Hotuba ya bajeti kambi ya upinzani mambo ya nje 2019/2020

issenye

JF-Expert Member
Feb 2, 2011
3,781
5,205
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHESHIMIWA ESTHER NICHOLAS MATIKO (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020

A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko (Mb) nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili yake, kwa kuendelea kumlinda na kumtia nguvu na ujasiri wa kukabiliana na dhoruba mbalimbali za kisiasa zinazomkabili ikiwa ni pamoja na kuwekwa gerezani kwa zaidi ya siku mia moja bila kutiwa hatiani.

2. Mheshimiwa Spika, pili napenda kuwashukuru na kuwapongeza sana wabunge wote wa upinzani na viongozi wote wa CHADEMA kwa ujasiri wao wa kuendelea kuchapa kazi bila woga licha ya mazingira magumu ya kufanya siasa hapa nchini. Aidha, nawatia moyo wale wote waliokamatwa na kuwekwa kizuizini magerezani; walioumizwa na kujeruhiwa kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki shughuli za kisiasa. Napenda kuwaambia wasikate tamaa kwani mateso wanayoyapata ni kielelezo cha ukombozi wa watanzania walio wengi.

3. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia wasaa huu kuishukuru sana na kuipongeza Jumuiya ya Kimataifa na hususan Umoja wa Ulaya na Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwa kuendelea bila kuchoka kupaza sauti dhidi ya vitendo viovu vya ukandamiziaji wa demokrasia na haki za binadamu na dhidi ya vitendo vyenye sura ya ugaidi vya utekaji, utesaji, majaribio ya mauaji, na mauaji ya viongozi wa kisiasa hasa wa vyama vya upinzani katika mataifa mbalimbali duniani. Mungu atawalipa kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuhakikisha kwamba uhai na uhuru na utu wa mwanadamu vinalindwa na kuheshimiwa duniani kote.

4. Mheshimiwa Spika, leo tunajadili uhusiano wa kimataifa tukiwa katika zama mpya za utandawazi na soko huria ambapo nguvu ya soko ndiyo inayoendesha uchumi na kuamua mustakabali wa nguvu za madola mbalimbali duniani. Kwa maneno mengine, nguvu za kiuchumi ndizo zinazolipa taifa nafasi ya kuheshimiwa na kuthaminiwa miongoni mwa mataifa mengine. Pamoja na uchumi wa soko huru; utawala wa sheria unaoheshimu haki za binadamu na demokrasia ya kweli ni nguzo muhimu za utandawazi ambako ndiko ulimwengu ulipo sasa, ndiko unakoendelea kuwa na ndiko utakakokuwa.

5. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia vigezo vya kuheshimika kimataifa, Serikali hii ya CCM haina kigezo hata kimoja cha kulifanya taifa liheshimike. Kwanza kwa kigezo cha uchumi peke yake, Serikali imeshindwa kuheshimu kanuni za soko huru na badala yeke Serikali ndiyo inayodhibiti uchumi badala ya soko (mfano mzuri ni Serikali kuingilia biashara ya korosho). Matokeo yake uchumi umeshuka kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na mpaka sasa Serikali inahangaika kuficha ukweli wa ripoti hiyo ya IMF ili uchumi uonekane kuwa ni mkubwa.

6. Mheshimiwa Spika, kuhusu utawala wa sheria, haki za binadamu na demokrasia; Serikali hii ya awamu ya tano ndio imetia fora kwa utawala usiozingatia sheria, kukanyaga katiba na haki za bidamu na demokrasia ndio iko hoi – ICU. Na ushahidi wa jambo hili, ni Tanzania kunyimwa misaada mingi ya kibajeti na jumuiya ya Kimataifa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uminyaji wa demokrasia .

7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inatoa changamoto kwa Serikali hii ya CCM; iliambie Taifa, ni kitu gani cha kutolea mfano ilichokifanya au inachokifanya ambacho kimeipandisha hadhi nchi yetu katika medani za kimataifa?

B. TANZANIA IMEKUWA NA KIGUGUMIZI CHA KURIDHIA MKATABA WA MAKUBALIANO YA ENEO HURU LA BIASHARA BARANI AFRIKA

8. Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 21/03/2019 Jijini Kigali Rwanda, viongozi wakuu wa nchi za Kiafrika na wale walioziwakilisha nchi zao walitia sahihi makubaliano ya kuanzishwa eneo huru la kibiashara barani Afrika. (African Continental Free Trade Area - AfCFTA). Lengo la makubaliano hayo ni kuondoa vikwazo vya biashara baina na miongoni mwa nchi za Afrika na hivyo kuongeza kiwango cha biashara ndani ya bara hili.

9. Mheshimiwa Spika, Eneo huru la kibiashara Afrika linakuja wakati kiwango cha biashara miongoni mwa nchi za Afrika kikiwa ni cha chini kabisa cha asilimia 15.4 ukilinganisha na mabara mengine. Aidha, inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2022, chini ya mkataba huu, biashara baina ya nchi za kiafrika zitaongezeka hadi kufikia asilimia 52 tofauti na asilimia 15.4 ya sasa.

