Hivi kweli tufanya uchaguzi 2020 na katiba hii ya 1977?

eden kimario

JF-Expert Member
Jun 13, 2015
10,227
16,178
Nashindwa kupata taswira kamili ya uchaguzi wa 2020 kwa kutumia katiba hii tuliyo nayo sasa. Iwapo tutaingia katika uchaguzi wa 2020 kwa katiba ya sasa, maana yake ni nini? Najaribu kueleza:

Tutaingia katika uchaguzi tukiwa hatuna tume huru ya uchaguzi. Kukosekana kwa tume huru ya uchaguzi limekuwa ni suala ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu sana.



Ni moja ya sababu ambazo zimekuwa zikifanya chaguzi zetu kulalamikiwa na kuzua manung’uniko. Ni wakati muafaka sasa wa kuliweka hili sawa. Ndio maana Tume ya Warioba ilipendekeza tuwe na tume huru ya uchaguzi na ilipendekeza namna nzuri ya kuwapata Mwenyekiti wa Tume, Makamu na Makamishina wengine wa Tume.

Tutaingia katika uchaguzi wakati bado raia wananyimwa haki yao ya uraia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kama wagombea huru (independent candidates).



Kwa mujibu wa katiba iliyopo eti ni lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa ili uweze kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hili linanyima haki Watanzania ambao si wanachama wa vyama vya siasa ambao ndio wengi.



Na Takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania ambao ni wananchama wa vyama vya siasa hawazidi takribani milioni kumi. Je, ni sahihi kuwanyima fursa wananchi milioni Zaidi ya 40 kuomba kuchaguliwa na Watanzania wenzao katika nafasi mbalimbali?

Tume ya Warioba hili nalo ililifanyia kazi na kupendekeza marekebisho ili kuwaruhusu Watanzania kugombea nafasi yoyote bila kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa.

Tutaingia katika uchaguzi ambapo matokeo ya kura za Rais hayawezi kuhojiwa au kupingwa na chombo chochote baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi.

Tume ya Warioba ilitoa nafasi kwa matokeo kuhojiwa na kupingwa. Tutaingia katika uchaguzi wakati hakuna mgawanyo ulio wazi wa madaraka kati ya vyombo mbalimbali, chama na serikali na taasisi mbalimbali.

Tutaingia katika uchaguzi ambapo matumizi ya raslimali za serikali katika uchaguzi yakitumika kukinufaisha chama kimoja cha siasa. Tutaingia katika uchaguzi ambapo uwanja wa ushindani haupo sawa. Vyombo vya habari na vyombo vingine na taasisi mbalimbali zikiendelea kuegemea upande mmoja wa Ccm

Tutaingia katika uchaguzi ambapo mfumo wetu wa sheria na hasa sheria mama ni dhaifu sana. Sheria haitoi nafasi kwa vyama kuungana na kusimamisha mgombea mmoja.

Uamuzi wa Duni Haji kulazimika kuhama chama chake cha CUF ili aweze kuwa mgombea mwenza wa Chadema ni kielelezo tosha cha mapungufu yaliyopo katika muundo wetu wetu wa sheria.

Aidha ni mfumo ambao hauwezi kutanzua migogoro na hautoi nafasi ya ushindani sawia. Mgogoro wa Zanzibar ni mfano mwingine hai. Haya ni baadhi tu ya mapungufu ya kikatiba ambayo yanaufanya uchaguzi wetu usiwe huru na wa haki na unazua malalamiko na kudhoofisha umoja, amani na mshikamano wa Taifa letu.

Kama Mtanzania, naendelea kujiuliza iwapo ni busara kushiriki katika uchaguzi wa namna hii au la!

Ni maoni yangu kuwa tutageuka kichekesho duniani iwapo zoezi hili halitakamilishwa. Tutaishangaza dunia kwa sababu tuliamua na tukiwa sababu nzuri na nzito. Na mchakato mzima ulianza vizuri ukiwa ni shirikishi, ingawa baadaye uligurugika na kukwama katika hatua ya Bunge maalum la katiba. Hapo ndipo tulipojikwa.

Moja ya mambo machache ambayo hatuna budi kujifunza ni uundwaji wa Bunge Maalumu. Bunge lile lilikuwa ni kubwa sana na hata muundo wake yaani ‘composition’ yake isingeweza kutupa katiba mpya.

Wabunge wa wakati huo na wawakilishi wakati huo kugeuzwa kuwa ndio wajumbe wa bunge maalum, kwa maoni yangu hilo lilichangia kukwamisha mchakato wa katiba.

Na baada ya hapo Bunge Maalum kudai kuwa lina mamlaka ya kubadilisha masuala ya msingi yaliyopendekezwa na wananchi na kuwekwa katika rasimu ya pili ya katiba.

Mathalani, ilipendekezwa kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa wabunge. Lakini hilo liliondolewa kwa sababu liligusa maslahi ya wabunge wa wakati huo. Ilipendekezwa viongozi wasiruhusiwe kuwa na akaunti nje ya nchi, lakini hili nalo likabaidilishwa eti kwa kuweka utaratibu maalum wa viongozi kufungua akaunti nje ya nchi.

Watetezi wakubwa wa rasimu hii walikuwa ni wanasiasa na wasomi kama Humphrey PolePole (ambaye sasa ni katibu Mwenzei wa CCM), Prof. Kabudi ( ambaye sasa ni Waziri wa Katiba Sheria), Said Awadhi, Mzee Joseph Butiku na Mzee Warioba mwenyewe.

