Hotuba ya kambi rasmi ya upinzani juu ya mpango wa maendeleo wa taifa 2014/15

The Conquerer

Member
Aug 16, 2012
79
94
Mhe. David Silinde, Mbunge wa Mbozi Magharibi - CHADEMA ndio anasoma hotuba hiyo sasa hivi. Fuatilieni.




HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO WA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
---------------------(Inatolewa chini ya Kanuni ya 94(5) (a) ya kanuni za Bunge Toleo la mwaka 2013)
________________________________


1. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 94(5)(a) napenda kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/2015.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inapenda watanzania wafahamu kwamba; kwa mujibu wa Kanuni ya 94(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Aprili, 2013 ni kwamba; Bunge katika Mkutano wake wa mwezi Oktoba – Novemba kila mwaka, linatakiwa kukaa kama Kamati ya Mipango kwa siku zisizopungua tano kwa madhumuni ya kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata. Aidha, ni katika mkutano huo huo, ambapo Bunge hujadili, kutoa maoni na ushauri kuhusu mwongozo wa kuandaa mpango wa Bajeti ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kujadili na kuishauri Serikali juu ya vyanzo vya mapato ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inapenda vilevile wananchi wafahamu kwamba Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya 2014/15 yaliyoletwa na Serikali ili yajadiliwe na Bunge hili ni ya nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16). Kwa maneno mengine ni kwamba imebaki miaka miwili tu kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inapenda pia kuwajulisha wananchi kwamba wakati imebaki miaka miwili tu kwa Serikali kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, umebaki mwaka mmoja tu kwa upande wa Chama cha Mapinduzi kukamilisha utekelezaji wa Mpango huo. Hii ni kwa mujibu wa Sura ya Tisa (9) Ibara ya 212 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ambayo inasema kwamba:
"Chama Cha Mapinduzi katika miaka mitano ijayo,(yaani 2010 - 2015) kinaelekeza nguvu kubwa katikakutimiza lengo la msingi la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa kuendeleza jitihada za ujenzi wa uchumi wa kisasa na taifa linalojitegemea. Katika kuzingatia jukumu hilo Ilani hii ya CCM ya 2010 hadi 2015 inatangaza nia ya modenaizesheni ya uchumi. Modenaizesheni ya uchumi ndiyo njia ya uhakika itakayobadili na kuleta mapinduzi katika uchumi wa nchi, kujenga msingi wauchumi wa kati unaoongozwa na viwanda, kuondoa umasikini wa wananchi wetu kwa kiwango kikubwa na hivyo kuwezesha nchi yetu kujitegemea…………..."
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inataka wananchi wapime na kufanya tathmini wenyewe juu ya mambo yafuatayo:

i. Miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa Upande wa Serikali na Miaka Minne ya Utekelezaji wa Mpango huo huo kwa upande wa CCM imeleta mabadiliko katika maisha yao yaliyokusudiwa na mpango huo?
ii. Je, ni kweli kwamba Mkakati wa CCM wa kufanya mapinduzi ya Uchumi (Modenizationi ya uchumi) uliotangazwa na ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010 umefanikiwa?
iii. Je, ni kweli kwamba msingi wa uchumi wa Tanzania unaongozwa na viwanda kama CCM ilivyoahidi kwenye ilani yake ya uchaguzi ya 2010
iv. Je ni kweli kwamba umasikini wa wananchi umepungua zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama CCM ilivyoahidi kupunguza umasikini kwa wananchi na kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania?
v. Je ni kweli kwamba sasa hivi Tanzania ina uwezo zaidi wa kujitegemea kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama ambavyo CCM iliahidi kwamba kabla ya 2015 Tanzania itakuwa na uchumi imara na hivyo kujitegemea?
vi. Je ni kweli kwamba hali ya ajira hasa kwa vijana ni bora zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama ambavyo Serikali ya CCM ilivyoahidi kutoa ajira ili kupunguza umasikini wa kipato?
vii. Je ni kweli kwmba Elimu yetu ni bora zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita kama Mpango wa Maendeleo ulivyokuwa umekusudia? Ikumbukwe kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano, ndipo taifa limeshuhudia kuporomoka kwa elimu kwa kiwango kikubwa kuliko vyote katika historia ya Tanzania. Ni kipindi ambacho tumeshudia zaidi ya asilimia 65 ya wanafunzi wa kidato cha nne wakipata alama sifuri katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012. Ni kipindi ambacho tumeshudia wanafunzi wanahitimu darasa la saba na kufaulu bila kujua kusoma na kuandika nk.
viii. Je ni kweli kwamba sekta ya wanyamapori na utalii vimeimarika zaidi kuliko miaka mitatu au minne iliyopita? Ikumbukwe kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano ndipo tumeshuhudia ujangili wa Tembo wa kutisha kuliko ilivyokuwa hapo kabla

