Hotuba ya Msemaji Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje

Cicadulina

JF-Expert Member
Sep 8, 2015
961
2,345
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA MHESHIMIWA PETER SIMON MSIGWA (MB) KUHUSU BAJETI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2016)

UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika, hii ni hotuba yangu ya kwanza ya bajeti nikiwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Namshukuru Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Freeman Mbowe (Mbunge) kwa wajibu huu mzito alionipa wa kushughulikia masuala nyeti ya nchi katika viwango vya kimataifa. Ninaahidi kuipa serikali hii ushirikiano wenye tija katika kuijenga Tanzania mpya, yenye kuheshimika na yenye kunufaika vya kutosha na diplomasia ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namtukuza Mungu wangu asiyeshindwa kamwe. Ukuu wake umetuma ujumbe kwa wana -CCM ambao wallidhani sitarudi kwenye bunge hili la 11.Walitoa kebehi nyingi wakidhani nilikuja hapa kwa kubahatisha. Wengine walikwenda mbali zaidi wakidai kuwa isingekuwa makosa ya uteuzi wa ndani ya CCM nisingeshinda mwaka 2010. Leo hii ni dhahiri wanajionea Msigwa kuwepo Bungeni hapa ni mpango wa Mungu na sio jambo la kuigiza.

Mheshimiwa Spika, leo nasimama kwa jeuri ya Mungu nikiwashukuru sana watu wa Iringa Mjini kwa upendo wao mzito juu yangu. Mwenyezi Mungu kawatumia kuonyesha umma kuwa mbeba maono hafi mpaka mpango wa Mungu utimie.
Kwa sababu hiyo, Ushindi wa Iringa ni ujumbe tosha kwa kila mwanasiasa na kwa mtu yeyote anayekatishwa tamaa na kauli za watu; akumbuke kuwa “Your value does not decrease based someone’s inability to see your worth and potentials”

Mheshimiwa Spika, hii ndiyo Iringa ninayoijua Miye. Iringa ya watu wanaojitambua, jasiri na wenye rekodi ya kipekee ya kuiduwaza Dunia. Naam – Iringa - intellectuals’ habitat, center of education, the home of knowledge, the land of Mkwawa. Kama hukusoma Tosamaganga basi ulisoma Mkwawa High School, au ulisoma Lugalo, Ifunda, Malangali au Iringa girls. Najivunia kuwa Mbunge wa Iringa Mjini. Sitawaangusha.

Mheshimiwa Spika, nyuma ya mafanikio yangu kuna Kisa Msigwa - huyu ndiye mama mchungaji - malkia wangu wa nguvu, rafiki yangu, mke wangu na Mama wa watoto wangu. Tumepitia mengi magumu, namshukuru kwa thamani yake kuu kwangu na kwa watu wa Iringa Mjini.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee namshukuru Naibu Waziri Kivuli Mheshimiwa Riziki Shahali Mgwali kwa ushirikiano alioutoa katika kuhakikisha hotuba inasheheni mawazo mbadala na yenye kutoa dira na kulisaidia taifa.
Mheshimiwa Spika, leo tunajadili uhusiano wa kimataifa tukiwa katika zama mpya. Zile enzi za kupigania uhuru na ukombozi wa Bara la Afrika zilizoipa Tanzania hadhi na heshima kubwa kimataifa zimeshapita; na wala Tanzania yetu haiwezi tena kutegemea sifa hizo za kihistoria kujijenga kimataifa. Hizi ni zama mpya. Ni zama za kusaka maendeleo ya kiuchumi kwa diplomasia ya kiuchumi.

SERA YA MAMBO YA NJE NA DIPLOMASIA YA KIUCHUMI


Mheshimiwa Spika, ni miaka 15 sasa tangu serikali ianze kutekeleza sera mpya ya mambo nje ya mwaka 2001 inayolenga kusukuma mbele diplomasia ya uchumi. Mwanadiplomasia mahiri na Waziri wa Mambo ya Nje wa 38 wa Australia - Julie Bishop – katika moja ya hotuba zake anasema, nanukuu: “Just as traditional diplomacy aims for peace, so economic diplomacy aims for prosperity' – not just as an end in itself but also as a vital support for peace in the region and for global peace and security. In this regard effective economic diplomacy must translates into economic growth, job creation and new sources of investment to further build on the quality of life and standards of living that people enjoy”, mwisho wa kunukuu

Mheshimiwa Spika, kama anavyosema Mwanadiplomasia huyu mashuhuri “wakati diplomasia ya kizamani ililenga amani, diplomasia ya uchumi inalenga ustawi, kwa kukuza ustawi wa maisha ya watu diplomasia ya kiuchumi inakuwa ndiyo msingi muhimu wa kudumisha amani. Ikitekelezwa vizuri, diplomasia ya kiuchumi ni lazima ilete matokeo ya kukua kwa uchumi, kuongezeka kwa ajira na kufunguka kwa vyavyo vipya vya uwekezaji wa ndani na wa kimataifa kuchochea ubora wa maisha ya watu wa nchi husika”. Kinyume na hayo, diplomasia ya uchumi ya Tanzania itabaki kuwa ni neno la kuiga na kubandika tu (copy and paste) kutoka kwenye nchi zinazojua nini hasa maana ya diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, miaka 15 iliyotumika kutekeleza sera hii ni sawa na muda uliotumika kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs kutoka mwaka 2000 -2015). Pia miaka 15 ndio muda ambao unatumika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia, yaani ‘Sustainable Development Goals –SDGs - kutoka 2015-2030. Aidha, kwa miaka yote 15, Bunge hili lilishaidhinisha mabilioni ya shilingi kila mwaka kwaajili ya kutekeleza sera hiyo. Hakuna kisingizio cha muda tena, wala hakuna kisingizio cha pesa tena. Huu ni wakati wa serikali kutupa matokeo.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanataka kujua na Kambi ya Upinzani inataka kujua;
Ni mafanikio gani makubwa na ya maana ambayo Serikali ya CCM imeyaleta kwa kutekeleza sera ya diplomasia ya uchumi?
Je, ni ajira ngapi mpya zimetengenezwa kwa kutumia fursa za uwekezaji wa kimataifa, ikiwa hadi leo Watanzania wengi bado hawana ajira?
Sera hii imeongeza ubora gani kwenye maisha ya Watanzania, ikiwa watu wengi bado wapo kwenye umaskini uliopitiliza?