Hao walisikika katika mijadala na makongamano mbalimbali wakitetea rasimu ya pili ya katiba, wakitetea muundo wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Warioba. Natumai wananchi wataendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa sana misimamo ya viongozi hawa na hasa katika mazingira mapya ya kisiasa.

Je, wataendeleza ajenda yao? Kama wataizika ajenda hii, tunajifunza nini Watanzania kwa viongozi wetu? Hapa ndipo Watanzania watamjua kiongozi ambaye anasimamia misingi anayoiamini na mzalendo wa kweli.

Hayati Bob Marley aliimba na kusema “Soon we will find out who is the real revolutionary”. Maana yake: Hivi karibuni tutajua Mwanamapinduzi wa kweli. Tanzania hivi sasa inapitia katika kipindi ambacho Watanzania watawajua wanamapinduzi wa kweli au watafuta maslahi na fursa.

Pia tukumbukue kuwa, tulitumia raslimali nyingi sana kwa zoezi ambalo kwa masikitiko makubwa halikuweza kukamilika. Ni vizuri tukajifunza wapi tuliteleza ili tusirudie makosa yaliyopelekea baadhi ya watu kususia mchakato na hatima yake mchakato wenyewe kukwama. Mchakato huu unahitaji maridhiano, mashauriano na kusikilizana.

Mchakato huu hauhitaji ubabe, jeuri wala kiburi cha sisi ni chama tawala au sisi ni chama cha upinzani. Ni vyema safari hii tukalianza zoezi hili mapema ili tulifanye kwa umakini.

Tukumbuke kuwa imebaki miaka miwili tu kuingia katika uchaguzi mkuu mwingine wa 2020. Tusipoteze muda tukajikuta hatuna muda wa kutosha kukamilisha zoezi hili. Ni nani wenye jukumu la kujenga ushawishi ili mchakato huu utazamwe upya na kujenga muafaka wa kuanza tena? Ni wazi kuwa ni asasi za kiraia, taasisi zisizo za kiserikali, wasomi, wanasiasa na hasa chama kikuu cha upinzani na wananchi wote kwa ujumla.

Inaeleweka kuwa ili kufanya kampeni hii unahitaji fedha ambazo asasi nyingi za kiraia hazina uwezo wa kifedha. Vyama vya siasa kwa siasa vimepigwa marufuku kufanya mikutano. Hali hii inanifanya nione giza nene huko mbele.

Ujumbe kutoka sauti ya mnyonge kwa Watanzania ni kuwa katiba bora ndio itatupa taasisi imara, ndio itatupa uwajibikaji makini, viongozi bora, matumizi mazuri ya raslimali zetu, matumizi mazuri ya madaraka, uongozi wenye maadili, tutaweza kutokomeza rushwa.

Na haya yakitokea ndio tutaweza kuwa na maendeleo na ustawi wa jamii. Tutaweza kuwa na maji safi na salama. Tutaweza kuwa na barabara zinazopitika vizuri. Huduma za jamii nzuri, dawa katika hospitali na zahanati na vituo vya afya (kwa sababu kuna uwajibikaji na matumizi mazuri ya raslimali zetu).

Tutaweza kumiliki ardhi na kukomesha migogoro ya ardhi. Watoto wa kitanzania watapata elimu bora. Utawala bora na utawala wa sheria utaimarika. Katiba ndio sheria mama, ndio kipaumbele chetu cha kwanza. Tusidanganyike.

Tuikatae katiba hii ya mwaka 1977 maana inaweza kusababisha uasi katika taifa letu kama zilivyo baadhi ya nchi nyingine barani Africa na watawala walione hili wasijigambe eti wana jeshi na police wa kutosha maana uasi humlenga yeyote bila kujali dini au kabila lake au chama chake
images.jpg


E&K
 
Kwakweli umeongea mawazo niliyonayo. Mi nimewaza kwa kukaa kimya, bora wewe umewaza kwa kubonyeza kwenye keyboard. Nionavyo bila katiba mpya watanzania walio wengi nikiwepo na mimi sitaona haja ya kupiga kura kwasababu kawaida kura hutangazwa za kubuni. Siamini kuwa kura zinazotangazwa zinakuwa sahihi.
Vilevile watanzania inabidi tujifunze viongozi wanaojiita wapinzani, kumbe waliowengi njaa ndizo zinawasumbua. Kati ya ulio wataja umewasahau pia kama Prof Kitila Mkumbo, Mama Anna Mgwira, Mwita Waitara, Abdul Mtulia, Patrobas Katambi, Julius Mtatiro na maana kwamba yale yote waliokuwa wakihoji wakiwa wapinzani yametekelezwa? Hapo ndo inabidi watanzania tujitathmini kwamba je tunayosafu inayo tetea maslahi wa wananchi? au ni njaa, mara wanapopewa ugali au chakula wanaona inatosha na kusaliti walio nyuma yao.
 
HOJA yako ni muruwa kabisa na naiunga mkono ila jiwe na chama chake wako tayari maana wakija na katiba ya Warioba that will be the end of ccm forever. This is the last thing jiwe will do. Unaandaliwa mkakati wa kumwongezea muda na siyo katiba mpya.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Waliokwenda Dodoma kutuvurugia bunge la katiba, hadi leo wapo tu wanatusanifu!

Sent using Jamii Forums mobile app
Lkn wote ni waathirika wa kusoma no pia,hata waliokuwa kwenye system na uwezo wa kuleta mabadiliko wakaona hayawahusu Leo yanawahusu Lkn ni to late hata walio kwenye system Kwa sasa wenye nafasi ya kufanya mabadiliko wanaona hayawahusu wako Salama, wataelewa wakiwa nje ya system, apandae miba njiani kuna siku itamchoma.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom