Historia ya taarabu na uhuru wa Tanganyika na alhaj Abdallah Tambaza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,922
30,271
Shajara ya Mwana Mzizima:

TAARABU NA UHURU WA TANGANYIKA

Na Alhaji Abdallah Tambaza


Mwalimu Subeti Salum Subeti
(1903 - 1974) mmoja katika wapiga
fidla (violin) maarufu wa Egyptian
katika miaka ya 1940 - 1970




KUPATIKANA kwa Uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961, kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na uhodari, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi na umahiri wa viongozi wa vyama vya siasa wakati huo; hasa chama cha TANU kilichoongozwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Lakini, kwa upande mwengine, harakati za kudai uhuru zilinogeshwa (spiced) na uwepo wa vikundi mbalimbali vya burudani na sanaa vilivyokuwa vikihamasisha na kuwatia hamasa wananchi kila palipokuwa pakifanyika mikutano— hususan ile ya hadhara— kwa kutoa burudani mbalimbali zilizoleta shamrashamra, nderemo, vifijo na hoihoi.

Kwenye mikutano ile ya wazi hapa Dar es Salaam, kabla ya kuhutubiwa na wale viongozi waandamizi wa TANU—Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi na Nyerere—kulitanguliwa na usomaji wa mashairi pamoja na tenzi zilizobeba ujumbe mzito kwa waliohudhuria.

Pia, nyimbo za kwaya zenye kusisimua zilizoimbwa kwa madaha na weledi mkubwa na bingwa wa kwaya siku hizo, hayati Mzee Makongoro; zilibeba ujumbe mzito: Uhuru! Uhuru! Uhuru na Umoja.

Kwa upande wa ngoma alikuwapo Mzee Morris Nyunyusa (alikuwa haoni kabisa), ambaye pia alikuwa akipata nafasi ya kupiga kwa ustadi mkubwa zile ngoma zake kumi kwa wakati mmoja. Mmoja wa nyimbo zake ni ule mashuhuri unaopigwa kwenye Radio Tanzania mpaka leo kuashiria kwamba ni wakati mwengine tena wa kusomewa taarifa ya habari.

Mzee Ramadhani Mwinamila wa Unyanyembe Tabora, pia alikuwa akihanikiza na kikundi chake cha ngoma ya kiasili ya Kinyamwezi kilichojulikana kama ‘’Hiyari ya Moyo,’’ huku akiwa amejiviringisha na joka kubwa ambalo hurandaranda nalo mgongoni akienda huku na kule kwa midundo ya kiasili ya Kinyamwezi ya ‘igembe nsabo’ na ‘mipanga lolo’.

Mwamko ule; hamasa ile; na vuguvugu lile lililosababisha maelfu kwa maelfu ya Wananchi kufurika kwenye mikutano, ulimtisha na kumshitua Gavana wa Kiingereza, Lord Twinning. Hakukuwa na namna nyingine bali TANU kuipenda tu!

Kutokana na watu wengi mno kupokea na kuelewa ujumbe, sasa ikawa ni lazima mikutano ile ifanyike viwanjani Jangwani, kwani Mnazi Mmoja pakawa hapatoshi tena kubeba mzigo ule mkubwa.

Nyerere wakati fulani, alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara, hali iliyosababisha harakati za ukombozi kudorora.

Wananchi wa Dar es Salaam, walisononeka sana kukatishwa kwa uhondo ule wa kumsikiliza kijana mdogo wa Kizanaki, msomi kutoka Butiama, akiwaliwaza na maneno yake mazuri yaliyojaa lafudhi ya Kikurya, lakini yaliyobeba ujumbe mzito wenye mazingatio na matumaini makubwa.

Mmoja wa watu walioathirika kwa kusitishwa na kutokuwapo kwa mikutano ile, ni mama yangu mlezi nyumbani kwetu, hayati Bi. Fatuma Kigwe, ambaye daima alikuwa akituchukua sisi tukiwa bado vijana wadogo siku hizo— iwe Mnazi Mmoja au Jangwani— kwenda kumsikiliza Nyerere na Titi na yale waliokuja nayo.

