... wajiepushe na kutoa maneno ya uongo na kukashifu vyama vingine", na kuzingatia Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa.15

SSP Majula aliwaonya CHADEMA Wilaya ya Iramba kwamba: "Kinyume na kuendana na matakwa haya, mikutano yenu itasitishwa mara moja na wakati wowote." OCD Majula alinakili barua yake kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Iramba na Mkuu wa Usalama wa Taifa Wilaya ya Iramba ‘kwa taarifa tafadhali.' Aidha, Wakuu wa Vituo vya Polisi vya Kiomboi, Shelui, Kinampanda na Ndago walipewa maelekezo ya kusimamia usalama kwenye mikutano hiyo na "hakikisheni Sheria za Nchi hazivunjwi na atakaevunja Sheria achukuliwe hatua za kisheria mara moja."

Hata hivyo, kabla ya kufanyika mkutano hata mmoja na bila sheria yoyote kuvunjwa na CHADEMA au na mtu mwingine yeyote, kesho yake – tarehe 16 Mei, 2015 – SSP Majula aligeuka ghafla. Kwa maneno yake: "Ninakujulisha kwamba kutokana na taarifa za kiintelijensia mkutano wa Kiomboi Stand hautakuwa salama. Hivyo ni rai yangu kuwa mkutano huo usitishwe ili kuwaweka wananchi salama ambao ndio tunategemea kuwaongoza. Hii ni kutokana na dhana iliyozoeleka kuwa machafuko yanapotokea wanaoathirika ni wananchi wa kawaida wa hali ya chini nasi viongozi tunabaki salama."

Pengine bila kujua, SSP Majula alitoa sababu halisi za kuzuia mikutano ya CHADEMA wilayani Iramba: "... Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Iramba ameamuru kusitishwa kwa mikutano yote ya Vyama vya Siasa hapa wilayani ... kwa sababu za kiusalama." Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, ni Mkuu wa Wilaya. Kwa sasa, nafasi hiyo katika Wilaya ya Iramba inashikiliwa na Bi. Lucy Mayenga, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha CCM ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imepigia kelele mara nyingi nafasi ya Wakuu wa Wilaya kama Mheshimiwa Mayenga katika mfumo wa ulinzi na usalama wa nchi yetu. Kwa mfano, katika Maoni yetu ya mwaka 2012/13, tuliliambia Bunge lako tukufu kwamba "... wengi wa Wakuu wa ... Wilaya wa Tanzania ya leo ni makada wa CCM. Mamlaka ya watu hawa hayatokani na wananchi kwani hawachaguliwi na mtu yeyote; na, kwa sababu hizo hizo, hawawajibiki kwa wananchi kwa utekelezaji wa kazi na majukumu yao.... Kwa vyovyote vile, lengo la uteuzi wa Wakuu hawa wa Wilaya ni kudhibiti wananchi – na katika zama hizi za vyama vingi vya siasa, vyama vya upinzani - kwa manufaa ya CCM."

Katika Maoni yetu hayo, tulithibitisha – kwa kutumia Katiba ya CCM yenyewe – kwamba Wakuu wa Wilaya ni makada wa CCM: "Wakuu wa ... Wilaya wote ni, na wanatakiwa kuwa, wanachama wa CCM. Hii ni kwa sababu, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM katika ngazi ya Wilaya. Kwa mfano, kwa mujibu wa Katiba ya CCM ..., Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ...; ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ...; na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya...."

Na kama utakumbuka, Mheshimiwa Spika, tulihoji kama Wabunge wote walioteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa au Wilaya kama Mheshimiwa Mayenga bado wana sifa za kuendelea kuwa Wabunge, kwa vile ibara ya 67(2)(g) ya Katiba inamwondolea mtu sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge '"... ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano...."'

Kwa vyovyote vile, Mheshimiwa Spika, vitendo vya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na maandamano halali ya vyama vya siasa kwa visingizio finyu na vya kijinga kama taarifa za kiintelijensia' havikubaliki tena. Vyama vya siasa vilivyopata usajili wa kudumu vina haki, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni zake, ya kufanya mikutano na maandamano.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kama Idara ya Usalama wa Taifa, vimepewa wajibu na Sheria hiyo wa kutoa ulinzi katika mikutano na maandamano ya vyama vya siasa. Hivi ndivyo inavyofanyika katika mikutano yote ya CCM na kwenye ziara za viongozi wake mbali mbali; na ndivyo inavyopaswa kuwa kwa vyama vingine vyote. Aidha, Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kama Mheshimiwa Mayenga, hana mamlaka yoyote kisheria kukataza au kupiga marufuku mkutano wowote wa hadhara au maandamano ya vyama vya siasa.

Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu itashangaa sana endapo, baada ya vitendo vyake vya uvunjaji wa sheria, Mheshimiwa Mayenga ataendelea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba au Wilaya nyingine yoyote katika nchi yetu. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itamshangaa sana Inspekta Jenerali wa Polisi endapo SSP Majula ataendelea kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Iramba au wilaya nyingine yoyote ya Tanzania, baada ya kuruhusu mamlaka yake kisheria kupokwa na Mkuu wa Wilaya Mayenga kwa namna tuliyoielezea hapa.

MATUMIZI HARAMU YA NGUVU ZA KIJESHI!

Mheshimiwa Spika,
Sehemu hii pia imechukuliwa, kwa sababu zile zile, kutoka kwenye Maoni yetu ya mwaka jana. "Serikali ya CCM imewageuka Watanzania walioipigia kura na kuwaua, kuwatesa na kuwatia vilema vya maisha, kuwabaka, kuwafukuza kwenye maeneo yao na kuwafanya wakimbizi wa ndani au internally displaced persons (IDPs). Badala ya kulinda mali zao, Serikali ya CCM imekuwa mwizi wa mali za wananchi. Serikali ya CCM imeendesha Operesheni Kimbunga kwa kisingizio cha kuondoa wahamiaji haramu nchini. Matokeo ya Operesheni hiyo ni kwamba maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wa mikoa ya Kagera na Kigoma – inayopakana na Burundi na Rwanda – walikamatwa, kuteswa na kuporwa mifugo, fedha na mali zao nyingine na makazi yao kuharibiwa.

"Utaratibu wa kisheria wa kuwakamata watuhumiwa, kuwapeleka mahakamani, kuwapata na hatia na kuwaadhibu kwa mujibu wa sheria umepuuzwa. Cha kushangaza Operesheni Kimbunga haikuihusu mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mara, Mbeya, Mtwara, Rukwa na Ruvuma ambayo inapakana na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Msumbiji na Zambia ambayo nayo pengine ina wahamiaji haramu. Katika mazingira haya, ni sahihi kuamini kwamba Operesheni Kimbunga ilikuwa ni lengo la kuwaadhibu watu wenye asili ya Rwanda kwa sababu ya mgogoro wa kidiplomasia kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

"Hata kabla vumbi lililotimuliwa na Operesheni Kimbunga halijatulia, Serikali ya CCM ilianzisha vita nyingine kubwa dhidi ya Watanzania. Hii ni Operesheni Tokomeza Ujangili. Licha ya jina lake, Operesheni hiyo imetokomeza maisha ya Watanzania wasiokuwa na hatia yoyote. Makumi ya watu wameuawa, mamia wamejeruhiwa, maelfu wamekamatwa na kuteswa, vijiji vizima vimechomwa moto na makazi ya wananchi kuharibiwa, mifugo imeuawa ama kuporwa kwa mtutu wa bunduki, mashamba na mazao yameharibiwa na maelfu ya wananchi wametiwa umaskini mkubwa na Serikali hii ya CCM.

"Hatimaye, baada ya kelele kubwa ndani na nje ya Bunge, Operesheni Tokomeza ilisitishwa na Mawaziri wa Ulinzi, Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii na Mifugo wakaondoshwa madarakani kwa sababu ya Operesheni hiyo. Walioua, kutesa na kulemaza Watanzania na kuwaibia au kuharibu mali zao hawajakamatwa wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.

"Operesheni Kimbunga na Tokomeza zilikuwa Operesheni za Kijeshi. Zilianzishwa, kuongozwa na kutekelezwa na maafisa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vikosi vingine vya ulinzi na usalama. Operesheni hizi za kijeshi zimefanyika wakati Tanzania haiko vitani na wala haiko katika hali ya vita. Rais Kikwete hakutangaza vita wala kuwepo kwa hali ya vita kwa mujibu wa Katiba ili kuweza kuamuru kutekelezwa kwa Operesheni hizi za kijeshi.

"Hakukuwa na maasi au vurugu zozote zozote za kijamii. Kwa sababu hiyo, hakuna Mkuu wa Mkoa yeyote aliyeomba msaada wa kijeshi ili kuwezesha matumizi ya Majeshi ya Ulinzi katika kusaidia mamlaka za kiraia kama inavyotakiwa na Sheria ya Ulinzi wa Taifa, 1970 na Kanuni zake. Kwa kila namna inavyoonekana, Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza zilikuwa ni matumizi haramu ya nguvu za kijeshi dhidi ya raia.