Mheshimiwa Spika, yapo maswali mengi ya kujiuliza ili kujua kama mpango umefanikiwa au la lakini bila shaka majibu ya maswali haya yako wazi kwa kuwa kila kukicha malalamiko ya wananchi kwamba hali ya maisha inazidi kuwa ngumu yanaongezeka.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa mwaka 2014/15 ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ambao nao ni sehemu ya Kwanza kati ya sehemu tatu za mipango ya nchi ili kufikia Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Lengo la ujumla la sehemu ya kwanza ya dira ya 2025 ni "kutoa fursa ili hazina ya raslimali za nchi zitumike ipasavyo ili kuweka mazingira wezeshi na kutanua wigo wa ukuaji wa uchumi ili watu maskini waweze kukua kiuchumi".

Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA katika hotuba za mpango wa uchumi zilizopita imejitahidi sana kuishauri Serikali namna mbali mbali za kusimamia utekelezaji wa Mpango lakini mara zote Serikali imekuwa ikipuuza ushauri na matokeo yake ni kwamba mipango hiyo imekuwa haitekelezeki kwa ufanisi jambo ambalo limesababisha wananchi kuzidi kuwa maskini na rushwa kuzidi kuongezeka. Tunaendelea bila kuchoka kuishauri serikali hii ya CCM inayojiita sikivu lakini isiyosikia mapendekezo muhimu na kuyazingatia katika uandaaji wa Mpango unaoweza kutekelezeka na ambao unaakisi hali halisi ya uchumi na wananchi wetu.
2. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO
Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa Serikali kwa ushauri wa Tume ya Mipango iliweka vipaumbele kwa miaka mitano (2011/12 - 2015/16) ambavyo katika utekelezaji wake vitaleta matokeo ya haraka katika kuchochea maendeleo ya maeneo mengine ya uchumi (multiplier effect); uwezo wa mradi husika kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, na hivyo kuongeza ajira. Vipaumbele vilivyochaguliwa ni kama ifuatavyo:
i. Miundombinu, ii. Kilimo iii. Viwanda: iv. Maji v. Rasilimali watu:[1].

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tathmini ya utekelezaji wa miradi iliyotajwa hapo juu sambamba na taarifa ya matumizi ya fedha zilizotumika katika utekelezaji wa Miradi hiyo ili tuweze kupima malengo tuliyojiwekea katika Mpango wa Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16.

Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kubwa sana kati ya Maendeleo yaliyoandikwa kwenye Mpango na Maendeleo halisi kwa wananchi. Sababu za tofauti hii ni kama ifuatavyo:
i. Tunapanga maendeleo yetu kwa kutegemea misaada au uwezeshaji toka kwa wahisani (Misaada na mikopo 30% +)
ii. Tunapanga mipango ambayo hatuwezi kuitekeleza. Miradi mingi inachukua muda zaidi ya muda uliopangwa na hivyo kuongeza gharama.
iii. Miradi mingi ya maendeleo haina uhalisia wa malengo/mahitaji ya jamii inayolengwa (Miradi inakuwa si shirikishi na hivyo utekelezaji wake hauhusishi wananchi).
iv. Serikali haijatekeleza vipaumbele ilivyoviweka (Yaani kupanga bajeti yake kulingana na maazimio iliyoridhia).
v. Serikali imeshindwa kutoa fedha za maendeleo hata zile zilizopangwa kwenye bajeti yake, kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango.
vi. Miradi mingi inayokamilika ku haikidhi viwango, jambo linalosababisha ukarabati wa mara kwa mara kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Spika, kuna usemi mmoja wa Wajapani unaosema kuwa "Planning without action is a day dream But Action without planning is a nightmare." Hapa "action" ina maana ya bajeti itakayowezesha utekelezaji. Lakini jambo la ajabu ni kwamba Serikali ya CCM huwa inapanga bila kuwa na bajeti ya utekelezaji. Na ndio maana mawaziri wanapoulizwa maswali na wabunge maswali juu ya utekelezaji wa miradi fulani hukimbilia kujitetea kwamba kuna ufinyu wa bajeti ndio maana utekelezaji umekwama. Kupanga bila bajeti ndio tunaambiwa na wajapani kuwa ni kuota ndoto za mchna. Je, Watanzania wataendelea kusubiri Serikali iote ndoto za mchana hadi lini?

