Hatua 8 za kuchimba kaburi kabla ya kuuhifadhi mwili

Ambakucha

JF-Expert Member
Aug 16, 2019
277
445
Inajulikana toka enzi na enzi na tangu kuumbwa kwa mtu kwa kwanza kwamba, binadamu mwisho wake ni kifo na baada ya kifo ni kuuzika mwili wake katika Kaburi, wengi huamini hapo ndipo kwenye nyumba yake ya milele, japo zipo tamaduni nyingine, marehemu anachomwa moto.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaotumia utamaduni wa kuzika mwili ndani ya kaburi, hawajui kama kupatikana kwa kaburi hilo ni lazima kupitia hatua muhimu nane tangu kuchimbwa mpaka kuuhifadhi mwili.

Lengo la makala haya ni kutoa elimu kwa jamii jinsi 'nyumba ya milele' hiyo inavyopatikana.

HATUA YA KWANZA; KABURI HUCHIMBWA MAHALI PENYE SIFA ZIFUATAZO
Kuna maeneo ya aina mbili ambayo yana sifa ya kuchimbwa kaburi. Mosi, ni juu ya ardhi ambayo juu yake hakuna nyumba au ujenzi mwingine wowote unaondelea ambao unahusisha shughuli za kila siku za kibinadamu, kama vile shule, soko, vituo vya mabasi, polisi, zahanati n.k.

Pili, mahali hapo lazima patambulike na serikali ya mtaa au jamii husika kama familia. Hapa nazungumzia kwa familia ambazo zinazika miili ya wapendwa wao mashambani au kando ya makazi. Hiyo ni hatua ya kwanza.

HATUA YA PILI; KABURI HUCHIMBWA KWA KUFUATA UELEKEO WA MENGINE
Makaburi yote, iwe mijini au vijijini, utayaona yamepangana kufuata mwelekeo mmoja. Katika mazingira ya kijamii, unaweza kusema makaburi yana mitaa. Kama umewahi kufika Tanga mjini, kuna barabara zinasifika sana. Barabara ya kwanza hadi ya ishirini na moja. Au ile mitaa yenye majina ya mikoa ya Tanzania pale, Ilala Ndivyo makaburi yanavyotakiwa kuwa.

Lakini pia, makaburi yana mwingiliano. Unaweza kukuta yamepangika hamsini kwa mstari mmoja, lakini mbele, yakawepo mengine yamekata kona na kutengeneza mtaa mwingine. Lakini katika mpangilio.

Hakuna uchimbaji wa makaburi unaokinzana. Mfano; kaburi moja likiangalia Kusini halafu la pembeni yake likaangalia Mashariki.

HATUA YA TATU; VIFAA VYA KUCHIMBIA KABURI
Kwa kawaida, kaburi huchimbwa kwa kutumia sululu, jembe, chimbio, panga, beleshi (chepe au koleo). Wingi wa vifaa hivyo siyo kigezo, hutegemea na upatikanaji wake.

Sululu, jembe au chimbio ni kwa ajili ya kuchimbia kaburi lenyewe. Chepe ndiyo inayotoa udongo au mchanga ndani ya ardhi ili kupata shimo ambalo ndiyo kaburi lenyewe. Mnaweza pia kuwa na panga kwani wakati mwingine wakati wa kuchimba kaburi hupatikana mizizi migumu ambayo lazima ikatwe.

HATUA YA NNE; UREFU WA KABURI HAUFANANI
Lazima kabla ya kuanza kuchimba kaburi, familia ya marehemu iwe imetoa kipimo cha mwili wa marehemu kwa kamba, kulingana na urefu wake. Hivyo, huwezi kuchimba kaburi kwa kufikiria tu kwani unaweza kukuta umechimba kaburi pana lakini fupi. Au refu lakini jembamba jambo ambalo linaweza kuleta usumbufu wakati wa kushusha jeneza ndani ya kaburi na kulazimika kuliongeza huku waombolezaji wakiwepo.

Kama mwili wa marehemu upo mbali na mahali atakapozikwa na ni mpaka usafirishwe, basi utasubiriwa mwili huo ufike ukiwa kwenye jeneza au ukiwa katika hifadhi nyingine yoyote ile. Mara nyingi kinachopimwa ni jeneza.

Ila kwa wasiyojua, urefu wa kaburi kwenda chini ni kuanzia futi tatu mpaka sita. Hii hutegemea mahali linapochimbwa kaburi au marehemu mwenyewe alivyo. Mfano, maiti ya mtoto wa miezi miwili, huwezi kuchimba kaburi la futi tano mpaka sita kama kwa mtu mzima. Mtoto hata futi tatu linamtosha.

Pia kwenye uchimbaji wa kaburi, linaweza kufika futi sita (urefu wa kitanda) kama eneo hilo lina maji yanayotembea au lina mporomoko. Kwa vile mporomoko hauna uwiano kutoka juu kwenda chini kama ilivyo mahali tambarare.