Na Wizara hii inapata wapi uhalali wa kuomba tena mabilioni mengine ya bajeti ikiwa kwa miaka 15 mfululizo imeshindwa kuleta mafanikio yanayoonekana na yanayoendana na uhalisia wa mabilioni yanayotengwa kila mwaka kwa ajili ya Wizara hii?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imebaini kuwa Serikali haiko serious katika kufukuzia fursa za kiuchumi na kusukuma maslahi ya nchi katika siasa za kimataifa. Diplomasia ya kiuchumi inataka utaalamu, inahitaji, viongozi wenye maono,wenye ushawishi, na mikakati madhubuti yaani nikimaanisha ( visionary leadership, strong negotiators, lobbyists, and smart strategies) ndipo nchi ipate mafanikio.Tanzania tumepungukiwa vyote hivyo. Nchi haina maono, haina mikakati na haina wataalam wa kutosha kusukuma sera hii. Nitoe mfano;

Mheshimiwa Spika, katika nchi yoyote ile Duniani, Mkuu wa nchi ndiye Mwanadiplomasia namba moja. Na ndiye anayepaswa kutoa dira na msukumo wa kutekeleza sera ya mambo ya nje kwa maslahi ya Taifa. Hakuna nchi inayojua kila kitu na hakuna Kiongozi anayejua kila kitu. Hii ni Dunia ya kutegemeana, hii ni Dunia ya kujifunza na kubadilishana mikakati na uzoefu wa kushughulikia maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hii, nchi yoyote ile Duniani inayoongozwa na Kiongozi local, asiye na interest na masuala ya kimataifa, anayekimbia Mabalozi wa nchi Rafiki, anayeogopa na asiyependa kushiriki mikutano muhimu ya kimataifa, asiyejua nini kinaendelea katika ajenda za kimataifa, na asiyependa kujifunza kutoka kwa viongozi wa mataifa mengine, basi nchi hiyo haiwezi kufanikiwa kamwe. Huwezi kuongoza nchi inayotafuta fursa za uchumi wa dunia, halafu unajifungia Ikulu. Maendeleo ya nchi hayawezi kuja tu kwa kutumbua majipu ya ndani, bali kwa kutekeleza mikakati makini ya kiuchumi ambayo kufanikiwa kwake kunahitaji kushirikiana na mataifa mengine.
Mheshimiwa Spika, serikali yetu haipo serious na diplomasia ya uchumi.

Ukitaka kuuthibitisha ukweli huu, tazama aina ya mabalozi wanaoteuliwa. Uchunguzi unaonyesha kuwa chini ya serikali hii ya CCM ubalozi hutolewa kama zawadi kwa makada waliosaidia kampeni; hutolewa kama pole kwa wanajeshi wastaafu wenye uswahiba wa karibu na CCM; na pia hutolewa kama adhabu kwa wanasiasa wanaoonekana kuwa tishio kwa vigogo wa CCM wakati wa kuwania nafasi mbalimbali, hasa zile za kiserikali. Ni nadra sana kukuta fulani kapewa ubalozi kwasababu ana sifa za msingi.

Mheshimiwa Spika, makada hawa wa CCM wasiokuwa na weledi kuhusu diplomasia ya uchumi, ndio wanaokabidhiwa dhamana ya kuhakikisha eti Tanzania inafanikiwa kimataifa. Kambi ya Upinzani inazitambua juhudi za Mhe. Rais Magufuli za kuwarudisha nyumbani baadhi ya mabalozi. Kwa dhamira njema kabisa tunaishauri Serikali kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kufanya kwanza performance appraisal ya mabalozi ili kuwabaini vizuri wale wasio na sifa. Mabalozi wasioendana na wakati tulionao, waondolewe katika nafasi hizo. Wengi wao wangeweza kuwa mabalozi wazuri sana wa nyumba kumi-kumi lakini sio kutuwakilisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mabalozi wana wajibu mkubwa katika kubaini fursa za kiuchumi zilizopo kwenye mataifa mengine na kuiongoza serikali katika kushawishi na kuzitumia fursa hizo. Katika zama hizi mpya, tunahitaji mabalozi wenye uwezo wa kijasusi wa kiuchumi (economic espionage), ili wawe na tija kwa taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua ni chombo gani hasa kinachotumika kama kiunganishi kati ya balozi zetu na wizara hii na hata wizara nyingine ili mabalozi hao waweze kujua na kujifunza mambo mengine mazuri yanayofanywa katika Wizara mbalimbali? Je, ni namna gani Wananchi wanaweza kupata ripoti za Balozi mbalimbali kwa njia rahisi ili wahamasike katika kutafuta fursa za kiuchumi katika nchi hizo zenye wawakilishi wetu?

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina uhaba mkubwa wa wataalam wa diplomasia ya uchumi. Randama ya Wizara inathibitisha ukweli huu. Wakati serikali inaanza kutekeleza sera hii mwaka 2001 ilikwishajua vizuri kuwa haina wanadiplomasia wa kutosha. Cha kusikitisha, iliichukua wizara hii miaka 12 ndipo ikaanza kutoa mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu (mwaka 2013) kwaajili ya kuzalisha economic diplomats. Matokeo yake, hadi kufikia mwezi Mei mwaka jana (2015) ni watumishi 32 tu ndio waliokuwa wamehitimu mafunzo ya muda mfupi ya diplomasia ya uchumi. Tuache mzaha, tuache ukada, tuliokoe taifa.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kufika kwa mwendo huu wa Konokono. Tunaposema CCM imeshindwa kuliongoza Taifa hili huwa tuna maana kuwa mambo madogo-madogo mnayoyafanya hayalingani hata kidogo na muda mwingi mnaotumia wala na fedha nyingi mnazotengewa. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge hili jinsi Serikali inavyojipanga kukabiliana na uhaba huu mkubwa wa wanadiplomasia na jitihada inazokusudia kuzichukua kumaliza tatizo hili kwa haraka.

