FIKIRISHI: Kisa cha mkulima na sekeseke la magugu shambani

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
386
Fikirishi za Ngumbalu 01

Palitokea mkulima aliyerithi shamba toka kwa babu zake wa kufikia baada ya kupiga kelele kwa majirani wa mbali pale alipochoka kuwafanyia kazi mababu hawa kama kibarua . Mababu wakampa shamba likiwa bado lina rutuba safi ya kuotesha mimea na kutoa mavuno ya kuridhisha.
Haikuchukua muda mrefu, shamba hili likaanza kushambuliwa na magugu kadhaa. Nasikiasikia tu kwamba magugu haya yanaweza kuwa yametoka sehemu tatu. Ama yaliota shambani yenyewe mara tu mkulima alipokabidhiwa shamba na mababu wa kufikia ama yalikuwa machipukizi kutoka kwa magugu mama yaliyokuwemo shambani awali wakati linamilikiwa na mababu ama ni yale ambayo kibarua aliyeajiriwa na mkulima kama hisani ya kumsaidi kupata shamba toka kwa mababu aliyaotesha ili kuzuia mengine yasikue na haya tutayaita 'magugu dhibiti'.
Kwa ufafanuzi tu kabla sijasahau, baada ya mwenye shamba kufanya kazi kama kibarua wakati likimilikiwa na mababu wa kufikia kwa muda mrefu aliamua kuajiri kibarua aliyemsaidia sana kulirejesha toka kwa mababu. Alimwajiri ili amsaidie kulima na awe anamletea mazao tu na mwenye shamba alizidi kutoa vitu vyote ambavyo kibarua alimuomba kufanikisha zoezi la kulima na hata kuvuna.
Tukirejea kwenye magugu, yale yaliyojiotesha yenyewe ama kukua kutokana na mama zao yalikuwa na sifa kuu mbili. Kwanza, yalikuwa na uwezo wa kufyonza virutubisho vyote vilivyomo shambani na yakafaidi yenyewe pamoja na machipukizi yake, hapa nayaita 'magugu fyonza'. Mimea mingi shambani pamoja na machipukizi yake ikakosa virutubisho na hata iliyokua kwa tabutabu sana ikatoa machipukizi ama matunda ambayo pia hayana vitamini ama vitamini visivyoweza kutumika sawasawa, ngoja niseme tu kwa ufupi tuseme machipukizi mengi yalikuwa na utapiamlo ama matunda yake yalikuwa meusi badala ya wekundu uliotarajiwa.Sifa ya pili ya magugu haya, yalikuwa imara sana na yakaweza kutambaa mpaka juu ya mimea mingine shambani na kuizongozonga mpaka ama ikafa ama ikadumaa. Hii ilitokana na si tu unene wa magugu haya bali pia uimara wake kutokana na kuvimbiwa na virutubisho. Uimara huu uliyawezesha ama kuyazonga hata magugu dhibiti ambayo kibarua wa mkulima aliyapanda kupambana na haya mafyonza. Nilisahau kukwamba kuwa kibarua aliruhusiwa na mwenye shamba kupanda magugu ambayo yangeweza kuyatafuna haya magugu fyonza. Hata hivyo haya mafyonza yaliweza ama kutoa miba iliyoyachoma haya aliyopanda kibarua 'magugu dhibiti' ama yaliweza kuota juu yake na kuyazongazonga hadi yakadhoofika ama yaliweza kuyaonjesha ladha ya virutubisho yalivyofyonza kwa muda mrefu ama kuyafanya sehemu ya kinga yake pale mkulima anapopita shambani kukagua na akaanza kumlilia kibarua kuwa magugu yamekuwa mengi. Miba hii pia iliweza hata kutishia kumchoma kibarua ambaye hata hivyo alikuwa na viatu imara vya kujizuia. Lakini bahati mbaya mwenye shamba hakuwa na kinga yoyote na alichomwa na miba ya magugu fyonza muda wote alipoyakanyaga mule shambani. Pia, yale aliyopanda kibarua 'magugu dhibiti' kupambana na magugu fyonza nayo yaligeuka kuwa mafyonzaji ama kwa kuwa kibarua alipoyapanda hakuweka kinga imara ya kuyadhibiti pia ama yalijigeuza mafyonzaji kwa makusudi ama kama nilivyosema kwa kuzongwa zongwa na mafyonzaji ama baada ya kuonjeshwa virutubisho kidogo na yale mafyonzaji. Mwisho wake yakapuuzia jukumu lake la udhibiti nayo yakaanza kufyonza