Mama, alikuwa na kipaji kikubwa sana cha kuigiza sauti za watu (personification). Sasa, jioni baada ya mikutano ile, wakati tumekusanyika kwenye mduara wa chakula cha usiku, alikuwa akitoa burudani upya kwa kumwigiza ‘Nyerere wa Butiama’ na namna alivyokuwa akizungumza mkutanoni.

“Nisikilizeni … ‘babe zangu’ na ‘mame zangu’, Mkoloni Mwingereza huyu anatapatapa tu, anatapatapa tu …ataondoka, ataondoka tu …ataondoka atuachie nchi yetu, ndiyo…ndiyo, ni mtu mbaya sana …hana huruma huyu hata kidogo!” Mama alikuwa akimpatia kweli kweli Mwalimu, hasa pale alipokuwa akirudiarudia neno moja mara mbili. Hapo tulikuwa tukipata burudani upya kumsikiliza ‘Nyerere wa Butiama’ akikonga nyoyo za Watanganyika wenzake waliokuwa wamechoshwa na kutawaliwa.

Sasa, pamoja na mambo mengine mengi, mbinu mpya ikabuniwa ya kumpiku Gavana Twinning na amri yake ya kukataza mikutano: Watu wa kawaida tu, wakawa wanaandaa shughuli majumbani mwao; hasa zile za harusi, ambapo kwa zamani, kwa mila ya watu wa Mrima, ni kawaida Bwana na Bibi Harusi watolewe uwanjani kuonyeshwa kwa ndugu na jamaa huku muziki wa taarabu ukitumbuiza.

Sasa, ikawa inapotokea mtaani kuna harusi, viongozi wa chama wa eneo husika humwendea mwenye shughuli kumtaka kutumia shughuli yake kwa kumwalika Nyerere kuja kuwa mmoja wa wageni ili baadaye apate nafasi ya kuhutubia hafla ile. Halikuwa jambo gumu lile kutekelezeka, kwa sababu wakati huo Nyerere alikuwa ni raia wa kawaida tu, ambaye kuhudhuria kwake kwenye shughuli yoyote halikuwa jambo lililowahusu watu wa usalama ama wakoloni wenyewe.

Mbinu ile, ikawa na mafanikio makubwa sana, kwani kila fursa ilipopatikana, ilizungumzwa siasa tupu na maendeleo ya harakati za chini kwa chini za kudai nchi yetu kutoka kwa Wazungu wale wababaishaji kutoka Ulaya Ingereza. Vinanda na nyimbo za hamasa za taarabu pia huchukua nafasi hiyo kuimba nyimbo za siasa tu, badala ya ‘kimasomaso mwanangu usimwone’. Kadi mpya ziliuzwa hapo pia.

Egyptian Musical Club, ni moja ya bendi kongwe za muziki wa taarabu hapa nchini ambayo ilisheni waimbaji wazuri na wenye vipaji haswa, pamoja na wapigaji ala mahiri sana kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki. Wao ndio waliofanya kazi hiyo kwa kiwango cha juu sana. Maskani ya bendi hiyo, kwa muda mrefu yalikuwa palepale New Street (sasa Lumumba) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mita chache tu—mkabala— na mahala lilipokuwepo jengo la Makao Makuu ya Chama cha TANU.

Muziki wa Taarabu asilia, asili yake ni mchanganyiko wa muziki wa Kiswahili na ule wa Afrika Kaskazini (kwenye nchi kama Egypt, Tunisia na Morocco) uliosheheni ala mbalimbali mithili ya Ochestra ya bendi za Muziki ya Kizungu ama kihindi inayohusisha zaidi vinanda na ala nyingine kama vile accordion, magitaa ya bass na rythim, udi, ghanoon, tumba na violin.

