Hivi kesi ya tuhuma za kutoa rushwa dhidi ya Kitumbo na Mwakingwe ni ya kusilizwa na kuamuliwa siku moja?

Mzalendo_Mkweli

JF-Expert Member
Jan 30, 2012
1,989
1,179
WIKI iliyopita, tukio lililotikisa anga za soka ni lile la kufungiwa maisha kwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora, Yusuf Kitumbo akituhumiwa kujihusisha na kupanga matokeo ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza sambamba na kocha Ulimboka Mwakingwe.

Kitumbo ni kiongozi wa Kitayosce ambayo imefanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Bara kwa msimu ujao baada ya kufanya vizuri katika mechi zake, ikiwemo hiyo ambayo kiongozi huyo anatuhumiwa kuhusika kupanga matokeo.

Kwa jinsi kosa la upangaji matokeo lilivyo sumu katika soka, ni rahisi kila mmoja kurusha laana zake kila awezavyo kwa wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo.

Na ubaya wa kosa hilo unaweza kusababisha hata vyombo vya haki, kama Kamati ya Maadili, kuharakisha kufanya maamuzi kwa kujua kuwa, kila mtu atafurahia mtuhumiwa wa upangaji wa matokeo kuadhibiwa.

Na kwa sababu Kitumbo alishawahi kutuhumiwa kupanga matokeo miaka michache iliyopita, kumtia tena hatiani bila ya kufanya utafiti wa kina kuziba mapengo yote inakuwa rahisi kwa kuwa kila mtu atasema ndio kawaida yake.

Lakini ubaya wa kosa hilo ndio unaohitaji zaidi umakini katika kufanya maamuzi kuliko haraka za kuhukumu na baadaye ikadhihirika kuwa kulikuwa na udhaifu maeneo kadhaa na mtuhumiwa kubakia huru kuliko wakati mwingine wowote.

Kimpira kosa la kupanga matokeo ni sawa na kosa la kuua katika maisha ya kawaida. Mtu anayetuhumiwa kuua hatakiwi aadhibiwe kwa hisia labda kwa sababu tu inaonekana kama kosa lake ni dhahiri. Ni lazima ibainike bila shaka yoyote kuwa mtuhumiwa aliua kweli.

Huenda hiyo ikawa moja ya sababu kubwa za kesi za mauaji kuchukua muda mrefu kwa kuwa ushahidi wa kumtia hatiani mtuhumiwa moja kwa moja ni ngumu kupatikana.

Kwa sababu adhabu yake ni kuondoa maisha ya mtuhumiwa, ni lazima kuwe na umakini wa hali ya juu katika mchakato wa kesi ili kupata uhakika kabla ya kuchukua uamuzi wa kuondoa maisha ya mtuhumiwa.

Hii ni kwa sababu ikija kudhihirika baadaye mtuhumiwa hakuhusika na mauaji, haitawezekana kurejesha uhai wake kama adhabu ya kunyongwa ilishatekelezwa.

Hata kosa la upangaji matokeo ambalo huhusisha rushwa, haliwezi kuadhibiwa kirahisi rahisi kama adhabu yake ni kumwondoa kabisa mtuhumiwa katika soka. Ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike na hasa ikizingatiwa kosa hilo linaangukia kwenye jinai, ambayo si rahisi kwa chombo cha soka kufanya uchunguzi wa kina.

Ni kama ilivyo kwa makosa mengine kama ya kughushi na wizi ambayo mamlaka za nchi hutaarifiwa ili kutumia stadi zake kubaini.

Kwa kujua hilo, Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) liliunda Kamati ya Maadili yenye idara mbili zinazofanya kazi kwa uhuru. Kamati ya Maadili ya Fifa inaundwa na Investigatory Chamber, ambayo ni idara huru inayojihusisha na uchunguzi na Adjudicatory Chamber, ambayo kazi yake ni kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa.

Idara hizo hufanya kazi zake kwa uhuru wote na zina sekretarieti zake. Zinafanya kazi kwa uhuru wote kwa kuwa yeyote katika soka anayetuhumiwa, awe rais wa Fifa, katibu wake au kiongozi wa chama mwanachama, anawajibika mbele ya kamati ya maadili na hawezi kuzuia uchunguzi unaofanywa na Investigatory Chamber.

