Furaha iliyoje, Tanzania ya matamaniyo yangu imewadia na kuishuhudia!!

Steve Dii

JF-Expert Member
Jun 25, 2007
6,402
1,254
Bila kujali nani atachukua kiti cha urais, bila kujali ni chama kipi kinaongoza nchi, bila kujali kama mimi au wewe tunashikilia kadi za CUF, CCM, Chadema, NCCR, au TLP; leo, Novemba Mosi 2010 Tanzania ya matamaniyo yangu hatimae imewadia.

Ni ile Tanzania niliyoiwaza na kuiombea iharakishe itufikie. Ni ile Tanzania ambayo wananchi wake wanaendelea kuwa wema, wakarimu na wajasiri. Tanzania yenye amani na mwamko mkubwa wa mabadiliko, haswa nyakati za chaguzi kuu. Jambo ambalo kwa pahala pengi Afrika limekuwa tata na chanzo cha maangamizi ya baadhi ya mataifa.

Ni ile Tanzania ambayo kiongozi anateuliwa kwa ubora wake na siyo pesa zake, jina lake wala hila zake. Wananchi wanapohabarishwa na kutathmini utendaji wa waliyemchagua wanapatwa na ujasiri, na ari ya kidemokrasia ya kuweza kuendelea kumweka katika uongozi au kumng'oa na kumweka mwingine anayeonekana atawafaa zaidi.

Tanzania niliyoitamani na kuomba iwadie mapema ni ile ambayo wananchi wake kwa mshikamano wanatambua nguvu waliyo nayo katika kuleta mabadiliko yao wenyewe kupitia kura kwa kung'amua hali waliyonayo na kulinganisha matarajio yao dhidi ya utendaji uliopo. Ni lile Taifa lililojaa wananchi wenye maamuzi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa lao kwa ujumla. Hakika Tanzania hii imewadia na nina imani itaendelea kudumu na kuimarika.

Ni siku ya furaha kwangu na kwa Watanzania wenzangu, kwani kwa mara ya kwanza kabisa maishani mwangu natarajia kujionea Bunge litakalosimamia maslahi ya wananchi wake likiapishwa.

Mungu Ibariki Tanzania.

Steve Dii
 
Back
Top Bottom