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa yanaonesha kwamba utendaji wa Serikali katika kuimarisha uchumi kwa kpindi cha 2013/14-2015/16 umefikia malengo katika baadhi ya maeneo na pia umevuka malengo katika baadhi ya maeneo. Uchunguzi uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Unaonesha kwamba Serikali katika kupanga, ilijiwekea malengo madogo ambayo ni rahisi kuyafikia na kwa matumizi ya fedha nyingi na inapoyafikia inajigamba kuwa imevuka lengo. Kwa mfano, katika utekelezaji wa Mpango tunaambiwa kuwa makusanyo ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa mwaka 2013/14 ni asilimia 20.2 ya pato la taifa, na shabaha ilikuwa ni asilimia 19.1 ya pato la Taifa. Hivyo basi Serikali inajipongeza kwa kuvuka malengo. Hoja hapa ni kwamba lengo hilo katika shabaha ni halisia katika uendelezaji wa mipango tuliyojiwekea? Je makusanyo hayo yanaweza kutekeleza hata robo ya miradi iliyo katika mpango wa mwaka huu? Kambi Rasmi ya Upinzani inasema shabaha na misingi hii haiakisi hali halisi ya rasilimali zetu na watu wake na hivyo ni mkakati wa kifisadi wa kuifanya nchi yetu iendelee kuwa maskini.

Mheshimiwa Spika, Ni katika utekelezaji wa Mpango huu wa Miaka mitano ambapo kumekuwepo na ukwepaji mkubwa wa kodi na utoroshaji wa fedha za umma kwenye mabenki nje ya nchi. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa hoja binafsi hapa Bungeni na Bunge likaazimia kwamba Serikali ifanye uchunguzi ili wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria na kuinusuru nchi yetu na janga la uhujumu uchumi. Hadi nasoma hotuba hii, Serikali haijaleta taarifa Bungeni kuhusu utekelezaji wa Azimio hilo la Bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, kwa mtindo huu, Serikali itawezaji kutekeleza Mpango wa Maendeleo wakati fedha zinazotoroshwa zingeweza kuongeza bajeti ya Serikali na hivyo kuepuka kuendelea kuwa tegemezi kwa nchi wahisani?

Mheshimiwa Spika,takwimu zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 2001 na 2011 uchumi wa Tanzania ulikuwa kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka lakini umaskini ulipungua kwa asilimia 2 tu. Ukuaji mkubwa wa uchumi ulitokea kwenye sekta ya madini na sekta ya huduma. Kwa bahati mbaya ni kwamba ukuaji huo haumlengi mwananchi maskini, kwa maana rahisi ni kwamba jamii maskini za watanzania zimeendelea kuwa maskini hadi sasa. Tafiti zinadhihirisha kuwa mapato ya kodi kutokana na uwekezaji yamekuwa ni kidogo sana na ajira zimezidi kupungua sana hasa kwa wachimbaji wadogo wamezidi kuhangaika kwa kukosa kazi wakati makampuni makubwa yamezidi kupata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misingi ya Mpango kwa mwaka 2014/15 kifungu cha "c" kinasomeka kuwa ni kuimarisha utekelezaji wa miradi iliyoibuliwa mwaka 2012/13 ya Programu ya Matokeo Makubwa sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona hapa hakuna umakini katika kuhakikisha Mpango wa miaka mitano. Miradi hii haikuibuliwa mwaka 2012/13, bali miradi hiyo ilitakiwa iwemo ndani ya Mpango wa miaka mitano na sio kweli kwamba Matokeo Makubwa Sasa ni Mpango!!!!! Kiuhalisi ni kwamba Matokeo Makubwa sasa ni Monotoring Tool ya Mpango wa Miaka Mitano ili kuhakikisha malengo ya mpango yanapatikana kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa ni kwamba wasifu wa mtu na record yake ya nyuma ndiyo inatoa imani kwa watu, hivyo basi bado watanzania wanamakovu ya Kampuni yao ya simu na ile kampuni yao ya Celnet. Jinsi ambavyo uhujumu ulivyofanywa na kuiua na celtel ya MO Ibrahim ikaingizwa nchini rasmi na kuchukua mali zote za iliyokuwa Kampuni ya simu. Celtel ilikiwa chini ya uratibu wa Mratibu wa sasa wa Matokeo Makubwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mpango huu ambao umeletwa kwa ajili ya Bunge kuupitia na kutoa ushauri ni sehemu ya nne ya mpango wa miaka mitano, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tathmini ya sehemu ya kwanza, pili na tatu kama malengo ambayo yalikusudiwa yamefikiwa kwa kiasi gani na kama tumeshindwa tumeshindwa wapi.

Mheshimiwa Spika, kuna usemi unaosema kuwa "IF WE CAN NOT MEASURE WE CAN NOT MANAGE" (yaani kama hatuwezi kupima, basi hautwezi kuthibiti") hivyo basi ni jukumu letu kama Bunge kwa niaba ya wananchi kabla ya kukubaliana na Serikali kwanza tupime yale yote tuliyokubaliana kuwa yatatekelezwa katika awamu zilizopita za Mpango wa miaka mitano na ndipo twende mbele. Kinyume cha hapo ni ukweli usiopingika kuwa tunawalaghai watanzania na hata wale wote wanaochangia fedha zao kwa ajili ya kutusaidia kujikwamua katika umaskini.