Hata hivyo, kuna makosa ambayo Fifa yenyewe imeeleza kwenye kanuni zake yanakwenda nje ya mamlaka yake na hivyo vyombo vya dola vya nchi vinaweza kuingilia na kushtaki pale vinapoona kuna tatizo.

Nimeeleza hayo yote kujaribu kuonyesha ukubwa wa tatizo la upangaji matokeo na jitihada zinazoweza kufanywa katika kulichunjguza na hatimaye kufikia maamuzi makubwa kama ya kuwafungia Kitumbo na Mwakingwe.

Nilishangaa suala hilo limeshughulikiwa kama kesi ya kawaida na kutolewa uamuzi bila ya hata Kitumbo kuwepo, huku utetezi wa Mwakingwe ukifanywa kwa njia ya maandishi, kana kwamba ni kosa la kutukana mtu au kumpiga mwamuzi.

Hili si kosa la kukimbilia kutoa adhabu ambayo inamwondoa mtuhumiwa katika soka milele, bali kulichunguza kwa kina. Kama kweli lipo, wahusika wanaweza kuwa zaidi ya Kitumbo na Mwakingwe kwa kuwa linahusisha timu zenye wachezaji 22 uwanjani na wengine 38 wakiwa benchi au jukwaani.

Kama upangaji matokeo ulimhusisha kocha, basi ni lazima kocha alihusisha wachezaji na ni lazima upande wa pili ulijua japo kidogo, kile kinachoendelea. Kukimbilia kufanya maamuzi, ni kuacha chembechembe nyingine za rushwa ndani ya mpira na hivyo kushiriki kwenye mchakato wa kuua soka taratibu.

Na kama kamati haikuona umuhimu wa kulichunguza suala hilo katika mapana yake, basi lazima kuwe na tuhuma za siasa za uchaguzi, hasa kutokana na harakati na uwezo wa Kitumbo linapofikia suala la uchaguzi.

Lengo langu si kutaka kumtetea Kitumbo, ambaye alishawahi kuhusishwa na upangaji matokeo, au Mwakingwe, ambaye aliwahi kuhusishwa kutaka kumrubuni kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado. Lengo langu ni kutaka mamlaka zinazohusika na utoaji haki, kutokuswa na haraka katika kufanya maamuzi hyanayohitaji uchunguzi wa kina wa masuala hatari kwenye soka.

Nisingetegemea tuhuma za upangaji matokeo zifanyiwe maamuzi siku moja kwa kuwaita watuhumiwa kwenye kikao. Wakati mwingine tuhuma kama hizi ambazo ni jinai zinaweza kuwasilishwa katika mamlaka husika za nchi kwa ajili ya uchunguzi ili kutoa maamuzi yanayousaidia mpira na si kufurahisha genge fulani na watu wachache.

Kote ambako kulikuwa na rushwa za upangaji matokeo, mamlaka za nchi zilihusika. Katika kashfa ya upangaji matokeo ya vigogo wa Ufaransa, Olympique de Marseille, licha ya mchezaji wa Valencienne kusema hadharani kuwa alikataa rushwa ya Rais wa klabu hiyo, Bernard Tapie ya kuwataka yeye na wenzake kucheza chini ya kiwango, bado mamlaka zilishughulikia kesi hiyo na kutoa uamuzi. Tapie, Jean-Jacque Eydelle walihukumiwa kwenda jela wakati wengine, wakiwemo wachezaji waliopokea rushwa walipewa kifungo cha nje.

Hata suala la Juventus lilishughulikiwa na mamlaka za nchi na halikuchukua siku moja kama Kamati ya Maadili ya TFF.

Kama kweli kuna uhakika Kitumbo na Mwakingwe walihusika katika upangaji matokeo, basi tatizo ni kubwa kuliko hao wawili na uchunguzi wa kina unahitajika ili kuweka bayana ukubwa wa tatizo hilo na kulipatia dawa ya kweli.

Kama ni huo wa uamuzi wa kukaa siku moja, hakuna shaka kuwa tumeamua kufuga tatizo na si kulishughulikia kwa mapana yake ili kuondoa kirusi hicho kikubwa katika soka duniani.
Source : Mwanaspot​
 
Back
Top Bottom