Vifaa vyengine ni saxophone, organ, tarumbeta, piano na marimba. Ukiacha mpigaji wa gitaa la bass na mwimbaji, wapigaji wengine wote huwa wamekaa kwenye viti vyao wakivurumisha vinanda kwa mpangilio na uongozaji wa kiongozi wa bendi (band master).

Egyptian Musical Club, ni bendi iliyoanzishwa miaka mingi nyuma mnamo karne ya 18 hivi, jijini Dar es Salaam ikiwa moja ya uendelezaji wa utamaduni wa Mswahili wa Mrima uliochanganyika na ujio wa walowezi wa Kiarabu kutoka nchi za Kaskazini mwa Afrika.

Mara zote nyimbo zake, pamoja na kubeba ujumbe, hutungwa kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Mswahili wa Mwambao na lugha yake adhimu ya Kiswahili ndiyo iliyotumika, ingawa mara chache nyimbo hizo hupigwa kwa mahadhi ya Kihindi na Kiarabu. Ni aghlabu sana taarabu kuimbwa kwa Kingereza ingawa wasanii wajanja wa kileo wamefanikiwa kufanya hivyo.

Ukiacha bendi hii ya Egyptian, bendi nyengine zilizokuwepo wakati huo jijini Dar es Salaam ni Alwatan Musical Club na Bombay Musical Club (baadaye ikajiita Jamhuri pale uhuru ulipopatikana). Tofauti na sasa, muziki huu siku za nyuma ulikuwa ukipigwa kwa ajili ya kuburudisha watu na si kwa ajili ya kujipatia chochote kwa wasanii husika kama ambavyo sasa imezoeleka.

Kule Tanga nako kulikuwa na bendi kadhaa za muziki huu, ikiwamo Lucky Star ya mwimbaji maarufu hayati Bi Shakila, aliyejizolea sifa kemkem hapa nyumbani na Afrika Mashariki yote kwa sauti yake nyororo na maudhui yenye mafunzo. Habari zinasema mbinu hii iliyokuwa ikitumika hapa Dar es Salaam kutumia taarabu kisiasa ilifanikiwa pia kule Tanga na kwengineko.

Kule Zanzibar, ingawa hakukuwa na marufuku yoyote kukataza wanasiasa kufanya kazi za ukombozi, lakini pia nako taarabu ilitumika kwa kutunga nyimbo zenye maudhui ya kudai kujitawala wenyewe miongoni mwa jamii ya Waafrika.

Mara zote wakati wa Sikukuu za Pasaka, Wazanzibari wakati ule walishuhudia kumwona Nyerere akihutubia kwenye kukaribisha wageni wa ‘Sports’ kulikokuwa kukifanywa na vilabu vya mpira vya Sunderland (sasa Simba) na Yanga.

Wimbo kama, Abeid nenda, Oya! Oya!; Tunakutuma, Oya! Oya! Ulitungwa mahsusi na Bendi ya Culture ya Unguja kumhamasisha Abeid Karume katika safari yake ya kule kwenye Mkutano wa Lancaster House, mjini London uliojadili mustakabali wa Zanzibar mpya baada ya kujitawala.

Kwa muktadha huu basi, hapana budi kwa wale wasomi watakaokuja kuandika historia sahihi ya mapambano ya uhuru wa nchi yetu kutilia maanani jambo hili la kuwakumbuka wapigaji vinanda wale wa Bendi ya Egyptian Musical Club. Ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba kwa kiasi kikubwa tu katika kipindi kile kigumu, kwa kushirikiana na wazalendo wa kawaida tu, waliweza kupeleka mbele harakati zile.

Mara chache hupata watu wakaitaja klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kwamba ilikuwa na mchango mkubwa katika ukombozi wa taifa hili. Kwa kiasi fulani ni kweli maana wengi wa wanachama wake walikuwa ni watu weusi, hivyo wakawa pia na kadi za TANU, lakini vyovyote vile iwavyo, Yanga hawakuwa na mchango unaoikaribia au kuipiku bendi ya Egyptian Musical Club; kwani wao walipiga na kutumbuiza kwenye shughuli nyingi ambazo ‘Mheshimiwa’ Julius Nyerere alipata fursa ya kupenyeza maneno yake, wanawake wakapiga vigelegele na wanaume kushangilia kwa makofi kuchangamsha harusi na harakati za ukombozi kuzipa nguvu.