10. Mheshimiwa Spika, Mpaka sasa nchi 23 ikiwemo Zimbabwe iliyoridhia hivi majuzi tarehe 25 Mei, 2019; zimesaini mkataba huo na mabunge ya nchi hizo pia yameshapitisha azimio la kuridhia mkataba huo na kwa maana hiyo soko huru litaanza kufanya kazi mwezi Julai 2019. Kwa upande wa Afrika Mashariki, nchi za Kenya, Rwanda na Uganda tayari zimeshakamilisha hatua zote.

11. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa serikali inajinasibu kutekeleza diplomasia ya uchumi na kwa kuwa AfCFTA ni fursa nyingine ya kuinua kiwango cha kibiashara ndani ya Afrika hasa kwa mataifa yanayojipanga kimkakati, ni jambo lisiloelezeka kuona mpaka sasa Tanzania imekumbwa na kigugumizi kikubwa juu ya makubaliano haya na hivyo kutowasilisha bungeni kuridhiwa na hatimaye kuwasilisha nyezo za utekelezaji wake kwa Kamishna wa Umoja wa Afrika.

12. Mheshimiwa Spika, Kwa taifa makini, mkataba huu ni hitaji la muda mrefu ambalo ni fursa kwa uchumi wa taifa hili kukua kwa kasi na kusaidia kupunguza kiwango cha umasikini. Kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza uchumi; Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia Chadema imeeleza bayana katika Sera yake ya Mambo ya Nje Sura ya 12.1 kuhusu namna ambavyo uhusiano wa kimataifa utatumika kujenga diplomasia ya uchumi. Sera hiyo inatamka kama ifuatavyo; “Chadema itaweka sera ya mambo ya nje ambayo itazingatia masuala ya uchumi, ulinzi, diplomasia na masuala mengine muhimu katika uhusiano wa kimataifa. Balozi za Tanzania zitakuwa na jukumu la kufanya diplomasia ya uchumi kwa kuwavutia wawekezaji na mitaji kutoka nje bila kuathiri ulinzi na maslahi ya nchi”.

13. Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba, AfCTA ni nyenzo muhimu ya kukuza mahusiano yetu na mataifa mengine barani Afrika hasa yale ambayo sio ya EAC na SADC ambamo sisi ni wanachama. Aidha, tunaona kwamba AfCFTA ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa watanzania na taifa letu kwa ujumla kwani inatoa fursa kwa watu wetu kufanya biashara kwa urahisi zaidi na wenzao Afrika.

14. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba kuendelea kuchelewa kwa Serikali kuleta mkataba huo ili uridhiwe na Bunge, ni kuendelea kuchelewa kuchangamkia fursa za biashara jambo ambalo halina afya kwa maendeleo ya uchumi wetu na kunakwenda kinyume na azma ya Serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni lini italeta mkataba huo ili uridhiwe na Bunge.

C. SERIKALI KUINGIA MKATABA NA KAMPUNI HEWA KUTOKA NJE KUNUNUA KOROSHO NA KUWASABABISHIA WAKULIMA WA KOROSHO HASARA KUBWA

15. Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 30 Januari, 2018, Serikali ya Tanzania iliingia mkataba na Kampuni ya Indo Power Solutions ya Kenya kununua korosho za wakulima wa mikoa ya kusini ambayo mpaka sasa inaonekana kudoda kwa kukosa soko. Taarifa za baadae za kiuchunguzi zilizofanywa na gazeti la Daily Nation la Kenya zilibaini kuwa kampuni hiyo ni hewa na haina hata ofisi nchini Kenya. Matokeo ya uzembe wa Serikali wa kuingia Mkataba na Kampuni ya Nje bila kuifanyia upekuzi – yaani due diligence ni kwamba mpaka sasa hakuna korosho yoyote iliyonunuliwa, jambo ambalo limeisababishia Serikali hasara kubwa.

16. Mheshimiwa Spika, Kitendo cha serikali kuingia mka taba na kampuni hewa kutoka nje kinadhihirisha yafuatayo;

i. Kwamba, balozi zetu nje ya nchi hazina kazi za kufanya hasa katika utekelezaji wa hicho kinachoitwa diplomasia ya uchumi kwani kama zingekuwa zinafanya kazi yake ipasavyo, ubalozi wa Tanzania nchini Kenya ungekuwa na taarifa zote muhimu kuhusu kampuni ya Indo Power Solutions na kuishauri serikali ipasavyo kuingia ama kutokuingia makubaliono na kampuni hiyo

ii. Na kwamba, balozi zetu nje ya nchi chini ya serikali ya CCM hazina weledi wala ufanisi kutokana na kutoelewa majukumu yao ipasavyo. Hii inatokana na ukweli kwamba uteuzi wao hauzingatii taaluma na weledi, bali mihemuko ya kisiasa ambayo ina madhara makubwa kwa taifa kama ilivyotokea kwa Indo Power Solution.

17. Mheshimiwa Spika, katika sakata hili la korosho ambalo linaakisi uhujumu uchumi wa taifa, kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa ufafanuzi juu ya mambo yafuatayo;

i. Nini ilikuwa wajibu wa ubalozi wa Tanzania Kenya katika mkataba wa Indo Power na Tanzania

ii. Ni kwanini mpaka leo pamoja na hasara kubwa iliyotokea Waziri wa mambo ya Nje, Balozi wa Tanzania nchini Kenya pamoja na maafisa wake wanaendelea na nyadhifa zao?

iii. Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua na kuwaburuza mahakamani wale wote waliohusika na mkataba feki wa Indo Power katika sakata la Korosho Nchini.

iv. Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha zao la Korosho nchini linaendelea kubaki kwenye mzunguko wa kimataifa.

18. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kuwa balozi nyingi za Tanzania kwenye nchi mbali mbali zina changamoto ya rasilimali watu wa kutosha. Lakini ufinyu wa rasilimali watu hauondoi uwajibikaji wa hao wachache waliopo. Kwa maneno mengine hata kama watendaji ni wachache haiwezi kuwa sababu ya kuruhusu nchi kuingia kwenye mikataba ya hovyo na ya aibu ya namna hii.

19. Mheshimiwa Spika, sakata hili la kuingia mkataba hewa ni kielelezo kingine cha udhaifu mkubwa wa serikali kwenye mahusiano yake na mataifa mengine hasa majirani zetu. Hata kama ubalozi wetu ulishindwa kufanya utafiti wa kina na kupata taarifa za ndani za kampuni ya Indo Power Solutions, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda bado ilikuwa na wajibu wa kuwasiliana na wenzao wa Kenya ili kujua kwa kina watu wanaoingia nao mkataba. Lakini kutokana na mahusiano baridi yaliyopo kati ya Kenya na Tanzania hasa kwenye mizania ya biashara, suala hili halikufanyika.

20. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mamlaka zilizokuwa na wajibu wa kuishauri Serikali kuingia mkataba huo hazikutimiza wajibu wao ipasavyo na hivyo kuifanya Serikali kuingia mkataba hewa ulioisababishia Serikali hasara; na kwa kuwa suala hili lina sura ya uhujumu uchumi; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali, mosi, kuwaondoa katika nyadhfa zao wale wote waliokuwa na wajibu wa kuishauri Serikali kusaini mkataba huo ikiwa ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

D. SIASA ZA NDANI NA TASWIRA YA NCHI KIMATAIFA

21. Mheshimiwa Spika, Tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015, kumekuwepo na ongezeko kubwa la ukiukwaji wa haki za binadamu, uminywaji wa demokrasia na uvunjwaji wa sheria mbali mbali tulizojiwekea wenyewe kama Taifa.

22. Mheshimdiwa Spika,Matukio ya utekwaji wa watu mbali mbali hasa wanaonekana kuikosoa serikali, kupotezwa kwa watu pasi na hatua madhubuti kuchuliwa na vyombo vya dola, majaribio ya kuuwawa kwa viongozi wa kisiasa na kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari ni mambo ambayo yanaichafua Tanzania kwenye ulimwengu wa kimataifa. Kwa kipindi hiki, Serikali ya Tanzania imegonga vichwa vya habari kimataifa si kwa uzuri wala ukarimu wake kama ilivyokua imezoeleka, bali kwa ukatili dhidi ya raia wake.

23. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya haki za binadamu ya State Department ya Marekani kwa mwaka 2018 inaonyesha hali ya hatari kwa Tanzania kwa kubainisha matukio ya mauaji, kutekwa na kupotezwa kwa watu, uvunjifu mkubwa wa sheria na katiba ya nchi pamoja na ukandamizwaji mkubwa wa vyama vya upinzani. Hali hii pia inashajihishwa na ripoti ya Freedom House kwa Tanzania kwa mwaka 2018.

24. Mheshimiwa Spika,Mambo haya sio tu yameichafua na yanaendelea kuichafua Tanzania bali yana athari za moja kwa moja taifa kama ifuatavyo:

i. Kudorora kwa Shughuli za Kiuchumi

25. Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kiwango kikubwa unategemea na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (Foreign Direct Investiment). Taarifa ambazo ziko kwenye ripoti ya IMF zinaashria kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kutoka 7.1% mwaka 2016 hadi asiliia 4 % mwaka 2018/19. Hii maana yake ni kwamba kumekuwepo na kuzorota kwa shughuli za uzalishaji nchini zinazotokana kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa makampuni ya nje.

26. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo huo, taarifa ya UNCTAD (United Nations Conference on Trade and Development) ya Uwekezaji Duniani ya mwaka 2018 inaonyesha kwamba kuna anguko la asilimia 14 la kiwango cha uwekezaji kwa Tanzania. Anguko hili ni kielelezo cha kwamba wawekezaji wanaikimbia Tanzania kutokana na mambo ya hovyo yasio ya kibinadamu yanatokea chini ya utawala huu pasi na hatua madhubuti kuchukuliwa na zikaonekana kweli zinachukuliwa.

27. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatafsiri kuporomoka kwa kiwango cha mitaji ya uwekezaji kutoka nje (Foreign Direct Investments) nchini kama kielelezo cha Serikali hii ya CCM ya awamu ya tano kushindwa kutelekeza kwa vitendo Diplomasia ya uchumi.

28. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba, kukimbia huku kwa wawekezaji kunatokana, pamoja na mambo mengine, vitendo viovu wanavyofanyiwa raia wa Tanzania na watu ambao mpaka leo serikali ni ama serikali inawajua na haitaki kuwachukulia hatua ama haina uwezo wa kuwabaini na kuwachukulia hatua na hivyo kutishia usalama mpana wa raia na mali zao. Aidha, maelezo ya kijichanganya yanayotolewa na vyombo vya dola dhidi ya matendo haya yanaongeza hofu zaidi kwa raia yoyote nchini kuishi kwa amani na kufanya kazi zake kwa utulivu. Kwa mazingira haya hakuna mwekezaji makini atakayetekeleza mitaji yake kuwekeza sehemu ambapo serikali inashindwa kutoa uhakika wa usalama kwa raia.

29. Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Shiriki la Bartelsmann ya ukanda wa Afrika yenye kichwa cha habari “A Divided Content” ya mwaka 2018 inataja uchumi wa Tanzania kuanza kusinyaa kuanzia mwaka 2016. Ripoti hiyo inabainisha kwamba kusinyaa huku kunatokana na maamuzi juu ya uchumi yanayotokana na mihemko na sifa za kisiasa kuliko uhalisia (Populism). Ripoti hiyo inaweka bayana kuwa mambo haya yameshusha morali ya wawekezaji kutoka nje na uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa.

30. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya ripoti hiyo inasema kwamba; naomba kunukuu… “in a small but significant number of states including Tanzania and Zambia, this was compounded by the emergence of populist leaders who sought to intervene in the economy for political as much as economic goals, undermining investor confidence. One consequence of these changes has been the failure to effectively harness potential international support”

31. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuiarifu Serikali hii ya CCM, kama ilikua haijui na ijue sasa, kwamba; kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa sera ya nje ya nchi yoyote duniani, kunatokana na jinsi nchi hiyo inavyoendesha siasa zake za ndani. Siasa za ndani zina athari ya moja kwa moja na mahusiano ya nchi na jumuiya ya kimataifa.

32. Mheshimiwa Spika, tunaikumbusha pia Serikali kuwa, suala la usalama wa ndani kwa upana wake ni kichocheo kikuu cha kuvutia wawekezaji kutoka nje. Ni kwa maana hii Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza katika Diplomasia ya Uchumi na Usalama na si vinginevyo. Usalama unatokana pamoja na mambo mengine kuheshimu utawala wa sheria, haki za msingi za binadamu na misingi madhubuti ya demokrasia tofauti na ilivyo sasa.

ii. Kudorora kwa Mahusiano baina ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa

33. Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa matendo ya utekaji wa raia, kupotezwa kwa watu bila maelezo yanayoeleweka ya serikali, majaribio ya kuua bila wauaji kutiwa nguvuni, kuonewa na kukandamizwa kwa vyama vya upinzani nchini kumepelekea wadau mbali mbali wa kimataifa kupaza sauti zao kukemea matendo haya. Hata hivyo serikali imewaona wadau hawa kama maadui wa taifa na hivyo kuweka mbinyo juu yao. Hili linadhihirishwa na mahusiano mabovu yaliyoko kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya ambayo imekiri kuwa ilimwita balozi wake kurudi Ubelgiji kutokana na shinikizo la serikali ya Tanzania juu yake.

34. Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Jumuiya ya Ulaya ambayo imekua mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania katika sekta mbali mbali haina balozi wake nchini na kwamba jumuiya hii inapitia upya mahusiano yake na Tanzania. Kutikisika kwa mahusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya hakuwaathiri viongozi wa CCM bali wananchi wanaonufaika na misaada ya Jumuiya hii katika maeneo mbali mbali.

35. Mheshimiwa Spika, uthibitisho wa mdororo wa mahusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni tamko lililotolewa na Makamu wa Kamisheni ya EU anayeshughulikia mambo ya nje na masuala ya sera ya ulinzi, Federica Mogherini la tarehe 15/11/2018.

36. Mheshimiwa Spika, sehemu ya tamko hilo inasema hivi: “In this context, the Tanzanian authorities have consistently increased their pressure on the EU Ambassador. This eventually led to his forced departure and recall for consultations. This unprecedented attitude is not in line with the long established tradition of bilateral dialogue and consultation between the two parties, which the EU deeply regrets. The EU calls on Tanzanian authorities to refrain from exerting undue pressure and limitations on diplomatic missions”. Tamko hili linaonyesha sio tu EU waliokuwa na shinikizo la serikali bali balozi mbalimbali.

37. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kuelewa kwamba hakuna Serikali duniani inayoweza kufanikiwa bila kuwa na mahusiano na mataifa mengine. Ni bahati mbaya sana kwamba, Serikali ya awamu ya tano inagombana mpaka na wahisani wanaoipatia misaada ya kibajeti.

38. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na taifa, ni kwa nini ilimuwekea shinikizo balozi wa Umoja wa Ulaya nchini hata kupelekea kuondoka kwake? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa pia kujua ni kwa nini serikali hii ya awamu ya tano imeanza kuwa na tabia ya kuziingilia na kiziwekea mashinikizo balozi zinazoziwakilisha nchi zao katika utendaji wao wa kazi ikiwa haziendi kinyume na Mkataba wa Vienna? Hata kama serikali inaona balozi hizo zimekua zikikiuka Mkataba wa Vienna katika utendaji wao wa kazi Bunge na Taifa linapaswa kuelezwa ni mambo gani hayo balozi hizo zimekua zikifanya mpaka kustahili mashinikizo

E. KANZI DATA YA WATANZANIA WAISHIO NJE YA NCHI (DIASPORA DATABASE)

39. Mheshimiwa Spika, Dunia sasa inatambua mchango mkubwa wa uchangiaji uchumi unaofanywa na watu mbalimbali wanaoishi nje ya nchi zao (yaani Diaspora). Hatuna budi kama Watanzania kuendelea kutabua na kuthamini mchango huu mkubwa unaofanywa na kaka na dada zetu wanaoishi nje ya nchi kwani uwepo wao huko unachangia kukuza jina la nchi yetu na kuboresha mahusiano na nchi hizo.