*Kibarua aweka mikakati kadhaa*

Baada ya kuona magugu dhibiti nayo yamegeuka kuwa mafyonzaji akaamua kuweka mbinu kadhaa. Kwanza akamuomba mkulima amchagulie ndege ambao watakuwa na uwezo wa kumpigia kelele wakiona magugu fyonza yanafyonza zaidi ama magugu dhibiti yanapuuzia jukumu lao. Mkulima akakubali na akawaweka ndege, na mwanzoni wote walikuwa ndege waliokuwa na nguvu za kawaida japo walimwimbia mkulima vizuri sana wakati wa intavyuu. Kisha,Ndege wakachagua msemaji wao mkuu. Pia,mkulima akawaomba ndege hawa wakishapiga kelele wateme mate ambayo mkuu wao atayakusanya yote na kumpelekea kibarua ambaye akiona yanafaa atayawekea gundi na kuyamwaga shambani ili kuyanasa magugu fyonza na kuyapa nguvu magugu dhibiti ili yadhibiti magugu fyonza. Hata hivyo, mbinu hii sijui kama ilifaa. Nasikia ndege waliishia ama kuimba nyimbo nyingi za kumsifia kibarua kwa uchapa kazi shambani ama kupiga miluzi tu muda wote, miluzi ambayo hata magugu yaliisikia na kuipuuzia. Magugu fyonza mengine yakatoa fursa kwa wale ndege kuyakalia ama kuyalalia bure ama kuyatumia kujenga viota vyao na vya watoto wao....Bahati mbaya pia, kibarua alipoona ndege kadhaa wanatema mate yenye rangi ya sumu ambayo yangeweza kuua magugu yote, akayaua na mengine akayaficha. Haijulikani kwa nini alifanya hivi labda aliogopa mkulima asingemhitaji tena kama magugu yameisha.Tuyaache haya.
Kibarua pia akaondoa miba aliyokuwa ametengeneza kama Fensi ya Shamba na kuruhusu magugu yatambae kwenda mashamba ya jirani. Pia alimshawishi mkulima atembelee mashamba ya jirani kuona kilimo stadi. Akayapeleka pia magugu dhibiti huko mashamba jirani yajifunze udhibiti. Watoto wa mkulima wengine walivyorejea wakafanya urafiki ama kushirikiana na ndege ama wengine na magugu dhibiti na wachache na magugu fyonza. Nia yao ilikuwa baadaye wachukue majukumu haya kabisa kabisa.Sijui kama walifanikiwa.Tuliache na hili pia.
Pia mkulima aliweka mawe kadhaa shambani. Lipo jiwe moja kubwa ambalo kazi yake ilikuwa kuyaponda magugu dhibiti yanayoshirikiana na magugu fyonza na ilisemekana yale ambayo yangeota juu yake yangekufa. Lakini baadae magugu fyonza yaliota mpaka kwenye kivuli cha jiwe hili kubwa.