Mheshimiwa Spika, tatizo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba linakwamisha utekelezaji wa Mpango ni kutoshirikishwa kikamilifu kwa wananchi katika hatua zote za uandaaji na utekelezaji wa Mpango. Kwa mfano, ni kwa kiasi gani Mpango wa miaka mitano unaeleweka kwa wananchi? Hii ni muhimu kwani kuna maeneo ambayo jamii inawajibika kuwa ni washiriki katika utekelezaji wake. Mfano sehemu ya nguvu kazi, badala ya kuleta nguvu kazi toka uchina au maeneo mengine vijana wa maeneo husika wanaweza kufanya kazi. Je ni mkakati gani umefanyika wa utekelezaji wa Mpango katika ngazi zote za Serikali za mitaa kwa kuanzia ngazi ya Halmashauri, kata hadi vijiji unaweza kupimika?

Mfumo wa Uwajibikaji kwa Jamii (The Social Accountability Monitoring (SAM)

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza matumizi ya Mfumo wa Uwajibikaji kwa Jamii (Social accountability monitoring – SAM) ambao ni utaratibu unaojali na kuimarisha uwajibikaji ki-mfumo huku ukijenga uwezo kwa jamii, wadau na waajiri wa serikali kuhoji na kupata ufafanuzi toka kwa waliopewa mamlaka ya utekelezaji kwa maamuzi, matendo na taarifa zao za uwajibikaji wao katika shughuli za umma.

Mheshimiwa Spika, Mfumo huu unawarejesha wananchi kwenye nafasi yao ya asili ya ukuu wa kuiwajibisha serikali na vyombo vyke na watendaji wake. Unawakumbusha viongozi na watendaji katika huduma za umma juu ya uwajibikaji wao kwa matumizi ya rasilimali za umma, mipango ya matumizi, mgawanyo wa rasilimali; matokeo na ufanisi wa matumizi ya rasilimali hizo; mifumo iliyopo ya uwajibikaji na vyombo vya usimamizi.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa mfumo huu unarejesha hadhi ya dola kuwajibika kwa wapiga kura wake, huku ikiwarejeshea hadhi yao kwa kupata taarifa,Uwazi, kujadili mipango ya maendeleo, kujishirikisha kwenye utekelezaji mipango, kuchambua ufanisi na kuhoji maamuzi na utendaji.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama haya yasiyokuwa na uwajibikaji, je tunaweza kutimiza malengo yetu ya mipango?


Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2013/14 kifungu cha 5.3 kinachohusu uratibu wa kusimamia fedha za maendeleo inaonyesha kwamba Wizara,Idara na wakala/Taasisi za Serikali kujaza fomu TFN 358 kwa miradi iliyopata idhini ya Tume ya Mipango na kuwasilisha Wizara ya Fedha kwa ajili ya ufuatiliaji wa tathmini, na Pia taasisi hizo za Serikali zitatakiwa kuwasilisha Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha taarifa ya kila robo mwaka si zaidi ya wiki mbili baada ya robo mwaka unaotolewa taarifa husika kwa uchambuzi.

Mheshimiwa Spika, hoja hapa ni taarifa ya fedha inayokwenda na hali halisi ya miradi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni bora Bunge likapewa taarifa ya hali halisi ya maendeleo ya mradi, kwa fedha zilizotarajiwa kutolewa na zilizotolewa, mradi umetekelezwa kwa kiwango kipi na unatarajia kukamilika lini? Hii inawapa hata wananchi kuweza kupima utendaji kazi wa Serikali yao na sio wangoje kuambiwa na washauri waelekezi kuwa mambo ni mazuri kama inavyofanyika sasa.