40. Mheshimiwa Spika, hakuna takwimu za kitaifa zinazoonyesha idadi kamili ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi na taarifa za kile wanachokifanya huko. Umuhimu wa kuwa na taarifa ni kubaini kwa wepesi idadi na aina ya watu wenye ujuzi na uzoefu ambao serikali inaweza kuutumia kwa maslahi ya nchi. Aidha, kujua idadi ya wananchi walio nje ya nchi kutapelekea kutengeneza milango ya kiuchumi kati yao na nchi (economic gateway),kutafungua fursa za kibiashara ikiwa ni pamoja na soko la nje (export market) kwa bidhaa zetu za Kitanzania na hivyo kutaachia fursa kwa soko la ndani kuboresha bidhaa zao ili ziweze kupata masoko nje.

41. Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa data base hiyo pia yenye kila Mtanzania aliyepo nje ya nchi kutasaidia kupunguza idadi ya raia wa nchi nyingine wanaotumia jina la nchi yetu vibaya huko nje ya nchi kwa kujifanya ni wakimbizi kutokea Tanzania. Tutaweza kuwatambua na kuwabaini kwa kutumia balozi zetu.

42. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuhakikisha kuwa jambo hili la kutengeneza database linazingatiwa kwa uzito wake kwa kuwa lina manufaa kwa wananchi wetu walio katika kila pembe ya dunia na pia manufaa kwa ya uchumi wa nchi yetu.

43. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza uwepo wa kanzi data hiyo kwa kuwa Diaspora ina mchango muhimu katika kukuza uchumi wetu. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, Watanzania waishio nje (Diaspora) waliochangia 0.8% ya GDP yetu kwa kutuma kiasi cha dola za kimarekani milioni 430 kwa mwaka 2018. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kwamba, ni muhimu kuwa na takwimu za watanzania washio nje sambamba na shughuli wanazofanya ili iwe rahisi kufanya makisio ya fedha zitakazopatikana (diaspora remittance) na kuziingiza kwenye bajeti ya Serikali.

44. Mheshimiwa Spika, utengenezaji wa kanzi data hiyo uende sanjari na kutungwa kwa sera na sheria mpya itakayoruhusu watanzania kuwa na haki ya uraia pacha, ambao utamwezesha mtanzania aishiye nje kuwekeza kwa uhuru nje ya nchi na hapa nyumbani Tanzania. Kumzuia mtanzania anayeishi nje kuwa na uraia pacha ni kumwekea shinikizo la kutowekeza kikamilifu nje kwa kuwa anaishi kule kama mgeni na kwa sababu hiyo mchango wake wa fedha (remittance) hapa nchini utakuwa pia wa mashaka kutokana na kutokuwa na uhuru wa uwekezaji mkubwa nje.

45. Mheshimiwa Spika, suala la uraia pacha kwa dunia ya leo ni fursa. Kimkakati, uraia pacha ni kichocheo cha maendeleo kwa taifa. Mathalani, kwa majirani zetu Kenya wenye uraia pacha, diaspora yao imechangia kiasi cha dola za kimarekani milioni 2,720 kwa mwaka 2018 sawa na asilimia 3 ya Pato lao la Taifa(GDP). Hii ni kutokana na Wakenya wenye uraia wa nchi nyingine kuwa na (confidence) ya kuwekeza nyumbani bila bugudha ya aina yoyote.

46. Mheshimiwa Spika, umuhimu wa uraia pacha kwa Watanzania na wasio Watanzaia hauko tu kwenye michango ya kifedha bali upatikanaji wa ujuzi na maarifa(skills) mbali mbali kutoka kwenye mataifa mengine ambazo ni vigumu kupatikana Tanzania kwa mazingira yake.

47. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa uraia pacha katika kukuza diplomasia ya uchumi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia CHADEMA, inakusudia kuanzisha sera na sheria ya kuruhusu uraia pacha pindi ikipewa ridhaa na wananchi ya kuendesha Serikali. Sera ya Chadema ya Mambo ya Nje, Sura ya 12.3 inasema hivi: “Chadema itaanzisha sera na kutunga sheria ya kuruhusu uraia pacha ikiwa ni pamoja na kuwahimiza Watanzania wanaoishi nchi za nje kuwekeza Tanzania. Aidha, itaweka utaratibu wa hati fungani ambazo zitaongeza hifadhi ya fedha za kigeni nchini”.

F. MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA KUPINGA UBEBERU NA UKOLONI, NA UONEVU DUNIANI

48. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekuwa na historia iliyotukuka duniani, ya kuwa mstari wa mbele kupinga aina zote za uonevu, unyonyaji na utumwa hususani ubeberu na ukoloni. Kutokana na tunu yake ya kujali utu na usawa miongoni mwa binadamu wote, Tanzania ya enzi za Mwalimu Nyerere, ilifikia hatua ya kujitoa kupigana vita vya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, ili kuhakikisha kwamba ubeberu na ukoloni katika nchi hizo unatokomezwa na uhuru wa kweli unapatikana.

49. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kwamba Tanzania ndiyo iliyokuwa mwasisi wa nchi za Mstari wa Mbele chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere katika miaka ya 1960 kwa lengo la kupinga ubaguzi wa rangi na utawala wa wazungu wachache katika nchi za kusini mwa Afrika.

50. Mheshimiwa Spika, Tanzania ilienda mbele zaidi hadi kufikia hatua ya kuvunja mahusiano yake ya kidiplomasia na mataifa mengine yaliyokuwa na tabia za ubaguzi wa rangi, unyonyaji, ubeberu na ukoloni dhidi ya mataifa mengine. Itakumbukwa kwamba Tanzania ilivunja ushirikiano wake wa kidiplomasia na Israeli kutokana na Israeli kuwa na tabia za kibeberu za kutaka kuikalia ardhi ya Palestina kwa nguvu. Aidha, Tanzania ilivunja mahusiano yake ya kidiplomasia na Morocco, kutokana na nchi hiyo kuikalia Sahara Magharibi kwa nguvu.

51. Mheshimiwa Spika, Tanzania ilipinga pia utawala wa ki-dikteta miongoni mwa nchi za Afrika, kwa kuwa udikteta ulikuwa na tabia zote za unyonyaji, ubaguzi, uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu – mambo ambayo Watanzania hawakuamini katika hayo - na ndio maana Tanzania kwa wakati huo, haikumuunga mkono Mobutu Seseseko wa iliyokuwa Zaire – sasa Kongo DRC, haikumuunga mkono Muamar Gadafi wa Libya na pia ilimng’oa madarakani dikteta wa Uganda Idd Amin Dadah.

52. Mheshimiwa Spika, siku za hivi karibuni tumeshuhudia nchi yetu ikuhuisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi nilizozitaja, ambazo hapo awali tulikuwa hatuna mahusiano nazo kutokana na kukalia mataifa mengine kimabavu au kufanya uonevu dhidi ya mataifa mengine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ni sababu zipi zimepelekea Tanzania kubadili msimamo wake, kuhusu ushirikano na mataifa hayo?. Je, Morocco imeacha kuikalia kimabavu nchi ya Sahara Magharibi? Na Je, Israeli imeacha kuionea Palestina? Na kama Serikali imebadili msimamo wa nchi kuhusu ushirikiano na mataifa hayo, Je, mabadiliko hayo ya msimamo wa nchi, yaliridhiwa na Bunge hili?

53. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua pia, ni nini msimamo wetu kama Taifa, juu ya tabia za kidikteta, ukiukwaji wa haki za binadamu, unyanyasaji na uonevu zinazoanza kuibuka na kujionyesha wazi miongoni mwa baadhi viongozi wa mataifa mbali mbali duniani ?

G. BREXIT NA ATHARI ZAKE KWA TANZANIA

54. Mheshimiwa Spika, Tanzania haijajiandaa kukabiliana na Brexit. Inafahamika kuwa Tanzania ni mshirika wa kibiashara na EU na pia imekuwa na mahusiano ya Karibu na Muda mrefu na UK ambayo wananchi wake walipopiga Kura za maoni waliamua kuwa nchi Yao ijitoe kwenye Umoja wa Ulaya. Hali hii imeifanya nchi ya Uingereza kuanza harakati za kutafuta nchi washirika na hasa zilizowahi kuwa makoloni yake ili kuwafanya washirika wake endapo watajitoa EU.

55. Mheshimiwa Spika, katika hilo Tanzania haijaonyesha kwa uwazi kuwa itakuwa upande upi hasa ikizingatiwa kuwa hatujasaini mkataba wa kibiashara na EU maarufu kama (EPA) ambao nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)wameonyesha wazi kuwa watasaini na kuiacha Tanzania na Burundi nje ya mkataba huo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge kuhusu msimamo wake wa wazi juu ya Brexit.

56. Mheshimiwa Spika, Sambamba na hilo kumekuwa na mdororo wa kidplomasia Baina ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya (EU) hasa kutokana na kitendo cha Serikali ya Tanzania 'kumtimua' nchini aliyekuwa Balozi wa Umoja huo mwaka 2018 na EU wakaamua kutokumteua mtu mwingine kuja kuwawakilisha nchini. Kitendo hiki ni dalili za wazi kuwa mvutano ni mkubwa na Serikali haikuwahi kutoa kauli hadharani jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa minong'ono mingi mitaani. Tunaitaka Serikali iweke wazi msimamo wake kuhusu mahusiano ya kidplomasia Baina yake na Umoja wa Ulaya na hasa sababu zilizopelekea kuondolewa kwa Balozi wa Umoja huo nchini mwishoni mwa mwaka 2018.

H. TISHIO LA KUSAMBARATIKA KWA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI - EAC

57. Mheshimiwa Spika, Nchi ya Tanzania haijaonesha kwa vitendo wala kisera nia thabiti ya Kuunga mkono na kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, mfano, sera ya Elimu haisisitizi kuimba wala kufundisha wimbo wa Afrika Mashariki na pia Ofisi na taasisi mbalimbali za Serikali hazipeperushi Bendera ya EAC kama ilivyo kwa nchi zingine wanachama.

58. Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki iko hatarini kusambaratika, kufuatia mahusiano yenye mashaka baina ya nchi wanachama wanaounda umoja huo. Kwa mfano zipo taarifa na pia vipo vitendo vya wazi vinavyoashiria kwamba mahusiano baina ya Tanzania na Kenya yanaporomoka kwa kasi jambo ambalo halina afya katika uendelevu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona iibue jambo hili kwa kuwa kuvunjika kwa ile Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya kwanza mwaka 1967 kulisababishwa na mahusiano baridi kati ya Tanzania na Uganda.

