Dk Shein Aahidi Kuwachukulia Hatua Waliofuja Mali ya Umma

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482





Na Mwantanga Ame

BAADA ya serikali kukabidhiwa ripoti ya Kamati teule ya Baraza la Wawakilishi, iliyochunguza mambo mbali mbali yaliyoibuka kwenye majadiliano ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, ameahidi kuwachukulia hatua watu waliotajwa ndani ya ripoti hiyo baada ya kufuja mali ya umma.

Dk. Shein, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari huko katika Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake aliojiwekea wa kuzungumza na Wananchi kila baada ya mienzi mitatu.

Alisema tayari ripoti hiyo imepokelewa na serikali lakini inalazimika kuridhiwa kwa ajili ya kuwachukulia hatua watu waliotajwa ndani ya ripoti hiyo kama tuhuma zilizo juu yao.
Alisema kama serikali ina njia zake za kupita katika kulifanyia kazi suala hilo ni lazima zifuatwe na si vyema kukurupa bila ya kufanya utafiti kwa kuwa ripoti hiyo inaelezea mambo mengi.

Alisema kama yeye ndio kiongozi wa nchi hatoacha kuwawajibisha watumishi watakaowaona kuwa wanastahiki kufanyiwa hivyo kwani nchi ni lazima suala la utawala bora ni moja ya jambo la msingi ambalo linalazimika kulisimamia.

Alisema ni kweli Chama cha Mapinduzi, kilitoa tamko la kutaka kuwawajibishwa watu waliotajwa kufuja mali ya umma katika Serikali ya Muungano, lakini kabla ya kufanya hivyo serikali ilipata nafasi ya kujiridhisha na uchunguzi uliofanywa kwa Mawaziri waliotajwa kuhusika na masuala hayo.

Kutokana na hali hiyo Dk. Shein, alisema na serikali ya Zanzibar kwa kufuata mfumo huo wa ndani ya Chama cha Mapinduzi atahakikisha kazi hiyo inatekelezwa bila ya kumuonea mtu ambapo wakati ukifika jamii itaelezwa bayana.

"Taarifa imeletwa kuna taratibu tunazifanya kama serikali hakutakuwa na siri mtayasikia wakati wa kufanya maamuzi hata Serikali ya Muungano iliyapima mwisho nasi tutaamua wakati ukifika," alisema Dk. Shein.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa Nne wa Baraza la Wawakilishi ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya Bajeti, Baraza hilo liliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi kuchunguza mambo mbali mbali.

Matokeo ya Kamati hiyo iliyoifanya kazi hiyo chini ya hadidu rejea saba imetoa mapendekezo mbali mbali huku ikiwataja baadhi ya Mawaziri waliopo madarakani kuhusika na matukio mbali mbali ya uharibifu wa mali za umma.

Baadhi ya mapendekezo hayo kwa Idara ya Mrajis serikali imetakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Wananchi wote waliohusika katika udanganyifu uliojitokeza katika Upatikanaji wa Mikataba ya Mauziano kutoka katika Mamlaka ya Serikali na kumuuzia Juma Ali Kidawa na mauziano baina ya Juma Ali Kidawa na Amina Aman Abeid Karume.

Aidha Kamati hiyo imeagiza zichukuliwe kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati waliohusika na upatikanaji wa Mkataba wa Mauziano ya Nyumba Namba 755/56 kwa thamani ya shilingi. 5,000,000/- baina ya Wizara hii na Kidawa pamoja na Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali walioshiriki katika upatikanaji wa Mkataba wa Mauziano hayo.

Watu wengine waliotajwa kutaka kuchukuliwa hatua ndani ya ripoti hiyo ni pamoja na Viongozi na Watendaji wote waliohusika na kadhia ujenzi wa jengo jipya la Wizara ya Fedha, Pemba wawajibishwe kisheria, kwa sababu imethibitika kwamba, Wizara ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo imechangia kutokezea kwa tatizo la kujengwa jengo hilo chini ya kiwango.

Hali hiyo imeelezwa na ripoti hiyo ilitokea baada watendaji waliosimamia hilo kushindwa kufuata taratibu za Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za Serikali , Namba 9 ya mwaka 2005, katika kumtafura Mjenzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara.

Kamati hiyo pia imependekeza Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora waliohusika na kadhia kufanya ajira katika Wizara ya Mawasiliano baada ya kudaiwa kuwapa jamaa zao wawajibishwe kisheria.

Pendekezo jengine lililotolewa na kamati hiyo ni hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe kwa Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege waliohusika na upotoshaji wa Kamati kwa kutoa taarifa zisizo za kweli.

Vile vile kamati hiyo imeagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano; Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.
 
Back
Top Bottom