Mheshimiwa Spika, inawezekana kuwa miongozo hiyo ya ufuatiliaji na kufanya tathmini ipo kama hili dudu lililoletwa kuchukua raslimali za watanzania la "matokeo makubwa sasa", lakini tatizo ni kwamba mkakati wa utekelezaji wake ni tatizo kubwa kwani nyaraka zote na wanaoelewa ni wataalam washauri tu (consultants) nao wako serikali kuu lakini kwenye ngazi zingine za Serikali hakuna uelewa wa hilo. Kama wananchi na watekelezaji wengine hawashirikishwi kuelewa ni vigumu sana kufanikiwa katika mipango yetu. Mipango ya TASAF ilileta matunda kwa sababu kubwa ya kuwa shirikishi na hivyo hata tathmini yake ilikuwa shirikishi na matokeo yake yako wazi.
3. MAENEO YA KIPAUMBELE KATIKA MWAKA WA 2014/15
Mheshimiwa Spika, taarifa ya mpango huu umeainisha maeneo ya kitaifa ya kimkakati kwa mwaka wa 2014/15 ambayo ni miundombinu, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu, huduma za fedha na utalii huku maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi yakiwa ni elimu/mafunzo ya ufundi, afya na ustawi wa jamii,mifugo na uvuvi, misitu na wanyamapori ,madini, ardhi, nyumba na makazi, usafiri wa anga, hali ya hewa, biashara na masoko, ushirikiano na kikanda na kimataifa, utawala bora,vitambulisho vya taifa, sensa ya watu na makazi, kazi na ajira na mazingira.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inachambua maeneo hayo ya kimkakati kwa kuweka kipaumbele katika maeneo yafuatayo ambayo kimsingi ni lazima Serikali iyatolee ufafanuzi ili Bunge linapokaa kujadili Mpango wa mwaka 2014/2015 yatolewe ufafanuzi na Serikali;
a. Miundombinu
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa ndiyo kipaumbele katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, na kwa kuangalia fursa ya nchi yetu kijiografia ili kuhudumia mataifa ambayo hayana fursa hasa ya Bandari. Serikali imeshindwa kutekeleza matakwa ya Mpango ya kuifufua reli ya kati na kuifanya kuwa katika kiwango cha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa nchi jirani. Aidha kwa kuwa miundombinu imegawanyika katika aina mbili (Hard and soft infrastructure). Soft inayohusisha umeme na mawasiliano mengine, miradi ya umeme imekuwa ni kitendawili mgawo wa kimyakimya umeendelea na hivyo uchumi wetu umezidi kuwa ghali na kufanya watanzania kuzidi kutegemea bidhaa kutoka nje. Kwa tathmini rahisi kwa uapnde wa nishati tumeshindwa.
b. Elimu
Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kuwa Serikali imeshindwa kuboresha elimu nchini na ni jambo la kushangaza kuwa Serikali inaendelea kupiga danadana mustakabali wa elimu hapa nchini kana kwamba ni jambo la mzaha. Inatamka kuwa elimu ni kipaumbele katika nyaraka zake lakini katika ugawaji wa raslimali fedha haionyeshi kama ni kipaumbele. Kwani inajisifu kwa suala zima la kuongeza madarasa na walimu huku kukiwa na madai ya malimbikizo ya mishahara ya walimu, mishahara ya walimu ikiwa katika kiwango ambacho si tu kinawaumiza walimu bali kinachangia pia kwa kushuka kwa kiwango cha ufaulu, hali duni ya mazingira ya ufundishaji, kukosekana kwa nyumba za walimu, ubovu na kushindwa kwa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tunajadili mpango wa maendeleo wa Taifa utakaoleta mapendekezo ya uboreshaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge hili kupitia kiti chako kuitaka Serikali kuleta ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda iwasilishwe rasmi Bungeni na kujadiliwa ili kwa pamoja tuazimie hatua na utakaoweza kunyanyua sekta ya elimu kwa mwaka 2014/2015.
c. Ardhi, nyumba na makazi
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa migogoro ya ardhi nchini imeendelea kuongezeka huku Serikali ikionekana kukwepa moja kwa moja uwajibikaji ambao umesababisha upotevu wa maisha pamoja na uharibifu wa mali uliotokana na migogoro mingi sehemu mbalimbali. Pamoja na Serikali mara kadhaa kuahidi kutatua migogoro hiyo ikiwemo kuwalipa fidia wananchi, kuyarudisha mashamba na maeneo ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza na pia Serikali iliahidi kufanya ukaguzi wa mashamba kila mara ambapo Kambi rasmi ya Upinzani imekua ikihoji.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza migogoro ambayo ipo na inaendelea ni kwa serikali kupima na kutoa umiliki wa ardhi kwa wananchi, katika kadhia hiyo ni dhahiri Serikali itanufaika kukusanya kodi (land rent). Faida kubwa zaidi ni kuwezesha ardhi yenyewe kutumika kwa manufaa na kupunguza ardhi kubaki bure bila matumizi kwa muda mrefu, matumizi yasiyo na faida au kuiweka ardhi kusubiri soko. Wenye ardhi watalazimika kuitumia kwa manufaa ili iweze kulipa kodi tajwa. Hii ni njia nyingine ya kuiongezea mapato Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika kuujadili Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2014/15 Kambi ya Upinzani inaitaka serikali, kupitia Wizara ya Ardhi yenye jukumu pana la kusimamia sekta ya ardhi kuhakikisha kwamba Mpango unajumuisha pia kusimamia maeneo yote ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji yarejeshwe Serikalini bure bila fidia kwani wahusika wamekiuka masharti ya mikataba ya wao kupatiwa ardhi husika. Aidha Kambi inahitaji mrejesho wa usitishwaji ugawaji na umilikishaji wa ardhi kwa wawekezaji wa nje kama maazimio ya wabunge yalivyohitaji, baada ya Mheshimiwa Halima kuwasilisha hoja yake Bungeni.
d. Kilimo
Mheshimiwa Spika,Sekta ya kilimo ndio sekta mama katika utoaji wa ajira hapa nchi na inayoweza kuibadilisha hali nzima ya uchumi wan chi kutoka uchumi tegemezi kwenda uchumi uliosima bila utegemezi, utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kilimo la "PELUM ASSOCIATION" unaonyesha kwamba, kwa kipindi cha kati ya mwaka 2000/01 hadi 2008 fedha zilizotengwa na Serikali na zile zilizotolewa na hazina kwa ajili ya kilimo zilikuwa na upungufu wa kati ya asilimia 6 hadi 49?
Aidha, takwimu zinaonyesha kuwa mwaka wa fedha 2010/2011 fedha za ASDP, hazina ilitoa shilingi bilioni 107.1 kwa wizara zinazojihusisha na moja kwa moaja na programme hiyo, lakini zilizotumika ni shilingi bilioni 77.9 tu sawa na (72.8%) zilizobaki asilimia 27.2% hazijulikani zilitumika vipi[2].