*Kibarua apendekeza kuwe na mchanganyiko wa ndege*

Kabla kibarua hajaamua kusema anapumzika kazi, alifanikiwa vitu kadhaa. Kwanza, alifanya ndege wawe mchanganyiko. Alimuaminisha mkulima kuwa ndege wakiwa mchanganyiko wanakuwa na ustadi zaidi wa kuimba nyimbo chache za kuliwaza na nyingi zaidi zinakuwa ni kelele za kumstua yeye na magugu yote na wangetoa mate mazito zaidi. Awali ndege wote walikuwa wa aina moja tu.Walikuwa weusi tii, wenye midomo mifupi ila makucha mareefu. Walikuwa na sifa za ziada, kwanza, walikuwa wengi sana na wakimya sana hasa wawapo kwenye mti wao. Ila sifa yao kuu ni kuwa walikuwa na mpangilio mzuri sana wa sauti hasa wanapotaka kuimba nyimbo za kumsifu kibarua na walikuwa na mshikamano sana kwa suala hili. Pia, kucha zao ndefu ziliwezesha kuwararua ndege wa aina nyingine kiuraisi, nasikia wengi pia walipanda magugu fyonza ama dhibiti shambani kwa siri sana. Wengi wao walihamisha viota vyao toka pembezoni wa shamba hadi katikati mara tu baada ya kushinda intavyuu ya mkulima.Hivyo basi, kibarua akamshauri mkulima kuwa awachanganye ndege hawa na wale weupe,wenye midomo mirefu na makucha mafupi lakini sifa yao kubwa ilikuwa ni kuwa wanapiga kelele nyingi saana kutokana na midomo mirefu. Pia hawa weupe waliweza kutafuna vitu vigumu ambavyo walipowapa ndege wausi matafuno yao, walishindwa kuyatafuna ama kuyameza japo wana midomo mifupi na imara na makoo marefu kuliko ndege weupe. Baada ya kufanya hivyo, kibarua akajipumzisha japo alimshauri mulima ni kibarua gani ambaye angemfaa baada yake.

*Mkulima aajiri kibarua wa Pili*

Baada ya kibarua wa kwanza kupumzika na kumpendekezea mkulima kibarua anayefaa, mkulima akamwajiri huyu kibarua aliyependekezwa. Mwanzoni alionyesha dalili za kuyafyeka magugu. Hata hivyo, yale magugu yaliyopandwa kupambana na manyonyaji pamoja na ndege mchanganyiko ilionekana kama hawana kazi tena. Nilisahau kuwa kibarua wa kwanza alinunua pia mafyekeo kadhaa aliyomrithisha kibarua wa pili, hili nitaliongelea baadae kidogo. Mwanzoni kibarua alitoa fursa hata mimea michanga kuota na kimsingi mimea iliweza kukua sambamba na magugu. Ndege pia walikuwepo lakini hawakupiga kelele sana maana nao walifaidika na mazao ya shambani. Baada ya muda kibarua naye akaamua kupumzika lakini kimsingi muda wake wote wa utumishi shambani, mkulima na watoto wake walifurahi sana bila kujua kuwa shamba lilikuwa linahitaji mbolea.

*Mkulima aajiri kibarua wa Tatu*

Kibarua wa tatu aliyeajiriwa na mkulima mwanzoni alionyesha ustadi sana wa kuyatumia mafyekeo kukata magugu na ama kwa kutyatupia kwenye mashamba jirani ama kukata magugu marefu ya shamba jirani na kuyaleta ndani ya shamba la mkulima ili yakikauka yaongeze rutuba. Badala yake haya ya shamba la jirani yalipofika yakachipua na yakaungana na magugu fyonza ya shambani yakazidi kufyonza virutubisho zaidi. Fyekeo mojawapo alilonunua kibarua mwanzoni likafanya kazi lakini baadaye mkulima akawa anashangaa badala ya kufyeka magugu linatifua udongo na kunatisha virutubisho kadhaa kwenye kingo zake na vingine likarushia kifuani mwa kibarua. Yaani baada ya miaka kadhaa virutubisho vilivyodondokea juu ya kifua cha kibarua vikamfanya awe mzito sana. Hata hivyo, ndege weupe wakapiga kelele za kumlaumu kibarua kuwa kwa nini fyekeo zake hazifyeki mizizi na badala yake zinatifua udongo na kumdondoshea virutubisho kifuani na akachukia sana. Kuna wakati aliikamata midomo mirefu ya wale ndege weupe na kuizungushia kamba.Muda ukafika mkulima akamweka kibarua pembeni na kuajiri mwingine.