TUME YA UCHUNGUZI YA JAJI MSUMI

"... Tume ya Uchunguzi iliyoahidiwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchunguza masuala yanayohusu ukiukwaji huu wa haki za binadamu imeundwa Rais kupitia Tangazo la Serikali Na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014. Tume hiyo inaongozwa na Jaji Kiongozi mstaafu Hamisi Amir Msumi na Makamishna wenzake Majaji wastaafu Stephen Ihema na Vincent Kitubio Damian Lyimo.

"... Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu na kutambua utumishi uliotukuka wa Jaji Kiongozi Msumi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani kabisa na uteuzi wa Makamishna Ihema na Lyimo. Itakumbukwa kwamba tarehe 13 Julai, 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu "... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi' ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya Majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni."

"Ushahidi tuliowasilisha mbele ya Kamati ya Haki, Madaraka na Maadili ya Bunge baada ya Msemaji wa Kambi kushtakiwa kwenye Kamati hiyo kwa kile kilichoitwa ‘kuwadhalilisha' majaji uliwahusisha Majaji wastaafu Ihema na Lyimo katika kundi la Majaji ambao uteuzi wao tuliupigia kelele. Sehemu ya ushahidi huo inaonyesha kwamba tarehe 16 Juni 2003, aliyekuwa Mwenyekiti CCM wa Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute alimwandikia Rais Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ‘kwa uzembe na kukosa maadili.

' Mzee Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia' uamuzi kwa zaidi ya miaka minne hadi aliponyang'anywa faili la kesi hiyo na kukabidhiwa Jaji mwingine aliyeandika uamuzi huo ndani ya wiki tatu! Mwezi mmoja kabla ya barua ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu Barnabas Samatta kulalamikia ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao walidai: "Hadhi na heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi ya miaka mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi ya pingamizi."

"... Sio tu kwamba Jaji mstaafu Ihema ana rekodi mbaya ya kijaji, bali pia ana rekodi ya kutumiwa na Serikali hii ya CCM kuisafisha Serikali kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na watendaji wa Serikali. Mwaka 2012, mara baada ya Jeshi la Polisi mkoani Iringa kumuua marehemu Daudi Mwangosi, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi alimteua Jaji Ihema kuongoza Kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi kuchunguza mauaji hayo.

"Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati ya Jaji Ihema ni mfano wa namna ya kuisafisha Serikali kutoka kwenye lawama ya mauaji ya raia wake. Taarifa hiyo ilitofautiana kimsingi na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo, iliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; na Ripoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa, iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

"Kwa upande wake, Jaji Lyimo aliteuliwa tarehe 28 Machi 2007, mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika tarehe 26 Oktoba, 2007 Katibu Mkuu Kiongozi wa wakati huo Phillemon Luhanjo alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete "... ameamua kusogeza mbele muda wa kustaafu wa Mhe. Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo ... kwa miaka mitatu ... kuanzia tarehe 28 Machi 2008, siku ambayo angestaafu kwa lazima."

"Uteuzi wa Majaji hawa na wengineo wenye sifa kama hizo ulilalamikiwa mno na majaji wengine kiasi kwamba ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu' chini ya Ofisi ya Rais, kilihitimisha, katika Taarifa yake tarehe 7 Machi 2008, "inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri wa kustaafu ni kinyume cha Katiba."

"Sasa Majaji hawa ndiyo wamepewa jukumu la kuchunguza matukio ya ukiukwaji haki za binadamu ambayo hayana mfano katika historia ya Tanzania tangu uhuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani yoyote na uteuzi wa Majaji Ihema na Lyimo na inapendekeza uteuzi wao ufutwe na majaji wenye sifa bora zaidi wateuliwe kwa ajili ya kazi hii muhimu. Vinginevyo matokeo ya Tume ya Msumi hayatakubaliwa na umma wa Watanzania."

Mheshimiwa Spika,
Tuliyoyasema mwaka jana kuhusu Tume ya Jaji Msumi sasa yametimia. Licha ya Tume hiyo kukiri kwamba kulikuwa na mauaji, utesaji na vitendo vingine vya kinyama dhidi ya Watanzania wasiokuwa na hatia yoyote, Tume hiyo ‘imewasafisha' Mawaziri na ‘wakubwa' wengine waliowajibishwa na Bunge lako tukufu kwa kushindwa kusimamia idara au taasisi zao zilizohusika na mauaji na unyama huo.