e. Wigo wa hifadhi ya jamii
Mheshimiwa Spika, suala la hifadhi ya jamii ni jambo ambalo Serikali haliwezi kuliepuka. Dhana ya hifadhi ya jamii ni chombo kimojawapo cha kupambana na kupunguza umasikini katika jamii. Hivyo basi ni jukumu la nchi kuhakikisha hifadhi ya jamii inahusisha wananchi katika sekta rasmi na isiyo rasmi. Kwa hivi sasa watanzania wanaonufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii ni asilimia 6% tu ya Watanzania wote. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Mpango huu wa 2014/2015 ujumuishe yafuatayo;
· Upanuzi wa wigo wa mifuko ya Hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi hasa wakulima wadogo na ambao ni takribani asilimia 80 ya watanzania.
· Uimarishaji wa hifadhi ya Jamii kwa wakulima kwa kupitia vyama vyao vya ushirika ili waweze kujumuishwa katika mifuko ya hifadhi za jamii.
· Kuipitia upya na kuiboresha Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2008.
f. Pensheni kwa wazee
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali ya CCM kutimiza ahadi yake ya kutoa Pensheni kwa wazee kama ambavyo Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kilele cha siku ya Wazee duniani tarehe 1 Oktoba 2010 alipowaahidi wazee kupata pensheni yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaikumbusha Serikali ya CCM kuwa ni takribani miaka kumi imepita toka sera ya wazee itungwe mwaka 2003 hata hivyo utekelezaji wake chini ya Serikali inayoongozwa na CCM umekuwa ni wa kusuasua. Kwa kuwa Mpango huu ni wa mwaka 2014/2015, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa Pensheni ya Wazee inaingia katika maeneo ya Kipaumbele.

4. UGHARAMIAJI WA MPANGO
Mheshimiwa Spika, mpango wa maendeleo ya serikali wa mwaka 2014/2015 ni dira ya kuakisi mpango wa kibajeti kwa mwaka 2014/2015, na ili kuweza kutekeleza mpango kwa ufanisi ni dhahiri kuwepo kwa umuhimu wa kubainisha vyanzo vya mapato vya uhakika ambavyo vitawezesha kugharimia miradi ya maendeleo inayokusudiwa, kuna haja ya serikali sasa kutafakari kwa kina na kuona kazi kubwa inayofanywa na kambi rasmi ya upinzani bungeni kuishauri serikali juu ya uongezaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa kibajeti kila mwaka inaweza kuijengea heshma nchi yetu na pia kuboresha huduma kwa wananchi wake na si kwa kutegemea mapato ya nje ambayo yameendelea kuidhoofisha nchi yetu mbele ya uso wa dunia kwa kuwa taifa tegemezi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inapendekeza kukusanya mapato ya ndani 25% ya GDP ili kuweza kuendesha miradi yetu wenyewe. Uwezo wa makusanyo hadi kufikia hapo tunao, kwanza ni kupambana na makampuni makubwa ya kimataifa ili yalipe kodi stahiki na kuacha ujanja wa kukwepa kodi, kuondoa misamaha ya kodi na kuzuia upoteaji mapato ya ndani.
Ni dhahiri kuwa mapato ya ndani yaweza kutekeleza vipaumbele vyetu, ambavyo ni vifuatavyo ili kukabiliana na matatizo tuliyoainisha kuwa ni:
1) Utafutaji na ukusanyaji wa raslimali ikiwemo za wakwepaji kodi na watoroshaji wa fedha.
2) Ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kuwekeza kwa wakulima wadogo kwenye mashamba ya pamoja ie integrated production schemes. 3) Barabara, Maji na Umeme vijijini

Mheshimiwa Spika, katika miaka kadhaa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa nia njema ya kuijenga nchi yetu ilipendekeza mambo kadhaa ili kuweza kuongeza mapato ya serikali na moja ya mambo yaliyopendekezwa ni kuhakikisha kwamba serikali inakusanya kodi kwa kiwango cha asilimia 30 kama ‘ongezeko la mtaji' (‘capital gains') kutokana na mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania. Je, utekelezaji wa ushauri huo umefika wapi?