*Mkulima aajiri kibarua wa Nne*

Kibarua wa nne alikuwa na sifa kuu mbili. Moja alikuwa anajua kuvalia sana mavazi ya kazi akiwa shambani. Yaani mavazi yake yalikuwa masafi na ya kung’aa muda wote kama malaika na mkulima alijisifu kuwa pengine Mungu amesikia maombi yake kwa kumpa kibarua mwenye sifa zote za utumishi mwema. Pili , alikuwa ni mwongeaji mzuri sana.Alikuwa na uwezo wa kumsimulia Mkulima vichekesho vingi sana na uso wake ulijaa tabasamu muda wote akiwa shambani.Kibarua alianza kazi shambani kwa mbwembwe nyingi sana. Kwanza kabisa, alianza kukokota virutubisho mashamba ya jirani maana alimwambia mkulima kuwa kwa jinsi ambavyo magugu fyonza yamefyonza shamba muda mrefu hata ukiyafyeka na kuyaondoa magugu yote bado virutubisho vya shambani havitoshi mazao yote. Mkulima akakubali kibarua 'aombe' virutubisho shamba la jirani ili kuongeza rutuba shambani mwake. Pia, kibarua akamshawishi 'waazime' mbegu shamba la jirani na watarejesha wakishavuna.Kweli, kibarua alivyoenda kueleza shida alizopata bosi wake mkulima, majirani wakampa pole nyingi sana na mbegu nyingi sana. Nilisema awali kuwa kibarua alikuwa mwongeaji mzuri sana . Wale ndege weupe waliwahi kupiga kelele zilizoashiria kumlaumu kibarua kwa mambo kadhaa. Kwanza,ati alikuwa na mifuko miwili. Ati mfuko wa kulia aliushona kiujanja ili ukiweka mbegu zikifika nusu mkulima anadhani umejaa halafu wa kushoto akaufanya mreefu hata ukiwekwa mbegu hazionekani. Ati, alipopewa mbegu akaweka kidogo kwenye mfuko wa kulia na kidogo mfuko wa kushoto.Ati, kwa kuwa mkulima hakuweza kuona ule wa kushoto kutokana na urefu wake, alivyoona ule wa kulia umejaa mbegu akafurahia na kumsifu sana kibarua. Ati, kibarua pia alikuwa na tabia ya kuwapa mbegu kidogo rafiki zake na nyingine kuwalisha ndege weusi waliomwimbia nyimbo za kumsifu na mwisho wa siku mavuno hayakuwa ya kuridhisha. Pia, walimlaumu kuwa ati hata vile virutubisho alivyokokota toka shamba la jirani ama viligandia kwenye kingo za fyekeo la nyumbani kwake alilopenda kulitumia au yale mafyekeo ambayo alikuwa amewapa rafiki zake kushika na vilivyosalia vikamwagwa shambani vililiwa kwa kasi sana na magugu fyonza na magugu dhibiti mara tu vilipotua ardhini. Deni la mbegu kwa mkulima likaongezeka maradufu kwa ustadi wa kibarua kuazima mashamba mengi ya jirani.Pia, ndege walimlaumu ati kibarua anatumia muda mwingi kutembea kwenye mashamba ya jirani kwa kisingizio cha kutafuta mbegu za kuazima ama virutubisho vya kukokota. Kama kawaida, ndege wale weupe wakapiga kelele sana hadi vifua vikawatuna. Hoja yao ilikuwa kwa nini kibarua akeshe mashamba ya jirani wakati shambani magugu yanakua. Kuna mara kadhaa kibarua aliwaridhisha kwa kuyang’oa kabisa baadhi ya magugu na ndege wakajisifu sana. Muda ukafika kibarua akaonyesha dalili za kutaka kupumzika japo mkulima na wale ndege weusi walitamani sana aendelee kuwa kibarua.

