BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
Miaka sita ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ilikuwa mwiba kwa Chadema, inayotimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kwa kuwa zilifunguliwa kesi nyingi zilizowahusu viongozi, wanachama na wafuasi pamoja na kushambuliwa, kuuawa na wengine kutoweka.

Licha ya mfumo wa siasa za vyama vingi kurejeshwa nchini kwa mujibu wa Katiba na Serikali ya awamu ya pili mwaka 1992, Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilizuia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani.

Zuio hilo la mikutano ya hadhara lilipingwa kwa kuwa lilikuwa kinyume cha sheria, lakini liliendelea hadi Rais Samia Suluhu Hassan alipoliondoa Januari 3, mwaka huu.

Maoni ya wadau

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameishauri Chadema kuitumia vizuri fursa ya kuruhusiwa mikutano kwa kufanya siasa makini na kuacha siasa za malumbano.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Conrad Kabewa anasema Chadema kwa kutimiza miaka 30 wamekomaa, ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita.

“Kipindi cha nyuma Chadema walikuwa chini sana, ukiwatafuta wilayani hawakuwepo, waliweza kufanya mikutano mikubwa, lakini chini kwa wananchi hawakuwepo,” anasema Kabewa.

Anasema hali hii iliwafanya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wakose wagombea ubunge kwenye majimbo 70 na kwenye maeneo walikopata wagombea walikuwa dhaifu.

“Hata sehemu walikopata wagombea ubunge walikuwa ‘substandard’ (chini ya kiwango), hawakuwa na ushindani ndani ya chama na wala hakukuwa na mchujo. Ni mtu amekwenda ofisini na kuchukua fomu na kujaza kugombea,” alisema Kabewa.

Amesema baadaye Chadema ilishituka na kuanzisha Chadema ni Msingi na walifanikiwa sana kukijenga chama chao na kufika hadi chini kwa wananchi.

Kabewa amesema kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 Chadema walisimamisha wagombea ubunge kwenye majimbo yote na wagombea udiwani walifikia asilimia 90.

“Walifanikiwa sana kwenye kampeni ya Chadema ni Msingi, walianza kuonekana hadi vijijini na kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji wa 2019 walisimamisha wagombea wenyekiti kwenye vijiji vyote, vitongoji vyote na mitaa yote,” alisema.

Amesema hata kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Chadema kilisimamisha wagombea ubunge kwenye majimbo yote na wagombea udiwani kwenye kata zote nchini.

Kabewa amewataka Chadema waendelee kukijenga chama chao na kwamba wasibweteke na ruhusa ya mikutano ya hadhara.

“Watoe elimu ya uraia, wananchi hawana elimu ya uraia. Zamani elimu ya uraia ilikuwa ikitolewa na asasi za kiraia, lakini zimefungiwa.

“Chadema waache siasa za malumbano, watoe elimu ya uraia. Siasa za malumbano wafanye wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, siku 90 za kampeni zinawatosha,” alisema Kabewa.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, Edwin Soko amekishauri Chadema kutumia vizuri fursa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mabadiliko nchini.

“Nawashauri Chadema watumie fursa ya Rais Samia vizuri kwa kufanya siasa makini zenye mashirikiano makini katika kufanikisha kuleta mabadiliko ya Katiba, sheria na kanuni mbalimbali,” alisema.

Soko amesema Chadema watumie mazingira ya siasa yaliyoonyeshwa na Serikali ya awamu ya sita kutafuta kuungwa mkono na wananchi kwa kunadi sera zao.

Amesema pia Chadema wasikate tamaa kushindwa uchaguzi kwa kuwa demokrasia katika Afrika upinzani unapita wakati mgumu.

“Wasikate tamaa, wazungumzie matatizo ya wananchi kwa kunadi sera zao kuonyesha namna watakavyoweza kuondoa shida za wananchi na kuwapa maisha bora,” alisema Soko.

Amesema anafahamu Chadema imepita kwenye mazingira magumu ya kisiasa, hasa katika Serikali ya awamu ya tano, lakini wameweza kuonyesha kuwa wao ni chama kikuu cha upinzani nchini.

Kuzuia mikutano ya siasa

Mara tu baada ya kuingia Ikulu, Rais John Magufuli aliweka wazi msimamo wake kuwa hatapenda kuwaona wanasiasa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara.

Hoja yake kubwa ni kuwa “watu waachwe wafanye kazi na kulijenga taifa” na wanasiasa wasubirie kampeni za Uchaguzi wa 2020 ili kuzunguka nchi kujinadi.

Chama kikuu cha upinzani cha Chadema kilitangaza operesheni ya kupinga kile walichokiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na kudhamiria kufanya mikutano na maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, 2016, lakini waliisitisha kabla ya kuanza.

Baada ya agizo hilo polisi walianza kuwashughulikia wafuasi na viongozi wa upinzani waliodaiwa kukaidi marufuku hiyo na takriban wabunge 17 wa upinzani walifikishwa mahakamani.

Magufuli alionya wapinzani kupitia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa amehamia Chadema kwamba awaeleze wenzake kuwa wasipotii sheria wataishia jela.

Matukio mengine

Kipindi hicho viongozi wa Chadema walipata misukosuko mingi, mfano aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alikaa mahabusu kwa zaidi ya miezi minne akikabiliwa na kesi za uchochezi.

Matukio mengine ni kunusurika kifo kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017. Pia, tukio la mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo lililotokea Novemba 14, 2015.

Februari 11, 2018 yalitokea mauaji ya kiongozi wa Chadema, Daniel John ambaye kwanza alitekwa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni na baadaye kukutwa amekufa.

Pia, kupotea kwa Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akimsaidia kufanya tafiti na uchambuzi katika masuala ya siasa na uchumi.

MWANANCHI
 
IMG_3368.jpg
 
Back
Top Bottom