UONEVU WA MAKAMPUNI YA KIMATAIFA.

Mheshimiwa Spika, ni jukumu la Wizara hii kuvutia wawekezaji. Lakini wizara haipaswi tu kuvutia wawekezaji, bali pia inapaswa kuhakikisha wawekezaji wanafanya shughuli zao katika namna isiyoathiri maslahi ya nchi na wananchi. Tathmini ya Kambi ya upinzani inaonyesha kuwepo kwa udhaifu mkubwa wa Wizara hii katika kutekeleza jukumu hili. Matokeo yake, makampuni ya kimataifa, hasa ya Madini, yamekuwa chanzo kikuu cha malalamiko na migogoro isiyokwisha miongoni kwa wananchi wetu na kuleta hali ya hofu, vifo, na kukata tamaa.

Mheshimiwa Spika, kuna mifano mingi ya aina hii ya migogoro na uonevu unaofanywa na makampuni makubwa ya nje (multinationals). Mfano ni migogoro isiyoisha katika migodi ya Nyamongo huko Tarime ambapo wananchi wamekuwa wakilalamika kudhulumiwa haki zao na kampuni ya Acacia Mining (Barrick Gold) huku wizara husika, ikiwamo wizara ya mambo ya nje ikifumbia macho mambo haya.

Mheshimiwa Spika, kampuni hii ya Acacia Mining (Barrick Gold) imeendeleza tabia yake ya kukandamiza haki za wazawa kwa kusaidiwa na baadhi ya maafisa wa serikali kukiuka taratibu na sheria za nchi yetu. Tunazo taarifa za kampuni ya Acacia kuidhulumu kampuni nyingine ya wazawa iitwayo Bismark Hotel Mining Ltd ya Mwanza, kwa kupora na kudhulumu kitalu cha kampuni hiyo kilichopo Mgusu Geita.

Mheshimiwa Spika, tabia hii ya Makampuni ya Nje kuyadhulumu Makampuni ya Wazawa bila Wizara kuingilia kati, ni hatari kwa maslahi ya wananchi wetu na ni hatari pita kwa uhusiano wetu na Mataifa ya Nje. Wizara ichukue hatua madhubuti za kutatua migogoro yote inayosababishwa na makampuni ya nje. Wizara ianze na migogoro ya kampuni ya Acacia Mining (Barrick Gold), ukiwemo huu wa kuidhulumu kitalu cha Kampuni ya Bismark Hotel Mining Ltd, kwani kuuacha ni kuruhusu Wazawa kudhalilishwa na Makampuni makubwa ya Nje.

MAHUSIANO YA KIMATAIFA

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni serikali imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na Mabalozi (NoteVerbale) kuelekeza kuwa kabla ya Mabalozi au Maofisa wa Ubalozi kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha serikali kupitia Wizara ya Mambo Nje.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu wa kuwataka mabalozi kuomba kibali serikalini unaminya uhuru wa mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali wa kimataifa kufanya kazi zao hapa nchini. Kimsingi, amri hiyo ya serikali inakiuka utamaduni uliokuwepo awali na inakiuka Masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kibalozi Duniani. Huu ni ushahidi mwingine kuwa serikali hii ya Awamu ya Tano imeamua kudhibiti uhuru wa habari nchini na imevuka mipaka kiasi cha kuingilia uhuru wa mabalozi na wanadiplomasia wanaofanya kazi zao hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Kimataifa wa Vienna unaoshughulika na masuala ya mahusiano ya kidiplomasia na kibalozi ya nchi mbalimbali Duniani, kwenye ibara yake ya 27 (1) inatoa masharti ya nchi inayopokea mabalozi kuwalinda na kuwapa uhuru wa mawasiliano yao yote na kutoyaingilia kwa namna yoyote ile. Katika Mkataba huo wa Vienna Ibara ya 41(1) inasema kuwa bila kuathiri masharti ya haki na kinga, Mabalozi wanajukumu la kuheshimu sheria na taratibu za nchi zinazo wapokea na wanatakiwa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi husika.

Mheshimiwa Spika, maneno haya bila kuathiri (without prejudice) katika uandishi wa Sheria yana maana kubwa sana, hii ni kwa sababu serikali imekuwa ikitumia ibara hii kuwabana mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini katika kutekeleza majukumu yao. Hii ina maana kuwa pamoja na Mabalozi kuwa na jukumu la kuheshimu sheria za nchi yetu bado jukumu hilo haliondoi uhalali au uwepo wa haki na kinga walizonazo – za kutoingiliwa - kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna.

Mheshimiwa Spika, neno “bila kuathiri” (without prejudice) kwa tafsiri ya Kingereza lina maana ya “without detriment to any existing right or claim” “without any loss or waiver of rights or priveleges”. Ni wazi kuwa serikali haitatumia kifungu hiki kama utetezi wa namna yoyote ile ya kuwabana Mabalozi kwa kutumia utaratibu wa sasa wa serikali
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuondoa utaratibu huu inaoutumia kwa sasa kwa sababu inaminya na kuua uhuru wa mawasiliano kwa Mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali waliopo nchini na hali hii inapelekea Taifa letu kuwa na sifa mbaya kwenye medani za kimataifa. Kambi ya Upinzani haioni msingi wowote wa kuwanyima mabalozi hawa waliotumwa na nchi zao kufanya mawasiliano halali na taasisi, vyama vya siasa au wadau wengine bila kuathiri sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inayoogopa mabalozi wa nchi za kigeni wasiwasiliane kwa uhuru na vyama vya siasa na taasisi nyingine hadi itoe kibali, ni serikali isiyojiamini. Mabalozi ni wawakilishi halali kwa mujibu wa sheria, na vyama vya siasa viko kihalali kwa mujibu wa sheria, hii hofu inatoka wapi? Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kutengua amri hiyo mara moja. Aidha, natoa wito kwa mabalozi wote nchini kuwa huru kuwasiliana na vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kwani wanalindwa na Mkataba wa Vienna ambao Tanzania imeuridhia. Watanzania tunaoheshimu diplomasia, haki na uhuru wa kuwasiliana tupo tayari kushirikiana kwa karibu na jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha serikali ya Tanzania inaheshimu Mkataba muhimu wa Vienna, ikiwa itaendeleza udikteta katika hili.