*Mkulima aajiri kibarua wa Tano*

Kama kawaida, kabla ya kibarua wa nne hajapumzika alimpendekezea mkulima kibarua wa kumfaa. Akamsifu kuwa anajua kushika kila kifaa cha kulimia iwe trekta ama jembe. Ndege weupe pia wakajiapiza kuwa watapinga chaguo lolote la mkulima kwa nguvu zote na wakamwonyesha mbadala mwenye nguvu sana na wakaimba nyimbo nyingi sana kumsifu. Wale weusi nao wakaimba nyimbo nzurisana kumsifu kibarua mteule, maana ni wataalamu sana wa kuimba nyimbo za aina hii . Kama kawaida mkulima akamsikiliza kibarua wa nne na wale ndege weusi, na kibarua wa tano akaingia shambani.
Alipofika tu akaanza kung’oa magugu dhibiti kwa mikono yake bila kuvaa glovu hasa yale ambayo yalionyesha kushindwa kazi. Hali hiyo iliyashtua magugu fyonza na magugu dhibiti yaliyokuwa yamegeuka mafyonza na walau nayo yakaanza kuparangana kuonyesha kuwa yanaweza kuyadhibiti magugu fyonza. Tatizo kubwa la kibarua wa tano, ni kuwa aliamua kuuingilia hadi ule mti wanaokaa ndege weusi na weupe. Kwanza, nasikia ndege weupe walipiga kelele sana kuwa alifanya ujanja ujanja kwa kushirikiana na ndege weusi kuweka wakuu wawili wa wale ndege wote wale anaowataka yeye.Hasa yule mkuu wa pili mdogo. Kibarua hakusikia kelele hizi. Huyo mkuu mdogo wa pili alifanya vitu vikubwa viwili. Kwanza, akisaidiana na ndege weusi, waliuhamishia kwenye bonde lenye giza ule mti uliokuwa kwenye kilima chenye mwanga na ambao mkulima aliweza kuuona akisimama kibarazani. Huko bondeni penye giza ulipopelekwa mpaka mkulima aweke jiwe juu ya mlima asimame juu yake ili auone. Pili, akaishika midomo ya wale ndege weupe na siyo tu kuifunga kwa kamba midomo yao mirefu bali pia wale wanaopiga kelele sana aliwanyonyoa baadhi ya manyoya kwenye mabawa na kuwashusha juu ya mti ili wasubiri manyoya yaote tena. Yule mkuu mkubwa wa kwanza haijulikani vizuri alienda wapi.

*Maswali kwa wasomaji*

Ni kweli shamba lilikuwa na magugu mengi sana lakini maswali ya kujiuliza ni haya 1) je kibarua huyu anayeng’oa magugu kwa mikono yake peke yake tena bila glovu ataweza kulisafisha shamba zima ama mikono itaota sugu na vidonda achoke kuyang'oa? 2)si angeweka utaratibu mzuri ili mkulima pia amsaidie kung'oa magugu mara apatapo fursa? 3)Je ule mti wa ndege uliopelekwa bonde lenye giza utamsaidia chochote? 4)Je uamuzi wa kuwafunga mdomo, kuwang’oa manyoya na kuwashusha juu ya mti wale ndege weupe wanaopiga kelele sana utamsaidia lolote kibarua? 5) Ndege weusi wataweza kubadili sauti zao toka nyimbo za kumliwaza kibarua hadi kumpigia kelele? 6) Je magugu fyonza yanayoonekana yamekaa kimya toka kibarua alivyoajiriwa yatakoma kufyonza kweli ama ndiyo ule mtindo wa ukiona Kobe kainama atunga sheria?

Tuendelee kufuatilia kisa hiki cha mkulima na magugu shambani
 
Back
Top Bottom