HATUA YA TANO; MUDA WA KUCHIMBA KABURI
Muhimu kuzingatia kwamba, muda wa kuchimba kaburi haufanani bali unazingatia siku ya kuzikwa marehemu.

Wahenga walituachia utamaduni kwamba, kaburi halitakiwi kulala bila mwili wa marehemu. Kwa maana hiyo, mara zote kaburi huchimbwa siku ambayo mwili wa marehemu utazikwa. Kama atazikwa siku husika, saa kumi jioni, basi siku hiyohiyo kaburi litachimbwa.

Ndiyo maana hata kama kaburi litasakafiwa kwa zege au litajengewa tairizi, lakini itakuwa ni siku hiyohiyo ya mazishi.

Inapotokea kaburi limechimbwa mapema halafu mwili wa marehemu ukachelewa kuzikwa hadi usiku kwa sababu ya usafiri, wahenga walipendekeza kaburi hilo kuingizwa mgomba ulale humo mpaka siku inayofuata ambayo mwili wa marehemu utakuwa umefika tayari kwa mazishi.

HATUA YA SITA; ANAYEWALISHA CHAKULA WACHIMBA KABURI
Kila kazi na ujira wake. Lakini kazi ya kuchimba kaburi ujira wake hutegemea na mazingira. Mfano, vijijini wachimba makaburi huwa hawana malipo kama mijini ambapo kuna ujira wake kutokana na eneo husika.

Wachimbaji wa vijijini hawana ujira zaidi ya kupelekewa chakula kutoka kwenye shea ya waombolezaji msibani.

Kama wachimbaji wataanza shughuli asubuhi, basi kuanzia chai mpaka chakula cha mchana, kinatakiwa kuwafikia wachimbaji. Tena wao wanatakiwa kuandaliwa kwanza kabla ya waombolezaji wengine. Na kama watakuwa hawajashiba, lazima wapewe kipau mbele, ikiwezekana waongezwe chakula.

HATUA YA SABA; MABAKI YA MWILI YANAYOKUTWA WAKATI WA KUCHIMBA KABURI JIPYA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, huwa inatokea wakati kaburi linachimbwa mahali ambapo pameaminika kuwa hapajawahi kuwepo kaburi, mifupa ya binadamu hukutwa. Hapo huwa ni chini ya kuanzia futi tano na kuendelea.

Ikitokea hali hiyo, wachimbaji huikusanya mifupa hiyo kwenye mfuko na kuichimbia shimo dogo mahali, mlemle kaburini na kuizika. Kaburi jipya huendelea.

Sababu kubwa ya kupatikana kwa mifupa hiyo ni kutokuwepo kwa uangalizi wa familia.

Mfano, mwili ulizikwa mwaka 1967. Sasa toka kuzikwa, kaburi hilo halijawahi kufanyiwa matunzo, kama kulijengea. Hapo lazima kaburi litafutika. Na kaburi likifutika, juu panaonekana kama ardhi ya kawaida. Hapo sasa pakichimbwa kaburi lingine mwaka 2021, yaani miaka 54 mbele ndipo mifupa hukutwa chini.

Makaburi ya aina hii ni yale ambayo unakuta familia baada ya kumzika marehemu wao, ilihamia sehemu nyingine mbali na ilipomzika marehemu wao.

HATUA YA NANE; VIFAA VILIVYOTUMIKA KUCHIMBA KABURI HULAZWA UDONGONI
Hatua ya nane ambayo ni ya mwisho katika uchimbaji ni kuviweka juu ya udongo vifaa vyote vilivyotumika kuchimbia kaburi lengo ni kuondoa usumbufu baada ya mwili kufika na kuingizwa kaburi tayari kwa mazishi.

Hivi vifaa, ndiyo vile vilifanya kazi yote ya kuchimba kaburi mwanzo hadi mwisho. Lakini kwa kawaida, vifaa muhimu kuwekwa juu ya udongo ni chepe na majembe ambayo hufanya kazi kubwa ya kuvutia udongo ndani ya kaburi mpaka kukamilika na kuwa na mwonekano wake.

Photograph-of-a-poor-mans-grave-in-Sinza-Makaburini-Photo-by-author~2.jpg
 
Unataka kusema Kabuli ka Mwenda zake lilichimbwa siku anazikwa?
 
Mbona mada za makaburi makaburi ni nyingi sana siku hizi?

Mwingine alikuwa na kina cha kaburi ni futi 6.

Mtuache aisee bado tunataka kufaidi mema ya nchi!
 
Nimekusoma ila hapo uliposema mifupa itakayokutwa ndani ya kaburi ifukiwe mule mule kwenye kaburi atakapozikwa marehemu ndio sijakuelewa, kwanini isichimbiwe sehemu nyingine?
 
Back
Top Bottom