Mheshimiwa Spika, lakini pia kambi rasmi ya upinzani bungeni ilipendekeza kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa kama wenzetu wa Uganda na Kenya. Serikali ilikubaliana na pendekezo hili kwa maneno lakini imeshindwa kulitekeleza licha ya kutoa ahadi za kufanya hivyo kila mwaka. Hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia 4.3 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, pia kambi rasmi pia ilipendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwa kufuta sehemu ya Kodi ya Mapato inayotoa fursa kwa kampuni za madini kutumia sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 iliyofutwa (grandfathering). Pendekezo letu lilikuwa na lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation' ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini ufanya ‘100 percent depreciation' kwenye mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax'. Pendekezo hili ambalo lingeipatia Serikali mapato mengi na kwa sasa bado halijatekelezwa kwa Kampuni za madini zenye mikataba.

Mheshimiwa Spika, kupuuzwa kwa mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani kunatafsiriwa kuwa wanavyanzo vingi vya mapato vya kuweza kutekeleza matakwa ya mpango wake. Ukweli ni kuwa Serikali iko hoi bin taaban katika kukusanya mapato, na hili ni wazi kwani fedha za maendeleo zinategemea misaada na mikopo toka nje.
Mheshimiwa Spika, Tozo ya kodi ya matumizi ya simu za mkononi, pamoja na wabunge kupinga hatua ya serikali kutoza kodi hiyo kwa wananchi na serikali kukaidi kuiondoa kwa sababu zake binafsi, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaona kuna haja ya serikali kuwajibika kutoa huduma kwa raia wake na sio kuendelea kumnyonya mwananchi kwa kuweka kuwa ndio chanzo cha mapato ya serikali, hivyo kuacha mianya katika vyanzo vya uhakika hususani vile tunavyovipendekeza kwa maslahi ya wananchi na nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mpango umezungumzia swala la kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, kuna tafsiri mbalimbali za sekta binafsi kwanza inayozungumzwa katika mpango na nyingine inayozungumzwa na viongozi wa serikali, kumekuwepo na mjadala katika kukuza uchumi wa taifa katika Nyanja ya uwekezaji, viongozi wa serikali bila aibu wameendelea kuidhalilisha nchi na watu wake na kunadi wawekezaji wa nje, ni lazima sasa tujifunze kwa historia kama si ya nchi yetu juu ya kushindwa kwetu basi twende nje tuone walifanikiwa vipi, tumnukuu Mwanauchumi mmoja aliefanya kazi benki kuu ya dunia Joseph Stiglitz aliwahi kusema "On average, resource-rich countries have done even more poorly than countries without resources".

Mheshimiwa Spika, moja ya sababu kubwa kwa nchi zenye rasilimali asili kutonufaika nazo ni pamoja na uongozi mbovu na rushwa, tunaanza kupata shaka sasa juu ya mabishano ya sisi kwa sisi kama serikali na wananchi je yana tija gani kwa taifa? Kuna nini kwa wawekezaji wa nje hadi tuwapuuze wawekezaji wa ndani?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka Serikali tunapoelekea kutoa muongozo wa mpango na bajeti ya serikali ni vema kama nchi kuona umuhimu wa kukaa chini na kujadili kwa pamoja kama nchi na sio kuishi kwa imla kwa minajili ya kwamba nchi hii ni ya serikali na sio wananchi, kuna haja ya kuhitaji teknolojia kutoka nje lakini wawekezaji wa ndani wakilindwa na kupewa fursa ndio watajenga uwezo kiuwekezaji bali kupuzwa ni dalili za kuanza kushindwa kwa serikali na kufikia kutonufaika na rasilimali zetu kama nchi.


5. UTEKELEZAJI, UFUATILIAJI NA TATHMINI
Pamoja na kutaka majibu ya kina juu ya masuala yote tuliyoyahoji kwenye hotuba hii kuhusu utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/2013, 2013/2014 na mapendekezo ya 2014/2015; Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka maelezo mahususi kuhusu masuala yafuatayo:
· Sababu za kutokuwasilisha bungeni mpaka sasa muswada wa sheria mpya au wala kufanya marekebisho ya kisheria kuwezesha uwajibikaji katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inaboresha usimamizi wa utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini na ufanisi wa Tume ya Mipango. Serikali itekeleze ahadi zake ilizotoa bungeni mwaka 2011 na 2012.
· Sababu za kuanzisha Kitengo kingine cha utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini (Presidential Delivery Unit-PDU/PDB) na kukiweka chini ya ofisi ya Rais kama ilivyo pia kwa Tume ya Mipango; badala ya kuwa na sheria iliyotungwa na Bunge ya kuwezesha taifa kuwa na mfumo thabiti wa uwajibikaji katika kushughulikia udhaifu wa upangaji, utekelezaji na ufuatiliaji.
Sababu za kukwepo kuwasilisha Bungeni mikataba inayoelezwa kuingiwa chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now) wa Mawaziri husika kuwajibika pale wanaposhindwa kufikia malengo yaliyowekwa