USALAMA WA WATANZANIA WANAOISHI NJE YA NCHI


Mheshimiwa Spika, Watanzania wanauwawa nchi za nje, Watanzania wanabaguliwa na kudhalilishwa huku serikali hii ya CCM ikikaa kimya bila kuchukua hatua zozote. Miongoni Watanzania waliouwawa kikatili hivi karibuni huko ughaibuni ni; marehemu Andrew Sanga maarufu kama “King Drew” aliyepigwa risasi - tena na mtu aliyefahamika - na baadaye kupoteza maisha baada ya kupata majeraha makubwa; marehemu Robert John Mpwata aliyeuawa kwa sumu nchini Ujerumani; marehemu Caroline Mmari aliyeuawa huko Los Angeles Marekani; marehemu Imran Mtui aliyeuawa huko India; marehemu Jerry Issack Mruma aliyeuawa huko Kenya; marehemu Method Clemence Mengi aliyeuawa kwa kuchomwa visu huko nchini Marekani pamoja na wengine wengi ambao sijawataja hapa.

Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote hao mahali pema peponi – Amina. Mbali na mauji hayo yuko binti wa Kitanzania aliyefanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwa kuvuliwa nguo zake na kisha kutembezwa uchi mitaani. Serikali isiyopaza sauti kulaani mauaji ya raia wake na inayoshindwa kulinda uhai wa raia wake, ni serikali inayopoteza uhalali wa kuongoza. Jukumu la kwanza na la msingi la serikali yoyote ile duniani ni kulinda uhai wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitegemea serikali ikemee vikali kitendo cha serikali iliyohusika ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahusika.Je, kuna uhalali gani wa mabalozi wetu kuwa katika nchi hizo endapo wanashindwa kuchukua hatua kali dhidi ya nchi zinazohusika kwa kuwa zimeshindwa kutoa ulinzi kwa watu wetu ?Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliambia bunge lako ni nini inategemea kufanya endapo tabia hizi zinazokiuka haki za binadamu zinaendelea kufanywa dhidi ya wananchi wetu?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya sababu na mazingira yaliyosababisha kushamiri kwa mauaji ya Watanzania katika miezi na miaka ya hivi karibuni. Aidha, kwa kuzingatia matokeo ya ripoti hiyo, Bunge lako lijadili na kushauri hatua za kuchukuliwa na serikali na balozi zetu ili kuepusha mauaji ya raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walisaini Azimio la Kutetea na Kulinda Haki za Binadamu; na kwa mauaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaowadhuru Watanzania hufanyika kwenye miongoni mwa nchi rafiki zilizoridhia Azimio hilo; Kambi ya Upinzani inashauri pia serikali yetu ivunje ukimya, ipaze sauti kuzitaka nchi husika ziongeze juhudi za kulinda usalama wa raia wa Tanzania na wa nchi nyingine dhidi ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

KANZI DATA (DATABASE) YA WATANZANIA WAISHIO NJE YA NCHI

Mheshimiwa Spika, Dunia sasa inatambua mchango mkubwa wa uchangiaji uchumi unaofanywa na watu mbalimbali wanaoishi nje ya nchi zao (yaani Diaspora).Hatuna budi kama Watanzania kuendelea kutambua na kuthamini mchango huu mkubwa unaofanywa na kaka na dada zetu wanaoishi nje ya nchi kwani uwepo wao huko unachangia kukuza jina la nchi yetu na kuboresha mahusiano na nchi hizo.

Mheshimiwa Spika, hakuna takwimu za kitaifa zinazoonyesha idadi kamili ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi na taarifa za kile wanachokifanya huko. Umuhimu wa kuwa na taarifa ni kubaini kwa wepesi idadi na aina ya watu wenye ujuzi na uzoefu ambao serikali inaweza kuutumia kwa maslahi ya nchi.Aidha, kujua idadi ya wananchi walio nje ya nchi kutapelekea kutengeneza milango ya kiuchumi kati yao na nchi (economic gateway),kutafungua fursa za kibiashara ikiwa ni pamoja na soko la nje (export market) kwa bidhaa zetu za Kitanzania na hivyo kutaachia fursa kwa soko la ndani kuboresha bidhaa zao ili ziweze kupata masoko nje.
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa database hiyo , Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuhakikisha kuwa jambo hili la kutengeneza database linazingatiwa kwa uzito wake kwa kuwa lina manufaa kwa wananchi wetu walio katika kila pembe ya dunia na pia manufaa kwa ya uchumi wa nchi yetu.

URASIMISHAJI WA FEDHA KWA WATANZANIA WANAOISHI NJE (FORMALIZATION OF DIASPORA REMITTANCES)

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanaoishi nje wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kuchangia uchumi wa nchi hii japo serikali imekuwa haiwapi ushirikiano wa kutosha. Hii ni kwasababu serikali kuwa imejitenga na watu wake wanaoishi nje ya nchi, basi hata michango inayoingia nchini imekuwa ni kidogo tofauti na matakwa au matamanio ya ndugu zetu hao.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo linashangaza sana. Mtanzania anapotaka kutuma kiasi chochote cha pesa kwenda nje ya nchi imekuwa ni rahisi sana, lakini anapotaka kuingiza fedha ndani ya nchi kutoka nje inakuwa ni vigumu sana kwasababu kuna urasimu mkubwa na wenye kukatisha tamaa. Yote hii ni kwasababu serikali haijajiwekea utaratibu wa kuwasaidia Watanzania kutafuta mbinu za kuingiza fedha nchini. Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali ya CCM ijifunze kutoka kwa majirani zetu Somalia, Ethiopia, Kenya na Rwanda wanavyofanya.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 mwezi Novemba serikali ya Kenya ilizindua taasisi inayotoa elimu kuhusu masuala ya remittances chini ya Tume ya Umoja wa Afrika (African Union Commission).Taasisi hiyo inayojulikana kama African Institute for Remittances (AIR) ilizinduliwa ili kutoa fursa kwa Wakenya wengi kujifunza masuala ya remittances na kuona ni kwa namna gani nchi hiyo itanufaika zaidi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014/2015 Benki ya Taifa ya Ethiopia (National Bank of Ethiopia) ilikusanya remittances kutoka $1.5 bilioni mpaka dola $bilioni 2 kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee fedha zilizochangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa uchumi wa nchi hiyo. Ni vyema sasa na sisi Tanzania tuanze kubuni mbinu za kunufaika na michango hii, kwa faida ya uchumi wa nchi yetu na kuwakwamua Watanzania wengi katika umaskini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutambua, kuthamini na kuheshimu michango ya wananchi wanaoishi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na shughuli zote za kimaendeleo wanazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu. Hivyo basi, pamoja na yale yote yaliyopendekezwa na Kambi hii katika kipindi chote cha Bunge la Kumi kuhusu remittances, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri yafuatayo:

Serikali iagize Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutengeneza kitengo maalumu chenye mfumo wa ufuatiliaji wa fedha yaani (tracking system), zinazoingizwa nchini kwa njia mbalimbali kutoka kwa Watanzania waishio nje ya nchi ili kuweza kujua mchango wao kwa Taifa. Hii pia itasaidia kutambua fedha zinazoingia nchini kwa njia ya utakatishwaji, au kufadhili vikundi yovyote haramu ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa Taifa letu
Serikali ije na muswada wa kutengeneza Sera ya Taifa ya Diaspora (National Diaspora Policy).Sera hii iwe mahususi kwa ajili ya kushughulikia maswala ya Wananchi wetu wanaoishi nje ya nchi, kama nchi jirani ya Kenya ilivyotengeneza sera ya namna hii ili kulinda maslahi ya wananchi wake wanaoishi nje ya Kenya (National Diaspora Policy of Kenya).

Vilevile, serikali ije na muswada wa kuwa na sera ya uwekezji wa Diaspora (Diaspora Investment Policy) ili kuweza kuwasaidia Wananchi wetu walio nje ya nchi kuweza kusaidiwa na serikali katika kutafuta maeneo ya uwekezaji, kutoa fursa za uwekezaji ndani ya nchi, kusaidia mazingira ya uwekezaji wa wananchi wetu nje ya nchi (Facilitation of investment abroad).Hii ni kwa sababu serikali imekuwa ikizungumzia na kutekeleza “foreign investment policy” na kusahau kuwa wananchi wetu wanahitaji msaada mkubwa wa serikali yao ili na wao waweze kuwekeza nje ya nchi na hivyo faida kurudi nyumbani. Kwa kuweza kufanikisha hili hata remittances itaongezeka.
Serikali iwaagize mabalozi katika nchi husika kuratibu na kutoa semina kwa Watanzania waishio nje na kufanya kazi nje ya nchi juu ya umuhimu wa kuwekeza katika nchi yao,ili kwa kufanya hivyo waweze kuchangia Pato la Taifa na hatimaye kukuza ukuaji uchumi wa nchi yetu.

HADHI YA BALOZI ZETU KWENYE NCHI MBALIMBALI

Mheshimiwa Spika, balozi zetu ndio taswira halisi inayomulikwa na nchi rafiki kuhusu Tanzania.Tunatia aibu. Majengo ya balozi nyingi ni chakavu, utendaji kazi hauridhishi, na nyingi zimeonyesha uwezo finyu wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na uchumi wa kidiplomasia. Hata Jengo la Wizara hii nalo linatutia aibu kama Taifa. Majengo mengi yanavuja, hayana miundombinu ya kisasa na muonekano unaokidhi hadhi ya Kimataifa. Wakati mwingine serikali inalazimika kukodi majengo ya bei rahisi ambayo kimsingi hayana hadhi ya kutumika kama balozi.

Mheshimiwa Spika, tuna maeneo mengi ambayo tumepewa viwanja ili tuweze kujenga balozi zetu na mpaka leo viwanja hivyo havijafanyiwa lolote. Pia kuna maeneo ambayo serikali ilishaweka jiwe la Msingi mpaka leo hakuna lililoendelezwa. Mfano, tarehe 17/10/2012, Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete aliweka jiwe la Msingi na kuahidi kujenga ubalozi wa Oman kabla ya hajaondoka madarakani. Mpaka sasa hakuna kilichofanyika. Kwa udhaifu huu uliokithiri umepelekea Kambi rasmi ya Upinzani kugundua sababu ya Serikali kuizuia Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama isifanye ukaguzi wa Balozi zetu. Huu mchezo wa kufunika Kombe Mwanaharamu unaidhalilisha nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali iboreshe balozi zetu. Serikali iepuke kulipa fedha nyingi kupanga majengo kwa ajili ya ofisi za balozi. Serikali itumie wadau mbalimbali yakiwemo makampuni na mashirika binafsi ndani na nje ya nchi ili iweze kujenga majengo ya kudumu na kuacha kuwa wapangaji. Tunaitaka Serikali ielewe kuwa kuonekana maskini sio sifa wala mkakati wa kuhurumiwa, bali ni fedheha inayoishushia nchi yetu hadhi na nguvu ya kiushawishi mbele ya mataifa mengine.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo kumekuwepo na uzembe mkubwa katika kusimamia mali za umma kwenye balozi zetu. Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya June 2015, Ubalozi wa Tanzania ulioko Kampala Uganda hauna hati miliki ya Ardhi ambayo jengo la Ubalozi limejengwa.Hali hii inaweza kuisababishia serikali kupoteza haki yake ya umiliki endapo itatokea kutokuelewana katika umiliki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutupa sababu za Kimsingi ni kwa nini mpaka leo hati ya ardhi ya ubalozi huu wa Kampala haijapatikana na inachukua hatua gani kuhakikisha hati hiyo inapatikana kwa uharaka? Na ni lini kwa haraka kiasi gani serikali itafanikisha uwepo wa hati hiyo.

USIMAMIZI WA FEDHA KWENYE BALOZI ZA TANZANIA

Mheshimiwa Spika, balozi zetu nyingi bado hazitumii mfumo funganifu wa usimamizi wa fedha kwa njia za kieletroniki za kompyuta IFMS-EPICOR, ambayo ndiyo njia bora zaidi za kusimamia matumizi ya kifedha na kuharakisha uandaji wa ripoti mbalimbali za kifedha katika Taasisi za Umma, kama ilivyoelezwa kwenye Ripoti ya CAG 2015. Balozi ambazo bado hazitumii mfumo huo ni ubalozi wa Tanzania Cairo,Tokyo,Harare,Abuja,Brusssels,London,Ubalozi wa Umoja wa Mataifa Geneva nk.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha balozi hizi kutotumia Mfumo huu kama ilivyoamriwa na serikali ni kukiuka kabisa taratibu ambazo serikali yenyewe imejiwekea. Kuendelea kutumia mfumo wa kizamani usio wa kompyuta ni kuruhusu watu wasio na nia njema kupitisha fedha zisizo halali. Jambo hili linaweza kuhatarisha imani ya nchi yetu katika mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali ichukue hatua dhidi ya mabalozi au watendaji wanaoshindwa kutekeleza maazimio na maagizo ya serikali. Aidha, tunaitaka serikali ipeleke wataalamu wenye uwezo, wanaoendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia dunia (Global technology) ili waweze kutumia mfumo huu kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza. Serikali iandae mafunzo kwa ajili ya wataalamu wake katika balozi hizi ili waweze kutambua umuhimu wa kutumia mfumo huu.

X. JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, ni miaka 16 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), lakini bado Tanzania haina Sera yake ya Utengamano kwenye jumuiya hii kama ilivyo kwa nchi za Kenya na Uganda. Kwa kukosa sera hii muhimu Tanzania inakuwa haina dira ya nini hasa tunasimamia au tunataka kwa maslahi ya nchi yetu kwenye jumuiya hii. Kwa kutokuwa na sera hii, Wabunge wetu wa Afrika ya Mashariki wanakuwa hawana muongozo wowote muhimu wa kusimamia maslahi ya nchi wanapokuwa kwenye vikao vya Bunge hilo.
Mheshimiwa Spika, hiki ni Serikali imeshindwa kuwapatia ofisi wabunge wetu wa EAC kiasi cha kulazimika kufanyia shughuli zao za kibunge nyumbani au hotelini
Serikali imeshindwa kuwapatia usafiri Wabunge wetu wa EAC licha ya kuombwa kupatiwa mikopo ya magari isiyolipiwa kodi kama ilivyo kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali imeshindwa kuwatumia wabunge wetu wa EAC katika kuhamasisha wananchi kuzifahamu faida na fursa za jumuiya hii. Matokeo yake miaka 16 tangu kuanzishwa kwa EAC, uelewa wa Watanzania bado ni mdogo sana.
Serikali imeshindwa kuwapatia Mtafiti (researcher) wabunge wetu wa EAC na kuwaacha wakichangia mijadala kwa kutegemea tu utashi wao badala ya ushahidi wa kitafiti. Serikali zilizo serious duniani huwa hazifanyi uzembe kama huu.
Kambi ya Upinzani imebaini kuwa mpaka sasa wabunge wetu wa EAC hawajui wako chini ya nani na wanapaswa kuripoti kwa nani hasa, kwa Wizara au kwa Bunge? Huu ni udhaifu mwingine wa serikali wa kushindwa kutoa miongozo na kufanya kazi kwa karibu na wabunge wetu.

Kambi ya Upinzani inazo taarifa kuwa Serikali ya Tanzania ndiyo inayoongoza kwa urasimu na uzembe wa kushindwa kufanya maamuzi kwa wakati kwa masuala yanayoihusu Tanzania. Udhaifu huu umekuwa ukichelewesha kufikiwa kwa maamuzi kadhaa ya Bunge la EAC katika kupitisha miswada.

Mheshimiwa Spika, mapungufu yote haya yanathibitisha jinsi Serikali yetu isivyo serious katika kusukuma maslahi ya nchi kwenye EAC. Aidha, huu ni ushahidi kuwa Tanzania bado haijajiandaa na wala haina wataalamu wa kuiongoza vizuri Serikali katika kusukuma diplomasia ya kiuchumi hata kwa nchi jirani za Afrika Mashariki. Na kwa mapungufu haya, Kambi rasmi ya Upinzani haioni tija yoyote ya fedha ambazo serikali imekuwa ikitengewa na Bunge hili kwaajili ya shughuli za Afrika Mashariki. Kwa udhaifu huu, wizara hii inabaki kuwa ni wizara ya safari, vikao na mikutano visivyokuwa na tija yoyote kwa maendeleo ya nchi kwasababu ya serikali kushindwa kujipanga na kutimiza wajibu wake. Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali ijitathimini, ijipange upya na itupe mkakati makini na endelevu kuhusu ushiriki wenye tija wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

DEMOKRASIA NA HAKI ZA BINADAMU

Mheshimiwa Spika, nchi ya Burundi ilifanya Uchaguzi wake Mnamo Mwezi Julai 2015, na Uganda tarehe 18, Februari 2016. Makundi ya wanasiasa na wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu walishutumu tume za uchaguzi, walishuhudia ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, mauaji ya viongozi wa Upinzani na kila alama ya udikteta dhidi ya wananchi wa nchi hizo. Nchini Uganda, viongozi wa Upinzani akiwemo Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini humo, Kizza Besigye, aliwekwa korokoroni katika kipindi cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, serikali ya Tanzania ilipaswa kukemea uovu huo waziwazi kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa akikemea vitendo vya kidikteta, unyonyaji na ubaguzi wa rangi kabla na baada ya kupata uhuru. Hata hivyo, kambi ya upinzani haikushangazwa na hatua ya serikali kubariki yaliyofanyika kwenye nchi hizo. Hayakuwa na tofauti yoyote na yale yaliyofanywa na CCM kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 na ule wa marudio wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, sasa ni dhahiri kuwa vyama tawala vya nchi hizi vinashirikiana katika kukandamiza wapinzani na kung’ang’ania madaraka kwa style ya kuitisha chaguzi zisizo za kidemokrasia na kujiweka madarakani. Kambi ya Upinzani inaonya kuwa mchezo huo ni hatari sana kwa amani ya nchi na kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Ni vema ikazingatiwa kuwa mchezo huu wa CCM na washirika wake hauwezi kudumu siku zote bila kusababisha machafuko yatakayodhuru pande zote – upinzani na vyama tawala. Kwa hiyo, kwa mara nyingine tena naishauri serikali hii ya CCM iache kubaka demokrasia na ikome kubariki uvunjifu wa demokrasia na haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika, amani ya Afrika Mashariki ndio amani ya dunia. Kambi ya upinzani inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kupitia balozi zake zote zilizopo hapa nchini, kwamba ianze bila kuchelewa kutafuta suluhu ya kujenga demokrasia ya kweli katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki; vinginevyo upo uwezekano wa kutokea uvunjifu mkubwa wa amani katika siku za usoni utakaokuwa na athari pia kwa dunia .