59. Mheshimiwa Spika, katika mdororo wa sasa wa mahusiano kati ya nchi yetu na Kenya ni kwamba, kumekuwa na ubaguzi kwa upande wa Tanzania ambapo wananchi wa Kenya wanaoingia Tanzania wamekuwa wakitakiwa kulipia visa za kuingia Tanzania pindi wanapofika kwenye vituo vya uhamiaji na wamekuwa wakitakiwa kulipia dola 100 za Kimarekani, tofauti na watanzania wanapoingia Kenya hawadaiwi visa Kwani wenzetu wanaheshimu itifaki tuliosaini wa 'free movement' na biashara ya pamoja.

60. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe maelezo bungeni ni kwanini sisi tunawadai visa wananchi wa Kenya ilihali wanaotokea nchi za SADC wanaingia bure tena kwa kutumia vitambulisho vyao vya Taifa na sio Visa? Serikali haioni kuwa kufanya hivyo, kunaharibu utengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

61. Mheshimiwa Spika, Sambamba na hilo, mazingira ya biashara mipakani yamekuwa mabaya sana ambako bidhaa kutoka Kenya zimeshuhudiwa kuharibiwa kama ilivyofanyika kwa vifaranga vya kuku katika mpaka wa Namanga kinyume na sheria za haki za wanyama ya 2008 na pia kinyume na azma ya kudumisha udugu na ujirani mwema.

61. Mheshimiwa Spika, matarajio ya wengi ni kwamba, Tanzania ingechukua nafasi ya uongozi katika kuzilea nchi nyingine washirika katika kuikuza na kuiendeleza Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka na uzoefu wake na pia historia yake iliyotukuka ya kuwa na amani, na kujenga taifa moja lenye mshikamano; lakini tofauti na matarajio hayo, Tanzania inaonekana kuwa chanzo cha mafarakano badala ya kuwa kiini cha muungano. Wachambuzi wanasema kuwa “Tanzania has become the centre of disintegration instead of fostering deep integration among the EAC member states”.

62. Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la msingi la mahusiano baina ya nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mfano, mahusiano baridi baina ya Uganda na Rwanda na Burundi na Rwanda, jambo ambalo ni tishio la kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama matatizo hayo hayatashughulikiwa mapema. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili na Taifa kwa jumla ni hatua gani za kidiplomasia zimechukuliwa hadi sasa kusuluhisha mivutano baina ya nchi wanachama zenye migogoro? Katika hatua hizo, Tanzania ambayo imekuwa nembo ya amani na msuluhishi wa migogoro katika ukanda wa maziwa makuu imefanya nini mpaka sasa ili kuhakikisha kwamba nchi wanachama zinashirikiana kwa upendo na amani ili kuiimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki?

I. UNYANYAPAA DHIDI YA WAANGALIZI WA KIMATAIFA WA UCHAGUZI MKUU WA 2020

63. Mheshimiwa Spika, ni utaratibu wa kimataifa kuwa na waangalizi wa kimataifa wa chaguzi katika nchi nyingine kwa lengo la kuhakikisha kuwa chaguzi zinakuwa huru na za haki. Pamoja na uhalisia huo, na licha ya nchi yetu kufanya hivyo mara nyingi, safari hii kuna dalili za wazi za Serikali hii ya CCM kupitia Tume Taifa ya Uchaguzi, kutowaalika waangalizi hao kuja kutazama mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

64. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa UNDP ambao wamekuwa washirika wakubwa wa Tume ya Uchaguzi hawajapelekewa mialiko rasmi kama ilivyo utaratibu ili waweze kujipanga kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kushiriki kama waangalizi wa kimataifa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

65. Mheshimiwa Spika, Jambo hili linaonyesha wazi kuwa Serikali haitaki waangalizi hao kwani pamoja na mashirika na mataifa hayo kuikumbusha Tume ya Uchaguzi kuhusiana na mwaliko rasmi hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa tume kuwaalika kama ilivyo utamaduni wa miaka mingi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iseme wazi kuhusiana na jambo hili na itoe sababu za kwanini imeamua kufanya hivyo au ndio maandalizi ya bao la mkono?

66. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua niwaangalizi gani wa kimataifa ambao wameshapewa mialiko rasmi mpaka sasa kwa ajili ya kushuhudia uchaguzi mkuu ujao. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Jumuiya ya Kimataifa kutonyamaza au kukaa pembeni kusubiri mwaliko kwani kufanya hivyo ni kukubaliana na chaguzi ambazo sio huru na zenye mizengwe.

J. KUNA DALILI ZA UBAGUZI WA ITIKADI ZA KISIASA KATIKA UBALOZI MBALI MBALI HUSUSAN UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA

67. Mheshimiwa Spika, licha ya mabalozi wetu nje ya nchi ni makada wa chama cha mapinduzi waliotunukiwa nafasi hizo kwa sababu mbalimbali, haiondoi ukweli kwamba wao ni watumishi wa umma na kwamba ofisi wanazofanyia kazi ni ofisi za umma. Kwa kutambua uhalisia huo, mabalozi wetu hawana budi kuwatumikia wananchi wote kwa usawa bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa. Kwa maneno mengine mabalozi wetu wanapaswa kutambua kwamba wanaiwakilisha nchi kwa maana ya watanzania wote na sio Chama cha Mapinduzi.