6. HITIMISHO
Kwa kuangalia hali halisi ya utekelezwaji wa mipango ya miaka miwili iyopita ni dhahiri kwamba, kama nchi inatubidi kuanza kupanga upya "drawing board" . Hii inatatokana na hali halisi kuwa raslimali tunazotarajia kutekeleza mpango wetu tunatarajia zitoke kwa wahisani na pia kile tulichonacho tunashindwa kukitumia kwa mahitajio ya mpango.
Mheshimiwa Spika, nidhahiri kabisa lengo kuu la sehemu ya kwanza ya dira ya taifa ya mwaka 2025 hatujaweza na hatutaweza kuitimiza kutokana na hali halisi ya jinsi tunavyopanga na kutekeleza yale yaliyomo kwenye Mpango wa miaka mitano ambayo ni sehemu ya kwanza ya dira ya taifa ya 2025.
Mheshimiwa Spika, Mpango umeonyesha kila lengo na kiashiria chake cha mafanikio pamoja na bajeti yake ya jinsi ya kufikia lengo tajwa. Kwa bahati mbaya ni kwamba mambo hayo yamebaki katika maandishi na vitabu tu. Kambi Rasmi ya Upinzani ishawishika kuammini kwamba utekelezaji duni wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo hautokani na ukosefu wa rasilimali kama ambavyo Serikali imekuwa ikijitetea kila mara bali ni ukosefu wa uongozi madhubuti katika kusimamia rasilimali za nchi na kuzigawa ipasavyo katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo. Hivyo dawa ya kutibu tatizo hili ni mabadiliko ya Mfumo wa Utawala tu! Na ndio maana tunatoa wito kwa wananchi kuchagua Serikali itakayoongozwa na CHADEMA kumaliza malalamiko Serikali ya CCM yasiyo na msingi kwamba miradi inashindwa kutekelezwa kwa kuwa bajeti haitoshi. Wakati Serikali ya CCM inalalamika kuwa bajeti ni finyu, mafisadi wanatorosha fedha kwenda Uswisi na kwingineko hawashughulikiwi, Wakati ardhi yetu inaporwa na wageni Serikali inapuuzia azimio la bunge la kufanya tathmini ya ardhi, wakati tembo wa nchi hii wanakwisha kutokana na ujangili uliokithiri, Serikali inawakumbatia majangili hata wale ambao tayari wametajwa nk. Kwa jinsi hii tutaendelea je? Kwa vyovyote vile tunahitaji utawala mwingine unaojali maslahi ya taifa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.


………………………..
David Ernest Silinde (Mb)
K.n.y Msemaji Mkuu, Kambi Rasmi ya Upinzani –Wizara ya Fedha na Uchumi.
30.10.2013




[1] Hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb), akiwasilisha Bungeni Makadirio ya matumizi ya fedha kwa ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa mwaka 2011/12 Dodoma
4 JULAI,

[2] PELUM- Review and analysis of Agricultural sector budget trends and outcomes in Tanzania at National and Local govt levels (FY 2003/04-FY 2012/13)

 

Attachments

  • MPANGO - REFINED FINAL.doc
    115.5 KB · Views: 308
Wakati kipindi cha Bunge kikiendelea na mjadala wa maji na umeme jioni, ndipo Mbunge moja wa CCM aliposimama na kuonyesha jinsi watu wasivyo na huruma kwa kuwapiga wanyama risasi.
Ndipo aliposimama Kamanda LEMA NA KUHOJI HUYO MBUNGE KWA NINI ASIJIULIZE MBONA WATU WANAPIGWA RISASI HADHARANI NA POLISI NA AWAHOJI NA PIA WENGINE KUBAMBIKIZIWA KESI NA HAKUNA ANAEHOJI.

Pia Mbunge huyo amezungumzia kukauka na kutoweka kwa ziwa Manyara kuwa ita hathiri shughuli za utalii nchini.
 
ndo kama hivyo, CCM washangae wanyama kupigwa risasi, CHADEMA washangae raia kupigwa risasi, Pinda katoa amri.
 
Ukiwa mwongo usiwe msahaulifu....soma kipengele na 4 cha hotuba ya upinzani
 
Back
Top Bottom