HITIMISHO

Mheshiwa Spika, nahitimisha hotuba hii nikionya na kusisitiza yafuatayo:
Kwanza, serikali iwekeze kwenye kusomesha na kutoa mafunzo yatakayoipatia nchi wanadiplomasia wa uchumi wa kutosha. Investment in knowledge is the best investment.
Pili, tabia ya kung’ang’ania madaraka ya baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania itasababisha machafuko yatakayodhuru pande zote. Serikali Ijifunze kutoka Zambia, Nigeria na kwingineko ambapo demokrasia inaheshimiwa. Serikali iepuke kuwa mpambe wa nchi zinazofanya siasa za kijima katika karne hii ambayo kila nchi inajitahidi kuwa na dola iliyostaarabika. “Let us be slow walkers, but never walk back”

Nne, serikali itengeneze fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye ushindani wa kibiashara na kiuchumi ndani na nje ya nchi hususani katika nchi marafiki.
Tano, Serikali izingatie kuwa “uhusiano mzuri wa kimataifa wa nchi yoyote ile duniani unategemea sana ustaarabu wa ndani na mwenendo mzuri wa Serikali ya nchi hiyo kwa watu wake. Nchi yenye Serikali katili, ya kidikteta, isiyopenda kukosolewa, ya kifisadi, isiyoheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na inayokandamiza uhuru wa wananchi wake – kama Tanzania - haiwezi kuheshimiwa wala kuwa kivutio kwa mataifa mengine katika kujenga na kudumisha uhusiano mzuri na wenye tija kimataifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha

Mchungaji Peter Simon Msigwa (Mb)
WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA RASMI YA UPINZANI BUNGENI KARIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA.
31 Mei, 2016
 
Msigwa hajasusa ili kupinga kitendo cha wabunge wenzake kutimuliwa bungeni?
 
Hotuba imetulia sana hii, inabidi Serikali wawe wanakuja kupata semina elekezi ya uandishi wa hotuba kwa mh. Msigwa
 
hawa jamaa Ukawa wanatakiwa wapewe nchi maana kila wasemalo ingawa mabwanyenye yanabisha lakini baadae yanakubali ushauri wa Ukawa. shame of them.

swissme
 
Duuh aya ya mwisho msumari kamati ya maadili haikupitia
 
Duuh aya ya mwisho msumari kamati ya maadili haikupitia
Sasa hivi hiyo kamati imepagawa baada ya kuona watanzania wameamua kulaani kitendo chao cha uonevu walicho kifanya kwa wabunge wa upinzani
 
Hotuba hii inaashiria kuwa Kambi ya Upinzani ina uelewa finyu katika masuala ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa. Haishangazi, kwa sababu ni masuala yanayohitaji uzoefu mkubwa ambao, kwa bahati mbaya, wengi wa viongozi wa Kambi ya Upinzani hawana. Masuala mengi yamepotoshwa. nitoe mifano miwili:

Kwanza, Ushirikiano wa Afrika mashariki. Kwa nini Tanzania inashutumiwa kwa kuonesha kasi ndogo katika mikakati ya utangamano. Yapo masuala ya msingi ambayo kama Mheshimiwa Msigwa angefanya utafiti mdogo angeelewa. Akitaka, arejee taarifa ya Kamati iliyosimamiwa na Mheshimiwa Kamala au Hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete (sasa mstaafu) wakati dhana ya 'Coalition of the Willing (CoW)' iliposhika kasi na atafiti pia kwa nini CoW inaelekea kufifia. Hotuba ya Mheshimiwa Msigwa, sijui kwa makusudi au kwa dhamira ya kupotosha, kwa nini hatoi pongezi kwa Diplomasia makini ambayo imefanikiwa katika kuishawishi serikali ya Uganda kukubali kupitisha bomba la Mafuta kwenye ardhi ya Tanzania. Kama uamuzi huo si chochote au lolote kwa Kambi ya Upinzani basi kuna walakini mkubwa katika uelewa wao wa dhana ya diplomasia ya uchumi au utekelezaji wa kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa 38 wa Australia - Julie Bishop.

Pili, nafasi ya Diaspora katika uchumi wa taifa lolote lile. Hili liko wazi, lakini idadi yao na aina ya shughuli zinazofanywa na wanadiaspora hao haziwezi kupuuzwa kwa sababu ndio msingi mkubwa wa mafanikio yao. Mheshimiwa Msigwa ametoa takwimu ya remittances za wanadiaspora wa Ethiopia. Zinaweza kuwa sahihi. Bahati mbaya, kwa kutoelewa tena, kwa makusudi, au katika kupotosha ukweli, hakueleza mamilioni ya raia wa Ethiopia wanaoishi mataifa ya nje (pamoja na shughuli wanazofanya), kwa mfano Marekani, Italia, Sweden na hata Saudi Arabia, Lebanon na Falme za Kiarabu. Vile vile, Wasomalia wangapi wanaishi mataifa ya nje kama Uarabuni, Uingereza, Canada na Marekani. Mheshimiwa Msigwa anaishitumu Wizara kwa kushindwa kufanya utafiti, lakini yeye mwenyewe na Kambi ya Upinzani hawajawatendea haki Watanzania kwa kushindwa pia kufanya utafiti na kuleta hoja zilizojikita kwenye matokeo ya utafiti huo na hivyo kuwa na mashiko. Inasikitisha kuona hoja za Kambi ya Upinzania zinakuwa nyepesi kiasi hiki. Mheshimiwa Mao alishasema, "no research, no right to speak".
 