Kikundi cha Egyptian ya miaka hiyo ya 1950 na 60s, ilikuwa na wazee kama Mzee Bom Ambaroni aliyeshirikiana na Mzee Salum Mboga na Mwalimu Subeti Salum katika upigaji wa ‘violin’. Maalim Abubakar Mzinga yeye ghanoon na kuimba nyimbo pia.

Shamas bin Abubakar, Hamis George, Abbas Mzee, Saleh Mtumwa na Muhiddin Kingaru, hawa wao walikuwa waimbaji wa zile nyimbo maarufu zilizotokea kupendwa kwa muda mrefu za: ‘’Kharusi Jambo la Kheri;’’ ‘’Kila Mwenye Uwezo Asaidie Yatima;’’ na ‘’Umaridadi si Kufua Nguo, Bali Usafishe Wako Moyo.’’ Nuru bint Suud na Mtumwa Rajab wao walikuwa miongoni mwa waimbaji wanawake.

Bendi nyengine iliyoundwa baada ya uhuru kupatikana kwa msaada mkubwa wa mwanasiasa nguli kutoka hapa Mzizima hayati Kitwana Kondo, ilikuwa ni New Extra Musical Club. Ikiwa na makao yake pale Mtaa wa Mafia na Livingstone jijini Dar es Salaam, New Extra ilitumika sana katika kuhamasisha wananchi kutilia maanani suala la kilimo kwa kutunga wimbo maarufu wa ‘Shambani Mazao Bora Shambani’. Khamis Juma Mzinga ndiye aliyeuimba wimbo huo ambao mpaka leo unatumika na kupigwa na Radio Tanzania linapokuja suala la Kilimo Kwanza.

Ni bahati mbaya sana muziki huu wa Taarabu Asilia umetoweka katika medani ya muziki hapa kwetu Tanzania Bara, kule Zanzibar ndio kwanza ‘mkoko unaalika maua’, kwani huwaambi kitu katika kumuenzi na kumtukuza hayati Bi Kidude na Siti bint Saad aliyekufa miongo kadhaa nyuma kabla uhuru kupatikana.

Ni sehemu muhimu sana ya utamaduni wa Mtanzania ukiangalia kule nyuma tulikotoka. Ilikuwa ni muziki huu wa taarabu asilia, serikali ya awamu ya kwanza ya hayati Baba wa Taifa, iliyoutumia kwa kuwastarehesha wageni wote wakubwa wa siserikali walioitembelea nchi yetu siku za nyuma, kwenye dhifa za chakula cha usiku (state banquets), pale Ikulu na kwenye holi la Diamond Jubilee, Upanga.

Wageni wakubwa wa kukumbukwa ambao walipigiwa taarabu ni pamoja na Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkurumah wa Ghana, Kenneth Kaunda wa Zambia, Huophet Boigny wa Corte de Voire na Chou en Lai wa Jamhuri ya Watu wa China.

Wengine ni Rais Tubman wa Liberia, Modibo Keita wa Mali, Ahmed Sekou Toure wa Guinea, Houari Boumedienne wa Algeria na Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria pamoja na wengine wengi.

Taarabu Asilia, ilikuwa kwenye programu zote za mikutano mikuu ya Chama cha TANU na baadaye CCM, kwa kuwaburudisha wajumbe baada ya mchoko wa mikutano.

Hivyo, kama ulivyopotea muziki wa dansi wa kina Mbaraka Mwinshehe, Juma Kilaza, Michael Enock – huu wa kina TX Moshi William na Muhiddin Gurumo nao unaelekea huko huko— taarabu asilia nayo imekwenda na maji mbele ya macho yetu! Ni msiba mkubwa.

Alamsiki!

atambaza@yahoo.com

Simu: 0715808864
 
Back
Top Bottom