Fahamu kuhusu Samuel Macvea (ngumi jiwe)

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,590
2,088
Ndondi ni moja ya mchezo bora sana ila hatari katika orodha ya michezo duniani, ni mchezo ambao mabondia hutoka na fedha nyingi sana iwe amepigwa au ameshinda inategemea mkataba wake upo vipi, ila ndondi ni mchezo ambao kiukweli una uzuri wake sana, karne ya 16 mpaka 18 ndipo mchezo huu ulipata kuwa na umaarufu mkubwa sana huku watu wengi wakianza kujifunza na kujifua zaidia ili waende kupambana na wengine.

Bondia kama Gene Tunney ambaye huyu aliwachakaza wenzake kwa mtindo wa KO zaidi ya mara 49, Tunney yeye alishiriki kwenye mapambano 88 na kushindia mapambano 82 huku katikaa hayo akiwacharaza mabondia kwa mtindo wa KO katika mapambano 49, Tunney aliwadondosha na kuwavurugia siku mabondia wakubwa kama, Harry Greb, Jack Dempsey pamoja na Bobby Dawson.

Mashabiki wa ndondi watakuwa wanamkumbuka vyema sana Bwana Archie Moore bondia ambaye aliwachapa vibaya sana watu kama Harold Johnson pamoja na Joey Maxim. Pia Ezzard Charles maarufu kama Cincinnati Cobra, ama Emile Griffith ambaye aliwatesa sana mabondia miaka ya 1960 mpaka 1970 kipindi ambacho Griffith alishinda mikanda mitano ya ubingwa wa dunia.
images%20(21).jpg

Wengine watasema kuwa bondia bora alikuwa ni Tony Canzoneri ambaye yeye tunamfananisha na Mayweather kwa mtindo wake wa upiganaji huku akiwavuruga vibaya sana mabondia kama Jimmy McLarnin, Barney Ross pamoja na Billy Petrolle. Kuna kundi jingine litasema bondia wa kipekee sana kutokea ni Muhammad Ali, bondia ambaye kabla ya kukutana na Sonny Liston ulingoni basi aliwachapa mabondia wanne waliokuwa kwenye orodha ya mabondia 10 bora kwa kipindi hicho.
images%20(7).jpg

Wapo wachache watamtaja Joe Louis maarufu kama The Brown Bomber, Louis alitetea mkanda wake katika mapambano 25 mfululizo, na ajabu ni kuwa kuanzia mwaka 1930 mpaka 1956 mabondia tisa walivaa ubingwa basi Louis aliwachapa mabondia saba, hii ikiwa ni pamoja na KO bora sana kwenye ulimwengu wa ndondi ambayo Louis alimpatia kwenye mzunguko wa kwanza Bondia Max Schmeling.
images%20(14).jpg

Lakini ngoja mimi leo niende tofauti na mawazo na maono ya wote hapo, leo natamani sana nipate kusimulia maisha ya bondia mmoja ambaye alikuwa na mchango mkubwa sana sio tu kwenye mchezo wa ndondi bali hata katika kupigania haki za mtu mweusi.

Kama wewe ni mpenzi wa mchezo huu basi jina la huyu bondia utakuwa umepata kulisikia likitajwa mara kadhaa na watu, ingawa alifaraiki yapata miaka mia moja na moja hivi ila bado ameacha alama kwenye dunia haswa katika ulimwengu wa ndondi. Wapo wale wakongwe wa mchezo wa ndondi ukiwauliza kama wanamfahamu Oxnard Cyclone basi wanaweza kukusimulia mengi sana kuhusu huyu mtu ingawa Oxnard Cyclone sio jina lake rasmi bali ni jina la utani tu.
Sam_McVey.jpg

Tarehe 17 mwezi Mei mwaka 1884 huko Waelder Texas Marekani alizaliwa mtoto wa kiume katika familia ya watu weusi ama waafrika wanaoishi Texas Marekani, na kupewa majina ya Samuel MacVea, mtoto huyu alikuja kufungua dunia mpya ya mchezo wa ndondi kwani ni MacVea ndo alikuja kukaa kwenye orodha moja na mabondia kama Jack Johnson, Joe Jeanette, Sam Langford pamoja na Harry Wills ambapo wote hawa walikuwa ndo mabondia wakubwa wenye rangi nyeusi.

Kumbuka kipindi cha nyuma mchezo wa ndondi ulikuwa na ubaguzi wa rangi kupita maelezo na wazungu walikuwa wakipambana kivyao na watu weusi wakipambana kivyao.

Ripoti zinadai kuwa katika mapambano 96 ambayo MacVea aliyacheza kwenye nchi tofauti tofauti zaidi ya 10 basi alipoteza mapambano 16 tu, kwa maana ya kwamba mapambano 80 aliwachakaza vibaya sana mabondia wenzake, na katika mapambano hayo kuna pambano dhidi ya bondia Sam Langford, pamoja na Harry Wills, na ndo alipopata nafasi ya kuchukua ubingwa wa dunia wa World Colored Heavyweight Championship.

Ingawa pia Macvea alitumia muda wake kufundisha wazungu na watu weusi mchezo wa ndondi haswa katika mapambano muhimu.Oxnard Cyclone ni jina la utani alilopewa likiwa na maana ya Kimbunga cha Oxnard, na Oxnard ndo sehemu ya mji ambao MacVea alikuwa akiishi kwa wakati huo. MaVea alikuwa akipigana kwenye uzani wa kilo 93 mpaka kilo 100 sasa jiulize uzito wote huo je ni mabondia wangapi wanaweza kucheza ndondi?

MacVea alijifunza zaidi kutumia mikono yake kupiga ngumi zenye nguvu sana kuliko utaalamu na akili, yaani akiona umeshachoka basi anakutupia ngumi nyingi nzito kiasi kwamba lazma utadondoka tu.
images%20(24).jpg


Pambano la kwanza la MacVea lilikuwa ni mwaka 1902 yaani akiwa na miaka 18 tu ingawa gazeti moja la mwak 1902 lilionesha kuwa kabla ya pambano la MacVea dhidhi ya Jack Forgarty kulikuwa na mapambano matano ambayo MacVea alipambana akiwa Australia na alishinda yote, pamoja na mapambano mengine wawili yaliyofanyika California.
images%20(23).jpg

Kipindi hicho ilikuwa ni ngumu sana kwa bondia mweusi kupata pambano dhidi ya mzungu hivyo basi MacVea alikuwa akicheza mapambano mara kwa mara na mabondia wenzake weusi kama vile Sam Langford ambaye walipambana mara 15, Joe Jeanette walipambana mara 5, Harry Wills walipambana mara 5 pia, pamoja na Jack Johnson walipambana mara 3, kiujumla matokeo ya MacVea yalikuwa ni jumla ya mapambano 65 ya ushindi, alipoteza mapambano 16 na sare mapambano 12.

Baada ya kupata umaarufu MacVea alianza kusafiri na kwenda nchi zingine kupambana na mabondia wengine, mwaka 1907 alikwenda Ufaransa pale Paris na kucheza ndondi kwa miaka minne, akiwa huko ndipo alipopewa jina la L’ldole de Paris. Siku ya mkesha wa mwaka mpya wakiwa wanasubiria mwaka 1909 huko London Uingereza MacVea akapata nafasi ya kucheza pambano na mtaalamu wa Jujutsu kutoka Japani Tano Matsuda, ambaye huyu alikuwa ni Bingwa wa World Championship of Ju-Jitsu.
View attachment 2795176

Mwanzoni MacVea alikuwa na wasiwasi sana kuhusu pambano hilo huku bondia Sam Langford akimvuruga zaidi kwa kumwambia kuwa “Lord Almighty, Sambo, [bold]He’ll snap youse bones like matches”[/bold] akiwa na maana ya kwamba akienda kuambana na Tano Matsuda basi Mifupa ya MacVea itavunjwa kama jiti za kiberiti.

Na sentensi hii ilitosha kumpa hofu kubwa MacVea ukizingatia kuwa Sam Langford ni bondia mkubwa na anafahamiana na watu wengi, inaweza kuwa kweli. Basi mfukunzi wa MacVea, Bwana Duke Mullins alimpa ushauri MacVea kuwa akiingia ulingoni basi afanye kumpatia Tano Matsuda ngumi moja nzito sana ya kumaliza mchezo.

Ila mkufunzi aliongeza kuwa Matsuda akikwepa hiyo ngumi basi jiandae kukutana na mateke ya uso mengi na ukumbi kumshangilia sana, mwishoni MacVea alijisema kuwa “Sitomkosa hakika, Mungu nisaidie”. Ila cha ajabu ni kwamba MacVea alimpiga KO ndani ya sekunde nane tu kwenye mzunguko wa kwanza, baada ya kumpa ngumi moja kwenye taya na kumuacha Tano akiwa na maumivu ya ajabu.
View attachment 2795180

Kumbuka kuwa nyakati hizo mapambano kama haya yalikuwa ni mengi haswa mabondia kutoka Marekani na Ulaya walikuwa wakipambanishwa na wataalamu wa mapigano ya Judo pamoja na Jujutsu ndani ya nchi ya Japani. MacVea aliondoka na paundi 2,000.

MacVea aliwahi kupambana pia na mtaalamu wa Ju-Jitsu, Profesa Stevenson ambaye huyu alikuwa ni mtaalamu kweli kweli kiasi cha kupata nafasi ya kwenda kufundisha wanajeshi na polisi huko Australia. Kisa cha Stevenson kujifunza mapigano haya ni kutoka kwa Mjapani ingawa binafsi Stevenson hakuwahi kumfundisha mzungu Ju-Jitsu.

Mzawa kutoka Broken Hill, Bondia Reynolds aliwacharazwa vya kutosha na Stevenson katika pambano la mizunguko tisa ambapo katika mzunguko wa sita Stevenson alimtegua bega Reynolds.Sasa Profesa Stevenson akamtamani sana MacVea mara baada ya kuona mwenzake Tano Matsuda kachezea ngumi moja ya taya. Siku moja Stevenson alinukuliwa akisema “Ninajiamini kuwa naweza kuwapiga Sam MacVea pamoja na Sam Langford ndani ya saa moja tu” na alitumia muda wake mwingi kuelezea kuwa mchezo wa ndondi sio mchezo hatari kuliko sanaa kutoka Japani ya Ju-Jitsu na hata bondia awe na nguvu kiasi gani hawezi kumpiga mtaalamu wa Ju-Jitsu yoyote.

Na Stevenson aliweka kiasi cha paundi 150 kwa kucheza na mmoja kati ya McVea ama Langford kwenye mpambano wa mizunguko 12 ya dakika tano tano. “Wao ni bora kwenye dunia yao ila mimi ni bora hata kwenye dunia yao na nina uwezo wa kumpiga bondia yoyote yule.”

Wote wawili (MacVea pamoja na Langford) walimpuuza Stevenson ila dharau zilizozidi basi Macvea akaamua kuonesha utaalamu wake na kuomba mapambano na mabondia kadhaa ambao walitaka kuosha nyota zao. Basi baada ya kuonesha makeke yake na nguvu zake za kuweka ngumi nzito kwenye ukumbi wa Rink Hall, McVea alisimama na kuomba pambano rasmi dhidhi ya Stevenson, na kuweka dau la paundi 25 lakini kwa dharau kubwa Stevenson alikataa dau hilo na kuweka dau la paundi 100 yaani zaidi ya paundi 75! Duuh!

Sheria za pambano hilo ni zile zile, hakuna kung’ata, kupiga kichwa na kupiga sehemu zenye hatari kama kwenye kende, kisogoni, pamoja na moyo. Ila kumchapa mwenzio kwenye mbavu haswa kwenye upande wa figo unaruhusiwa pamoja na namna zingine za hatari za kushambulia. McVea alikuwa na uzito zaidi kwa kilo 23 ila kiburi cha Stevenson kikakubali kupanda ulingoni na jitu hili.