Watanzania waliuawa na kuteswa na mali zao kuharibiwa au kutwaliwa kwa nguvu lakini hakuna mkosaji na hakuna atakayewajibika kwa mauaji hayo. Hapa ndipo CCM ilipoifikisha nchi yetu baada ya zaidi ya nusu karne ya utawala wake. Wakati umewadia wa kuondoka na utawala wa aina hii. UKAWA, kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, ndio tumaini pekee la Watanzania!!!

---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA



Bonyeza HAPA kusikili audio.
 

Attachments

  • 4_456663338345037831.doc
    112.5 KB · Views: 433
  • hotuba ya Lissu bungeni.mp3
    12.1 MB · Views: 986
"Wakati sisi wa UKAWA ndani ya Bunge lako tukufu tulipolazimisha mjadala wa dharura kuhusu vitendo viovu dhidi ya viongozi na wanachama wa CUF tarehe 28 Januari, wapo Wabunge – wa CCM pekee – waliojaribu kuutetea au kuukosha udhalimu huu wa Jeshi la Polisi. Sasa Tume ya Haki za Binadamu - iliyoteuliwa na Rais na Mwenyekiti wao, Profesa Dakta Jakaya Kikwete – imewaumbua. Sasa na wajitokeze hadharani na kulitetea Jeshi la Polisi kwa ujasiri ule ule waliouonyesha tarehe 28 Januari"-Lissu

Wabunge wa CCM hawana aibu na wala hawataomba radhi au kuyakana maneno yao......wananchi ndio tutawaadhibu.

 
Porojo ndeeeeefu, mbona kasahau kufanya "postmortem" ya alivyomshambulia Nyerere BMK?

Hapo sasa!
 
Ngoja waje wenye Chama Chao watakavyoiponda.Ila inatia hasira sana na uchungu mwingi..........
 
Dogo hilo?
Tundu Lisu anasema:
‘Bunge
Maalum’ lenye wajumbe wa
chama cha waliohusika na EPA,
Richmond/Dowans, Tegeta
Escrow, Operesheni Tokomeza
Wafugaji na Operesheni
Kimbunga dhidi ya Watanzania
waishio mipakani, kilipitisha
Katiba Inayopendekezwa
 
Lissu, Tanzanians are truly proud of you! You are a rare gem in this failed state!!!!
 
Tundu Lisu anasema:
‘Bunge
Maalum’ lenye wajumbe wa
chama cha waliohusika na EPA,
Richmond/Dowans, Tegeta
Escrow, Operesheni Tokomeza
Wafugaji na Operesheni
Kimbunga dhidi ya Watanzania
waishio mipakani, kilipitisha
Katiba Inayopendekezwa

Yaani kwenye hii hotuba lazima walisema pooooooooooooooo
 
figganigga

Hivi CCM huwa wanajisikiaje wakisoma HOJA NZITO kama hizi? Hasa katika dunia hii ambapo kila mtu can put two and two together!

I wish hotuba hizi ziwe zinaandikwa pia kwa kiingereza ile ziweze kusomwa na watu wengine pia. Mathalani Ban Ki Moon akisoma hii hotuba ya TL ataridhika kabisa kwamba alikuwa sahihi kabisa kumfukuza kazi Dr Asha Rose Migiro.

Kweli CCM is a mental disease! Kama mnafikiri mimi ninaongopa subiri majibu ya mtoa hoja Waziri wa Katiba na sheria uone kama atajibu POINT ZOTE 11 alizotoa TL kuhusu katiba pendekezwa.

The writting is already on the wall. Masaju CA jaribu kuokoa jahazi kama unaweza.
 
Last edited by a moderator:
Safi sana kamanda wetu Tundu lissu kipoko wakutetea raia katika haki zao za msingi,,,october tutakupa kuwa Mwanasheria mkuu wa serikali ndo title yako ipo loading, ,,,,,,,
 
Dogo sana hilo! Wala haliumizi kwani hakutukana ila aliweka ukweli hadharani! Mbona hujaongelea tofauti ya riport ya Ihema na ile ya tume ya haki za binadamu kuhusu Mwangosi

Ahsante Njaare, wewe una mtazamo kama mimi. Kutukanwa Nyerere na Tundu Lissu ni jambo dogo sana?

Sijuwi wengine wana panic nini?

Heko.
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom