Dkt. Mwigulu asema Tanzania inakopa kwa sababu inaweza kulipa

Mjanja M1

JF-Expert Member
Oct 7, 2018
3,660
12,306
Serikali imesema nchi inaendelea kukopa fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kimkakati kwa sababu ina uwezo wa kulipa.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Februari 23, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, akisema kadri nchi inavyokuwa tajiri ndivyo viwango vyake vya madeni huwa vikubwa.

Kauli hiyo ameitoa wakati ambao Serikali imeongeza matumizi ya fedha kwa ajili ya kulipa madeni kutoka Sh9.1 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh10.4 trilioni kwa mwaka 2023/24.

Dk Mwigulu amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akisaini mikataba miwili ya mikopo yenye thamani ya Sh398.7 bilioni.

Mikataba hiyo ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Tabora – Kigoma – Uvinza – Malagarasi, na mkataba wa kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk Mwigulu amesema ukiona nchi inakopa maana yake anayekopesha anajua kuwa atarejeshewa fedha zake.

"Mtu mwenye uwezo ndiye mwenye deni kubwa hata mataifa yale tajiri duniani ndiyo yenye madeni makubwa zaidi, zile nchi zilizoendelea kabisa zina madeni makubwa kuliko Tanzania," amesema.

Amesema watu wanapaswa kuelewa nchi itakapokuwa tajiri zaidi na deni litakuwa kubwa kuliko sasa, na inakopa kwa sababu ina uwezo wa kulipa.

"Tunazichukua tufanyie kazi, fedha zilezile ambazo tungechukua kidogo-kidogo kufanyia kazi kwa miaka 40, tunachukua mikopo kwa sababu tuna fedha ya kurejesha, badala ya kujenga reli kwa kila mwezi kukusanya hela tunachukua fedha tunajenga halafu reli ikiwa inafanya kazi tunalipa deni," amesema.

"Tunakopa kwa sababu tuna miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi kwa wakati mmoja kutekelezwa.”

Amesema hadi sasa madeni ambayo ni mzigo mkubwa kwa nchi ni yaliyokopwa kwa masharti ya kibiashara.

Dk Mwigulu amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alitaka mikopo yenye riba nafuu, akieleza hiyo ndiyo sababu ya AfDB kushiriki ujenzi wa SGR na Benki ya Dunia (WB).

"AfDB na WB ina mikopo ya chini ya asilimia mbili lakini benki ya biashara unapata asilimia 10 hadi 11 mara tano zaidi," amesema Dk Mwigulu.

Amesema hilo pia linafanyika kwa sababu makandarasi si mali ya Serikali, bali ni watu wenye kazi ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo ni ngumu kumuweka kwa miaka 60 akijenga mradi wako.

Source - Mwananchi
 
Mwisho wa siku tunasimangwa tuhamie burundi,tule nyasi,tupige mbizi
 
Back
Top Bottom