Hatuna serikali, sababu nyingine ya kutomwongezea JK awamu ya pili !

Mag3

Platinum Member
May 31, 2008
13,070
22,766
Waziri agoma kuivunja TRL
na Irene Mark

LICHA ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omary Chambo, kuihakikishia Kamati ya Bunge kwamba mkataba kati ya serikali na Kampuni ya Rites utavunjwa mwezi ujao, Waziri wake, Dk. Shukuru Kawambwa ameshangazwa na kauli hiyo na kushindwa kueleza hatma yake.
Akizungumza kwa tahadhari mbele ya waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Waziri huyo aligoma kueleza kuhusu mchakato wa kuvunjwa kwa mkataba huo badala yake kwa namna isiyo ya wazi, alikuwa akitetea kuendelea kuwapo kwa mwekezaji huyo.
Dk. Kawambwa, alisema Rites inayoendesha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ni mwekezaji pia katika njia ya reli nchini Msumbiji ambako kwa mujibu wa maelezo yake, inafanya kazi vizuri, huku akilinganisha aina ya mkataba huo na uliosainiwa hapa nchini.
“Kampuni hii ya Rites ndiyo inayoendesha reli nchini Msumbiji...huko wamefanya vizuri, tena masharti ya mkataba wao ni kama huu wa kwetu, kule wamepewa asilimia 51 na menejimenti pia ipo chini yao kama hapa.
“Tatizo letu kila kitu tunaona ni ufisadi tu. Sasa iweje kule wafanye vizuri hapa waharibu?” alihoji Dk. Kawambwa na kuongeza kwa methali kwamba ‘mnyonge mnyongeni haki yake mpeni’.
Awali, waziri huyo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba ameyasoma magazeti ya jana, yaliyoeleza kuvunjwa kwa mkataba huo, kauli iliyotolewa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, lakini alishindwa kabisa kukiri ama kukanusha kuwapo kwa mpango huo.
Badala yake, alisema hafahamu chochote kuhusu kauli ya katibu wake na kukiri kuwepo kwa mchakato wa kurekebisha baadhi ya kasoro zinazojitokeza kwenye mkataba kati ya kampuni hiyo kutoka India na serikali chini ya wizara yake.
“Serikali haina kigugumizi kama ambavyo inasemekana, kwenye mkataba wowote matatizo yapo, tumekumbana na changamoto mbalimbali na mkataba huwa unahusisha pande mbili, sasa upande mmoja usiporidhika basi ni mambo yanayozungumzika haya,” alisisitiza waziri huyo na kubainisha kuwa serikali haina tatizo la usimamizi wa mikataba yake.
Aidha, Dk. Kawambwa alisema mchakato wa kumpata mwekezaji huyo ulifanyika kwa miaka saba kabla ya uamuzi wa kuingia mkataba pamoja naye.
“Tulifanya mchakato wa kumpata mwekezaji huyo kwa miaka saba, walikuwepo wawekezaji wengi, lakini mwisho wa siku akabaki peke yake. Sasa hapo utampa nani rushwa? Kwa hiyo haya maneno kwamba mkataba huu unarushwa si kweli. Rushwa hutolewa kwenye watu wengi, lakini kwa Rites alikuwa peke yake,” alisisitiza huku akikwepa baadhi ya maswali kutoka kwa waandishi waliomsubiri kwa zaidi ya dakika 45 ili kufahamu ukweli wa uvunjwaji wa mkataba huo.
Juzi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisema mpango wa kuvunjwa kwa mkataba huo upo katika hatua za mwisho za kuangalia namna ya kuuvunja kisheria bila kuipa hasara serikali.
“Tatizo kubwa lililopo ni uongozi ambao kwa mujibu wa mkataba, Rites walitakiwa waweke uongozi wao, lakini kwa bahati mbaya uongozi ule haukufaa.
“Kamati ya Bunge na Katibu wa Wizara ya Fedha tulikaa tukaona muhimu mkataba huo uvunjwe. Lakini vipo vipengele vingi ambavyo tukivunja tutapata hasara ya fedha nyingi sana,” alisisitiza Chambo na kueleza kazi hiyo inafanywa kati yake, ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi.
Tangu kuwapo kwa malalamiko ya kutaka mkataba huo uvunjwe, Waziri Kawambwa amenukuliwa mara kadhaa akisisitiza kutovunjwa ili kulinda mazingira ya uwekezaji nchini na kuhofia gharama kubwa inazoweza kutozwa serikali iwapo uamuzi huo utafikiwa.
Hii ni serikali au kikundi cha Zecomedy kilichoundwa na CCM baada ya uchaguzi wa mwaka 2005. Kwa mwendo huu hatufiki.
 
Hii ni serikali au kikundi cha Zecomedy kilichoundwa na CCM baada ya uchaguzi wa mwaka 2005. Kwa mwendo huu hatufiki.

Hahahaha hahaha hahaha ahhahahaha ahhaahah ahahahahaa...
This is Tanzania..
Ahsante kwa post hii mkuu.... Tanzania bila kikwete inawezekana..
 
Wanasiasa wa tz wametufikisha hapa tulipo na kututoa hawataweza!sina maoni tena wajamani lakini tutoke wenyewe bila watu hao yaani wanasiasa.tunaweza hatuwezi?
 
Sasa hapa tuseme Katibu Mkuu wa wizara husika aliidanganya kamati ya Bunge au vipi ? Itakuwaje Chambo aiambie kamati kuwa mkataba utavunjwa halafu waziri wake Kawambwa akanushe kuwa hakuna jambo kama hilo. Hiyo ni serikali au kikundi cha wasanii kikiongozwa na msanii mkubwa ndani ya Ikulu kwani kila siku tunashuhudia mikanganyiko isiyoweza kuelezeka kwa lugha yoyote ile na ikaeleweka.
 
Back
Top Bottom