Hotuba imetulia ina maono na mwelekeo wenye dhamira ya kweli kulikomboa, Taifa hili.
Sasa magamba chukueni ushauri huu na kuufanyia kazi na kuwashukuru wapinzani.
Sio mna copy na kupaste alafu mseme ni idea zetu mzivyo na haya.
 
Hotuba hii inaashiria kuwa Kambi ya Upinzani ina uelewa finyu katika masuala ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa. Haishangazi, kwa sababu ni masuala yanayohitaji uzoefu mkubwa ambao, kwa bahati mbaya, wengi wa viongozi wa Kambi ya Upinzani hawana. Masuala mengi yamepotoshwa. nitoe mifano miwili:

Kwanza, Ushirikiano wa Afrika mashariki. Kwa nini Tanzania inashutumiwa kwa kuonesha kasi ndogo katika mikakati ya utangamano. Yapo masuala ya msingi ambayo kama Mheshimiwa Msigwa angefanya utafiti mdogo angeelewa. Akitaka, arejee taarifa ya Kamati iliyosimamiwa na Mheshimiwa Kamala au Hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete (sasa mstaafu) wakati dhana ya 'Coalition of the Willing (CoW)' iliposhika kasi na atafiti pia kwa nini CoW inaelekea kufifia. Hotuba ya Mheshimiwa Msigwa, sijui kwa makusudi au kwa dhamira ya kupotosha, kwa nini hatoi pongezi kwa Diplomasia makini ambayo imefanikiwa katika kuishawishi serikali ya Uganda kukubali kupitisha bomba la Mafuta kwenye ardhi ya Tanzania. Kama uamuzi huo si chochote au lolote kwa Kambi ya Upinzani basi kuna walakini mkubwa katika uelewa wao wa dhana ya diplomasia ya uchumi au utekelezaji wa kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa 38 wa Australia - Julie Bishop.

Pili, nafasi ya Diaspora katika uchumi wa taifa lolote lile. Hili liko wazi, lakini idadi yao na aina ya shughuli zinazofanywa na wanadiaspora hao haziwezi kupuuzwa kwa sababu ndio msingi mkubwa wa mafanikio yao. Mheshimiwa Msigwa ametoa takwimu ya remittances za wanadiaspora wa Ethiopia. Zinaweza kuwa sahihi. Bahati mbaya, kwa kutoelewa tena, kwa makusudi, au katika kupotosha ukweli, hakueleza mamilioni ya raia wa Ethiopia wanaoishi mataifa ya nje (pamoja na shughuli wanazofanya), kwa mfano Marekani, Italia, Sweden na hata Saudi Arabia, Lebanon na Falme za Kiarabu. Vile vile, Wasomalia wangapi wanaishi mataifa ya nje kama Uarabuni, Uingereza, Canada na Marekani. Mheshimiwa Msigwa anaishitumu Wizara kwa kushindwa kufanya utafiti, lakini yeye mwenyewe na Kambi ya Upinzani hawajawatendea haki Watanzania kwa kushindwa pia kufanya utafiti na kuleta hoja zilizojikita kwenye matokeo ya utafiti huo na hivyo kuwa na mashiko. Inasikitisha kuona hoja za Kambi ya Upinzania zinakuwa nyepesi kiasi hiki. Mheshimiwa Mao alishasema, "no research, no right to speak".


KAZI YA UPINZANI NI KUKOSOA SIO KUPONGEZA
 
Yaani hawa jamaa wabaki kuwa fotokopi hivi hivi,akili kama za kuku wa kisasa.Kipindi cha kampeni walitoa hoja ya kupunguza au kuondoa safari za nje ya nchi wakimlaumu JK kwa kuifilisi ikulu kwa safari nyingi.Leo Huyu Mchunga mbuzi anakuja na hoja ile ile ya kudai safari.Ndio maana tunasema CCM inatawala kwa sababu KUB Mbowe na vivuli vyake ni mbumbumbu.
 
Msigwa hajasusa ili kupinga kitendo cha wabunge wenzake kutimuliwa bungeni?

Walisema wangesusa vikao vyote ambavyo naibu spika atakuwa anaviongoza.Wakapima wakaona watakosa posho.Wameamua kumpuuza Mbowe wabaki bungeni wasikose posho.Hiyo hotuba kaitoa geresha tu ili ajionyeshe kuwa yumo bungeni wasije mnyima posho ya kikao.Kaitoa kama ushahidi kuthibitisha kwa naibu spika kuwa yuko bungeni asije mnyima posho ya kikao.Ndio maana kaileta hiyo hotuba hadi huku Jamii forums ili tumsaidie ushahidi kuwa kweli alikuwemo bungeni.
 
Walisema wangesusa vikao vyote ambavyo naibu spika atakuwa anaviongoza.Wakapima wakaona watakosa posho.Wameamua kumpuuza Mbowe wabaki bungeni wasikose posho.Hiyo hotuba kaitoa geresha tu ili ajionyeshe kuwa yumo bungeni wasije mnyima posho ya kikao.Kaitoa kama ushahidi kuthibitisha kwa naibu spika kuwa yuko bungeni asije mnyima posho ya kikao.Ndio maana kaileta hiyo hotuba hadi huku Jamii forums ili tumsaidie ushahidi kuwa kweli alikuwemo bungeni.

Sawa tumekusukia na Wewe kachukue posho yako
 
Yaani hawa jamaa wabaki kuwa fotokopi hivi hivi,akili kama za kuku wa kisasa.Kipindi cha kampeni walitoa hoja ya kupunguza au kuondoa safari za nje ya nchi wakimlaumu JK kwa kuifilisi ikulu kwa safari nyingi.Leo Huyu Mchunga mbuzi anakuja na hoja ile ile ya kudai safari.Ndio maana tunasema CCM inatawala kwa sababu KUB Mbowe na vivuli vyake ni mbumbumbu.

Hata kuelewa tu umeshindwa , halafu pili umekuja kuthibitisha wew e Ndio mwandishi wa Ile Habari ya KUB , Wewe ni wa kupuuzwa
 
Back
Top Bottom