68. Mheshimiwa Spika, nimetangulia kusema hivyo kwa kuwa imebainika kwamba yapo mawasiliano ya Chama cha Mapinduzi kwenye tovuti (website) ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza jambo linaloashiria kwamba ubalozi huo unapokea maelekezo juu ya utendaji wake kutoka katika Chama cha Mapinduzi. Aidha, mawasiliano hayo yanatoa taswira kwamba ubalozi huo unafanya kazi kwa kuegemea itikadi zaidi jambo ambalo linaonyesha dhahiri hauwezi kuwahudumia watanzania wanaoishi nchini Uingereza kwa usawa kutokana na tofauti za itikadi za kisiasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge Mawasiliano ya CCM kwenye website ya Ubalozi wetu Uingereza yanahusiana vipi na Diplomasia ya Uchumi?

69. Mheshimiwa Spika, kwenye nchi ya inayofuata demokrasia ya vyama vingi tulitarajia taasisi za serikali kuhudumia watanzania wote bila ubaguzi wa aina yotote ikiwemo itikadi za vyama. Aidha, kwa mazingira ya leo, Balozi za nchi nje ya nchi ni kiunganishi muhimu cha raia wa nchi husika wanaoishi ugenini. Balozi zikianza kufanya kazi kwa mrengo wa kisiasa ni wazi kwamba kuna raia watakaobaguliwa hasa wale wanaotoka katika mrengo mwingine wa siasa.

70. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea tabia hiyo, na inaitaka Serikali kuondoa mara moja link ya mawasiliano ya CCM kwenye tovuti ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ili kuondoa dhana kwamba ubalozi huo unafanya kazi kwa maslahi ya CCM na sio maslahi ya Taifa.

K. HITIMISHO

71. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba duniani kote Wizara za Mambo ya Nje ni wizara za kimkakati. Kwa nchi yotote ile, Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo inayotekeleza mikakati ambayo nchi inataka kuifikia kutoka kwenye mataifa mengine. Kwa maneno mengine kutoichukulia kwa uzito Wizara ya Mambo ya Nje ni kutokuwa makini na malengo muhimu ambayo taifa linataka kuyafikia.

72. Mheshimiwa Spika, mikakati ya kimaendeleo ya ndani lazima ifungamanishwe kikamilifu na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuendana na hali ya dunia. Ndio maana mataifa yalioendelea huwa na mpango makakati kwenye wizara zao za nje. Kwa mfano nchini Uingereza wana mkakati wa maendeleo ya kimataifa kupitia Department for International Development - DFID na marekani wana makakati kama huo kupitia United States Agency for International Development – USAID.

73.Mheshimiwa Spika,ni kwa misingi hii Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuipa kipaumbele Wizara hii kwanza kwa kwa kuweka mpango mkakati wa kuandaa rasiliamali watu wenye maarifa na weledi wa kutosha kuendesha diplomasia ya kimataifa, lakini pili kwa kuitengea Wizara hii fedha za kutosha kwa ajili ya kuweza kutekeleza diplomasia hiyo.

74. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai hiyo, kwa sababu kumekuwa na viashira vya kudharauliwa kwa wizara hii na kuonekana kama haina umuhimu kwa nchi. Viashiria hivyo ni pamoja na kutenga bajeti ndogo jambo ambalo limepelekea balozi zetu huko nje kuwa na mazingira duni na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, kiashiria kingine ni muda mdogo unaotengwa kujadili bajeti yenyewe. Kutenga siku moja au masaa kadhaa kujadili mustakabali wa nchi yetu katika ulimwengu wa kimataifa kana kwamba ni idara au kitengo fulani ndani ya wizara kinajadiliwa ni kutojitendea haki sisi wenyewe na maana yake ni kwamba tutaendelea kubaki nyuma kwa takribani kila sekta kutokana na kuachwa na dunia.

75. Mheshimiwa Spika, Wizara hii inabeba mambo mengi mtambuka muhimu, zaidi Ulinzi na Usalama pamoja na uchumi wetu kwenye uso wa dunia. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kipaumbele stahili kwa Wizara hii.

76. Mwisho kabisa Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaisihi Serikali kupitia kwa Waziri mwenye dhamana kurejesha tena heshma ya Tanzania katika ulimwengu wa kimataifa iliyoanza kutoweka. Sisi si kisiwa, tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyotuhitaji sisi. Daima tukumbuke methali hii “tawi likijitenga na shina hunyauka” na huo ndio huwa mwisho wake.

77. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, namba kuwasilisha.

Salome Wycliffe Makamba (Mb)
 
Wataalamu wa bajeti hiii bajeti ya Upinzani Ni bajeti au porojo za Upinzani.Where are the numbers.Bajeti hata ya nyumbani huonyesha shilingi kadhaa zitatumika kwenye ABC.Upinzani nauliza Tena mlichosoma Ni bajeti au porojo za kijinga where is the budget? Mlichosoma na ku present Sio bajeti na Kama Spika kapokea kakosea hiyo Sio bajeti Ni porojo tu kuanzia mwanzo Hadi mwisho.shame on you
 
Back
Top Bottom