Mzunguko wa kwanza ulipoanza tu, Stevenson aliruka sarakasi na kumpiga teke McVea ambaye hakutetereka hata kidogo, katika mizunguko mine ya kwanza Macvea alizidiwa sana kwani mara kadhaa Stevenson alikuwa akifanya ujanja wa kumuwahi kwenye miguu sana sana na hii ilimfanya MacVea kushindwa kutupa ngumi vyema.
View attachment 2795175
Lakini katika mzunguko wa tano mambo yalibadilika mara baada ya upande wa MacVea kumwambia McVea kuwa aache masihala kabsa na amalize mpambano sasa, wakati huo ukumbi wote unajua kuwa Stevenson ndo anakwenda kumaliza pambano. McVea anakumbukwa kwa kuwa na shabaha kali sana na Stevenson alitambua hilo ila dharau zake zilimponza kwani alimfuata McVea na ghafla zilitupwa ngumi nne kwa haraka sana kiasi kwamba Stevenson alikwenda chini mzima mzima.

Ukumbi wote ulikaa kimya huku Stevenson akiwa haamini kinachoendelea. Aliporejea Stevenson alimrukia McVea na kumuweka chini kwa mtindo wa kumkaba ila alipopata nafasi tena MacVea alimpiga Stevenson ngumi tatu za nyuma ya shingo na Stevenson akalala tena chini, baada ya kuona kuwa kibano kimewageukia basi kona ya Stevenson iliamua kurusha taulo na hapo ndo ukawa mwisho wa shobo za Stevenson bingwa wa Ju-Jitsu kwa McVea.
View attachment 2795178
Mbinu ambayo ilimsaidia sana McVea ni kusubiria wakati sahihi wa kushambulia kwa kutazama udhaifu wa mpinzani wake ingawa Stevenson hakuongea chochote na aliondoka ulingoni akiwa amevimba shingo na aibu kutoka kwa mashabiki.

Tarehe 17 Aprili mwaka 1909 katika ukumbi wa Salle des Fetes Roubaix huko Paris, Sam MacVea alizichapa na Joe Jeanette kwenye pambano ambalo ndo linasadikiwa kuwa ndo pambano bora zaidi na pambano lililokuwa na mizunguko mingi kuwahi kutokea katika historia ya ndondi duniani.
View attachment 2795179
Pambano hili lilikwenda mpaka mizunguko 50 na lilichezwa kwa muda wa masaa matatu na nusu, hatari sana! Katika mzunguko wa 21 na 22 MacVea alimdondosha Jeanette ingawa mpaka kufikia mzunguko wa 40 Jeanette alijiteta na kurudi mchezoni na hapo MaVea alianza kupigwa mfululizo kiasi kwamba macho ya MacVea yalivia damu na kushindwa kabsa kutazama na ilimbidi kukubali na kutii amri hivyo Jeanette akashinda kwa TKO.

Siku saba tu baadaye alicheza Fred Drummond na kumchapa KO katika mzunguko wa tano katika ukumbi wa Nouveau Cirque huko Orleans Ufaransa.Mwaka 1911 alikwenda Australia ambapo huko alicheza ndondi kwa miaka matatu kabla ya kurudi Marekani, alipokuwa Australia katika mwaka 1912 MacVea alikuwa ni mmoja ya mabondia ambao walionesha ubora sana na kutegemewa kuja kuchukua ubingwa wa dunia wa World Colored Heavyweight Championship ambapo mapambano yalichezwa katika sehemu mbalimbali za nchi ya Australia.

Mpinzani wa MacVea alikuwa ni Sam Langford maarufu kama Boston Tar Baby moja ya mabondia bora sana kuwahi kutokea. Basi kabla ya mapambano mabondia walitakiwa kuonesha midadi na makeke yao, wapo walioonesha namna ya kupiga ngumi kwa uharaka zaidi, wapo wengine walionesha namna ya kukwepa ngumi kwa wepesi ila McVea aliwacha watu hoi na hofu kubwa.
View attachment 2795181
McVea yeye alionesha namna ya kupiga ngumi nzito tu na wala sio kujilinda na aliwahi kunukuliwa akisema kuwa yeye atajilinda endapo tu akiona kuna ulazima huo ila binafsi anatamani kumuona mtu akiwa amelala chini na maumivu tu.Sam Langford alikuwa ni bondia mwepesi sana miguuni na aliwahi kuwa mcheza dansi hivyo anafahamu namna ya kuutembeza mwili wake ila alipokutana na McVea na namna anavyozitupa ngumi hakika alikiona kile kimbunga cha Oxnard. Sam Langford aliamua kuwaita wakufunzi wake na kuwapatia maelekezo kuwa wafanya kumpiga ngumi nyingi akiwa mazoezini ili aanze kuzoea zaidi kipigo.

Katika pambano hilo liliofanyika kwenye Uwanja wa Sydney, McVea alimteremshia ngumi nzito katika sehemu ya tumbo kiasi kwamba Sam Langford aliona ni heri ya kukubali kushindwa kuliko kifo, pambano hilo liliisha kwa MacVea kushindia kwa alama.

Akiwa Australia aliwachapa mabondia kama Jack Lester,Bill Lang, Jim Barry, huku akizichapa na Sam Langfor mara tano mfululizo kuanzia tarehe 8 Aprili, 1912 mpaka Machi 24 1913 yaani mwaka mzima unapigana na bondia mmoja tu, pia Collin Bell, Arthur Pelkey nao walionja utamu wa ngumi za MacVea.
View attachment 2795177
Mwaka 1921 McVea alipata kupambana mapambano manne tu, akipambana na Jeff Clark na McVea alishinda kwa alama, na mapambano matatu ya mwisho ya MacVea yalikuwa ni baina yake na Jeff Clark na alipanda ulingoni mara ya mwisho kwenye ukumbi wa Rossmere Park, Pennsylvania Marekani Agosti mosi mwaka 1921, na baadaye McVea alikutwa na ugonjwa wa homa ya mapafu alipambana na matibabu sana.

Ila mwezi Disemba kwa bahati mbaya tarehe 23 Disemba siku mbili kabla ya sikukuu ya Krismas, Bwana Samuel MacVea alifariki dunia huko New York, kwa heshima ya MacVea basi Bondia Jack Johnson alijitolea kushughulikia mazishi ya MacVea.

Na mpaka MacVea anafariki dunia, bondia huyu alikuwa amepambana katika mapambano 112 na katika hayo alishinda mapambano 78, huku mapambano 60 yakiwa ni katika mtindo wa KO, amepoteza mapambano 18 na ametoka sare mapambano 13 huku akiwa na ushindi wa mapambano mawili ya All In ambayo kwa sasa yanajulikana kwa jina la UFC.

Mchango mkubwa wa MacVea ukiachana na ndondi ni kuwa yeye pamoja na mabondia wenzake weusi walitumia ubingwa wao kuonesha msimamo dhidi ya ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa umeshamiri sana ndani ya Marekani na Ulaya, kwani ukiachana na Johnson hakuna bondia mwingine ambaye alipata nafasi ya kushiriki kwenye kufauta ubingwa wa World Heavyweight Championship kutokana na kuwa na rangi nyeusi.
View attachment 2795182
Wazungu waliogopa sana kukutana na watu kama Herbet Sinnot, Jeff Clark, Cahrlie Wilson ama Hary Shearing.Ila McVea na wenzake wanabakia kuwa alama kubwa sana ya utetezi wa haki za watu weusi duniani kupitia ndondi kiasi kwamba kukatokea mabadiliko ya namna ya uendeshaji wa mashirikisho ya ndondi, kwa sasa hakuna cha World Colored Heavyweight Championship wala cha ubaguzi wa rangi, ndondi imepata kuheshimishwa sana hawa watu, waliwanyamazisha watu waliokuwa wakiongea maneno ya ovyo kuhusu ndoni kama vile, Stevenson pamoja na Matsuda.
Uendelee kulala mahali pema Mwamba!
Asante Samuel McVea.
 

Attachments

  • images%20(29).jpg
    images%20(29).jpg
    35.1 KB · Views: 10
Back
Top Bottom